NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, May 16, 2011

Shule ya Sekondari ya Buluba Mkoani Shinyanga Nayo Yapata Mtoa Kikombe !!!

  • Shule hii ya Buluba naifahamu vizuri kwani niliwahi kupangiwa kwenda kufanya mazoezi ya kufundisha hapo japo baadaye nilibadilisha na kwenda mgodini Mwadui kwenda kushangaa makaburu wanavyosomba almasi zetu huko na kuwaacha Wasukuma wakiwa hawana cho chote. 
  • Wapo vijana wengi wanaoacha masomo kwa sababu za kupita kama hizi halafu baadaye wanakuja kujuta. Mimi mwenyewe ni mfano mzuri kwani niliwahi kuacha shule kwa mwaka mmoja na nusu. Japo nilikuwa na sababu nzuri, mpaka leo hii huwa namshukuru kakangu mpendwa ambaye tu ndiyo alikuwa amerudi kutoka vitani Uganda kwa kunipiga mkwara mkali, mkwara ulionifanya nirudi shuleni japo kwa shingo upande. 
  • Japo nilikuwa sikusoma darasa la nne na nusu ya darasa la tano, ajabu ni kwamba niliporudi shuleni darasa la sita niliweza kuyamudu masomo bila matatizo sana na mtihani wa darasa la saba ulipofika nilifaulu. Na wakati ule hakukuwa na shule za kata! 
  • Sijui kama kuna ye yote anayehusika atakayesoma hapa lakini kijana huyu inabidi arudishwe shuleni kwa nguvu akamalizie masomo yake - atake asitake, akiwa na kikombe au bila kikombe !!! 
~~~~~~~~~~~~
Mwanafunzi aacha shule kutoa dozi ya ‘kikombe’

Imeandikwa na Marc Nkwame, Meatu; Tarehe: 14 Mei 2011

WIMBI la tiba ya kienyeji maarufu kama ‘Kikombe’ linaendelea kugubika nchi na safari hii mwanafunzi wa kidato cha tano wa sekondari ya Buluba, wilayani hapa, amelazimika kuacha shule na kujikita katika kutibu kwa ‘Kikombe.’ 


Akiwa na umri wa miaka 24, Sanagu Onesmo, ambaye ni miongoni mwa vijana wenye umri mdogo kati ya matabibu wa vikombe walioanza kuibuka Tanzania mwaka huu, anatoa huduma yake hiyo katika kijiji cha Mwambegwa kata ya Mwanuhuzi. 

Vijana wengine waliowahi kuibuka na vikombe ni pamoja na binti mwenye umri wa miaka 19 aliyekatisha masomo kidato cha tatu Singida na mwingine wa Mbeya. 

Onesmo ni mtoto wa Onesmo Mwigulu, Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Mwambegwa ambaye anadai kushangazwa na mwanawe kuanza kutoa dawa hiyo ya ‘miujiza’ kwani katika ukoo wao hakuna historia ya waganga wa kienyeji. 

“Onesmo alilazimika kuacha masomo akiwa kidato cha tano Buluba, baada ya walimu wake kugundua kuwa alikuwa akitumia muda mwingi darasani kulala, tena usingizi mzito,” alisema Mwigulu. 

“Ilibidi niache shule maana kila nilipokuwa darasani, nilijikuwa nimepitiwa na usingizi na ni katika hatua hiyo ndipo ghafla nilioteshwa dawa za mitishamba,” alisema Onesmo akiongeza kuwa katika ndoto hizo, aliletewa picha za miti na mimea ambayo hakuifahamu mara moja isipokuwa mmoja uliofanana na miti iliyokuwa katika eneo la nyumba ya marehemu babu yake. 

“Huu mti unaitwa ‘nditima’ kwa Kisukuma na ni kweli babu alikuwa ameipanda kwa wingi kwenye nyumba yetu ya zamani na nilishangaa, maana yeye hakuwahi hata siku moja kuitumia kwa dawa,” alisema Mwigulu. 

Hivi sasa Onesmo hupata wateja kati ya 100 na 200 kwa siku na anadai dawa yake, kama ile ya ‘Babu wa Loliondo’ –Ambilikile Mwasapile - pia inatibu Ukimwi na magonjwa mengine sugu, lakini kijana huyo ‘alitoa mpya’ alipodai kuwa tiba yake pia ina uwezo wa kurefusha maisha. 

Dawa hiyo mpya inatolewa kwa Sh 2,000 na mgonjwa ni lazima anywe vikombe viwili ikiwa ni kwa Sh 1000 kwa kikombe. 

Onesmo anasema kila kikombe kina dawa iliyotokana na miti tofauti. 

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Abihudi Saideya, alikiri kuwa uongozi wa wilaya umeshatoa kibali kwa Onesmo, aendelee kutoa tiba yake baada ya kuridhishwa kuwa mazingira ya eneo lake ni safi na dawa haina madhara ila kuhusu suala la uwezo wake wa kutibu, bado linafanyiwa kazi. 

“Nimemtuma Ofisa wa Afya wa Wilaya kuichunguza kwa makini dawa hiyo ya Meatu,” alisema Saideya. 

Tayari mwanamke (jina limehifadhiwa) ambaye ni mfanya biashara wa hapa, na anayedaiwa kuwa na Ukimwi, ametangaza kujisikia vizuri baada ya kupata ‘kikombe’ cha Onesmo. 

Wimbi la vikombe limeshika kasi karibu katika kila pembe ya nchini, tangu kuibuka kwa Mchungaji Mwasapila wa kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro ambaye pamoja na wengi kujitokeza `kuiiga’ tiba yake, bado umaarufu wake uko juu na ameendelea kupokea umati mkubwa wa wagonjwa, wakiwamo viongozi, watu mashuhuri wa kada za siasa na utumishi wa umma wa ndani na nje ya nchi.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU