NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, May 10, 2011

Tujadili Viboko Mashuleni: Vifutwe au Visifutwe ???

Picha hii iko HAPA
 • Kama ulisomea Tanzania hasa katika shule za serikali bila shaka utakuwa bado unawakumbuka wale walimu waliokuwa wakisifika kwa kutembeza viboko. Ukichelewa shuleni, unaambulia viboko. Ukiwa hujafua nguo, kukata kucha, kuchana nywele, kusugua meno au kukoga unaambulia viboko. Ukizungumza darasani, viboko. Ukiulizwa swali na mwalimu halafu ukaboronga jibu ni viboko. Ukitoroka shuleni viboko tu. Viboko vilikuwa kila mahali na kama ulikuwa na siku yenye balaa basi mtu ungejikuta jioni inapoingia tayari unakuwa umeshaambulia viboko zaidi ya kumi. Na ukifika nyumbani napo unaweza pia ukaambulia viboko. Viboko !
 • Kwa sasa ukikaa na kufikiri vizuri, unaionaje adhabu ya viboko? Ilikusaidia kuwa na adabu njema, kuzingatia masomo na hatimaye kuwa mwanafunzi mzuri na mwanajamii mwenye manufaa; au adhabu hiyo ilikufanya uwe sugu na mtu asiyejali? Ni sawa kuwapiga watoto viboko? Unaunga harakati za kuifuta adhabu hii mashuleni?
 • Tafiti mbalimbali kutoka nchi za Kimagharibi zinaonyesha kwamba viboko na adhabu zingine zenye kuleta maumivu hazisaidii cho chote na zinaweza kuwafanya watoto kuwa na tabia mbaya na wasiojali. Ndiyo maana katika nchi nyingi za Kimagharibi, adhabu ya viboko imeshapigwa marufuku. Tafiti kama hizi ni kweli zinaakisi hali halisi katika mazingira yetu na malezi ya Kiafrika? Tufute viboko mashuleni?

*********

Adhabu ya viboko shuleni haijafutwa

Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga; 6 Mei 2011

ADHABU ya viboko kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini inayotolewa na walimu na kuibua malalamiko miongoni mwa wazazi na walezi, haijafutwa kisheria, imeelezwa. 

Hayo yamebainishwa na Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Rukwa, Albert Mloka kwenye mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga uliofanyika katika Shule ya Sekondari ya Matai wilayani humo. 

Mloka alisema adhabu ya viboko shuleni imekuwa ikilaumiwa na wananchi wengi nchini kwa kuwa walimu katika kuadhibu, hawachapi viboko, bali wanapiga wanafunzi kwa mateke, viboko visivyo na idadi, ngumi na vichwa

“Kinachofanyika shuleni walimu wanakiuka taratibu na sheria zilizoainishwa na Serikali ambapo mbali ya kuwapiga viboko visivyo na idadi kwa wanafunzi wakosefu, lakini pia walimu wa kiume wanawapiga wanafunzi wa kike ambapo sheria haisemi hivyo,” alifafanua Ofisa Elimu wa Mkoa. 

Alisema mwanafunzi ataadhibiwa kuchapwa viboko pale itakapobainika kuwa kosa alilofanya ni ovu na adhabu yake ni viboko au kufukuzwa shule na si vinginevyo. 

Kuhusu viboko kwa wasichana, alisema wataadhibiwa kwa kuchapwa viboko na walimu wa kike pekee kama shule haina mwalimu wa kike, basi adhabu hiyo itatolewa na Mkuu wa Shule na Mwalimu Mkuu

Alisema ni viboko vinne tu vilivyoruhusiwa kisheria kwa wavulana kuchapwa kwenye makalio na wasichana mikononi na mwalimu akitoa adhabu hiyo, anaagizwa aandike kitabuni kuonesha tarehe na idadi ya viboko na aliyeadhibiwa lazima asaini kitabuni humo. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay aliwavunja mbavu wajumbe alipochangia  kwa kusema kuwa “mbona sisi (wanafunzi wa kiume) tunachapwa na walimu wa kike…this is not fair, mie ni Mmasai kule umasaini mtoto wa kiume kucharazwa viboko na mwalimu wa kike looh mwalimu huyo atapewa misukosuko kwa kweli atapata shida,” alisema. 

Wajumbe wengi wakichangia walidai kuwa walimu wanaotoa adhabu ya viboko visivyo na idadi shuleni hata kwa kosa la mwanafunzi kushindwa kujibu swali darasani, wengi wao hawana uwezo wa kutosha kufundisha au hawajiandai vizuri kufundisha. 

Si kweli shule zimeharibika, bali walimu baadhi yao wameharibika....viboko sio suluhisho la kumaliza utoro shuleni, walimu wanaotembea na fimbo mikononi kutwa nzima basi ujue wewe si mwalimu,” alisema mjumbe mmoja. 

Wajumbe hao pia walishauri kuwa adhabu hiyo ya viboko kwa wanafunzi kamwe isitolewe na mwalimu mwenye hasira kwani atapiga badala ya kuchapa. 

Baadhi ya wanafunzi ya Shule ya Sekondari ya Matai walioalikwa hapo, walikiri kuwa adhabu za viboko shuleni zimekithiri na ni mateso kwao. 

“Maisha ya shule yamekuwa ni mateso kwetu kwani adhabu za viboko zimezidi baadhi yetu wamekata tamaa ya kusoma na wanahudhuria shule kwa lazima na si kwa hiyari yao wenyewe” alisema mwanafunzi wa kidato cha nne, Paulo Maembe. 


Chanzo: Habari Leo.

 • Kwingineko, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Rungwa katika Halmashauri ya Mji wa Mpanda wamegoma kuingia madarasani kwa muda usiojulikana wakipinga Mkuu wa Shule hiyo kuwacharaza viboko visivyo na idadi. Kwa habari kamili soma HAPA.

2 comments:

 1. mie natoa mawazo yangu binafsi ambayo si ishara ya ufuasi wa kundi fulani. naweka interest awali kabisa kuwa binafsi viboko vilinisaidia huko shuleni. pengine nisingalikuwa hivi nilivyo. kwa nijijuavyo nilikuwa mwoga wa vitisho na adhabu. hivyo ili kuepuka kutishwa ama kupewa adhabu, nilitakiwa kufanya jambo fulani vema vinginevyo nilitandikwa sana. kutandikwa ndiko kulinishawishi ama kuacha ubaya na kukumbatia uzuri ili nisitandikwe tena.

  kinachotusumbua sasa ni ujio wa internet, tv, human rights na ujinga kama huo. tumukumbatia bila vipimo na ulinganifu wa hali yetu na hali ya huko vitokako.haishangazi hata sasa kuna nchi za kiafrika kama sisi tunavyojiuliza viboko viwepo ama visiwepo, kuna nchi zinagombana ushoga uruhusiwe ama usiruhusiwe.

  narudi katika ubora wa viboko/bakora (ita upendavyo). nilichelewa kidogo kujua hisabati za sehemu. nilipocharazwa barabara nilizijua na kuzifahamu vizuri. sina uhakika badala ya viboko ningepewa peremende ama mafenesi kwa kutokujua hisabati zile, ningezikua kama nilivyzijua kwa kucharazwa.

  nimetumia neno kucharaza. pengine hapa ndipo kwenye makosa. mtoa adhabu ya viboka anatakiwa kutoa kwa nia ya kufunza na si kukomoa, kuumiza ama kujionyesha ubabe wake. hapa ndipo tulipokwenda kombo nadhani. kunatofauti kati ya kutoa adhabu kwa kuchapa na kucharaza. baadhi ya walimu/wazazi wanacharaza watoto badala ya kuchapa. kuchapa kuna funzo ndani yake ilhali kucharaza kuna ukengeushaji badala ya unyooshaji.

  vidumu viboko

  ReplyDelete
 2. Mwaipopo: Mara yangu ya kwanza kupanda basi jijini Los Angeles nilishtuka na kusikitika sana. Wanafunzi wa High School walikuwa wanamtukana dereva na watu wengine wazima matusi ya nguoni. Wengi wao walikuwa weusi, wamevaa mitepesho, wametoboa masikio na ndimi zao na kujichora miili.

  Pembeni kulikuwa na Bi. Kizee mmoja akiwa amesimama. Watoto hawa hawakuona haja ya kumwachia kiti. Mimi niliona aibu nikasimama na kumpisha yule Bi. Kizee. Nami kumbe nikawa nimefanya kosa. Niliambiwa kwamba "nigger" nilikuwa najipendekeza tu na nikaishia kuporomoshewa matusi.

  Nilikuwa bado mgeni na japo hali hii nilikuja kuizoea baadaye lakini mpaka leo bado naamini kwamba sisi tunawalea watoto wetu tofauti na pengine viboko vinasaidia - potelea mbali wapigania haki za binadamu/watoto na mikatale yao.

  Mimi mwenyewe niliamua kuacha shule bila sababu ya msingi nilipokuwa darasa la nne. Lakini kwa bahati nzuri mwalimu Mkuu (sijui yuko wapi siku hizi - nshajaribu kumtafuta sijafanikiwa) siku moja akaja mpaka nyumbani kunitafuta. Baba mdogo alishangaa sana kwani hakujua kuwa nilikuwa siendi shuleni. Mwalimu yule alimwambia Ba Mdogo kwamba nilikuwa mwanafunzi bora kabisa shuleni na ilikuwa lazima nirudi shuleni. Nakumbuka mpaka leo kibano nilichopata jioni ile baada ya yule mwalimu kuondoka. Kesho yake pia Ba. Mdogo akanibeba mzobemzobe mpaka shuleni. Katika foleni ya saa mbili kabla ya kuingia madarasani shuleni nzima ikiwa imekusanyika Ba. Mdogo akaambiwa anicharaze viboko sita - tena viboko vya kwelikweli. Na tangu siku hiyo sikuwahi kukosa shule hata siku moja. Sijui leo hii ningekuwa wapi!

  Tatizo letu kubwa kama ulivyogusia ni kwamba tunaiga tu kila kitu hata bila kutilia ndani mazingira yetu halisi yakoje. Haya tufuteni viboko na muda si mrefu watoto wetu nao wataanza kwenda shuleni na bunduki na kuwatandika risasi wanafunzi wenzao.

  Inabidi tufikirie vizuri kabla hatujafuta viboko mashuleni !!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU