NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, May 6, 2011

Wanafunzi wadai Kiingereza kinawafelisha

  • Tafiti zimeshafanywa, makala mengi yameshaandikwa, vitabu vingi vimeshachapishwa na makongamano mengi yameshafanyika kuhusu matatizo ya sera yetu ya lugha mashuleni na utatuzi wake. Ajabu ni kwamba miaka nenda miaka rudi wahusika hawaonekani kulichukulia tatizo hili kwa uzito unaostahili na kulitafutia ufumbuzi. Tutatangatanga na sera hii kengeufu ya lugha mpaka lini? Kama elimu bora ndiyo mkakati mama katika  maendeleo na ukombozi wa jamii yo yote ile, tutawezaje kuendelea huku tukiwa na sera ya lugha ambayo kimsingi inawageuza vijana wetu kuwa kasuku wa kukariri mawazo na maarifa ambayo hawayaelewi kwa undani? Jambo hili linashangaza na hata kusikitisha sana !!! 
~~~~~~~~~~
Wanafunzi wadai Kiingereza kinawafelisha

Imeandikwa na Abby Nkungu, Singida

BAADHI ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chifu Senge, wamesema sababu kuu za wanafunzi wengi wa kidato cha nne kufeli Hisabati ni uelewa mdogo wa lugha ya Kiingereza inayotumika kufundishia mashuleni. 

Wakizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni kuhusu sababu za wanafunzi wengi wa sekondari kufeli hisabati, walisema msingi mbovu wa somo hilo katika shule za msingi umechangia.


Fadhila Solomon anayesoma kidato cha tatu mchepuo wa sayansi katika shule hiyo, alisema msingi hafifu wa lugha ya Kiingereza tangu shule ya msingi, umesababisha wanafunzi kushindwa kumudu somo la Hisabati. 

Mwanafunzi huyo alisema katika shule za msingi, lugha kuu inayotumika kwa karibu masomo yote ni Kiswahili lakini wanapoingia sekondari hukutana na Kiingereza kwa masomo yote na wakati mwingine walimu hawajali kuwa wanafunzi wanatoka shule zisizo na mchepuo wa Kiingereza. 

Maelezo hayo yaliungwa mkono na Asia Abdalla wa kidato cha pili na Regina Silas wa kidato cha tatu huku wakiwaomba walimu wachanganye lugha wakati wakifundisha ili wanafunzi wapate ujumbe kwa usahihi na ufasaha. 

"Kule tulikotoka ni Kiswahili tu kwa kila somo isipokuwa somo la Kiingereza...sasa hapa kila somo ni Kiingereza.... mwalimu anatema Kiingereza kitupu kuanzia mwanzo hadi mwisho, sisi tunatoka kapa...walimu wawe wanachanganya lugha ili tuwaelewe vizuri," alisema Asia. 

Regina alisema, lugha ya Kiingereza ni tatizo kubwa kwao na husababisha hata baadhi ya wanafunzi kumchukia mwalimu wa somo husika. 

Mwanafunzi Francis Sebastian na Makafoo Iddi walisema kuwa pamoja na sababu hiyo kuu, ukali wa baadhi ya waalimu, uchache wa vitabu na uhaba mkubwa wa walimu wa Hisabati ni sababu nyingine zinazochangia wanafunzi kufeli somo hilo. 

Sababu nyingine ni wanafunzi kutopenda somo la Hisabati na wengine kutojiamini; hasa wasichana. 

Mwalimu Benjamin Mayengela anayefundisha Hisabati katika shule hiyo, alisema kuwa wingi wa vipindi kwa mwalimu mmoja kutokana na uchache wa walimu, ukosefu wa vitabu na wanafunzi kutojituma ni sababu zinazochangia ufaulu duni wa Hisabati. 

Naye Ofisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Yusufu Kipengere alisema ufaulu duni wa Hisabati unatokana na uhaba mkubwa wa walimu. 

"Kwa mfano mwaka huu, Mkoa ulipokea walimu 300 kati yao, walimu 15 tu ndio wa hisabati," alifafanua Kipengere. 

Shule ya Sekondari ya Chief Senge iliyopo mjini hapa ina kidato cha kwanza hadi cha nne na ina mikondo 16 lakini ina walimu wa hisabati wawili tu.

Chanzo: Habari Leo

1 comment:

  1. Hivi Serikalini au Wizarani hakuna anayeliona hili jamani? Hivi ni nini maana ya elimu? Kujua Kiingereza au kuongeza maarifa? Tunaachwa kimaendeleo kwa sababu ya kukurupukia mipango ya wengine bila maandalizi. Kila mwaka kuna mabadiliko ya mitaala! Pamoja na hayo, hebu tufike mahali tujiulize, hivi tutegemee nini kwa mtoto ambaye kwa miaka saba amefundishwa masomo ya msingi kwa Kiswahili, halafu ghafla, anaingia kidato cha kwanza na kukumbana na Kiingereza katika kila somo? Hata kama ni kujisomea mtoto huyu ataweza? Tunawatendea haki vijana hawa? Kama tumekusudia kufundisha kwa Kiingereza, basi kwa nini kisianze tangu msingi? Na kama elimu ni kuongezea upeo wa maarifa, basi kwa nini tusifundishe kwa lugha yetu ambayo Mungu alitupa? Tunaachwa kimaendeleo na nchi kama Malaysia, Vietnam,na kwingineko kwa sababu hiyohiyo. Tumefika mahali leo, mtu ana digrii ya kwanza hata ya pili lakini kichwani hakuna kitu. Tanzania tunatakiwa kuamka, tufike mahali pa kuwa na wivu na wenzetu. Hivi hatuoni aibu kwa nchi kama Rwanda kututimulia vumbi tuliokuwa mbele sasa inatuacha?

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU