NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, May 7, 2011

Wataalamu: Kikombe cha 'Babu' ni Kinga Bomba


Japo mti huu wa Mugariga unaonekana kuwa na faida kibao za kiafya kama wataalamu hawa anavyothibitisha, muujiza bado ni ule ukweli kwamba kwa babu dozi ni kikombe kimoja tu, kwisha. Sijui kama kuna dawa nyingine ambapo mtu unakunywa mara moja tu halafu unapona magonjwa kibao namna hii. Miujiza!

**************

Wataalamu: Kikombe cha 'Babu' ni kinga bomba


Imeandikwa na Gloria Tesha; Tarehe: 6th Mei 2011

RIPOTI ya awali ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kuhusu tiba ya Mchungaji Ambilikile Mwaisapile, imeonesha tiba hiyo ina uwezo wa kukabiliana na magonjwa sugu ikiwemo Ukimwi, pumu, kisukari, saratani na shinikizo la damu.

Ripoti hiyo iliyolifikia gazeti hili, ambayo pia iliandaliwa na mtaalamu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), ni ile iliyotolewa serikalini baada ya wataalamu hao,

Dk.Hamis Malebo na Dk. Zakaria Mbwambo kufanya utafiti kuhusu usalama wa tiba hiyo maarufu kwa jina la Kikombe cha Babu. Baada ya Serikali kupata ripoti hiyo, ilitoa taarifa kuwa dawa hiyo ni salama, lakini ripoti hiyo imeonesha kuwa dawa hiyo ina mengi kuliko ilivyotangazwa na Serikali

Kuhusu Ukimwi, ripoti hiyo imeeleza kuwa utafiti wa mizizi na majani ya mti anaotumia Mchungaji Mwaisapile, kitaalamu mugariga, yana nguvu ya kupandisha kinga ya mwili.

Utafiti huo umenukuu utafiti uliofanywa Kenya na Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kenya (KEMRI) mwaka 2006, ulioonesha kuwa mizizi ya mti huo ina uwezo wa kukabiliana na virusi hivyo.

“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa mti una uwezo wa kupambana na moja ya virusi hatari vinavyoshambulia kinga ya mwili kwa mwanadamu, hivyo ni sahihi kwa Mchungaji Mwaisapile kudai kuwa tiba hiyo ya kijadi ina uwezo wa kupambana na HIV/AIDS,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Utafiti huo pia ulinukuu taarifa kadhaa za vitabu mbalimbali kikiwemo kitabu cha Activity of Liver, kilichoandikwa na Chatterjee na Roy mwaka 1965, kilichoonesha kuwa mti huo ni tiba kwa magonjwa sugu kama saratani na ini na una kinga kwa walemavu wa ngozi dhidi ya saratani ya ngozi. 

Kuhusu ugonjwa wa kisukari, wataalamu hao pia walinukuu utafiti uliofanywa mwaka 1996 kwa kumnywesha maji ya majani ya mti huo panya mwenye kisukari na matokeo kuonesha panya huyo akipunguza kiwango cha sukari katika damu yake katika saa tatu za mwanzo tangu anyweshwe. 

Katika utafiti huo wa 1996, panya asiyekuwa na kisukari alipopewa dawa hiyo, hakupata mabadiliko yoyote jambo linalodhaniwa kuwa dawa hiyo ina uwezo wa kutoa insulini kutoka katika kongosho ya mnyama wa kawaida. 

“Hivyo kuna usahihi kwa Mchungaji kueleza kuwa dawa anayoitoa ina uwezo wa kukabiliana  na kisukari,” ilieleza ripoti hiyo. Madaktari hao katika ripoti hiyo, wameonesha kuwa mti huo una uwezo wa kukabiliana na shinikizo la damu la kupanda kwa kuwa inashusha shinikizo na kufikia kiwango cha kawaida na hilo limedhihirishwa na utafiti wa kitabu cha Vohra na De cha mwaka 1963. 

NIMR imelithibitishia gazeti hili kuwa ripoti hiyo ni ya kweli, ndiyo iliyopelekwa serikalini kabla ya Babu kuruhusiwa kuendelea kutoa huduma yake, lakini ni taarifa ya awali, hawajaitoa rasmi. 

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela alilieleza gazeti hili jana kwamba katika  ripoti hiyo, vitu vingi vya kitaalamu vinakosekana na kuwashangaa watu walioitoa wakati haijakamilika, akiwalaumu kuwa wameitoa kwa makosa kwa kutafuta umaarufu. 

“Kuifahamu naifahamu, siwezi kusema ni ya kughushi ila ni ‘draft’ (rasimu) haijakamilika, nashangaa kuona mnayo, hii ni taarifa ya awali tu inayosaidia kutengeneza rasimu ya kufanyia kazi. 

“Kuna taarifa nyingine za kuambatanisha, haijakamilika kutolewa,” alisema Dk. Mwele alipoulizwa na mwandishi kuhusu ukweli wa ripoti hiyo. 

Hata hivyo, alipoulizwa lini utafiti kamili utakamilika, Mkurugenzi huyo alisita kutoa muda  kamili, lakini akasema itachukua muda mrefu. 

Hata hivyo, taarifa za kuaminika kutoka kwa wataalamu wa afya zilieleza kuwa uthibitisho wa kujua kama tiba fulani inatibu magonjwa, hukamilika baada ya utafiti wa miaka miwili. 

Katika utafiti wao, madaktari hao wamebaini kuwa kiwango cha dawa kinachopimwa na Mchungaji huyo kwenye kikombe cha ujazo wa mililita 200, kuchemshwa kwenye maji ya lita 60 yenye mizizi ya mti huo, ni salama kwa mtumiaji na hakuna sumu yoyote kwa kiwango hicho. 

Baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kwa nini taarifa ya jopo haielezi kiasi cha tiba ya kikombe kama kinafaa kwa tiba za magonjwa hayo sugu ama la, bila majibu, lakini ripoti hiyo imeonesha kuwa kiasi hicho ni tiba sahihi ingawa NIMR imesisitiza ni taarifa ya awali. 

Maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wameendelea kumiminika kwa Babu kupata tiba hiyo inayomtaka mgonjwa asirudie kikombe. 

Mchungaji Mwaisapile anadai kuoteshwa na Mungu miaka zaidi ya 10 iliyopita kuhusu tiba hiyo ya miujiza. 

Mbali na Tanzania, mti huo anaotumiwa na Babu unapatikana pia Australia, Botswana, Cambodia, Cameroon, Eritrea, Ethiopia, Ghana, Guinea, Japan, Kenya, Myanmar, Namibia, Nigeria, Papua, Saudi Arabia, Senegal, Afrika Kusini, Sudan, Thailand, Uganda, Vietnam na Yemen. 

Katika kabila la Wamasai, mti huo unajulikana kama Engamryaki, Olmuriaki au Engamryaga. 

Pia umekuwa ukitumika kama chakula na makabila ya Wagogo, Wakurya na Wabarbaigi. 

Matunda ya mti huo yameelezwa katika ripoti hiyo kuwa ni matamu na nchini Ghana huongezwa kwenye chakula cha wagonjwa kuwaongezea hamu ya kula na Sudan na Kenya hutumika kutengenezea jemu. 

Pia mti huo umekuwa ukitumika kutibu maumivu ya kichwa, kifua, magonjwa ya ngono ya  kisonono na kaswende, gauti, homa kali, ugonjwa wa anemia selimundu (sickle cell anaemia ) na ngiri.


Chanzo: Habari Leo

3 comments:

  1. Ripoti yenyewe haina kichwa wala miguu.Wasomi wa kibongo wamejaa magamba na uvivu wa kubukua. Wanatia kinyaa. Hakuna cha kikombe cha babu wala nini bali utapeli mtupu. Watakaofanya kosa wakamwamini tapeli huyu babu watapukutika kama mbu wapuliziwapo dawa ya kuua wadudu aina ya dumu. Haya shauri yenu na kalagabaho.

    ReplyDelete
  2. wewe uliesoma ambaye hutoi kinyaa basi fanya utafiti wenzio utafiti ndio huo na wewe fanya utafiti nyamwilu weeeeeeeeeeeeeeeeeeee

    ReplyDelete
  3. Kazi kwa watafiti wa afya ya jimii kuhakiki utendaji kazi wa dawa ya babu kwa kufanya CLINICAL TRIALS.

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU