NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, June 24, 2011

FIKRA YA IJUMAA: NATAMANI KUWA MWAFGHANISTAN !!!

Picha hii iko HAPA

Pamoja na kuwa na silaha bora kutuzidi pamoja na sababu zingine za kimfumo, wapo watu wanaodai kwamba sababu hasa iliyotufanya Waafrika tukauzwa utumwani na hatimaye kutawaliwa (mpaka leo hii) ni kutokuwa na utashi kamili. Wapo wanaokwenda mbali na kudai kwamba pengine Waafrika sisi (na watu weusi kwa ujumla) tuna akili pungufu tukilinganishwa na wakazi wa nchi za Kimagharibi. 

Ati, ni kwa nini tulikubali kuuzwa utumwani tena na wazungu wachache tu wenye bunduki na mizinga? Ni kwa nini tulikubali kutawaliwa na wazungu wakati wa ukoloni? Ni kwa nini tunakubali kutawaliwa hata sasa kupitia ukoloni mamboleo? Ni kwa nini tunakubali kuongozwa na wanasiasa mafisadi wasiotujali? Kwa nini Afrika kuna majanga ya kila aina: vita, magonjwa, umasikini wa kupindukia (japo Mungu katujalia kila kitu). Kwa nini? Narejerea hapa hoja zilizozushwa na Aika - binti machachari wa Kichaga aliyesimama kidete katika mjadala mkali kabisa kuliko yote  iliyowahi kurindima katika blogu hii (Tazama HAPA)

Ninaandika haya baada ya Wamarekani kutangaza kuwa wataanza kuondoka Afghanistan kuanzia mwaka huu. Baada ya kuivamia nchi hiyo kwa mbwembwe nyingi huku wakijidai kuwa na silaha kali na za kila aina, leo wanaondoka bila ushindi wo wote kama Warusi. Warusi pia walijaribu "kuitawala" nchi hiyo lakini baada ya miaka 10 waliondoka kwa aibu wakiwa wameshindwa. Waingereza pia walishajaribu kuitawala Afghanistan miaka ya nyuma lakini wakashindwa. Afghanistan haitawaliki! Swali tunalopaswa kujiuliza hapa ni kwamba: Kwa nini wa-Afghanistan hawatawaliki wala kushindika? Pamoja na sababu zingine za kijamii, kitamaduni na kihistoria, jibu rahisi linalotajwa sana ni utashi wao. Hakuna silaha hapa duniani inayoweza kuushinda utashi wa binadamu anayetaka kuwa huru, mtu ambaye yuko tayari kuutoa uhai wake ili kulinda akiaminicho, hadhi yake na watu wake. Majeshi, madege ya hatari yanayojiendesha yenyewe, mabomu ya kiatomiki na satelaiti zenye uwezo mkuu wa uoni kamwe haziwezi kufua dafu mbele ya utashi wa mtu aliyedhamiria kuwa huru. Kama unabisha kamuulize Hosni Mubarak atakwambia.

Natamani sana kama Waafrika tungejifunza kitu kutoka kwa wa-Afghanistan. Ati ingekuwaje kama tungekataa kutawaliwa na wanasiasa madikteta na mafisadi ambao lengo lao ni kushibisha matumbo yao yasiyoshiba? Ingekuwaje kama tungesimama kidete na kukataa kuchezewa na majibwa ya Kimagharibi? Ingekuwaje.....? Leo hii tungekuwa wapi?

Ni kwa sababu hii natamani kuwa m-Afghanistan masikini sana asiyejua kusoma wala kuandika lakini ambaye hataki kutawaliwa.  Na hii ndiyo fikra ya Ijumaa hii. Wikiendi njema! 

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU