NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, June 17, 2011

FIKRA YA IJUMAA: NIHIL EX NIHILO. TUTAFAKARI MAENDELEO YETU


Nihil Ex Nihilo ni Msemo kutoka katika falsafa ya Wagriki wa kale unaomaanisha kwamba ombwe daima huzalisha ombwe. Kwa hivyo hakuna cho chote kinachoweza kutokea au kutokana na ombwe. Mtazamo huu baadaye uliathiri mtazamo wa Wanasayansi waliofuatia waliodai kwamba mada, japo inaweza kubadilika umbo moja kwenda jingine, kamwe haiwezi kuundwa wala kuharibiwa. Hata nadharia mashuhuri ya ulinganifu kati ya uzito na nishati ya Albert Einstein (E=mc2) kwa kiasi fulani iliakisi mtazamo huu.

Mtazamo huu wa Nihil ex nihilo hata hivyo ulikuwa na matatizo kwa wanasayansi kwa sababu haukuwawezesha kuelezea chanzo cha dunia yetu, sayari zingine na malimwengu mengine. Hata nadharia yao inayodai kwamba mfumo wetu wa sayari ulitokana na Mtanuko Mkuu wa Ghafla (Big Bang) ulikuwa hauthibitishiki kwa sababu nadharia hii haielezi kuhusu chanzo hasa cha “Big Bang” ni nini. Ati, ni nini kilichotanuka kwa ghafla wakati wa Bing Bang na kilitoka wapi? Kulikuwa na nini kabla ya Big Bang? Kama hakukuwa na kitu (nihil), iweje Big Bang itokee na kuunda mfumo wetu wa sayari na mifumo mingine katika malimwengu mengi ambayo yametapakaa huku na huko?

Nihil ex nihilo iligusa hata dhana nzima ya uumbaji. Wanafalsafa na wanasayansi walianza kuhoji kwamba dunia iliumbwa kutokana na nini? Ni kweli kwamba iliumbwa kutoka katika ombwe (nihil)? Ni kwa sababu hii kwamba mtazamo huu haukupendelewa sana na mamlaka ya kanisa (Katoliki) enzi zile.

Katika miaka ya karibuni nadharia ya Big Bang imepata msukumo mpya baada ya Stephen Hawking – Mwanafizikia na mwandishi mashuhuri wa Uingereza kutoa ushahidi wa kinadharia kwamba inawezekana Big Bang ilitokana na mtanuko wa ghafla wa ‘Black Holes’. Alidai kwamba kinadharia hakuna kitu kinachozuia mada kuumbwa kutokana na ombwe, na pengine tunachodhani ni ombwe pengine ni mada na elementi nyingine ambazo hazionekani kwa macho na bado hatujawa na vifaa vya kisayansi kuweza kuzibaini. Ati, kuna ombwe?

Nimeikumbuka Nihil ex nihilo baada ya kutazama kipindi kimoja katika History Channel ambapo wanasayansi walikuwa wakijaribu kueleza chanzo cha maji hapa duniani; na hasa yale ya baharini. Hitimisho lao ni kwamba maji haya pengine yalitokana na vimondo vilivyokuwa vikidondoka kwa wingi duniani wakati dunia ilipokuwa ingali na umri mdogo (Tazama video hapa chini)

Tukiachana na kizungumkuti hiki cha wanasayansi, mtazamo huu wa Nihil ex nihilo umenikumbusha jitihada zetu za kujiletea maendeleo. Kama jamii ni kweli tuna nidhamu ya kufanya kazi kwa bidii au tunategemea kupata maendeleo kutoka katika ombwe (nihil)? Cha kushangaza zaidi ni kwamba hata sehemu kubwa ya kile kidogo tunachokizalisha nacho kinaishia katika matumbo ya mafisadi. Kwa mtindo huu tutapata maendeleo ya kweli lini? Bila kuchapa kazi kwa bidii na kuhakikisha kwamba kile kinachozalishwa kinatumika kuleta maendeleo ya wote, tutaendelea kupiga maktaimu ya kimaendeleo na mara moja moja tukienda hatua mbili mbele na kurudi nyuma hatua moja; na au hatua moja mbele na kurudi nyuma hatua mbili. Tukumbuke kwamba Nihil ex nihilo.

Na hii ndiyo Fikra ya Ijumaa hii. Tuonane tena Ijumaa ijayo panapo majaliwa. 

5 comments:

 1. Mkuu tupo pamoja na hii mada, nilikuwa na mengi ya kuandika, lakini `nimetingwa kidogo' TUPO PAMOJA DAIMA

  ReplyDelete
 2. Fikira Kibonge hii!Na inaendelea kunifikirisha!:-(

  ReplyDelete
 3. emu-three. Asante. Naona ile hadhithi yetu tamu bado inaendelea. Nimekosa matoleo kadhaa na itabidi nikazane ili kuwa nayo sambamba. U-mwandishi mzuri sana!

  Mtakatifu - nimekumbuka pia maswali kama haya yaliwahi kuulizwa na Okot B'Tek - yule mwandishi wa Wimbo wa Lawino. Ni dhana kengeufu kidogo kufikiria kwamba unaweza kuzalisha kitu kutoka katika ombwe ndiyo maana hata hii nadharia ya Big Bang kwa mtu wa kawaida kama mimi asiyefahamu masuala ya kinadharia ya wanasayansi ni vigumu kuelewa vizuri...

  Ila nilidhani kwamba kwa mwanafalsafa makini kama wewe pengine ungeweza kuliweka jambo hili katika mkabala wa kueleweka!

  ReplyDelete
 4. @Mkuu Matondo: Tatizo la kitu ``KUELEWEKA´´ hata kineno lahitaji kunyambulishwa! Kwa kuwa waelewao kitu hapa DUNIANI hata kitu kisicho husishwa na MUNGU ni vigumu kuwaelewesha kwa kuwa inabidi uchimbe misingi ya kuelewa kwao ikoje kwanza saa nyingine. Ntarudi lakini hapa baadaye kujazia hili somo.

  Kwa baahati mbaya bado ulichoandika kinanifikirisha na sijajulia bado kuliingia swala!:-(

  ReplyDelete
 5. Hii kitu umeiandika kirahisi ila ngumu kweli MKUU kimawazo!


  Ingawa bado inanifikirisha na ntarudi tena,...
  ...ningependa kusema:

  Ili utoke nungu LABDA lazima ugongwe na kitu au upigwe bonge la ngumi ,...
  .... na kitanuliwacho ,...

  ...labda kuna kitu kina tanua HICHO KITU ,...
  .... na kama katika hilo INGEKUWA NI RAHISI KUELEZEA ,...
  .....KAMA KIELELEZO INGEKUWA ni muingiliano wa kati ya mwanamume na mwanamke KISEHEMU ZA SIRI katika kitanuliwacho kitu ,...
  ... labda hata tusingekuwa tuna maswali mengi.:-(


  Na wakati tunatafakari maendeleo YETU!

  HIVI MAENDELEO ni nini kama si BINADAMU kimitazamo yake anafikia tafsiri ambayo maendeleo mengine ni kwa akina dada kuvaa chupi na sidilia hadharani NIKITU KITIACHO AIBU ila hivyo vidubwana vikiitwa bikini KIMAENDELEO ,...
  ....kisaikolojia HAOHAO wasio weza kutoka bila kanga chumbani wanatembea kwa madaha NJE YA NYUMBA kwa kuwa kimaendeleo BIKINI sio chupi na sidilia ila ni vazi la UFUKWENI?

  Naendelea kuwaza!:-(

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU