NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, June 28, 2011

HARAKATI ZA CCM KUJIVUA GAMBA ZITAMALIZIKA LINI ? NI ZOEZI LA KUDUMU ?

Ili kuepuka kuwa mmezwaji huko mbele ya safari, CCM ilibidi kijivue magamba

Juhudi za CCM kujivua gamba zilipokelewa kwa furaha na matumaini makubwa na wanachama wake pamoja na Watanzania wengine wakipendacho. Japo juhudi hizi zilipondwa na kubezwa na baadhi ya wapinzani pamoja na wachambuzi, kwa wengi zilionwa kama nafasi ya pekee kwa CCM kujaribu kurudisha imani yake kwa wananchi - imani ambayo ilikuwa imeanza kupotea kutokana na tuhuma za ufisadi na makundi ndanimwe; pamoja na kupoteza mwelekeo na malengo yake ya msingi. 

Ilitangazwa kwamba CCM ilikuwa imetoa siku 90 kwa watuhumiwa wote wa ufisadi kujiuzulu uanachama na kama wasingefanya hivyo basi wangewajibishwa. Kauli hii ilionyesha kwamba kweli chama hiki kilikuwa kimedhamiria kujisafisha. 

Jambo la kushangaza ni kwamba baada ya muda kidogo tu kupita wakuu wapya wa chama hiki walitangaza kwamba hawakuwa na majina ya mafisadi na kwamba ile kauli ya mwanzo ya siku tisini haikuwa ya kweli. Baada ya kigugumizi cha muda mrefu kuhusu mashambulizi ya CHADEMA, hatimaye CCM wameamka na kupitia kwa Katibu wao Mwenezi wanazunguka nchi nzima kujibu hoja za wapinzani wao na kuelezea mafanikio yao. 

Japo kuzunguka kwa CCM nchi nzima ni mkakati mzuri, sina uhakika kuhusu mafanikio yake. Ni kweli kuzunguka huku kunasaidia kurudisha heshima na imani ya CCM kwa wananchi? CCM imefanya tathmini na kujua wananchi wanataka nini? Isije ikawa kwamba juhudi hizi za kijasiri za Katibu Mwenezi zinaonwa na wananchi kama propaganda tu za CCM walizozizoea. 

Kwa maoni yangu naona kuwa CCM inapoteza nafasi ya muhimu sana ya kuonyesha dhamira yake ya kujisafisha mbele ya Watanzania kwa vitendo. Kama kweli ilikuwa imedhamiria kujivua gamba, mbona kazi hii ifanyike nusunusu? Ndiyo maana nimeshangaa kusoma leo katika Gazeti la Chama na Habari Leo CCM ikitoa ahadi nyingine kwamba wasaliti wote ndani ya CCM watawajibishwa na kwamba mafisadi ni lazima wavue gamba. Watawajibishwa na kuvuliwa gamba na nani? Lini?


Badala ya kuwa mkakati wa maana, dhana nzima ya kujivua gamba sasa inaonekana kama kichekesho tu cha kipropaganda. Pengine CCM bado hawajayasoma na kuyaelewa mabadaliko ya kisiasa, kifikra na kimtazamo yanayotokea barani Afrika na nchini mwetu. Kama wangejua, basi wangelichukulia zoezi hili la kujivua gamba kwa dhati na bila kusuasua. 

Na sijui ni kwa nini nafasi nzuri ya kujisafisha na kujirudishia imani yao kwa Watanzania inaachiwa tu ipotee namna hii. Siasa ni mchezo wa kula kuliwa na wakati mwingine inabidi kuchukua maamuzi mazito bila kujali uswahiba, utajiri na uzito wa mtu. Watanzania wanachotaka ni Maisha Bora kwa Kila Mtanzania na siyo propaganda na mikakati isiyo na meno! 

1 comment:

  1. yawezekana....na kama ikitokea ni baada ya muda mrefu pengine baada ya kizazi cha 'mapacha watatu' kuisha!

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU