NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, June 22, 2011

HEBU SIKIA "VITUKO" HIVI VYA WANYANTUZU !!!


(1) Asilimia 24.4 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wameacha kupata dawa za kupunguza makali ya VVU baada ya kunywa dawa ya Babu Loliondo. (Sehemu zingine hali ikoje?)

(2) Wanaume wanadai kwamba eti matumizi ya vyandarua yanasababisha wasiwe na uwezo wa kupata watoto.

(3) Tohara ya wanaume pia inashutumiwa kusababisha utasa.

**************
 • Ukiachilia mbali hili suala la tiba ya Babu, masuala (2) na (3)  ni mojawapo ya mambo yanayoonyesha changamoto za watunga sera ambao mara nyingi hukurupuka tu na kupitisha maamuzi hata bila ya kuwashirikisha walengwa
 • Fikiria kama mtu umemwaga vyandarua huko Unyantuzu Bariadi bila kwanza kufanya uchunguzi wa kina ili kujua kama hivyo vyandarua vinatumiwa kweli ama la. Basi unatoka hapo na kwenda kujikunja kuandika ripoti nzuri kwamba sera ya kutumia vyandarua ili kujikinga na malaria inaendelea vyema kumbe baadhi ya walengwa wako wanaviogopa ili wasije wakapata utasa. 
 • Badala ya kuwabambikiza sera na maazimio kwa kisingizio cha "ujinga", ukosefu wa elimu na imani potofu kuna umuhimu wa kukaa chini na kuifahamu jamii lengwa; na kuishirikisha katika kupitisha maamuzi. Vinginevyo sera nyingi zitakuwa zinaishia kuonyesha "mafanikio" vitabuni tu. 
**************

Waliokunywa dawa kwa ‘babu’ wasusa ARVs
Imeandikwa na Shangwe Thani, Bariadi; Tarehe: 21 Juni 2011

WATU 1,168 sawa na asilimia 24.4 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wilayani Bariadi, wameacha kwenda kwenye vituo vya kushauri juu ya matumizi ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) baada ya kunywa dawa ya Babu wa Loliondo. 


Kaimu Mratibu wa kudhibiti Ukimwi wa Wilaya ya Bariadi, Faustine Kaliche alisema idadi hiyo ni kati ya watu 5,861 wanaoishi na virusi wilayani humo. 


Alikuwa akizungumza katika mkutano wa Kamati ya Ushauri wa Maendeleo ya Wilaya (DCC) mjini Bariadi. 


Alisema wametoroka vituo vya huduma na tiba vinavyotoa ushauri na vidonge vya ARVs baada ya kupata tiba ya kikombe cha Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile katika kijiji cha Samunge, Kata ya Loliondo wilayani Ngorongoro. 


Kaliche alisema kundi hilo lililoacha huduma ni kubwa na ni hatari kwa afya zao na watu wengine watakaojamiiana nao bila ya kutumia kinga. 


Wakati huo huo akifunga mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Baraka Konisaga aliwataka viongozi wa vyama vya siasa, dini na watendaji wa vijiji na kata kuielimisha jamii iondokane na imani potofu kuwa tohara na matumizi ya vyandarua kwa wanaume vinazuia uzazi


Konisaga alisema, tafiti za kisayansi zimethibitisha kuwa mwanaume aliyefanyiwa tohara ana asilimia 60 ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ikilinganishwa na asilimia 40 kwa mwanaume asiyefanyiwa tohara. 


''Kuna uvumi unaoenezwa na watu wasiowatakia mema watu wa wilaya ya Bariadi kuwa wakitumia vyandarua kujikinga na mbu ili wasiambukizwe malaria hawatazaa tena na wale wanaume wanaofanyiwa tohara hawatazaa tena wakifanyiwa tohara kwa kuwa tohara huzuia wasizae,’’ alisema Konisaga. 


Akiwasilisha taarifa, Kaimu Mratibu wa kudhibiti Ukimwi wilayani Bariadi, Faustine Kaliche alisema kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, asilimia tisa ya watu waliopima afya wilayani humo wamebainika kuambukizwa virusi vya Ukimwi.


Chanzo: Habari Leo

3 comments:

 1. Pamoja na kuthibitishwa kisayansi kwamba kikombe cha Babu kinamanufaa yake, hiyo mandhari na utafiti ulietaja mkuu ndio ilikuwa uoga wangu juu ya Loliondo. Wanasayansi waitaja jina la "PLACEBO EFFECT" au tuseme kwa Kiswahili "POTELEA MBALI NIMEKWISHAPONA!"


  Ukweli ni kwamba mtu hawezi kupona kwa kikombe kimoja; na kama ni vijidudu vya ukimwi, wale ni wajanja wakubwa na watasubiri mpaka hapo nguvu za kikombe zimekwisha kojolewa na mgonjwa na wataanza shughuli zawo kama kawaida mgonjwa utasononeneka weee!


  Tatufuteni madaktari, Jamaanni licha ya mchango wa Babu wa Loliondo!

  Ni ushauri wangu hapa Bondeni!

  ReplyDelete
 2. Ni kweli Bwana Manyanya. Hii Imenishtua kwa sababu huko Bariadi ndiyo nyumbani.

  Kama hawa wote walioacha kunywa ARVs zao hawajapona kabisa basi itakuwa hatari zaidi. Sijui kama kweli wameenda hospitalini wakapimwa na kuthibitishwa kwamba vijidudu havipo tena na kama kweli wamepona kwani kama ulivyogusia hapo juu, hiki kirusi cha UKIMWI ni kirusi kijanja sana kinachoweza kujibadilishabadilisha mara kwa mara....

  ReplyDelete
 3. Mimi nadhani kuna tatizo kubwa sana vijijini, hasa usukumani ambapo mimi nina uzoefu. Kule hawana habari kuwa UKIMWI upo na unaua, pia hawaamini kuwa kondomu zinaweza kutumika kwa mwanamke malaya ambaye umempatia pesa ili ufanye naye mapenzi {mara nyingi hawa huja vijijini wakati wa mavuno na madisko vumbi na wananunuliwa kama peremende}, nimeshawahi kuongea na mtoto wa shangazi akashangaa sana nilipomshauri atumie kondomu kwa sababu anatoa pia pesa ili kumshawishi mwanamke yule afanye naye mapenzi.
  Kitu kingine cha ajabu ni kuwa kule dada zetu hawana noma hata kama mmewe atakwenda kulala kwa hawala, mke anamwandalia hadi kitenge cha kwenda nacho kwa hawala.... jaribu kufanya hivi mjini uone moto wake!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU