NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, June 29, 2011

SIMU ZA MKONONI NA KANSA YA UBONGO: BALAA JINGINE KWA AFRIKA?

Picha hii iko HAPA

Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala mkali kuhusu nguvu za mionzi ya mnunurisho inayotolewa na simu za mkononi kama zinaweza kusababisha kansa ya ubongo ama la. Hatimaye Shirika la Afya Duniani limetoa tamko kuhusu utafiti unaoonyesha kwamba simu za mkononi zinaweza kuwa zinasababisha kansa ya ubongo. Hatari hii inasemekana kuwa ni kubwa zaidi kwa watoto wadogo na matineja kwani mafuvu yao bado hayajakomaa sawasawa.

Naomba hii isiwe kweli kwani kama tunavyojua, Afrika ndiyo jalala la bidhaa feki, mbovu na zilizoisha muda wake. Bila shaka nitakuwa sahihi nikisema kwamba simu zinazotoa mionzi hatarishi kwa binadamu na zitakazokuwa zimepigwa marufuku sehemu zingine za dunia ndizo zitarundikana Afrika.

Kama utafiti huu ni wa kweli basi miongo kadhaa tu ijayo Afrika itakumbwa na mripuko wa kansa ya ubongo – mojawapo ya kansa hatari kabisa na inayohitaji tiba ghali sana!

Tunachoweza kufanya kwa sasa ni kufuata mapendekezo yaliyotolewa yakiwemo kununua simu zisizotoa mionzi mikali zaidi, kuweka simu mbali na sikio wakati wa maongezi na kwa wenye uwezo kununua vifaa vinavyosafirisha mawimbi ya sauti kama “Bluetooth”. Vifaa hivi huwekwa sikioni na vinaweza kudaka mawimbi ya sauti ya simu iliyowekwa mfukoni au sehemu nyingine na kuyasafirisha sikioni kwa msikilizaji bila madhara yo yote.

Aina mojawapo ya kifaa cha bluetooth

Hizi simu feki kutoka Uchina zitatufikisha pabaya. Ndiyo maana naomba hili la simu za mkononi kusababisha kansa ya ubongo lisiwe la kweli. Mungu Ibariki Afrika!

2 comments:

 1. Ha ha ha ha ha ha haaaaaa! Si kichekesho mkuu ila madhali tushaonekana jalala tutaona mengi...

  Anyway, tanzania twajivunia kuwa na mganga mkuu Rev. Mwaisapile atibuye kila kitu japo kwa sasa ni wa Kenya...I love africa!

  ReplyDelete
 2. Unajua Ng'wanambiti - tatizo mojawapo ni ile tabia ya kukimbilia kuiga vitu hata bila kuvielewa vizuri. Sasa kama una pesa zako ni safi sana kwenda kununua mahitaji yako supamaketi. Mbogamboga na matunda yaliyotoka Morogoro na Tanga hatuyataki tena. Ambacho hatukifahamu ni kwamba hivi vyakula vya kwenye masupamaketi hata hatujui vina makemikali gani masikini. Matokeo yake tunaona magonjwa ya Kimagharibi kama kansa sasa yanatunyemelea.

  Maisha ya deko, ulabu na mapochopocho haya sasa yanatuletea shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kisukari, kiharusi na kansa za kila aina. Sijui kama haya ndo maendeleo.

  Ndiyo maana nilishtuka niliposikia kwamba hili la simu na kansa ya ubongo....

  Sijui ni lini tutakuwa makini na kukataa kuwa jalala la bidhaa zilizoshindikana kwingine. Pengine ni mpaka pale tutakapoanza kujikomboa kutoka katika umasikini huu wa kutisha ambao, mbali na mambo mengine, unasababishwa na mifumo yetu mibovu ya uongozi.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU