NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Sunday, June 5, 2011

UKIMWI LEO UNATIMIZA MIAKA 30 TANGU UTAMBULIWE RASMI. TUTAFAKARI !!!

 • Tarehe 5/6/1981 Dkt. Michael Gottlieb wa Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA) alichapisha makala ya kihistoria ambayo yalielezea kuhusu ugonjwa wa kushangaza ambao mpaka wakati huu ulikuwa umewakumba wanaume watano mashoga.
 • Katika makala yake ya kihistoria, Dr. Gottlieb alibainisha kwamba wagonjwa wote watano walikuwa wanasumbuliwa na kifua kikuu, pamoja na magonjwa mengine nyemelezi. Ugonjwa huu baadaye ulikuja kugundulika kuwa ndiyo UKIMWI!
  • Jambo la kusikitisha ni kwamba: Kwa vile ugonjwa huu mpya ulikuwa unawaathiri zaidi mashoga  -watu ambao walikuwa hawatakiwi katika jamii hasa kwa maoni ya wahafidhina, serikali ya  Marekani haikuona haja ya kuufanyia uchunguzi mapema na ilijikongoja sana katika juhudi zake za kuweza kuutambua ugonjwa huu kama janga la kijamii. Mpaka wacheza sinema wa Holywood ambao hawakuwa mashoga walipoanza kuteketea ndipo hatimaye raisi wa Marekani wa wakati ule (Ronald Reagan) aliweza kubadilisha mtazamo na kuutambua ugonjwa huu kuwa janga la kijamii. Alikuwa amechelewa sana na ugonjwa huu tayari ulikuwa umeshajitandaza.
  • Baadaye iligundulika kwamba zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wa Hemophilia – wagonjwa ambao wanahitaji kuongezewa damu ili kupata protini muhimu inayosaidia damu kuganda walikuwa wameambukizwa UKIMWI. Cha kushangaza ni kwamba, hata baada ya ukweli huu kueleweka, makampuni ya madawa ya Marekani yaliendelea kuuza protini hii gandishi iliyokuwa imeambukizwa katika nchi nyingine duniani. Kumbe kwa kufanya hivyo UKIMWI ukapata nafasi ya kujitandaza zaidi ulimwenguni kwa haraka zaidi. Mpaka leo kuna watu ambao wanaamini kwamba jambo hili lilifanyika kwa makusudi ili kujaribu kusaidia kupunguza idadi ya watu duniani na kwamba nchi nyingi zilizolengwa katika "kampeni" hii zilikuwa ni kutoka Afrika na nchi zingine masikini duniani! Mpaka leo inaaminika kwamba UKIMWI umeshaua kati ya watu milioni 28-35 na watu zaidi ya milioni 75 tayari wameshaambukizwa !
  • Nilikuwa Mwanafunzi mdogo UKIMWI ulipoingia Bukoba. Wenyeji waliupachika jina la Juliana – jina la mashati fulani yaliyokuwa yanatoka Uganda. Kwa tuliokuwa wote Shule ya Sekondari ya Kahororo enzi zile nadhani watawakumbuka walimu na wanafunzi wenzetu wapendwa tuliowapoteza kutokana na ugonjwa huu hatari usiokuwa na tiba. Jamani, mnamkumbuka Mwalimu wetu wa Kemia Justin Kaijage? Vipi kuhusu Mwanafunzi mwenzetu William Manhyakenda? Walimu wetu wa Fizikia na Hesabu Mushaija na Mkewe? Vipi kuhusu Mwalimu wetu mpendwa wa Bayolojia Ntamakurilo? Mhasibu Gama, Wapishi wetu wapendwa na baadaye Mkuu wetu wa shule Ishengoma?
  • Kama vile kitambulishi cha ushoga kilichoambatishwa na ugonjwa huu kule Marekani, tulishuhudia unyanyapaa mkubwa kwa wagonjwa wa UKIMWI: Ulikuwa ni ugonjwa wa kuonewa aibu sana. Hili lilikuwa ni kosa na nchi zilizojidamka mapema katika kukabiliana na ugonjwa huu (mf. Uganda) zilipiga hatua kubwa katika kukabiliana nao. Nchi zingine za Kiafrika zikaendelea na unyanyapaa na matokeo yake tumeyaona. Ugonjwa wa UKIMWI umeibuka na kuwa janga kubwa kabisa katika kizazi hiki !
   • Baada ya miaka 30, Leo hii karibu kila familia imeshaguswa na UKIMWI kwa namna moja ama nyingine. Mimi binafsi nilishawapoteza kaka wawili kutokana na ugonjwa huu hatari.
   • Leo hii “tunaposherehekea” miaka 30 ya gonjwa hili hatari tukumbuke tu kwamba bado halina kinga wala tiba na bado linaua (pamoja na Loliondo yetu!). Uzuri sasa ni kwamba tunalifahamu gonjwa hili vizuri na tunaweza kujikinga nalo tukiamua. Wapendwa, tuchukue tahadhari !!!
    Makala ya kihistoria ya Dkt. Michael Gottlieb yanapatikana HAPA

     5 comments:

     1. ahsante sana kwa kutupa nafasi ya kuufikiri kwa makini ugonjwa huu

      ReplyDelete
     2. ahsante sana kwa kutupa nafasi ya kuufikiri kwa makini ugonjwa huu

      ReplyDelete
     3. Nahisi watu hawajahamasika kisawasawa kuhusu huu ugonjwa, kwani wengine husema ni ajali kazini kama unavyopata malaria...nashukuru mkuu kwa tafakari hili, ...ni kweli Tanzania bila ukimwi inawezekana, lakini muhimu ni elimu kwa watu waelewe nini `ukimwi'

      ReplyDelete
     4. Binadamu ni mwepesi wa kusahau; na pengine ni kutojali, hulka au sijui ni nini. Tuendelee kujilinda na pengine siku moja dawa na kinga ya ugonjwa huu vitagunduliwa na utaweza kutokomezwa.

      ReplyDelete

     JIANDIKISHE HAPA

     Enter your email address:

     Delivered by FeedBurner

     VITAMBULISHO VYETU