NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, July 4, 2011

CCM KUANZA KUSHEREHEKEA MIAKA 50 YA UHURU - TAARIFA YA KATIBU MWENEZI
Mwaka huu Sehemu ya nchi yetu, yaani Tanzania Bara itaadhimisha miaka hamsini ya Uhuru wake toka kwa Wakoloni. Uhuru huu uliopatikana miaka hamsini iliyopita ni kazi nzuri na ya Kizalendo iliyofanywa na Chama cha TANU. Chama Cha Mapinduzi katika kukumbuka kazi hii nzuri ya kutafuta Uhuru wa nchi yetu kimeamua kufanya shughuli mbalimbali za kukumbuka kuzaliwa kwa chama kilicholeta Uhuru wa Tanzania Bara yaani TANU.

Itakumbukwa TANU ilizaliwa tarehe 7/7/1954 hapa Dar es salaam katika mtaa wa New street ambao kwa sasa unafahamika kama mtaa wa Lumumba mahali ambapo sasa ni Ofisi Ndogo ya CCM Makao Makuu. Huo ukawa ndio mwanzo wa harakati za kudai Uhuru, Utu na Heshima ya Mwafrika katika nchi yetu.

Kwa kuienzi historia na kazi nzuri na ya Kizalendo iliyofanywa na TANU, Chama Cha Mapinduzi kimeamua katika kuadhimisha miaka hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara kuandaa shughuli mbalimbali za kijamii zikiwa na kauli mbiu Uhuru na Kazi, kauli maarufu katika miaka ya nyuma ambayo Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere aliitoa katika hotuba yake ya kusisimua siku ya mkesha wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961. Mwalimu Nyerere aliitumia hotuba hiyo kuwaeleza wananchi wajiandae kuanza kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea wao wenyewe na nchi maendeleo.

Maadhimisho haya yatafanyika nchi nzima kuanzia ngazi za matawi na kuwashirikisha wanachama wetu na wananchi wote kwa ujumla. Shughuli zitakazofanyika ni kama zifuatavyo:

i. Usiku wa kuamkia tarehe 7/7/2011 Vijana wa CCM nchini watakutana maeneo mbalimbali kufanya shamrashamra za kuzaliwa TANU

ii. Tarehe 7/7/2011 asubuhi wanachama wa CCM na wananchi watakutana kwenye matawi yao na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile, kufanya usafi, kusaidia ujenzi, kupanda miti, kutembelea wagonjwa mahospitalini n.k.

iii. Ikiwezekana kufanya matamasha mbali mbali yatakayowashirikisha vijana,wasomi,wanasiasa na wazee kujadili masuala mbali mbali yenye faida kwa Kata, Wilaya, Mkoa au Taifa kwa ujumla.

iv. Kufanya mikutano ya hadhara na kujikumbusha mafanikio yaliyopatikana kwa kila Mkoa na Wilaya katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru. Kwa Sehemu kubwa tunategemea walezi wa CCM wa Mikoa na Viongozi mbalimbali wa Kitaifa watashiriki shughuli hizo mikoani.

Sherehe hizi zitaanza usiku wa tarehe 6/7/2011 kwa vijana wa CCM sehemu mbalimbali nchini kukutana na kusherehekea ikiwa ni pamoja na kufyatua MAFATAKI saa sita usiku ya siku hiyo, kama ishara ya kuzaliwa TANU.

Mwenyekiti wa CCM Taifa Dr. Jakaya M. Kikwete atashiriki sherehe hizi mkoani Dar es salaam, usiku wa Tarehe 06/07/2011 na tarehe 07/07/2011 asubuhi atakutana na Mabalozi wa Nyumba Kumi Mkoa wa Dar es salaam. Ni mategemeo yangu vyombo vya habari vitashirikiana nasi katika kuuelimisha umma kuhusu historia hii muhimu ya Taifa letu na kutangaza matukio yote yatakayo ambatana na maadhimisho haya. Ahsanteni sana.


Nape M. Nnauye, KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA, ITIKADI NA UENEZI 03/07/2011
*************
Angalizo

Jambo la muhimu linalokosekana katika taarifa hii ni kuhusu matatizo na changamoto ambazo TANU na baadaye CCM i-li/me/mesha/na-pambana nazo. Ningependa sana kusikia, mbali na mafanikio yaliyopatikana, changamoto zinazotukabili kama taifa na la muhimu zaidi  - mikakati ya kupambana na changamoto hizo.

Ni nusu karne sasa imepita na japo ni wazi kwamba tumepiga hatua, ni lazima pia tujikumbushe wapi tulipojikwaa na tunachukua hatua gani kuzuia tusijikwae tena. Kama safari yetu haijaenda sawasawa kama tulivyotegemea, ni kwa nini? Zipi ni kero kubwa (na zipo nyingi tu) zinazowakabili watu wetu? Tutazitatuaje?

Kukusanyika ili kusherekea mafanikio pekee ni kujivika kilemba cha ukoka...

Vinginevyo Happy Birthday TANU/CCM. Na pengine si vibaya tukiisikiliza tena sauti hii yenye kuchoma kuhusu zimwi letu kuu angamizi linatotuandama na kukwamisha maendeleo yetu. Mungu Ibariki Tanzania !!!

3 comments:

 1. Nafikiri kwa mtizamo wangu TANU, ni mama wa vyama vyote...ni kwa mtizamo wangu tu!

  ReplyDelete
 2. CCM inafanya usanii, kwani si mrithi wa kweli wa TANU, kwa maana ya kuendelea mapinduzi yaliyoanzishwa na kuendeshwa na TANU katika mazingira ya miaka ile. CCM ilipaswa kuwa inaendeleza mapinduzi katika mazingira ya leo, na badala yake inaimarisha ukoloni mambo leo katika nchi yetu.

  Yeyote anayesoma "Azimio la Arusha," kwa mfano, ambamo dhana ya Mapinduzi imefafanuliwa, hawezi kuiita CCM chama cha mapinduzi. Lakini kwa vile waTanzania hawana utamaduni wa kusoma, CCM inaendelea kupeta kwa kujiita chama cha mapinduzi, wakati ni chama kinachohujumu mapinduzi.

  ReplyDelete
 3. Emu-three: Ni mama wa vyama vyote kwa maana ya kwamba ni chama cha kwanza cha kisiasa au ni cha kwanza kwa kuwa fikra na falsafa zake ndizo zimerithiwa na vyama vingine vya kisiasa. Kama alivyouliza Profesa Mbele, kama ni hili la pili, ni chama gani ambacho kweli kinaweza kusema kwamba kilirithi falsafa za TANU na kuziendeleza kwa vitendo?

  Profesa Mbele: Ukienda pale kwenye tovuti ya CCM Azimio la Arusha lingalipo; na imani na ahadi za MwanaCCM ni zile zile za MwanaTANU. Lakini kama tunavyojua ni jambo moja kuwa na falsafa nzuri, na utekelezaji wake ni jambo jingine. Na hapa ndipo CCM inapokwama kabisa.

  Ngoja tuone hizi juhudi za kujivua magamba zitakavyoendelea na kama kweli zitaweza kuirudisha CCM katika japo kivuli tu cha uadilifu wa TANU....

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU