NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, July 1, 2011

FIKRA YA IJUMAA: ATI, DAIMA MTOTO WA NYOKA NI NYOKA?

Katuni ya Nathan Mpangala

Kwa hali ya sasa nchini mwetu nani ni mla rushwa na yupi ni mwadilifu? Daima ni kweli kwamba mtoto wa nyoka ni nyoka? Ni lazima tuupime uadilifu wa mtu kwa kuzingatia wasifu na dhambi za wazazi wake? Historia inasemaje? Rushwa ni suala la kimfumo lakini utatuzi wake tunauchakura katika jalala la hulka na uadilifu wa mtu mmoja mmoja. Tutafanikiwa?

Samahani kwa maswali mengi yasiyo na maana. Ni hiki kibonzo cha Mpangala kimenifikirisha sana. Ijumaa na Wikiendi njema wadau!

5 comments:

 1. Mkuu kweli mwana wa nyoka ni nyoka, kwani kinachochumwa kwa rushwa kitaliwa na familia na nini matokea yake kama sio kujenga familia iliyojaa madhambi...lakini wakati mwingine najiuliza katika maisha kama haya ya bongo `rushwa' inaeleweka kama inavyotakiwa ielekweke...maana juzi tulimkimbiza mgonjwa hospitalini, tukakuta zinga la foleni, na hali ya mgonjwa ndio hiyo..tufanyeje, jamaa mmoja akapitisha mchango wa dharura, alipozipata zile hela akazunguka nyuma, mara akaja na ..mmmmh, mgonjwa wetu akaitwa kwa kupitia mlango wa nyuma, akapata matibabu....kwanza nilisikitika kimoyomoyo nilipowaona wazee, ...na wengine wamejikunayata wakisubiri zamu zao za kumuona docta...na ukiingia kwa docta, wakati mwingine anaonge na simu na...huko nisiende mbali, lakini kilichofanyika pale ni nini, ...ni rushwa...sasa inaeleweka hii kweli!

  ReplyDelete
 2. mh labda lakini haiko hivi, sio lazima mtoto wa padre kuwa padre, anawaeza hata kuwa shehe kama sio mganga wa kienyeji

  mimi nimetokea katika familia ambayo tabia zake karibia zote sina! ndani mwetu twaijua haki kuliko rushwa kwa hiyo toto laweza kuwa kinyume na mizazi mipakashume

  ReplyDelete
 3. Hapa tatizo au matokeo siyo vinasaba vya ukoo wake bali mazingira atakapokulia mtoto wa hawa mahabithi. Hamkumuona mtoto wa Idd Amin, Jaffar na wa Julius Nyerere, Madaraka wakikutana Butiama na kujadili mambo ya msingi? Kimsingi mazingira ndiyo humfinyanga mtu. Usishangae mtu kama Jakaya Kikwete angezaliwa Marekani huenda angekuwa kuli huku Boma akiwa mvuvi kule Kenya.Nani angeamini kuwa mwalimu Nyerere ni mtoto wa Chifu wa Kizanaki aliyekuwa na wake wengi lakini yeye akaishia kuwa na mmoja kwa maisha yake yote? Nani angeamini watoto wa wachunga mbuzi wa usukumani na umasaini wangegeuka kuwa mamilionea? Waangalie akina Lowassa na Chenge utajua nimaanishacho? Nani angeamini kuwa maprofesa wangekuwa mafisadi kuliko wale wasio na elimu? Watazame akina Maghembe, Kapuya na wengine ulinganishe na watu kama Paulo Sozigwa.

  ReplyDelete
 4. wana falsafa wanasema ukitaka kuuwa nyoka basi usitumie mkono wako muuwe nyoka kwa mkono wa adui yako.

  ReplyDelete
 5. Emu-three: pole kwa hicho kisa cha mgonjwa. Tumefikia mahali ambapo kila mtu anajua na kutegemea kwamba bila kutoa rushwa mambo hayaendi. Rushwa imegeuka kuwa ndiyo mfumo unaoendesha maisha yetu. Mtu ukitaka kwenda hospitali, na kama unataka huduma ya maana na ya haraka, basi ni lazima kabisa unaandaa na pesa za kumhonga Daktari kama ulivyobainisha hapa. Kila mahali utakakokwenda hali ni ile ile. Hata kulipia bili ya umeme! Ndiyo maana nikauliza, nani ni mla rushwa na yupi ni mwadilifu? Ndiyo maana nikasema kwamba rushwa ni tatizo la kimfumo na kutafuta mtu mwadilifu mmoja mmoja ni kubahatisha tu kwa mfumo tulionao. Je, ni lini rushwa itageuka na kuwa jambo la aibu? Ni nini kinasababisha Daktari au Trafiki apokee rushwa? Tunakijua?

  Ukishika madaraka makubwa halafu "ukazubaa" muda wako ukapita na ukastaafu bila kutajirika jamii inakucheka. Nimesikia kauli za kumdogosha Philip Mangula kwa sababu eti sasa siyo tajiri. Hivi karibuni zimeripotiwa habari kwamba familia ya Mzee Kawawa inagombea nyumba. Hii imetajwa kuwa ni hasara za kuzubaa na kuacha kujitajirisha. Waadilifu ndiyo wanachekwa! Kama jamii inashabikia na kuwaenzi wala rushwa na mafisadi, rushwa kweli itakwisha?

  Kamala: "Ndani mwetu twaijua haki kuliko rushwa kwa hiyo toto laweza kuwa kinyume na mizazi mipakashume" - Kweli tupu. Ndiyo maana nikauliza kama kweli daima mtoto wa nyoka ni nyoka! Amani ya ndani mwetu, ridhiko na furaha ya kujua kwamba umeishi maisha yako vyema - sidhani kama mafisadi wanavyo vitu hivi. Sijui huwa wanajisikiaje wakiwaona watu masikini hohehahe huku wakijua kwamba wamechangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo. Hulka zao kweli huwa haziwasuti? Kama haziwazuti basi pengine hawana roho za kibinadamu! Halafu siku ya siku inafika, roho inauacha mwili na wanauacha utajiri na mapesa yote yale ya kuiba yakizagaa tu!

  Mwalimu Mhango: Wataalamu wa taaluma ya vinasaba wamegundua kwamba ma-serial killers kama Dahmer, Teddy Bund na wengineo wana vinasaba tofauti na watu wengine wa kawaida. Sehemu za ubongo zinazotawala hisia za upole na huruma kwa watu hawa "zimezimwa" na kwao kuua mtu na hata kula nyama yake ni jambo la kawaida tu. Sitashangaa pia kama wataalamu wakigundua kwamba akina Mobutu, Amin - na mafisadi wetu uchwara tunaohangaika nao leo wana matatizo ya kiakili au ya kinasaba.

  Tabia na mwendendo wa mtu maishani ni muungano wa nasaba na mazingira yake. Hebu tuwafanyie uchunguzi wa kina wa DNA mafisadi hawa. Pengine kuna "genes" za ufisadi!

  Anony: Adui wa kutuulia nyoka tumpate wapi? Sisi hatuwezi? Au tusubiri watu kutoka nje waje watuondolee kero ya rushwa na ufisadi?

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU