NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, July 29, 2011

FIKRA YA IJUMAA: TUSIJE TUKAJENGA JAMII KAMA HII YA WAMAREKANI !!!

 
Uchambuzi mpya uliofanya kutokana na data za sensa hapa Marekani unaonyesha kwamba pengo la kipato kati ya walionacho na wasionacho linazidi kupanuka.

Uchambuzi huu umeonyesha kwamba kipato cha wazungu ni mara 20 ya kile cha watu weusi na mara 18 ya kile cha watu wenye asili ya Kilatino. Kipato cha wastani kwa familia za kizungu mwaka 2009 kilikuwa dola 113,149 ikilinganishwa na dola 6,325 katika familia za watu wenye asili ya Kilatino na dola 5,677 familia za watu weusi
 
Sote tunajua kwamba Marekani bado inasumbuliwa na ubaguzi wa rangi na kusema kweli watu ambao si wazungu bado wana uwezekano mkubwa zaidi wa kwenda jela, kutokuwa na elimu bora, kutopata kazi nzuri, kuishi katika umasikini na kufariki mapema kuliko wenzao wazungu. 

Matabaka haya yana madhara makubwa kijamii kiasi kwamba jamii nzima inaathirika. Marekani ndiyo nchi yenye wafungwa wengi magerezani na katika baadhi ya majimbo bajeti ya kuendesha magereza inazidi, inalingana na au kupungua kidogo tu ile ya elimu. Jamii ya aina hii ni wazi kwamba ina matatizo na hii ni mojawapo ya sababu inayotajwa sana kuwa ni tatizo kubwa la mfumo wa kijamii wa Kimarekani, mfumo ambao pengine utaweza kuchangia katika kuporomoka kwake.

Sisi tunaingiaje katika mtafaruku huu? Tunaendelea kulea matabaka: watu wachache wanajitajirisha sana tena kwa kutumia raslimali za wote wakati wananchi wetu wengi wanazidi kuwa masikini. Kama unabisha nenda huko vijijini ukaone. Bado hatujaweza hata kuwapatia watu wetu huduma za msingi kabisa wakati tunao mafisadi wanaofuja mabilioni ya pesa za umma, pesa ambazo kama tungezitumia vizuri zingeweza kusaidia kuinua hali za maisha za wananchi wetu ambao ni masikini hasa huko vijijini. 

Picha kutoka Mzee wa Matukio

Hali hii ikiachiwa kuendelea ni wazi kwamba tunakoelekea si kuzuri kwani binadamu ni mnyama mwenye kujua ukomo wake. Unaweza kumnyonya, kumsikinisha, kumdhulumu na kumtesa lakini siku moja atafikia kikomo na kusema liwalo na liwe. Akifikia hali hii basi jamii inaingia katika misukosuko mikubwa. Historia imejaa mifano mingi ya aina hii.

Ati, mahusiano yetu ya kitabaka leo yangekuwaje kama kweli tungezitumia raslimali zetu kwa faida ya wote?

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU