NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, July 7, 2011

MBUNGE WANGU JAMANI MBONA HAKIELEWEKI? MARA YUMO MARA HAYUMO...


Ni mbunge wangu bilionea Bwn. Andrew Chenge. Ni kuhusu lile sakata la ununuzi wa ile rada yetu ya bei mbaya. TAKURURU walishamsafisha. Na mwenyewe pia alishajitakasa. Wakati huo huo serikali kupitia kwa waziri wake wa Nchi Ofisi ya Rais, Mathias Chikawe imetangaza rasmi kwamba mbunge wangu hakuhusika kwa namna yo yote ile na sakata hili. 


Wakati huo huo timu ya Wabunge waliokwenda Uingereza hivi karibuni kufuatilia malipo ya rada hiyo imependekeza kwamba Bwn. Chenge pamoja na wenzake waliohusika na kashfa hii iliyoliletea taifa hasara kubwa wafikishwe mahakamani. Katika taarifa yao, Chenge anatajwa kuwa ni mtuhumiwa namba moja pamoja na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Dk Idrisa Rashid.


Baadhi ya wabunge wa timu hiyo: mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (kulia), mbunge wa Ilala, Idd Zungu (katikati) na mbunge ambaye pia ni  Naibu Spika Job Ndugai (kushoto).


Kutokana na taarifa hii, mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amechimba mkwara kwamba Chenge asipofikishwa mahakani basi CHADEMA watafanya maandamano nchi nzima mpaka kieleweke!

Mkanganyiko huu umeniachia maswali mengi. Kama mbunge wangu kweli ana hatia kama inavyodaiwa, kwa nini TAKURURU na serikali wameshamsafisha? Ningetegemea kwamba katika kipindi hiki cha kujivua magamba, chama tawala na serikali yake wangekuwa wakali na kutumia sakata kama hili kuonyesha kwamba kweli wamedhamiria kujisafisha. Je, huu ni mwendelezo wa ile tabia sugu ikerayo sana ya kulindana na kukingiana kifua?

Ndiyo maana imebidi niulize kama mbunge wangu ana hatia ama la kwani siamini kama kweli katika kipindi hiki cha mtandao na upatikanaji huru wa habari, wavua magamba wangali wanategemea kwamba wataweza kweli kuzima na kuifunika kashfa nzito kama hii. 


Kunakaribia kupambazuka sasa na anayedhani kwamba kungali bado usiku wa manane anajidanganya. Hebu ubaridi wa alfajiri na ukatusisimue na kutuondolea hofu, matongotongo na fikra zetu za kitwana. 

5 comments:

 1. Tatizo la kesi hii ni kuwa imeingiliwa na SIASA sana kiasi kwamba ni vigumu kuwa na uhakika kiendeleacho ni SIASA au UKWELi hasa ukizingatia nafasi ya uongo ilivyojaza mtuno kwenye siasa ya TANZANIA!:-(

  ReplyDelete
 2. Ni kweli Mtakatifu.Katika nchi za wenzetu hizi serikali ikitoa tamko inabidi wananchi wa kawaida msikilize kwani matamko ya kumtetea mtu huwa hayatolewi kirahisi. Pengine kwetu sivyo!

  Ngoja tuone sakata hili litakavyoisha. Ugomvi wangu pekee na mbunge wangu huu ni kutofanya mambo ya maendeleo ya msingi katika jimbo lake, mambo ambayo yangemfanya akumbukwe daima. Kutokana na utajiri wake huu uliopindukia kimo, mbona asiweze kuhakikisha kwamba angalau kila kijiji kina kisima cha maji? Mbona asiijenge barabara ya kutoka Bariadi mpaka Lamadi?

  Badala yake utajiri huu anautumia kwa kugawa pesa kwa watu wenye shida binafsi wanaofika kumweleza matatizo yao. Ningefurahi sana kama angechukua mkabala wa kimtazamo kuliko njia za mkato anazotumia sasa.

  ReplyDelete
 3. @Mt. Simon & MMN: ukiona hivo ujuwe kuwa kuna jambo lafichwa kwani sidhani kama Chenge ni mhusika pekee wa sakata hilo....lazima akibanwa wengine watakuwepo hasa ukitilia maanani kuwa kuna watu walikuwa na kiburi cha kusema 'hata ikibidi kula nyasi tutakula tu lakini rada itanunuliwa'.

  SWALI: alikipatapi kiburi hicho kama hakikuanzia kwa kiranja mkubwa?

  tusuburi!

  ReplyDelete
 4. Hapa kuna siri nzito, inaelekea skendo ya Chenge inawahusisha vigogo wengine wazito, ndiyo maana chenga nyingi zinachezwa ili asifikishwe mahakamani. Chenge akifikishwa mahakamani kwa vyovyote na wao hawatasalimika.

  ReplyDelete
 5. Ingekuwa huku kwa wenzetu kwenye siasa za kiwajibikaji, bila shaka Mbunge wangu huyu angekuwa ameshajiuzuru muda mrefu sana.

  Ngoja tuone sakata hili litakavyoisha lakini kitendo cha serikali kusimama na kumsafisha huku ushahidi ukizidi kurundikana kwamba ni mhusika mkuu wa kashfa hii kidogo kinashangaza. Mazingaombwe ya kisiasa!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU