NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, August 3, 2011

MBUNGE WANGU KWELI NI NG'OMBE DUME MWENYE MAPEMBE ???


Maendeleo hafifu ya operesheni ya kihiari ya kujivua gamba inayoendelea ndani ya CCM inaendelea kuzusha mijadala na hata mikanganyiko. Baada ya "Mheshimiwa" Rostam Aziz kujivua gamba hivi karibuni, watu wamekuwa wakisubiri kuona matokeo zaidi ya operesheni hii. Jina la mbunge wangu limekuwa likitajwa sana kuwa ni gamba nambari wani ndani ya CCM na kama kweli chama hicho kimedhamiria kujisafisha ni lazima gamba hilo livuliwe. 

Katika makala zake za Neno la Leo, mwandishi na mchambuzi mahiri Maggid Mjengwa ameandika kuhusu ng'ombe dume wenye mapembe (ambao hujulikana kama kambako kule Usanguni) na ugumu wa kuwatoa zizini (Bofya HAPA). Katika makala yake fupi lakini yenye kufikirisha, Mjengwa anaashiria kwamba mbunge wangu Andrew Chenge a.k.a Mzee wa Vijisenti ni "kambako" ambaye amegoma kutoka zizini hata baada ya kuumwa mkia. Katika kuchangia maoni yangu huko nimesema yafuatayo kuhusu ng'ombe dume anayegoma kutoka zizini hata baada ya kumuuma mkia.


*********************
"Kule kwetu Usukumani kambako huitwa nzagamba au nziku; na wakati mwingine huwa tunawatumia katika kilimo. Nzagamba akizira; na ukamtandika viboko bila mafanikio, njia ya uhakika ni kuushika mkia wake na kuupinda - kama vile wataka kuuvunja. Hapo ni lazima atanyanyuka tu atake asitake.

Tahadhari hata hivyo ni kwamba akinyanyuka aweza kuwa na hasira kutokana na maumivu na inabidi uwe mwangalifu kwani aweza kukutwisha mapembe. Au anaweza kunyanyuka na bado akazira kuvishwa minyororo kwenda kulima. Hapa inabidi utafute wanaume hasa tena wenye uzoefu wanaoweza kumvisha minyororo na kumtoa zizini kwa nguvu atake asitake.

Swali pengine ni kwamba kama tukipinda mkia na nzagamba bado akaendelea kuzira, tunao wanaume wa shoka wa kuweza kumtoa zizini kwa nguvu?"

************* 
 • Pamoja na kwamba nimekuwa nikiandika hapa mara kwa mara kuhusu mbunge wangu huyu, pengine umefika wakati wa kujiuliza kama kweli ni gamba a.k.a kambako a.k.a nzagamba. Serikali na TAKURURU wameshamsafisha na yaliyobakia ni maneno tu ya hapa na pale. Kama kweli ni gamba mbona asijivue au kuvuliwa mara moja? Kama anayo kesi ya kujibu kuhusu mabilioni ya rada, mbona asipelekwe mahakamani? Tetesi, uvumi na udaku tu utatufikisha wapi kwa mtu aliyeliingizia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi?  Ndiyo maana nauliza: Tunao ushahidi wo wote kwamba mbunge wangu huyu ni "kambako?"

6 comments:

 1. This comment has been removed by the author.

  ReplyDelete
 2. Prof Matondo,
  Maswali unayojiuliza yanafanana na maswali ninayojiuliza.

  Lakini mimi nimekwenda mbali kidogo katika kujiuliza. Nikajiuliza pia, 'ni hao tu wanaostahili kuvuliwa magamba?'

  Kwa kuwa, katika hali ya kawaida kabisa, hawa hawakuwa kisiwani!

  ReplyDelete
 3. Ni kweli Bwana Fadhy - ni mikanganyiko tupu. Kama hata hawa wanaotuhumiwa kuwa magamba wamegoma kutoka zizini, vipi kuhusu wale ambao tuhuma zao zingali gizani? Mazingaombwe!

  ReplyDelete
 4. Matondo, ni kweli hilo swali ulitakiwa uliulize kwanza kama kweli Mheshimiwa Chenge ni gamba au la kabla ya kuandika hapa na pale kwa yale yanajiri kutoka katika vyombo mbali mbali vya habari Tanzania.
  Tatizo la vyombo vingi vya habari Tanzania hasa vya kwenye mitandao vinakuwa na majibu wakati hata swali halipo.
  CCM haijatamka mbele ya kandamnasi kama huyu au yule ni mtuhumiwa wa ufisadi, lakini cha kushangaza vyombo vingi vya habari tayari wameishapata majina.
  Kitu cha muhimu, CCM ilitakiwa ihojiwe kwanza ili itoe majibu kwa mbele ya kandamnasi, ni nani inayemtuhumu kwa ufisadi katika falsafa yake iliyoileta ya ''kujivua gamba'', badala ya vyombo ya habari kutoa majibu. Ikumbukwe hata Mheshimiwa Chenge alishasema hata yeye hajui kama ni fisadi kwa vile hajawahi kuelezwa na chama chake(CCM) au kushitakiwa mahakamani.
  Kwa nini CCM inakuwa na kigugumizi katika hili wakati huohuo inapiga kelele kusema wale wote ambao wametumumiwa kwa ufisadi lazima waachie madaraka. Hapa ndipo ninapopatwa na wasiwasi katika hili, na ninaanza kuwashangaa kwa nini mnaanza kuongelea nzagamba(nziku) au kambako jinsi ilivyovigumu kumtoa zizini wakati hamjui hata nzagamba(nziku) au kambako ni yupi.
  Matondo, labda tu niulize, ni nani au chombo kipi kati ya vitatu vinavyounda nguzo za utawala nchini kimemtuhumu na kudhibitisha kama fisadi na katika ushahidi gani?
  Napenda nieleweke, simemi hivi tu kwa vile mheshimiwa Chenge ni ndugu yangu bali ninasema hivi kutokana na yanayojiri kutoka ndani ya CCM na vyombo vya habari.
  Fikira zangu ni kuwa, ninakubaliana pale watu wa nje wanapotubeza na kusema, Tanzania siasa nyingi, wakiwa na maana kuwa Watanzania wengi ni watu wa udaku wa siasa na CCM wanalijua hili ndiyo maana wanakuja na porojo nyingine kuwa watuhumiwa ''wameongezewa'' muda wa ''kujivua gamba'' mpaka mwezi wa tisa.

  ReplyDelete
 5. Ng'wanaMwamapalala;

  Asante kwa angalizo lako. Imenichukua muda kidogo kugundua kwamba vyombo vingi vya habari vya nyumbani - hata vile vinavyojidai kwamba viko makini - vinaandika habari za kiudakudaku tu, habari zisizo na ushahidi wowote na ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kina. Hatari zaidi ni ukweli kwamba watu wetu wengi bado wanaamini kwamba kila kinachoandikwa katika magazeti na hata kutangazwa katika redio/runinga ni cha kweli. Ndiyo maana ni rahisi sana kuchafua jina la mtu kama ukitaka.

  Nilipofikiria vizuri juzi nikaona pengine nimekuwa simtendei haki mbunge wangu huyu kwa kujiunga kwangu kushabikia maneno ya mitaani na udaku wa magazetini. Kama ushahidi upo kwamba kweli ni fisadi na kwamba alifaidika moja kwa moja na pesa za rada, basi ushahidi huo utolewe na kama CCM wana ubavu wamvue gamba na serikali impeleke mahakamani. Mwenyewe ameshajitetea na kujisafisha mara nyingi; na serikali imeshasema kwamba mbali na kuwa mwanasheria mkuu wa serikali wakati ule hakufaidika na ufisadi wa rada. Kama kuna mwenye ushahidi unaoonyesha vinginevyo basi autoe na hatua zinazopaswa kuchukuliwa zichukuliwe.

  Vinginevyo tutaendelea kupiga majungu na kudakuka tu na kubakia tu pale pale tukipiga maktaimu - maneno mengi na ahadi lukuki zisizo na maana, vitendo hamna na huku dunia inatucheka.

  Na sasa hali ya udaku wa kisiasa imezidi kuwa mbaya kwani sasa ni mpaka bungeni ambako "waheshimiwa" wanaropoka tu hata bila kuwa na data kuthibitisha miropoko yao.

  ReplyDelete
 6. Prof Matondo, Hapo umenena. Sina zaidi cha kuongeza zaidi ya kusema ''Taifa letu bado ni changa!!''na wananchi bado wanatambaa hata baada ya kutimiza miaka karibuni 50 katika dunia iliyoko katika karne ya 21.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU