NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, August 5, 2011

MZAZI ANAPOMSHAWISHI MTOTO KUJIFELISHA MTIHANI ILI KUKWEPA GHARAMA ZA KUMLIPIA !!!


Nikiwa Kama Mzazi Habari Hii Imenisikitisha

Karibu wazazi wote tunawatakia watoto wetu maisha mema. Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana ili angalau safari yetu ikishakamilika hapa duniani basi tuwaachie angalau kitu kidogo kitakachowasaidia wakati sisi hatupo. 

Na katika urithi bora kabisa ambao tunaweza kuwaachia watoto wetu ni elimu bora. Wenye uwezo wanatumia maelfu ya dola kuwasomesha watoto wao nchi za nje. Wengine wanajibidisha kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi wakiamini kwamba huko watapata elimu bora. Wazazi leo wanakazana kuwapeleka watoto wao wanaoanza shule katika "akademi" zinazofundisha kwa kutumia lugha ya Kiingereza ili kuwapa misingi imara ya lugha hiyo watoto wao. 

Na sababu kubwa iliyotufanya wengi wetu tuliolowea huku ughaibuni na kubeba maboksi ni elimu bora kwa ajili ya watoto wetu. Elimu bora ndio urithi bora kabisa tunaoweza kuwaachia watoto wetu.

Nilipoisoma habari hii hapa chini kuhusu wazazi wanaowashawishi watoto wao kufeli ili kuepuka gharama za kuwasomesha niliwasikitikia wazazi hao pamoja na hawa watoto. Je, serikali inalijua tatizo hili? Kuna utaratibu wowote wa kuweza kuwasaidia watoto kama hawa ili nao wakaendelea kusoma? Kama upo, unafahamika kwa walengwa? Iweje tunapoteza mabilioni kutokana na ufisadi lakini hatuwezi kuwasaidia watoto wetu hawa kujipatia elimu? 
 ********
‘Wazazi wanawashawishi watoto wao kufeli’
Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga; Tarehe 7 Mei 2011

MATOKEO mabaya ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kila mwaka mkoani Rukwa yanasababishwa na baadhi wazazi na walezi ambao wamekuwa wakiwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani ya mwisho ili kukwepa wajibu wao wa kuwagharamia kielimu katika ngazi inayofuata.
 

Diwani wa Kata ya Milepa iliyopo wilayani Sumbawanga, Apolinary Macheta alisema hayo wakati akichangia mada kwenye mkutano wa Wadau wa Elimu wa Wilaya ya Sumbawanga uliofanyika juzi katika Kata ya Laela wilayani humo.

Alisema kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa na tabia kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao ya kumaliza darasa la saba kwa lengo la kukwepa majukumu ya kuwalipia ada na michango mingine au wakati mwingine wakitaka kuwaoza watoto wao wa kike.
 
Diwani huyo aliongeza kuwa kwa upande wa watoto wao kiume, wazazi hao wamekuwa wakiwashawishi kufanya hivyo ili wajishughulishe na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo ni kilimo, uvuvi na biashara kwa madai kuwa ndizo zenye tija kuliko kuendelea na elimu.

“Tatizo la kutofanya vizuri kwenye mtihani wa mwisho kwa watoto wengi wa vijijini ni wazazi wenyewe ….. hawataki waendelee na sekondari kwa hiyo wanawashawishi kufeli kwa lengo la kukwepa gharama ya kulipa ada na michango mingine, pia kutaka kuwaoza watoto wao wa kike sasa inapotokea mtoto mwenye uwezo mzuri darasani anafeli tufuatilie matokeo yake tangu awali yalikuwaje,” alisema Diwani Macheta.
 
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Christian Lazer alisema kuwa ni aibu wilaya hiyo kuendelea kuwa na watu wanaosoma kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) na kusema kuna kila sababu watendaji wa vijiji kuhamasisha wazazi na walezi kuwaandikisha watoto wenye umri wa kwenda shule kwa wakati.

Alisema kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuondokana na udhaifu huo wa uandikishaji uliopo hivi katika halmashauri hiyo wenye zaidi ya vituo vya 23 vya MEMKWA ambavyo vinawanufaisha watu wasiojua kusoma na kuandika.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU