NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, October 20, 2011

Nguvu za Umma (na Mabeberu) Hazishindiki: Kama Unabisha Nenda Kamuulize Marehemu Gaddafi !!!

Hebu fikiria
Umetawala kwa miaka 42. Umefanya mema na mabaya na kwa hivyo wapo wanaokuona kuwa ni shujaa na wapo wanaokuona kuwa ni nondo mla watu. Wananchi wenzio wamekuchoka na wanataka mabadiliko. Mabeberu wa nje nao wanataka mafuta ya nchi yako. Watu wako wanaanza kuandamana kukupinga na kudai mabadiliko. Na badala ya kutumia ubinadamu na njia za amani, unaanza kuwaua wananchi wako mwenyewe. Hili linageuka kuwa kosa kubwa kabisa kuliko yote uliyowahi kutenda. Mwishowe mapinduzi yanashika kasi na wananchi wako pamoja na mabeberu wa nje wanashinda. Unaishia kuuawa na maiti yako kuburuzwa barabarani kama mnyama. Sasa endelea....
********************* 
 • Japo siyo ubinadamu wala ustaarabu kushabikia kifo cha binadamu mwingine kwani hiyo ndiyo njia yetu sote tuliozaliwa, ukaidi, ujinga na kulewa madaraka kunakoonyeshwa na baadhi ya watawala kama akina Gaddafi kunashangaza. Watu unaowaongoza wanapochoka na kufikia hatua ya kuchukua silaha dhidi yako, ni wakati mzuri wa kusikiliza matakwa yao na kuachia ngazi. 
    • Japo Historia inaonyesha wazi tena na tena kwamba nguvu za umma kamwe hazishindiki, watawala wetu hawa vichwamaji, kama vile mbuni, huishia kuficha vichwa vyao mchangani na kuufumbia macho matakwa na mateso ya umma. Wakiwa katika kunguku la umungu-mtu, ubilionea na madaraka yasiyo na kikomo, vichwangumu hawa hushindwa kabisa kuuona ukweli ulio wazi kwamba kamwe huwezi kumdanganya na kumtawala binadamu kwa wakati wote. Matokeo yake ndiyo haya - wanaishia kuuawa na mizoga yao kuburutwa mabarabarani kama vile wanyama. Inasikitisha sana na sijui kama viongozi na mafisadi wa Afrika wanajifunza lolote!!! 
    • Fuatilia habari mbalimbali zinazozidi kumiminika kuhusu kuuawa kwa Gaddhafi HAPA. Pumzika salama Kanali Muammar Gaddafi. !!!

    6 comments:

    1. kaka Matondo naungana nawe. naandaa makala ntaiweka jamvini kwangu leo leo. ahsante kwa huu mtazamo wako. tatizo, viongozi wetu hawajifunzi.

     ReplyDelete
    2. Watakuja kujuta tu, na miaka miwili ni mingi kuanzia sasa watakuja kugombana wenyewe kwa wenyewe watawala wepya. Kasoro yake Qadaffi alikuwa muungwana wa kibara ya Afrika na hakuwa na Mswahili wala Mwarabu. Nafikiri ndio sababu kuu alichukiwa na adui zake, sababu kubwa hata kuliko hiyo miaka mingi ya utawala wake na kutoruhusu upinzani.

     ReplyDelete
    3. Bwana Fadhy - hili ni jambo la kusikitisha sana kwa sisi Waafrika. Na pamoja na ukweli kwamba huu ni ushindi wa mabeberu, viongozi wa Afrika pia wanastahili lawama. Kwa nini waendeleze rushwa, ufisadi na kukandamiza wananchi wao? Sijui kama Wamarekani, Wafaransa na Waingereza (ambao naamini lengo lao hasa ni mafuta ya Libya) wasingeingilia kati, Gaddafi angeua maelfu mangapi ya wananchi wake. Swali ambalo inabidi tujiulize ni hili: Kuna nini Afrika? Mbona viongozi wetu wako hivi? Kwa nini njaa Afrika? Kwa nini umasikini wa kupindukia kimo Afrika wakati bara letu ni tajiri ajabu? Kwa nini magonjwa na njaa Afrika? Kwa nini UFISADI wa waziwazi Afrika? Waikumbuka Rada, Dowans na Richmond??? Danadana, dharau, udanganyifu, ubaradhuli na ushetani wa waziwazi!

     Najua baadhi ya majibu kwa maswali haya lakini siyo haki kulaumu kila kitu kwa mabeberu wa nchi za Kimagharibi. Na sina uhakika kama viongozi wa Afrika wamejifunza lolote kutokana na mkasa huu wa kusikitisha wa Kanali Gaddafi!

     Manyanya: Naamini kitakachofuatia sasa ni kile kinachotakiwa na mabeberu wa nje (Wamarekani, Wafaransa na Waingereza). Watakayemuweka madarakani bila shaka ni lazima awe tayari kuwapa mafuta ya Libya, vinginevyo naye atakwenda na maji.

     Gaddafi mimi binafsi sikumpenda kutokana na ukweli kwamba alimuunga mkono na kumpa silaha kali Idd Amini wakati ule Watanzania tukipigana naye. Pamoja na kwamba alikuwa na moyo wa kutetea Waafrika na Uafrika, Gaddafi pia alikuwa na tabia ya kutetea madikteta wenzake kama akina Amin, Mugabe, Bokassa, Mobutu na wengineo.

     Miaka 42 madarakani, kulikuwa na ugumu gani kuachia madaraka kwa amani? Mbona wenzake akina Nyerere na akina Mandela waliweza????

     ReplyDelete
    4. Kwa hiyari ya moyo wangu naomba nisichafue maneno ya kaka matondo na mdogo wangu fadhy mtanga.

     yatakayofuatia libya pia ni muendelezo wa dhambi kuu aliyoipanda gaddafi. haingii akilini kuwa mtu mmoja alizaliwa katika nchi yenye mamilioni ya watu na akatawala yeye tu. hadidhi iki hivi: tuko katika kijiji kimoja ambacho kina rasilimali tele na wanachi wananufaika nazo kutokana na usimamizi bora wa mtu mmoja. lakini ni rasilimali za wote. mgawa rasilimali aking'ang'ania kuwa yeye ndiye mgawaji bora na si mwingine kwa miaka mingi (42) pasi na kuandaa mgawaji mwingine au hata kufundisha wengine namna ya ugawaji bora watu wengine wataanza kujiuliza: KWA NINI MGAWAJI AWE YEYE TU ILHALI MALI NI ZETU ZOTE? ndio swali walilojiuliza walibya na walipoanza kusimamia msimamo huu, MABEBERU HAWAKULAZA DAMU. hakika roho ya marehemu gadafi ilazwe panapostahili

     john mwaipopo
     mbeya

     ReplyDelete
    5. Gadaffi amevuna alichopanda na ameacha somo kuwa madaraka si kitu cha kung'ang'ania wala kushikwa na mtu mwenye uwezo mdogo wa kusoma alama za nyakati. Bahati mbaya sana, Gadaffi sawa na watawala wengine wa aina yake, aliishi kwenye dunia bandia ya kujiona anapendwa na kuogopewa asijue madaraka si ujanja bali utashi na uamuzi wa umma. Ni bahati nzuri kuwa wale aliowaita panya na mende na wala unga wametimiza ahadi yao ya kumng'oa. Kuwa imla si kitu cha ajabu. Mbona mwenzake wa Tunisia alisoma alama za wakati na kutimua ingawa alikuwa amechelewa? Mauaji ya kinyama ya Gadaffi yamenikumbusha mauaji mengine kama haya ya imla Samuel Doe hapo tarehe 9.9.1990 baada ya kutekwa na kundi la PY Johnson.
     Nami naandaa makala kwenye jarida la The East African Executive Magazine ya Why don't they ever learn?
     Nimalizie kwa kusema kuwa Gadaffi ameuawa na wale aliowatengeneza kwa kuendekeza utawala wa kifamilia na kujuana kama inavyoendelea kujengekea barani kwetu. Heri joto na vuguvugu hili vingeelekea kusini mwa Libya ili Afrika iwe huru. Je tutegemee nini toka Libya baada ya mabeberu waliomwangusha Gadaffi kuwaachia walibya vurumai zao?
     Nkwazi Mhango

     ReplyDelete
    6. Mabeberu Oyeee! Jamani nasikia bila Mabeberu huko LIBYA Gadafi angeendelea kuwepo na pia Tanzania kiuchumi angalau ingeizidi KENYA!:-(

     ReplyDelete

    JIANDIKISHE HAPA

    Enter your email address:

    Delivered by FeedBurner

    VITAMBULISHO VYETU