NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, October 14, 2011

Tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere Tujiulize: NI NANI HASA ALIKUWA MFUASI WA KWELI WA ITIKADI ZAKE ???

  • Makala hii niliiandika zamani na ilichapishwa katika gazeti mfu la Kwanza Jamii la tarehe 20/10/2009.  Sijui kama bado makala hii  ina ukweli wo wote leo  lakini si vibaya tukiirejelea tena kwani, kama kawaida ya siku hii ya kumbukumbu ya Mwalimu, mwenge umewashwa, hotuba zimetolewa na tathmini mbalimbali zimefanyika. Pamoja na mafungufu yake yote, kwangu mimi Mwalimu Nyerere atabakia kuwa kiongozi wa pekee Tanzania na Afrika nzima hasa kutokana na uadilifu wake!
*************************
Makala haya yametoka katika gazeti la Kwanza Jamii la leo - 20/10/2009

Mwalimu Nyerere na Jangwa Lake la Kiitikadi
(Ati, ni Nani Hasa Alikuwa Mfuasi wa Itikadi ya Mwalimu?)
Na Dkt. Masangu Matondo Nzuzullima

Katika diwani ya Karibu Ndani (Euphrase Kezilahabi, DUP, 1988:27) kuna shairi liitwalo “Azimio”. Beti chache za shairi hilo zinasema hivi:

Azimio sasa ni
Mabaki ya chakula
Kwenye sharubu za bepari
Kalamu inayovuja
Katika mfuko wa mwanafunzi
Vumbi zito
Baada ya ng’ombe kupita
Kilichosalia sasa
Ni punje za ulezi
Zilizosambazwa jangwani
Na mpandaji kipofu

Hivi ndivyo Kezilahabi – ajulikanaye pia kama Shaaban Robert wa Pili – alivyoliona Azimio la Arusha mwaka 1988. Nimelikumbuka shairi hili wakati nikitafakari Historia ya nchi yangu Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo nchi hii nzuri inaadhimisha miaka 10 tangu muasisi wake atoweke hapa duniani. Ni kweli Mwalimu alisambaza ulezi wake wa Ujamaa na Kujitegemea jangwani? Kama ni kweli, ina maana Mwalimu hakuwa na mfuasi wa kweli hata mmoja katika genge lake la Makomredi waliokuwa wakiimba ahadi za usawa wa binadamu? Ati, ni nani hasa alikuwa mfuasi wa kweli wa itikadi kombozi za Mwalimu Nyerere?

Msukumo hasa wa kuandika makala hii fupi niliupata kutokana na visa vifananavyo vilivyotokea kwangu mwenyewe na dada Subi Sabato wa nukta77.blogspot.com. Katika kuadhimisha miaka 10 ya kifo cha Mwalimu Nyerere niliweka mkusanyiko wa video 17 za Mwalimu Nyerere katika blogu yangu (http://matondo.blogspot.com/2009/10/video-mbalimbali-za-mwalimu-nyerere.html). Subi Sabato pia alifanya hivyo hivyo katika blogu yake. Haukupita muda mrefu nilipata barua kutoka kwa watu waliokuwa wakijiita watumishi wa serikali wakinitaka niziondoe video za Mwalimu Nyerere katika blogu yangu mara moja kwani eti sikuwa na hati miliki na kwa hivyo nilikuwa navunja sheria. Waliendelea kunitisha kwamba nisipofanya hivyo basi sheria kali zingechukuliwa dhidi yangu. Subi Sabato naye alipata vitisho kama hivyo. Jambo hili lilinishangaza sana na nilijiuliza maswali mengi ambayo mpaka leo sijapata majibu na ndiyo maana naandika makala hii. Ina maana kuna mtu anamiliki hotuba za Mwalimu Nyerere? Niliwauliza watishaji wangu wanieleze aliko mmiliki wa hati miliki wa hotuba hizi ili niweze kuwasiliana naye lakini mpaka leo sijapata jibu. Mimi nilikuwa ninadhani kwamba hotuba za Mwalimu ni hazina ya taifa na Watanzania wote tuna haki ya kuzisikiliza bila kutishwa na mtu. Nilichukulia mfano wa hapa Marekani ambapo sheria za hati miliki ni kali sana lakini hotuba nyingi za marais wao ziko mtandaoni na ukienda katika maktaba za maraisi hao utaweza kuzisikiliza bure. Ni hazina ya taifa lao. Ni mali ya wote. Ni kumbukumbu ya historia ya nchi yao. Hotuba hizi hazimilikiwi na mtu! Hata hotuba nyingi za Rais Obama tayari zipo mtandaoni! Kuna tovuti nyingi zenye hotuba hizi na mojawapo nzuri ni hii hapa.
Mpaka nitakapopata ufafanuzi wa kina kuhusu ni nani hasa mmiliki wa hotuba za Mwalimu Nyerere, ninashawishika kuamini kwamba kuna kundi la watu ambao wanakerwa, kutishwa na kukoseshwa amani na hotuba za Mwalimu kwani wamegeuka kuwa wasaliti. Hawa inawezekana walikuwa ni watu wa karibu sana kwa Mwalimu na walijifanya kuwa “ardhi yenye rutuba” kwa mawazo na itikadi zake kumbe kwa ndani walikuwa ni “majangwa” tu yasiyootesha wala kustawisha cho chote. Ni mbwa mwitu waliokuwa wamevaa mavazi bandia ya “ukomredi” huku wakiimba na kudumisha “fikra sahihi za Mwalimu” kikasuku tu huku kimatendo wakiwa wamekakawana jangwani. Na baada ya Mwalimu kuondoka sasa wanajaribu kila wawezalo kufanya mawazo yake kombozi yasiwafikie Watanzania huku wakitumaini kwamba kwa njia hii hatimaye pengine Mwalimu ataweza kusahaulika.

Katika hotuba zake nyingi unaweza kumsikia Mwalimu akikemea rushwa na ufisadi; na utulivu wake wa akili, falsafa komavu na uwezo wa kuona mbali, kuonya na kutabiri mambo unaonekana waziwazi. Anasema waziwazi kabisa kwamba rushwa ikiachwa iendelee itaweza siku moja kuutikisa “msingi” wa nyumba (Tanzania). Mwalimu, pamoja na mapungufu yake yote, alitambua kwamba rushwa na utajiri wa kupindukia wa watu wachache kwa upande mmoja, na umasikini na uhohehahe wa asilimia 100 kwa walio wengi kwa upande mwingine siku moja utaitikisa Tanzania kwani ipo siku hawa wasio na kitu watachoka na kusema “liwalo na liwe”. Na hili likitokea hakuna jeshi litakaloweza kurekebisha mambo. Watu wakiamua wameamua na Historia imejaa mifano tele inayoonyesha kwamba nguvu za umma ni kama sunami. Badala ya kujaribu kurekebisha mambo na kuchukua ushauri wa Mwalimu kama vile mbuni asiye na upeo, kundi hili la “wanajangwa” inaonekana limeamua kuficha kichwa mchangani likiamini kwamba kutokomeza mawazo ya Mwalimu pengine ndiyo njia ya mkato ya kuendeleza “jangwa” lao wanalojaribu sana kuhakikisha kwamba linabakia kuwa jangwa. Kundi hili kwa hakika linajidanganya!

Hali hii inaibua hoja nyingine. Kutokana na “ujangwa” huu ambao sasa unaonekana waziwazi, haishangazi kuona kwamba sera nyingi za Mwalimu zilishindwa na kusema kweli inashangaza kidogo kuona kwamba baadhi ya sera zake zilifanikiwa mf. Elimu.

Historia inatuambia kwamba viongozi wengi waliofanikiwa ni wale ambao walikuwa na wafuasi wa kweli, wafuasi ambao walikuwa tayari hata kupoteza maisha yao ili kulinda na kutetea itikadi na harakati zilizoanzishwa na viongozi wao. Na hapa sizungumzii madikteta waliolazimisha itikadi zao kwa wafuasi wao kwa mkono wa chuma na kumwaga damu. Mara nyingi Historia huwa haina huruma na watu wa aina hii bali kuwatupa katika shimo lake la takataka. Huko ndiko waliko akina Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga, Jenerali Bokasa, Jenerali Field Marshal Idd Amin Dada na wengineo wa aina hiyo.

Viongozi ambao hawakupanda mbegu zao katika “jangwa” mara nyingi hawakuwa hata na haja ya kuandika mawazo yao. Wafuasi wao wa kweli walifanya hivyo. Yesu Kristo hakuandika kitabu cho chote lakini wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Buddha pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Lao-Tzu (mwanzilishi wa Taoism) pia hakuandika kitabu cho chote. Wafuasi wake wa kweli walifanya hivyo. Ferdinand de Saussure – mwanaisimu wa Uswisi ambaye anatambuliwa kama baba wa Isimu ya kisasa hakuandika kitabu cho chote pia wakati wa uhai wake. Wanafunzi wake walikusanya “notisi” na mihadhara yake aliyokuwa akiitoa wakati wa uhai wake na kuandika kitabu ambacho kilibadilisha kabisa mkondo mzima wa taaluma ya Isimu. Historia ina mifano mingi ya watu wa aina hii. Ni vigumu mno kwa kiongozi kufanikiwa kama amezungukwa na “jangwa” kama inavyobainika sasa kwa Mwalimu Nyerere.


Mwalimu Nyerere ataendelea kuenziwa na Watanzania, Waafrika na wapenda amani kokote duniani na juhudi za kundi hili linalojaribu kuzima mawazo yake linapoteza muda wake bure. Pamoja na makosa yake yote na kushindwa kwa sera yake ya msingi ya Ujamaa na Kujitegemea Watanzania wanaendelea kumuenzi na kumheshimu kiongozi huyu kwa msimamo wake na kutotetereka katika kutekeleza kile alichokiamini kwamba kilikuwa na maslahi kwa watu wake. Mwalimu Nyerere alihubiri na kutenda alichokihubiri na karibu kila kitu alichokitenda kilikuwa ni kitu ambacho aliamini kabisa kwamba kilikuwa ni kwa maslahi ya taifa lake changa. Jambo hili linawavutia sana Watanzania hasa wakiangalia maisha yake ya uadilifu aliyoishi – yeye pamoja na familia yake. Ni kwa sababu hii mimi naamini kwamba Nyerere na itikadi yake vitadumu!

Pamoja na “ujangwa” uliopo, wakati sasa umefika wa kumaliza ukiritimba katika hotuba (na vitu vingine ambavyo ni hadhina ya taifa letu). Hotuba za Mwalimu Nyerere siyo mali ya Redio Tanzania, mtu wala shirika au kikundi cha watu bali ni mali yetu sote. Ni wakati sasa wa kuziweka hotuba hizi katika mtandao. Hebu tuwe na tovuti maalumu yenye hotuba zote za viongozi wetu wote kuanzia Mwalimu Nyerere, Rais Mwinyi, Rais Mkapa na rais wetu wa sasa Rais Kikwete. Tovuti hiyo itangazwe na itunzwe vizuri kwani itakuwa mojawapo ya hazina muhimu sana kwetu kama Taifa kwa wakati huu na vizazi vijavyo. Wiki ijayo nitazungumzia kosa kubwa kuliko yote la Mwalimu Nyerere!
Nisome: matondo.blogspot.com

2 comments:

  1. Profesa Matono, nimejitahidi sasa nimeshindwa kanisa. Naomba nifahamishe ikiwa ulipata kifurushi nilichokutumia tafadhali. Nimejaribu kukuandikkia kupitia anwani yako (najua ilikuwa na matatizo kama ulivyonifahamisha), uliahidi kuniandikia lakini sijasikia toka kwako. Nasumbuka na kukosa amani kwa kuwa sifahamu kama niagize nyingine au nilizotuma zilifika. Tafadhali nifahamishe moja nifahamu ili niondokane na 'sifahamu' ambayo inakuwa kero kila ninapokumbuka sasa.

    Samahani kwa kutoka nje ya mada ila sina jinsi nyingine ya kuwasiliana nawe.

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU