NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, December 23, 2011

FIKRA YA IJUMAA: HIVI NI KWA NINI KILA KIONGOZI HUDHANI KUWA ANAPENDWA SANA NA WATU WAKE ?


"Wananipenda. Watakufa ili kunilinda. Watu wangu!"
Muammar Gaddafi (1942 - 2011)

Tumewaona. Wapo. Walikuwepo na Watakuwepo. Tena wamejaa tele katika jalala la Historia.

Hata muda wao wa kutawala ukiisha, utawaona wakihangaika kujaribu kubadili katiba za nchi zao ili waendelee kutawala. Utawasikia wakijigamba:

"Ninapendwa mno! Watu wangu bado wananihitaji. Siwezi kuiacha nchi yangu"

"Macho man" wa Urusi. Naye Anadai Anapendwa Sana!
 • Hata upepo wa mabadiliko unapoanza kuvuma, kama vile mazuzu, watawala hawa wapendwa waliojaa kiburi, dharau, ubilionea na ulevi wa madaraka hushindwa kujitafakari, kujisaili na kusoma alama za nyakati. Na matokeo yake daima huwa ni ya kusikitisha. Wengi wao huishia "kugadafishwa" na wengine hujikuta katika shimo la takataka la Historia kinyume na matarajio yao.
"Simba" wa Syria. Pia anadai anapendwa sana!
 • Kama kuna jambo ambalo hunifurahisha na kunifanya nijisikie vizuri na hata kunifanya nijimwambafai kama Mtanzania ni utaratibu wetu tuliojiwekea wa kubadilishana madaraka kwa njia za amani kila baada ya miaka 10 - tena bila kujali kama wanapendwa ama la. Natumaini kwamba tutauendeleza utaratibu huu. Mwalimu Nyerere alishatuonyesha njia. 
Mungu Ibariki Tanzania !!!  

8 comments:

 1. Najaribu kuwaza kwa sauti labda inawezekana hawa watu hawakuupata ule upendo wa dhati walipokuwa wadogo..ruksa kuwa tofauti.IJUMAA NJEMA KWA WOTE WATAKAOPITA HAPA.

  ReplyDelete
 2. Alizaliwa Sirte huko Libya.


  Akawanufaisha madarakani wanaSirte hasa wale wenye mbegu zake.


  Akakimbilia Sirte kwa wakati wa matatizo.  Akafia Sirte.


  LAKINI AMEZIKWA JANGWANI ASIPOPAJUWA MTU TENA MBALI SANA NA SIRTE !!!  (Afrika Kusini nasi tumewahi kumpata kiongozi wa aina hiyo sitamtaja jina naogopa mahakama...tena baada ya uhuru wetu 1994!)


  Lakini yote hayo ni ujinga tu wa kutupwa; na ndio maana siku Afrika itakapopata muungano wake, makao makuu ya Bara yatakuwa Tanzania. (Ili mradi mnaendelea kushika nidhamu yenu... na Hongereni Sana!)

  ReplyDelete
 3. Sababu ni rahisi kuwa watawala wengi hasa mafisadi , maimla na zandiki huishi kwenye ulimwengu wa ndotoni wakipumbazwa na waramba viatu wao ambao huwatumia kama mataahira. Wakipigiwa makofi kila waendapo kutokana na wananchi kuogopa kuadhibiwa na mashushu wao, hudani wanapendwa.
  Angalia wakorea ya kaskazini juzi walivyoangusha collective wailing kutokana na kifo cha imla wao. Si kwamba rohoni wanampenda. Hata kama wanamponda, watafanyaje iwapo kutokulia ni ishara ya kuasi jambo ambalo vidomodomo wanaojikomba na kufaidika na mabaki ya watawala wataripoti na wahusika watapata cha mtema kuni. Hebu fikiria kwa mfano Tanzania kwa sasa ambapo Kikwete anachukiwa kuliko hata Mkapa. Ukimwambia ukweli huu utaitwa mchochezi hata mhaini. Watawala wa kiswahili huwa hawapendi kuambiwa ukweli na hawana haja ya kuujua kwa vile wanaogopa utawaumbua na kuwaumiza.

  ReplyDelete
 4. Mhango :-)

  Kiswahili chako kitamu nami najifunza msamiati kwako:... "maimla" "warambaviatu"!

  ReplyDelete
 5. Wow! Bwana Phiri duniani ni kujifunza na kufundisha kila uchao. Warambaviatu siyo! Bootlickers tuseme. Merry Xmas and Happy New Year Bro.

  ReplyDelete
 6. Yasinta - Pengine ni kweli watu hawa wana matatizo ya Kisaikolojia na nadharia za akina Sigmund Freud (hasa mambo ya Ego, Super Ego) na wenzake zinaweza kutoa fununu. Wanajiona wao ni wao tu na hakuna mwingine.

  Manyanya - Kama kawaida, mawazo yako ni ya kufikirisha na kuchangamsha sana. Sikujua kama nanyi mmeshapata kiongozi wa aina hiyo kungali mapema hivi katika safari yenu.

  Tanzania mwasisi wetu alikuwa anaona mbali na mambo aliyolifanyia bara la Afrika na hasa wenzetu waliokuwa bado wanapigania uhuru kule Msumbiji, Zimbabwe, Angola na nyinyi huko Kusini ni makubwa sana. Na aliweka msingi imara alipoamua kuachia madaraka ingawa mimi naamini angeendelea tu kama angetaka. Na kwa bahati nzuri mfano wake bado ungali unazingatiwa. Wapambe wa mfuasi wake walipojaribu kuanzisha harakati za kutaka kubadili katiba ili aongezewe muda wa kuwa madarakani, Muasisi alikuwa mkali sana mpaka akamtungia kitabu!

  Mwalimu Mhango: Nakubaliana na maoni yako kuhusu sababu mojawapo ya viongozi hawa kushindwa kufahamu ukweli wa watu wanaowaongoza - kuogopwa na kuzungukwa na walamba viatu .

  Hata hivyo sikubaliani nawe unaposema kwamba eti JK anachukiwa. Anachukiwa na nani? Siye tunaojiita wasomi tuna tabia ya kufanya majumuisho ya "kisomi" bila ya kuangalia uhalisia wa mambo. Pengine JK anachukiwa na wasomi na wanaharakati. Kwa mfano ukitazama cheche zinazotemwa kule kwa ma-"Great Thinkers" unaweza hata kumhurumia. Lakini je, nani ameshakwenda vijijini na kusikia maoni ya wakazi wa huko (ambao ndiyo wengi?). Na hapa ndipo wasomi tunapokwama. Tunaendesha kura za maoni na kupanga mipango yetu bila kuzingatia wala kuwashirikisha wakazi wa kijijini. Halafu mambo yasipokwenda sawa, tunaanza kulalamika na kumtafuta mchawi.

  Manyanya tena - Mhango ni mtaalamu wa lugha huyo humuwezi. Kifaransa anakitema kuliko hata Wafaransa wenyewe. Kimombo chake ni kama cha Malkia. Kiswahili chake ndicho hiki unachokisifia hapa. Kila mtu na talanta yake bwana - hasa kama talanta hiyo haijafukiwa ardhini!

  Manyanya - Mbona hata wewe unafahamu lugha kibao? - Kiswahili, Kiingereza, Kiafrikana (Kikaburu?), Kizulu...Ongezea zingine. Na kwa jinsi unavyokitumia Kiswahili chako fasaha hapa (japo unadai eti kinakubabaisha kidogo), nadhani u bingwa kabisa kabisa katika lugha hizo unazozifahamu sawasawa....

  ReplyDelete
 7. Mwalimu Matondo hayo maujiko uliyonipa ni zaidi ya saizi yangu-najua kidogo kuliko hicho ulichosema kaka. Wewe ndiye gwiji na nguli ya lugha hasa kiswahili-siyo mimi mwanagezi. Tuyaache na kuombeana uzima mwaka huu unaoanza. Phiri naye si haba ni mtaalamizi wa lugha.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU