NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, December 30, 2011

FIKRA YA IJUMAA: KARMA (TENDA WEMA NA USIENDE ZAKO ???)

Wakati mwingine umsaidiaye ndiye mwokozi wako, tena wa papo kwa papo. Hebu soma tukio hili fupi kwa makini kama una muda.
**************
 • Bwana Victor Giesbrecht (61) na mkewe Ann walikuwa safarini kutoka Winnipeg Canada kwenda katika jimbo la Indiana nchini Marekani. Walipokuwa wanapita katika jimbo la Wisconsin, waliona gari lililokuwa limepata pancha kando ya barabara. Wanawake wawili (Sara Berg na Lisa Meie) walikuwa nje ya gari lililokuwa limepata pancha huku wakiwa hawajui la kufanya. Bwana Victor ndiye alikuwa anaendesha; na kutokana na wema na ubinadamu wake aliamua kuacha safari na kwenda kuwasaidia wale wanawake kubadilisha tairi.
 • Baada ya kufanikiwa kubadilisha tairi, Bwana Victor na mkewe waliendelea na safari yao. Waliendesha kidogo tu na ghafla Bwana Victor alipatwa na mshtuko wa moyo na kupoteza fahamu. Mkewe alipatwa na kiwewe, na baada ya kupiga simu ya dharura (911) alibakia akihangaika tu akiwa hajui cha kufanya.
 • Kwa bahati nzuri wakati akihangaika, wanawake wawili walifika na mmoja alikuwa ni nesi na anayefahamu vyema kupambana na dharura za kiafya kama hii ya mshtuko wa moyo. Mara moja mwanamke yule alianza kumpa huduma ya kwanza Bwana Victor kwa kumpulizia pumzi kinywani na kuminya kifua chake ili kujaribu “kuufufua” moyo wake uliokuwa umezimika.
 • Aliendelea kufanya hivyo mpaka wataalamu wa mambo ya dharura walipofika. Bwana Victor alichukuliwa kwenda hospitalini ambako alikaa kwa wiki moja na baadaye kuruhusiwa kuondoka. Yule mwanamke aliyempa matibabu ya dharura katika zile dakika za mwanzo kabla ya wataalamu wenyewe kufika ndiye alikuwa ameokoa maisha ya Victor kwa kuzuia moyo wake “usife” kabisa.
 • Cha ajabu ni kwamba  mwanamke huyu shujaa mwokozi alikuwa ni  Sarah Berg - mwanamke yule yule ambaye dakika chache tu huko nyuma alikuwa amepata pancha na Victor akamsaidia kubadilisha tairi lake. Baada ya mambo kutulia na wahusika wote kutambua lililokuwa limetokea kila mmoja alimshukuru mwenzake kwa wema aliokuwa amemtendea.
Bwana Victor akiwa hospitalini
 • Tukio hili limeacha gumzo kubwa huku wengine wakisema ni muujiza na wengine wakisema ni kanuni ya Karma tu inafanya kazi: Kila tendo tulitendalo hapa duniani hutuathiri kwa namna moja ama nyingine – jema kwa wema, na baya kwa ubaya. Na wakati mwingine athari zenyewe zinaweza kuwa za papo kwa papo kama ilivyotokea kwa Victor.

 • Matendo kama haya ni ya kutia moyo sana na yanauonyesha ubinadamu wa binadamu kwa uangavu wa kutosha hata katika kipindi hiki ambapo binadamu analaumiwa kuwa ameupoteza ubinadamu wake na kutawaiwa na ubinafsi na uchoyo. Ndiyo maana hata mimi sijausahau wema niliofanyiwa na mzee mmoja mwenye kibaraghashia na kandambili za bluu miaka 18 iliyopita nilipokuwa nimelazwa katika hospitali ya Muhimbili.  
 • Kisa hiki chenye mafunzo tele kinapatikana HAPA. Unaweza kutazama video ya kisa hiki HAPA. Unaweza pia kusoma kipengele cha UBINADAMU katika blogu yangu HAPA.
****************
Wikiendi njema wadau.

Hebu basi kutenda wema na likawe
 azimio letu mojawapo katika 
mwaka mpya ujao (2012) !!!


****************

3 comments:

 1. Ni tafakario ya kufikirisha kweli..kweli hapa ilikuwa tenda wema kwa akutendeaye si tenda wema na uende zake kama tulivyozoea. ijumaa njema kwa wote watakaopita hapa na mwaka mpya pia.

  ReplyDelete
 2. @MMN

  Vituko (labda ni "karma") kama hivyo ndivyo nami ninaokabiliana navyo katika ka post yangu ya sasa.

  Nauliza Mungu yupo? Na kama yupo, je yupo kwa ajili ya wake wachache tu? Je mtu ajiwekeje ila naye afaidi baraka zaMungu akiwa hai hapahapa duniani bila y akulazimishwa kwenda msikitini au kanisani?

  Soma tafadhali hapa http://ninaewapenda.blogspot.com/2011/12/little-i-know-about-royal-mysteries.html

  ReplyDelete
 3. Amina mkuu....hii ni fumbua macho japo wengine watasema ni 'coincidence' tu!!!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU