NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, December 20, 2011

HILI NALO NENO: ETI BABU WA LOLIONDO KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UTAPELI

 • Eti babu wa Loliondo anafunguliwa kesi za jinai na madai. Anafunguliwa kesi ya jinai kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kwamba eti aliwahadaa watu kwamba dawa yake inatibu wakati hakuna mtumiaji aliyepona. 
 • Pia anafunguliwa kesi ya madai ili aweze kulipa fidia za watu waliopoteza maisha na wote waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali huku wakitumia gharama kubwa ili kupata dawa isiyotibu.
Lakini je:
 • Vipi kuhusu mawaziri na vigogo wa serikali waliokuwa wakimiminika Loliondo huku wakiifagilia dawa hiyo kwamba ilikuwa imewasaidia na hivyo kuendelea kuchochea moto wa tiba hiyo?  Hawahusiki kwa namna yo yote na "utapeli" huu?
 • Maswali ya kujiuliza katika suala hili ni mengi na yote yanaonyesha jinsi tunavyoendesha mambo yetu kama jamii. Hatuko makini, hakuna uwajibikaji na mambo yetu mengi - hata yale ya muhimu kabisa - tunayafanya kimzahamzaha tu. Kama anavyosema mhusika mmoja katika vibonzo vya Pogo, adui wa maendeleo yetu si mwingine bali ni sisi wenyewe!
 • Jikumbushe habari mbalimbali kuhusu Babu wa Loliondo na "tiba" yake ya kimiujiza HAPA.

6 comments:

 1. Karibu tena Mkuu!


  KESI YA KICHEKESHO HIYO!


  Kuhusu jambo hili naomba niseme: mahakamani unaweza kufikisha jambo lolote lile, hata la kijinga kabisa. Kwa maoni yangu nikiwa mbali hili jambo ni mojawake.


  Labda tuchunguze zaidi: hao wanasheria wenye kumshughulikia wameamriwa (INSTRUCTED) na nani? Ukipata jibu la undani ndipo utaupata utamu wa habari hizi.

  Na kweli, Mwaka 2012 unaahidi vichekesho vyake, siyo?
  MSIMAMO WA SEREKALI JE?


  Kwa upande mwingine, ikiwa hatua hizi zimechukuliwa na serikali, basi ninafikiri haitakuwa na nia ya kumpa Babu-Kikombe hiyo miaka saba, wala kumlipisha hela zozote zile ingawaje kifungo (SENTENCE) kama sheria ya kubali, anaweza kabisa kupata kama amepatikana na hatia.


  Lengo la serikali (na nahisi ni lengo zuri sana kama itakuwa kweli ni serikali ikiwa inakwenda jinsi ninavyowaza) NI KUSAHIHISHA SHERIA ZA AWALI KUHUSU WAGANGA WA KIENYEJI ILI KUWAEPUSHA WANANCHI NA DIMBWI LA MATAPELI. Yaani Babu-Kikombe anatumika vile kama chombo cha kubadili sheria tu.


  Kuhusu vigogo wa serikali waliepata kunywa kikombe cha babu, mbona vigogo vyenyewe havikwenda huko Loliondo kama serikali bali kama Watanzania watu binafsi sawasawa na mgonjwa yoyote yule mwingine. Nasema kutakuwa na vichekesho ikiwa kesi hii imeanzishwa na ndugu wa wagonjwa wasiepona. Mbona hata Raisi wa Korea amekufa? Sasa daktari wake naye apelekwe mahakamani kwa kushindwa kuokoa maisha yake? Upuuzi tu!!!

  ReplyDelete
 2. Huyu babu na utawala mzima wa Tanzania ni matapeli wa kutupwa. Hata hivyo babu mwenyewe hayuko peke yake. Wapo akina Kakobe, Rwakatare, Gamanywa, mzee wa Upako, Mwakasege,, Halifa Khamis na wengine wengi wadogo na wakubwa. Kimsingi nchi yetu imegeuzwa shamba la bibi kwa kila tapeli kuja kuchuma. Nasikia kwa sasa Sinza imefurika mbwamwitu toka Nigeria. Hata hivyo kuna haja ya kuwaambia ukweli watu wetu kuwa waache kufikiri kuukata bila kutoa jasho.

  ReplyDelete
 3. @ N.N. Mhango


  Na kwakupitia mwenye kibaraza hiki naomba ruhusa kusema


  Heshima yako, Bwana Mhango!


  Umenichekesha lakini pia ukanivua kofia ili nikupe heshima yako jinsi unavyowaamsha Watanzania wenzetu... Mungu akubariki sana.


  Naishia kwa kukunukuu pale uliponikuna hasa msemo "kuukata bila kutoa jasho":
  “Huyu babu na utawala...ni matapeli wa kutupwa.....nchi yetu imegeuzwa shamba la bibi kwa kila tapeli kuja kuchuma. Nasikia kwa sasa Sinza imefurika mbwamwitu toka Nigeria. Hata hivyo kuna haja ya kuwaambia ukweli watu wetu kuwa waache kufikiri kuukata bila kutoa jasho.”

  ReplyDelete
 4. Bwana Goodman Manyanya Phiri,
  Habari za Sauzi? Nimefarijika kugundua kuwa kumbe mchango wangu licha ya kufikirisha unachekesha na kuchangamsha.
  Leo sichongi sana. Nakukaribisha kibarazani kwangu. Kila ukipata wasaa pita uache unyayo kama ulivyofanya hapa kwa ndugu yangu Ngw'ana Matondo.
  Nimalizie kwa kuomba usome The African Executive Magazine la leo uone Tanzania inavyotawaliwa na viumbe wa aina mbili yaani Mapanya na Matonya.

  ReplyDelete
 5. Maoni yenu Mwalimu Mhango na Kamanda Manyanya yamegusa kotekote. Kuna jambo ambalo haliko sawa katika jamii yetu. Kulikuwa na watoa vikombe zaidi ya 10 - wengine wakidai wameoteshwa na Mungu, wengine na ndugu zao waliokufa n.k. Sasa hivi wala hatuwasikii tena.

  Kwa upande mwingine kuna hawa manabii (wa kike na kiume) wanaoibuka kila leo. Hivi unabii unapatikanaje? Unausomea? Unaoteshwa na Mungu/Mizimu? Na kazi ya Nabii ni nini hasa? Manabii wa kwenye Biblia walikuwa wanafanya kazi nzuri sana ya kuwaonya wana wa Israeli kila walipopotoka. Na hata baada ya kuzaliwa kwa Yesu walikuwa na kazi muhimu ya kuonya kuhusu maovu na adhabu na majanga vilivyokuwa vikija. Leo hii kila mtu - kama vile hawa watoa vikombe - anaweza kuibuka na kudai kuwa ni nabii.

  Jambo linalotatiza zaidi - na hili ni la kuogofya- ni jinsi kila nabii anavyojipatia umaarufu, wafuasi wengi na mwishowe umilionea wa papo kwa papo. Dini sasa imegeuzwa biashara. Ndiyo maana mimi sikushangaa sana ilipobainika kwamba baadhi ya manabii na maaskofu wetu hawa walikuwa wanajitajirisha kwa kutumia madawa ya kulevya. Na wengi wao wanatuhumiwa kutenda "unabii" wao kwa kutumia nguvu za giza - hirizi na pete kutoka Naijeria. Ndiyo maana wengi wao ni watu wa kuogopwa sana na wanaabudiwa makanisani mwao kiasi kwamba hata wakisafiri mtu mwingine haruhusiwi kupanda mimbarini na kuhubiri. Badala yake kanisa inabidi lisikilize kanda zake. Mtu unabaki ukijiuliza, siku watakapokufa itakuwaje?

  Nilicheka sana juzi hapa baada ya kumsoma "nabii" mmoja akitamba kwamba yeye ndiye alimuua Sheikh Yahaya Hussein kwa vile hakumsikiliza na kutii masharti aliyokuwa amempa. Kama hii ni kweli basi inatisha.

  Ukristo umevamiwa na pengine hizi ndizo zile nyakati za maonyo tuliyopewa katika Kitabu cha Ufunuo "Kila Mtu na Ashike Sana Alichonacho!"

  ReplyDelete
 6. Eh, mbona ni watu wa ajabu hivyo? Mna uwezo kupita kiasi. Nilikuwa wapi siku zote nimeacha kutembelea blogu hii. Ni tumaini langu kuona kwamba kuna shushwa habari za maana na zenye ukweli kwa kufuata chambuzi mablimbali kutoka kwa Watanzania mbalimbali kama nyingi. Ajabu iliyoje!

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU