NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, December 29, 2011

HILI NALO NENO: ETI UFAULU WA KISWAHILI UMESHUKA ZAIDI UKILINGANISHWA NA ULE WA KIINGEREZA KWA WATAHINIWA WA DARASA LA SABA.

Ni wazi kwamba Kiingereaza kimeshatushinda, lakini je, hata Kiswahili nacho kinakaribia kutushinda? Lugha ya kufundishia ni nguzo muhimu katika mfumo wo wote ule wa elimu na kusema kweli bila kuwa na sera thabiti ya lugha ya kufundishia, elimu hugeuka na kuwa kama mchezo tu. Ni lini tutafanya marekebisho yanayotakiwa na kuhitajika sana katika sera yetu ya lugha ya kufundishia?
***********

Ni Aibu kwa Wanafunzi wa Tanzania Kufeli Kiswahili
(Ijumaa, 23/12/ 2011) 

HIVI karibuni tumesikia kuwa ufaulu katika somo la Kiswahili kwa matokeo ya darasa la saba mwaka huu, umeshuka ukilinganisha na  ufaulu wa somo  Kiingereza.

Hali hiyo inaweza kuwashangaza watu wengi waliopo nchini kwa wanafunzi kushindwa kumudu lugha yao ya taifa. 

Hasa kwakuwa  inafahamika wazi kuwa Kiswahili ndiyo lugha inayotumika kama  lugha ya mawasiliano kwa mwanafunzi  kwa ngazi ya shule ya msingi kwa kipindi chote cha  masomo kwa miaka saba, wakati Kiingereza kinafundishwa kama somo tu.

Kwa kiasi kikubwa, Watanzania wanaweza kuzungumza Kiswahili fasaha, lakini akiingia darasani kufanyia mtihani anaweza kufeli vibaya hata ukimshindanisha na mtu ambaye ni lugha yake ya tatu au ya kujifunza.

Waswahili husema “mdhaarau mwiba mguu huota tende,  hayo ndiyo tunayoyaona sasa katika kiwango cha ufaulu katika somo la Kiswahili. Lakini katika ngazi ya elimu ya msingi na shule za upili Kiswahili hutumika, ili kukidhi mahitaji ya mwanafunzi katika kumjenga ili kuwa na msingi mzuri katika kufahamu vyema lugha yake.

Tukiwa tunatafakari katika matokeo hayo, yapo mambo kadhaa yanayopaswa  kutazamwa na kuchukuliwa hatua ili kuepuka fedheha kwa wanafunzi kufeli somo hilo.

Hata hivyo kwa upande wa wanafunzi wa ngazi za juu ya elimu ya chuo kikuu na vyuo huwa, na rejesta zao mojawapo ni kukiona Kiswahili kuwa kigumu.

Hata hivyo usemi huo unaweza ukawa na athari chanya iwapo watu watachukua hatua kukabiliana na changamoto hiyo kwa  kubaini ugumu kwake uko wapi na kushirikiana na wenzake katika kupitia mada zinazomsumbua ama asizozielewa vyema kwa msaada zaidi, ikiwa ni pamoja na kupitia maandiko mbalimbali ya wataalamu wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.

Vilevile  wanafunzi wa shule za msingi wanapaswa kazingatia masomo na kwa kupunguza michezo na soga pamoja na mambo yasiyo na tija pamoja na kutafuta muda wa ziada kujisomea kwa bidii ili kuyatafutia ufumbuzi yale ambayo hayakueleweka vyema wakati wa vipindi vya darasani.

Upande wa walimu wanapaswa kuendelea kufundisha somo la Kiswahili kitaaluma zaidi kuliko kufundisha kwa mazoea na kurahisisha mbinu za kufundishia kwa wanafunzi hao.

Ushirikiano huo  wa walimu na wanafunzi ukiwa thabiti na kila mtu akatekeleza majukumu yake, hakuna sababu ya mwanafunzi kufeli  somo la Kiswahili katika  ngazi zote. 

Hii ni kutokana na mambo mengi yanayoelezwa katika lugha hiyo yanahusu mazingira yaliyo karibu na mwanafunzi. Hata hadithi zinazoelezewa  na watunzi wa vitabu ni kutoka mazingira hayo ambapo makabila ya Watanzania ni wazungumzaji wakubwa wa lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wa mwenendo wa kuendelea kushuka kwa ufaulu wa mwanafunzi nchini si jambo la kuachwa kwani hiyo inadhihirisha kwamba jamii ya Watanzania hawafahamu mambo mengi katika lugha yao licha ya kuzungumza kila wakati.

Kwa hali hiyo ningetegemea kuona somo la Kiswahili linakuwa la kwanza katika ufaulu wa masomo mengine licha ya kuwa masomo mengine  nayo yanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili kwa ngazi zote kinakofundishwa.

Ipo haja ya kubaini chanzo cha wanafunzi hao kutofanya vyema katika somo hilo ikiwa ni njia ya kuelekea kupata ufumbuzi wa moja kwa moja. Lakini chanzo moja wapo ni    wanafunzi kutofahamu sarufi ya lugha yao ya  Kiswahili. Kwani  sarufi katika lugha yoyote ndiyo uti wa mgongo wa lugha hiyo.

Kuwa na walimu wenye uzalendo na waliopikwa katika kufundisha somo la  Kiswahili hilo, watumike ipasavyo katika maeneo yenye uhaba na si mwalimu yeyote anayezungumza lugha hiyo apewe nafasi ya kufundisha Kiswahili. Hilo linaweza kuwa na tija katika kuleta maendeleo ya kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Jambo lingine la kuzingatia ni kuimarisha kwa kiwango cha zana za kufundishia. Huku baadhi ya walimu wamekuwa hawazingatii hilo kwa wa kwa kuona kuwa ni kupoteza muda na gharama, wakati hata zipo njia mbalimbali za kuunda zana hizo bila gharama yeyote.

Aidha katika kukabiliana na changamoto hiyo ya kuendelea kushuka kwa kiwango cha Kiswahili, pia walimu wa Kiswahili kwa umoja wao wanapaswa kuliangalia katika umoja wao walimu wa Kiswahili kwa ngazi mbalimbali.

Tunapojiandaa kuingia mwaka mpya, natumaini wanafunzi wataendelea kujizatiti ili kuhakikisha kuwa wanafanya vyema katika mitihani yao ya Kiswahili kwa mwaka unaokuja.
Walimu ambao ndiyo walezi wakuu wa wanafunzi hao, nao wanapaswa kuangalia njia nzuri za kuondokana na aibu hii ya kila mwaka kuendelea  kushuka kwa ufaulu wa somo la Kiswahili.

Njia pekee ni kuwa na mipango endelevu inayoakisi maendeleo ya Kiswahili katika kukikuza na kukieneza.

Baraza la Kiswahili nchini kwa kushirikiana na taasisi za lugha ya Kiswahili nchini nalo linapaswa kutoa mchango wake kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla ili kukifikisha Kiswahili katika hadhi na kukitangaza nje ya Tanzania.

Mathalani, kuwapo na ushirikiano baina ya walimu wa Kiswahili na watendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa, kutaleta tija katika kusukuma gurudumu  la maendeleo nchini.

Chanzo: Mwananchi

2 comments:

 1. Sijui kiswahili ni kigumu! Mimi nifaulu masomo yote ya kiswahili na kiingereza, japo kiingereza nilifanya vizuri zaidi kuliko kiswahili.
  Makala yangu ya leo, nilikuwa pia nazungumzia elimu ya shule za msingi na sekondari kwa uingereza, ambapo ni aibu tupu kuona vijana wengi wa Uingereza wanamaliza shule bila kujua kusoma wala kuandika kiingereza.

  Kamua hii http://ebchib.blogspot.com/2011/12/kiwango-cha-elimu-jijini-london.html

  ReplyDelete
 2. "Kwa kiasi kikubwa, Watanzania wanaweza kuzungumza Kiswahili fasaha, lakini akiingia darasani kufanyia mtihani anaweza kufeli vibaya hata ukimshindanisha na mtu ambaye ni lugha yake ya tatu au ya kujifunza."


  HAPO NILIKUWA NA NUKUU, MKUU.
  Na asante kwa hoja ya leo!

  Nataka niulize suali huenda linaweza kuchangia katika kupata jawabu.


  Je, siyo kwamba labda Baraza la mitihani ndilo lenye matatizo badala ya wanafunzi?

  Je chapisho la mwisho la kamusi ya Kiswahili lilikuwa mwaka gani? Au ni zaidi ya miaka mingapi sasa chapisho jipya ni hadimu?

  Wao kama Baraza la Mitihani wanachangia kiasi gani katika toleo hadi toleo la kamusi ya Kiswahili ili mwanafunzi aelewe kabisa "STANDARD AND MODERN KISWAHILI" anapokuwa darasani juu ya mitihani yake?

  Kama Baraza la Mitihani, wao wanachangia kiasi gani kupiga marufuku viingereza katika vyombo vya habari vyenye lengo la matumizi ya Kiswahili?

  Mimi nafikiri kazi yao ikiwa ni moja tu, yaani kuwanyemelea wanafunzi kwa mitihani ya Kiswahili mwisho wa mwaka nayo inaweza ikachangia katika tatizo tunalozungumzia leo.

  Lazima tu, ningependekeza mimi, wapewe mamlaka zaidi nao wapanuke pia na kama ndilo suluhisho la msingi, ipanuliwe hata katiba yao ili iwawezeshe kukemea viswahili vibaya katika jamii rasmi kama redio na televisheni.


  Mimi siMtanzania wala siishi Tanzania, lakini niliwahi kuchungulia na sidhani tofauti itakuwa kubwa katika Baraza la Mitihani Tanzania na Baraza hilohilo Afrika Kusini.

  Sambamba na maelezo hayo, niruhusu, Mkuu MMN, niseme hapa kwetu Afrika Kusini nimejifunza sana na ubabe waMswahili akipewa naye pengo na uadhifa ajionyeshe na kujigamba mulemule na lugha yake dhidhi ya lugha za Wakoloni kama Kiingereza.


  Tatizo lake Mswahili huyo akiwa katika Baraza la Mtihani wa Kizulu (ambacho ni lugha niliejifunza tangu siku yangu ya kuzaliwa) ANATAKA AJIONYESHE HUO UBABE WAKE KWA KUTUNGA MITIHANI MIGUMU NAKUTAKA WANAFUNZI WAELEWE ULE MSAMIATI UNAETUMIKA KWA WAANDISHI WA VITABU KAMA VYA KUBUNI VILE!


  Naam, tumekumbwa na tatizo hilohilo hata hapa Bondeni. Unafungua redio ya Kizulu unachefuka tu kwani kiu yako yakusikiliza Kiswahili, yaani unyonye tena ziwa la mama yako, kiu yenyewe itazimwa na huyo bwana mtangazaji nusu saa akitumia Kiingereza hicho-hicho uliekikimbia kutoka idhaa ya BBC na Kiingereza chake bwana mtangazaji ni uchwara tu!


  Wanafunzi wanamsikiliza kila siku bwana mtangazaji anavyoongea lugha yake mchanganyiko kwa jina la "Kiswahii" na hamna Baraza lenye kukemea.

  Unafika wakati mwanafunzi anaamua "kumbe kujifunza lugha ya Kiswahili sanifu ni mateso tu ya bure mbona watangazaji wa Kiswahili hawatumii Kiswahili"

  Wanafunzi wanaona ni safi sana kuelewa Kiswahili/Kizulu nusu ili mradi "nikifaulu mitihani yake tu pale chuoni"!


  Tunahitaji kupata suluhisho la dharura, kwani mtu ni kwao hata ukienda popote pale duniani!

  Na Kiswahili chako ukiwa kwenu au ugenini ndio salamu yako la sivyo unageuka popo hata wale wageni unaetaka kuwaburudhisha kwa ufasaha wako katika lugha yao huku ukidharau Kiswahili chako wanakuona kimoyomoyo wewe ni mpumbavu(usiwaone kucheka nawe: jino pembe!)

  Pili kadiri tunavyopoteza muda wa kupata suluhisho la matatizo haya, ndipo hali ya siasa na uchumi itakavyodhoofika zaidi Afrika, kwani lugha ya taifa ni nguzo kubwa ya umoja.

  (kumradhi kama nimekosea Kiswahili!)

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU