NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, January 31, 2011

"HUKU MJINI UTATUSUMBUA KUSAFIRISHA MAITI YAKO !"

KUMBE MH. ROSTAM AZIZ NDIYE ATALIPWA MABILIONI YA DOWANS !?!?!??

Picha kutoka gazeti la The East African
  • Nimeisoma hii habari katika gazeti la The East African kwa mshangao na mshtuko kidogo kwani huko mbele Mheshimiwa Rostam Aziz aliwahi kukana kwamba hahusiki kwa namna yo yote ile na kampuni ya Dowans (na mzaziwe Richmond), na hata majina ya wamiliki wake yalipotajwa, jina lake halikuwemo. Kumbe ndiye anatakiwa kulipwa haya mabilioni ya walipa kodi na yeye ndiyo atayawasilisha huko kwa wenzake. Mungu Aibariki Tanzania !!!
Kutoka blogu ya Said Michael.

Saturday, January 29, 2011

SHULE ZA KATA ZINAHITAJI MSAADA WA HARAKA !!!

  • Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne (Tazama pia HAPA) yaliyotolewa juzi yanasikitisha. Yanasikitisha kwa sababu, mbali na kuonyesha kwamba kiwango cha kufaulu kimepungua kwa asilimia 22, matokeo hayo yanaonyesha kwamba shule za serikali ndizo zimeongoza kwa kuboronga. Ni kwa sababu hii wasomi na wadau wengine wa elimu, wametoa kauli na kusema kwamba matokeo haya ni janga la kitaifa!
  • Na katika shule hizi za serikali zilizoboronga, shule za kata (mimi huziita majengo ya kata kwani nyingi hazina hata sifa ya kuitwa shule) ndizo zimeongoza kwa kuboronga zaidi. Nimeangalia shule za kata za nyumbani kule Wilayani Bariadi na kusikitika sana. Katika shule nyingi, hakuna mtahiniwa hata mmoja aliyepata daraja la kwanza, la pili na wakati mwingine hata la tatu. Unakuta watahiniwa wachache wamepata daraja la nne, na waliobaki wameambulia "FAILED"
  • Hali hii inaonyesha mambo mawili: Kwanza wanafunzi wa shule za binafsi (ambazo ni ghali sana kwa Mtanzania wa kawaida) ndiyo wamefanya vizuri. Pili - shule za serikali zilizoko mijini zimefanya vizuri ikilinganishwa na nyenzake zilizoko vijijini.  Kwa hivyo, watoto wa masikini - na hasa wale wanaoishi vijijini (ambako ndiko kuna wakazi wengi) ndiyo wanazidi kuachwa nyuma kielimu na kuendelea kuwa tabaka la kudumu la kilalahoi.
  • Hali hii nayo inaibua maswali mengine mazito zaidi. Matabaka haya tunayoyapalilia na kuyaengaenga kwa wakati huu yatakuwa na madhara gani huko mbele ya safari? Kwa kuwanyima elimu bora hawa watoto wa masikini ambao ndio wengi, tunajenga jamii ya aina gani?
  • Ni nani hasa anayetoa amri ya shule hizi za kata kufunguliwa na kuanza kupokea wanafunzi wakati inajulikana wazi kwamba hazina walimu, vitabu, nyumba za waalimu, maabara na vifaa vingine vya muhimu? Naamini mtoa amri huyu (ambaye pia aliniathiri mimi mwenyewe), watoto wake si ajabu wanasoma shule za Kimataifa ndani au nje ya nchi. Ati, kulikuwa na mkakati wo wote kuhakikisha kwamba shule hizi za kata zinapatiwa waalimu na vifaa vya kutosha kabla hazijafunguliwa? Inasikitisha sana kwani hapa tunaongelea maisha ya vijana wetu walio wengi - vijana ambao inaonekana kama vile jamii haiwataki na inawapiga teke na kuwafukuzia mbali. Kuna hata anayejua wanakwenda wapi? Kwa mtindo huu, kwa hakika tunakoelekea zi kuzuri kwani hawa masikini siku wakiamka na kuanza kukariri yale maneno ya Azimio la Arusha..."tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyanyaswa kiasi cha kutosha, tumedharauliwa kiasi cha kutosha...na sasa basi...", hata hawa wafanya maamuzi wanaosomesha watoto wao katika "akademi" za kimataifa hawatakaa wafaidi matunda ya elimu ya watoto wao pendelewa. Na kama hatuwekezi katika elimu, basi tujiandaeni kuwekeza katika magereza!
  • Ni taifa gani linalokaa na kukenua meno huku zaidi ya nusu ya vijana wake wakishindwa kuendelea na elimu ya juu - huku likiwa limekazana kuilipa mabilioni ya pesa  kampuni tata ya kifisadi? Kweli tuko siriazi na maendeleo yetu kama taifa????
  • Ni wakati sasa wa kukaa chini na kufanya upembuzi yakinifu ni kwa nini elimu yetu inazidi kudorora. Kwa vile hatuwezi kuendelea bila kuwa na elimu bora, nguvu zetu zote inabidi tuzielekeze katika kuwapatia elimu bora vijana wetu wote. Badala ya kuilipa Dowans (na upuuzi mwingine), pengine ni vizuri tukazitumia pesa hizo kwa kuanzisha programu maalumu kwa ajili ya walimu watakaokwenda kufundisha katika hizi shule za kata vijijini. Tuwape posho maalumu, tuwajengee nyumba nzuri za kuishi na kuwapatia vifaa ili wachape kazi.

  • Wazazi pia tuhakikishe kwamba watoto wetu wanasoma katika shule zenye angalau mahitaji ya msingi. Inabidi tufike mahali tusimame na kuhakikisha kwamba watoto wetu hawaendi kusoma katika majengo haya ambayo kimsingi yanawaandaa kupata hizi "FAILED!". Inabidi tuwe tayari hata sisi wenyewe kujinyima na kuchangishana; na kuhakikisha kwamba angalau watoto wetu wana vitabu au madawati. Ni wakati wa kuamka na kuwa siriazi na elimu ya watoto wetu!!!

  • Na kwa upande wa serikali, ni vizuri ianzishe mikakati maalumu ya kuzisaidia shule za kata na mahali pa kuanzia ni katika upendeleo katika mgao wa walimu. Elimu ni suala nyeti mno na halipaswi kutazamwa kama suala la kisiasa. Hili ni suala la uhai wa taifa letu!

Wednesday, January 26, 2011

MTOTO UMLEAVYO......



Hii niliiona kwa Dr. Phil. Wazazi kazi tunayo !

Monday, January 24, 2011

WACHAGA WABAKI JINA TU. WENGI HAWAJUI MILA NA DESTURI ZAO !!!

  • Shemeji zangu Wachaga eti wamebakia jina tu. Wengi hawajui Kichaga - hata kile cha "kuombea maji".
  • Kati ya watoto 10, ni wawili tu wanaoweza kuongea Kichaga vizuri. Watatu wanaweza kuongea maneno machache tu na waliobaki hawawezi kabisa. Na wote hawa ni watoto wanaokaa vijijini.
  • Hali hii ikiendelea kwa muda mrefu, Kichaga kinaweza kuwa katika hatihati ya kutoweka. Vipi kuhusu lugha na tamaduni za makabila mengine? Swali lilishawahi kuulizwa hapa kwamba, watoto wanapokoma kuongea lugha zao za mama, wanakuwa nani? Ati, inawezekanaje mtu uitwe Mchaga wakati hujui lugha wala utamaduni wa Kichaga? Wachaga mnasemaje kuhusu suala hili? Pengine itabidi angalau msome hiki kitabu kizuri kilichoandikwa na Mangi Petro Itoshi Marealle. Habari kamili inafuata hapa chini.
 ***************

Wachaga wabaki jina, wengi hawajui mila na desturi zao


‘Shimbonyi’ ni salamu kwa kabila la wachaga, salamu ambayo imekuwa maarufu hata kwa  baadhi ya watu ambao sio wa kabila hilo, lililopo mkoani Kilimanjaro.

Lakini kinachoonekana kama dalili za kupotea kwa kwa lugha ya kichaga ni jinsi watoto wa kabila hilo ambavyo wameshindwa kuitumia lugha hiyo kutokana na kushindwa kuzungumza kichaga.

Iwapo utatembelea maeneo ya Marangu, Kibosho, Machame na sehemu nyingine za uchagani,  utashangaa kuona watoto wengi wa kichaga  hawaongei lugha yao ya asili.

Kati ya  watoto 10 ni wawili tu wanaoweza kuongea vizuri kichaga, watatu wanaweza kusema maneno machache na waliosalia hawawezi kabisa kukiongea.

Ukiwauliza wazee wa kabila huwezi kupata jibu sahihi la tatizo hilo, hivyo kupata ukweli wa mambo ni lazima kuangaliwe historia ya kabila hilo japo kidogo.

Inasemekana kuwa wachaga walifika Kilimanjaro karibu miaka 500 iliyopita wakitokea maeneo ya Afrika Magharibi kwenye pembe za Mto Niger.  Kutoka kwao huko inasemekana kulitokana na ugomvi wa kikabila ambao uliwalazimisha kuhamia maeneo yaliyokaribu na mto Kongo uliopo Afrika ya Kati eneo ambalo vitabu vingi vya historia hulichukulia kama ndio chimbuko halisi la wachaga.

Hali ya hewa kwenye bonde la mto Kongo haikuwa nzuri,  hivyo iliwalazimu tena kuondoka mpaka eneo lililoko chini ya milima ya Upare na Usambaa


Hapa walikutana na Wamasai ambao kiasili walikuwa ni wapiganaji vita, hao walikuwa wakilitumia eneo la uwanda mpana  kama malisho ya ng’ombe zao. Baada ya mapambano ya mara kwa mara,  jamii ya wachaga ililazimika kuondoka kwa makundi huku kila kundi likichukua njia yake.

Endelea kusoma habari hii ya kusisimua HAPA.

DOWANS KUHATARISHA UHALALI WA SERIKALI - MB. DAVID KAFULIRA

Hivi hii Dowans ni nini hasa mpaka iyumbishe nchi namna hii?
Kwa nini watu wako tayari hata kuona serikali, nchi na hata madaraka yao vikiyumba kwa ajili ya hii Dowans? Kwa nini?

*********************

"Kama watalipa faster faster (haraka) watakuwa wameongeza upana wa hoja yangu, badala ya kuliomba bunge kumpigia kura Ngeleja ya kujiuzulu, nitaliomba bunge kadri litakavyoona inafaa, lipige kura ya kutokuwa na imani na serikali," alisema David Kafulil

Na Tumaini Makene 
(Blogu ya Majira)

SAKATA la Kampuni tata ya Dowans bado tete na bichi sasa imeelezwa kuwa kama halitafanyiwa kazi kwa umakini litaipotezea serikali uhalali wa kisiasa wa kuongoza wananchi walioiweka madarakani.

Iwapo serikali itafikia uamuzi wa kuilipa mabilioni ya fedha kampuni hiyo bila ukweli kuwekwa bayana ili kuondoa 'mazonge mazonge' yanayolizunguka sakata hilo, utakuwa uamuzi mbaya, ukifananishwa na kujitia kitanzi.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), Bw. David Kafulira, kama serikali itaendelea na mipango yake ya 'fasta fasta' kuilipa Dowans sh. bilioni 94 kama ilivyoamuriwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) kabla ya mkutano ujao wa bunge, ijiandae kupigiwa kura ya kutokuwa na imani nayo.

Akizungumza jana Dar es Salaam, katika mkutano wa wabunge wasiokuwa katika kambi rasmi ya upinzani bungeni na waandishi wa habari, Bw. Kafulila alilifananisha sakata hilo na kashfa maarufu ya Goldenberg nchini Kenya.

Alisema "inashangaza kuona serikali inakuwa na speed (kasi) ya ajabu kutaka kuilipa Dowans eti kwa sababu ni suala la kisheria, mbona hatujaona speed hiyo katika kuwalipa walimu waliokuwa wakiidai serikali kisheria pia, au kwa nini hatuoni kasi hiyo katika kuwalipa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanaoidai kisheria.

"Serikali itambue wazi kuwa hili si suala la lelemama wala masihara...Ngeleja (William, Waziri wa Nishati na Madini) asicheze na moto wa Dowans, chimbuko lake ni kubwa liliwahi kuiangusha serikali, alipojiuzuru waziri mkuu. Asikurupuke kufanya maamuzi. Maana hata ndani ya serikali inaonekana hawana mwafaka juu ya suala hili," alisema na kuongeza;

"Serikali iwe makini kuna mazonge mazonge mengi katika hili, ukweli haujajulikana. Serikali inapoteza legitimacy (uhalali) wa kisiasa wa kutawala, suala hili litaiondoa CCM madarakani kama kashfa ya Goldenberg ilivyoitafuna na kuiondoa KANU na Moi (Rais Mstaafu wa Kenya, Daniel Arap) madarakani.

"Kashfa ile nchini Kenya ilianza miaka ya 1993 huko, hivi hivi, lakini ikaja ikaiangusha KANU na Moi. Unajua unapopoteza uhalali wa kisiasa wa kuongoza unaweza kusababisha machafuko, hasa katika wakati huu ambapo kuna tatizo kubwa la uadilifu wa viongozi. Waache hoja iende kwenye mkaa wa moto wa bunge, kisha ndiyo walipe."

Ingawa alisema mpaka sasa hajajibiwa rasmi kama hoja yake itawasilishwa katika mkutano wa pili wa Bunge la 10 uliopangwa kuanza Februari 8, Bw. Kafulila aliongeza kuwa iwapo serikali itaamua kufikia maamuzi ya kuilipa Dowans, itakuwa imepanua wigo wa hoja yake binafsi, kwani ataliomba bunge 'kadri linavyoona' lipige kura ya kuiangusha serikali.

Mpaka sasa hoja yake hiyo, ambayo aliiwasilisha ofisi za bunge Desemba 10 mwaka jana na kujibiwa Desemba 14 kuwa inafanyiwa kazi, ina sehemu mbili, mgawo wa umeme unaoendelea kuathiri uchumi na hukumu ya ICC iliyoiamuru TANESCO kuilipa Dowans sh. bilioni 94 kwa kuvunja mkataba wa kuzalisha umeme.

"Hatuwezi kuendeshwa kwa mambo ya mission town (ujanja ujanja wa mjini), kama watalipa faster faster (haraka) watakuwa wameongeza upana wa hoja yangu, badala ya kuliomba bunge kumpigia kura Ngeleja ya kujiuzulu, nitaliomba bunge kadri litakavyoona inafaa, lipige kura ya kutokuwa na imani na serikali.

Endelea kusoma habari hii HAPA...

Friday, January 21, 2011

FIKRA YA IJUMAA: HEBU MUNGU NA AKAIBARIKI BARABARA YAKO ILIYOPONDEKA !!!

  • Mbali na nyimbo kombozi na za kiharakati za "Reggae", mimi hupenda sana nyimbo za "Country" kwani zimejaa hadithi za kweli, visa, misukosuko, shangwe, ushindi na hata huzuni na maanguko yetu hapa duniani kama binadamu. 
  • Ijumaa ya leo na wikiendi hii kwa ujumla napenda kuwashirikisha katika wimbo huu niupendao sana wa "God Blessed the Broken Road", wimbo ulioimbwa na bendi mashuhuri ya Rascal Flatts. Huwa napenda kuusikiliza wimbo huu nikiwa faraghani, na japo ni wimbo wa mapenzi, daima hunijaza fikra mpya, kunifurahisha na hata kuniliza na hatimaye kunipatia "utakaso (catharsis)" ambao hunifanya niyatazame maisha upya na safari yangu hapa duniani kwani wakati mwingine binadamu sie inatubidi tupite katika barabara zilizopondeka ili kufika tunakojaribu kwenda. 
  • Maisha yetu ni kama muziki. Na kila siku mstari mmoja mmoja unanyofolewa, na kabla hatujakaa sawa tunashtukia ubeti mzima umekwisha. Leo tunamaliza ubeti mmoja na kesho tunaanza ubeti mwingine katika nyimbo zetu za maisha. Tatizo ni kwamba hatukupewa uwezo wa kufahamu idadi ya mistari na beti zilizobakia kabla ya nyimbo zetu kufikia kikomo. Kwa hivyo tunakwenda tu kwa kubahatisha huku tukipapasapapasa huku na huko tukwa tumefungwa macho. 
  • Hebu Mungu na Akaibariki barabara yako iliyopondeka unayoipitia kwa wakati huu. Kaza macho upeoni na kamwe usitawe na kuiacha safari kwani inawezekana ili kufika huko uendako, ni lazima uipitie barabara hii kwa wakati huu. Safari ni lazima iendelee ati! Tunakutakia wikiendi njema sana. Upendo na ukatawale daima !!!

    ************** 

    Mashairi ya Wimbo huu

    "Bless The Broken Road"

    I set out on a narrow way many years ago
    Hoping I would find true love along the broken road
    But I got lost a time or two
    Wiped my brow and kept pushing through
    I couldn't see how every sign pointed straight to you

    [Chorus:]

    Every long lost dream led me to where you are
    Others who broke my heart they were like Northern stars
    Pointing me on my way into your loving arms
    This much I know is true
    That God blessed the broken road
    That led me straight to you

    I think about the years I spent just passing through
    I'd like to have the time I lost and give it back to you
    But you just smile and take my hand
    You've been there you understand
    It's all part of a grander plan that is coming true

    [Chorus]

    Now I'm just rolling home
    Into my lover's arms
    This much I know is true
    That God blessed the broken road
    That led me straight to you

    That God blessed the broken road
    That led me straight to you.
    **************

    Mashairi katika Kiswahili

    "Mungu Ibariki Barabara Iliyopondeka"
    (Tafsiri yangu ya haraka haraka)

    Na Rascal Flatts

    Ubeti wa Kwanza

    Miaka mingi iliyopita
    Niliazimia kuifuata njia nyembamba
    Nikitumaini kukutana na mapenzi ya kweli
    Katika barabara iliyopondeka
    Ingawa niliishia kupotea hapa na pale
    Nilijifuta kope zangu
    Na kuendelea na safari yangu
    Japo sikuweza kuona kwamba
    Kila ishara, ilinielekeza kwako moja kwa moja

    Korasi

    Kila ndoto ndefu iliyopotea
    Iliniongoza kuja kwako
    Na wengine walioumiza moyo wangu
    Walionekana kama nyota za Kaskazini
    Zilizonionyesha njia
    Ielekeayo katika mikono yako ya upendo

    Na hiki ndicho nikijuacho kwamba ni kweli
    Kwamba Mungu Aliibariki ile barabara iliyopondeka
    Iliyoniongoza moja kwa moja
    Kuja mikononi mwako

    Ubeti wa Pili

    Ninawaza miaka niliyopoteza nikizururazurura
    Na ningependa kuufidia muda nilioupoteza wakati huo
    Kwa kuwa pamoja nawe
    Lakini wewe huishia kutabasamu tu
    Na kuushika mkono wangu
    Kwani umeshayapitia hayo
    Na unaelewa kwamba
    Yote haya ni sehemu ya Mpango Mkuu
    Ambao sasa unatimia

    Korasi

    Na sasa niko naseserea kuja nyumbani
    Kwenye fumbato la mpendwa wangu
    Na hiki ndicho nikijuacho kuwa ni kweli:
    Kwamba Mungu Aliibariki ile barabara iliyopondeka
    Iliyoniongoza moja kwa moja
    Kuja mikononi mwako

    Kwamba Mungu Aliibariki ile barabara iliyopondeka
    Iliyoniongoza moja kwa moja
    Kuja mikononi mwako.

    ************** 
    Wimbo na Mashairi pamoja

    TAMKO LA JANA KUTOKA UMOJA WA VIJANA WA CCM (UVCCM); NA MENGINEYO

    • Tamko hili la UVCCM "limewasha moto" kwani lina maneno makali (hasa kwa Dr. Slaa!) na inavyoonekana vijana hawa hawataki "mchezo". Magazeti mbalimbali yamelisifia na mengine yameliponda tamko hilo hasa kutokana na lugha yake kali ambayo inaweza kuendelea kuchochea moto wa chuki na uhasama miongoni mwa Watanzania. Hata wanablogu pia wamefanya hivyo hivyo. Kama alivyosema Profesa Mbele, tuendeleeni kufanya hivi kwa njia za amani. Mungu Aendelee kuibariki Tanzania!!!
    Tamko hili ni kutoka Jamii Forum
     
    ***********
    Inaonekana sasa ni mwendo wa  matamko tu. 
    Kuna tamko jingine la Kamati Kuu ya CCM HAPA...

    Monday, January 17, 2011

    WATANZANIA WATUMIA SH. BILIONI 555 (DOLA MIL.396) KWENYE SIMU KWA MIEZI MITATU TU !!!

    • Nani anasema Watanzania ni masikini sana? Ripoti iliyotolewa na Tanzania Communications Regulatory Authority (TCRA) inaonyesha kwamba kati ya Julai na Septemba mwaka jana, Watanzania walitumia jumla ya shilingi bilioni 555 (sawa na dola za Kimarekani milioni 396!) kwenye simu. Hii ni sawa na shilingi bilioni 185 kwa mwezi.
    • Ripoti hiyo inaonyesha kwamba kuna watumiaji wa simu wapatao 20,771,487 nchini Tanzania na kwamba katika kipindi hicho cha miezi mitatu kila mtumiaji alitumia shilingi 26,724 kwenye simu
    • Kampuni ya Vodacom ndiyo inaongoza kwa kuwa na watumiaji wapatao 8,426,097 ikifuatiwa na Airtel (5,901,634), Tigo (4,575,534), Zantel (1,586,516), TTCL (256,064) na SasaTel (23,071)
    • Kama vile mdau mmoja alivyodai, hapa bado hujaongeza bajeti ya bia na michango ya harusi. Pengine ni kweli kwamba tatizo letu siyo umasikini bali ni kushindwa kuelekeza nguvu zetu katika mambo ya msingi. Uboreshaji wa njia za mawasiliano hususani simu na mtandao ni hatua nzuri katika kujiletea maendeleo hasa kama zitatumiwa vizuri na kwenye mambo yanayohusu maendeleo. Inabidi sasa tukaze macho vijijini ambako ndiko waliko wananchi walio wengi. Kwa hakika takwimu hizi za TCRA zinafikirisha!
    Picha na ripoti kamili ni kutoka gazeti la Citizen 
    na vyote vinapatikana HAPA...

      Friday, January 14, 2011

      FIKRA YA IJUMAA: "I ONLY HAVE TO OUTRUN YOU !!!"


      Hebu tusome na kutafakari kisa hiki kifupi. Kinaweza kutufundisha kitu kuhusu maisha. Wikiendi njema jamani.

      ****************
      Two lawyers walking through the woods spotted a vicious-looking bear. The first lawyer immediately opened his briefcase, pulled out a pair of sneakers and started putting them on.  The second lawyer looked at him and said:
      "You are crazy! You'll never be able to outrun that bear!" 
      "I don't have to," the first lawyer replied. 

      "I only have to outrun you!"

      Tuesday, January 11, 2011

      ETI HILI NDILO TAIFA LENYE WATU WANENE KULIKO MATAIFA YOTE DUNIANI !!!

      Picha hii inapatikana hapa.
      • Imejulikana kwamba kisiwa kidogo cha Nauru ndicho kinaongoza kwa kuwa na wakazi wanene zaidi kuliko taifa lingine lolote hapa duniani. Kisiwa hiki kidogo kina eneo la mraba la maili 8.1 tu na idadi ya watu wasiopungua 10,000. Hata hivyo, zaidi ya asilimia 95 ya watu wake wazima ni wanene; na asilimia 85 ya wanaume wote ni wanene futufutu (obese). Sasa kisiwa hiki kimebatizwa jina la utani la "kisiwa cha mapandikizi"
      • Kunenepa huku kumetokana na wenyeji wa kisiwa hiki kuacha kula vyakula vyao vya kiasili na badala yake kuanza kufakamia vyakula vya Kimagharibi huku wakiamini kwamba haya ndiyo maendeleo! Matokeo yake sasa karibia nusu ya wakazi wote wanaugua ugonjwa wa kisukari (Tazama pia hapa na hapa).
      • Nilipoisona taarifa hii nikakumbuka nyumbani kwani nasi tumeingia kwenye mkumbo huu na hasa mijini. Sasa tuna supamaketi karibu kila kona na kununua vyakula vya kwenye makopo na nyama zilizotoka viwandani Afrika Kusini ndiyo usasa. Sitashangaa kama baada ya muda tu magonjwa hatari ya Kimagharibi kama kansa na kisukari yataanza kutupukutisha. Japo mimi siyo daktari, huwa nafikiri na kuamini kwamba pengine unene wa mtu anayekula vyakula vya kiasili ni tofauti na ule wa mtu anayekula vyakula vilivyokuzwa na kusindikwa "kisayansi" na kujazwa makemikali kibao.
      • Tazama video hapa ili kuona hali halisi ilivyo kule Nauru. Orodha ya nchi zenye watu wanene zaidi duniani inapatikana hapa na hapa. Marekani imeshika nafasi ya 8,  Misri ni ya 15 na Uingereza ni ya 19.

      MWAKA MPYA ILIKUWA 1/1/11, LEO NI 11/1/11 NA NOVEMBA 11 ITAKUWA 1/11/11: WANAJIMU TAYARI WANAPIGA MAKELELE YA MWISHO WA DUNIA !!!

      • Mwaka huu unasifiwa kuwa ni mwaka wa "kipekee" kutokana na alama za kinajimu. Huu ni mwaka ambao utakuwa na namba 1 inayojirudiarudia mara nyingi kuliko miaka mingine mingi mfano 1/1/11 (mwaka mpya), 11/1/11 (leo) na 1/11/11 (Novemba mosi); na hii eti si dalili njema na inawezekana mwisho wa dunia umekaribia.
      • Wameanza kutaja matukio ya kushangaza yanayohusisha vifo vya halaiki vya viumbe mbalimbali duniani kama vile ndege na samaki kama ushahidi wa maangamizi yanayokuja. Hofu hizi zinazidi kupaliliwa na ule uvumi ulioenea kwamba dunia itakumbwa na tukio la kimaangamizi tarehe 21/12/2012.
      • Tarehe hii ilishatabiriwa na mtabiri maarufu aitwaye Nostradamus na pia imetajwa kuwa ndiyo siku ya mwisho katika kalenda ya kale ya waMaya (hata hivyo soma hapa). Wanasayansi kwa upande wao wamesema kwamba hawana ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba tukio la kushangaza litatokea katika tarehe hiyo au siku nyingine yo yote mwaka kesho. Na kwa Wakristo wengi, Biblia imetamka bayana kwamba siku ya mwisho haijulikani. Kuna haja ya kuwa na wasiwasi japo kidogo na matukio haya?

      Saturday, January 8, 2011

      FIKRA KOMBOZI ZA PROFESA MBELE ZABISHA HODI WILAYANI MBULU KWA MWANAHARAKATI MATIYA !!!


      • Fikra kombozi za Profesa Mbele zinaendelea kukubalika na sasa zimebisha hodi kwa Mwanaharakati Matiya ambako "wananchi wenye asili ya Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara wanaoishi nje ya wilaya hiyo wametakiwa kukumbuka walikotoka na kujaribu kutoa misaada ya kielimu, kiafya na kiuchumi."
      • Mbunge wa jimbo hilo Ndg. Akunaay amesema "umefika wakati wa kila msomi, mfanyabiashara na mwana Mbulu anayeishi nje ya wilaya hiyo kuchangia maendeleo ya jimbo lao ambalo kila mwaka linazidi kudidimia kielimu, kiafya na kiuchumi"

      Kusoma habari kamili kuhusu mada hii bofya hapa!

      NENO LA LEO: EXCUSE US, WE ARE STEALING !!!

      ************
      "Serikali inayomwibia Petro ili kumlipa Paulo daima itategemea kuungwa mkono na Paulo"

      -George Bernard Shaw (1856 - 1950)

      ************
      ....Na siku Petro akishtuka kwamba anaibiwa (na akagoma kuibiwa) itakuwaje? Jumamosi njema jamani!!!

      Friday, January 7, 2011

      FIKRA YA IJUMAA: LEO TUTAFAKARI UTAFITI HUU. ATI BINADAMU TUNAZIDI KUWA MAZUZU???

      Hoja: Wanasayansi wanasema eti ubongo wa binadamu unasinyaa tena kwa kasi. 

      Swali: Binadamu tunazidi kuwa mazuzu? Sasa endelea......

       
      Msimbo wa Kiikolojia. Binadamu yupo kileleni!
      • Japo kimaumbile binadamu ni kiumbe dhaifu sana, uwezo wake wa kufikiri, ikiwemo lugha inayomwezesha kuwasilisha mawazo tata dhahnia kumemfanya akifikie kilele cha msimbo tata wa maumbile na kumpa uwezo wa kuwatawala wanyama wengine.
      • Akili na uwezo huu wa kufikiri vinatokana na ukweli kwamba binadamu ndiye mnyama mwenye ubongo wenye ujazo mkubwa zaidi (ikilinganishwa na uzito wake) kuliko wanyama wengine wote. Kwa ujumla kuwa na ubongo wenye ujazo mkubwa ni jambo jema kwa kila kiumbe hapa duniani.
      • Ni kutokana na sababu hizi, wanasayansi wamepigwa na butwaa kugundua kwamba ubongo wa binadamu unazidi kusinyaa na tayari umepungua kwa asilimia 10 katika kipindi cha miaka 20,000 tu iliyopita. 
      • Kulingana na mahesabu ya wanasayansi hawa, asilimia 10 ya ubongo wa binadamu uliopotea katika kipindi hiki kifupi ni sawa na ukubwa wa mpira wa tenisi; na hiki ni kiasi kikubwa sana.
        • Japo wanasayansi hawa hawajui hasa sababu ya ubongo wa binadamu kusinyaa kwa kasi namna hii, wapo wanaodhani kwamba jambo hili si la kushangaza sana hasa ukizingatia kwamba katika dunia ya sasa binadamu hahitaji kutumia akili nyingi ili kuweza kuishi na hata kuzaliana. Kwa hivyo kimsingi, sababu zilizomfanya awe na ubongo mkubwa - mazingira ya kihasama huku akiwa kiumbe dhaifu, sasa zimeanza kupotea na hivyo hakuna sababu tena ya kuendelea kuwa na ubongo mkubwa zaidi. 
        • Je, madhara ya kusinyaa huku kwa ubongo ni yapi?. Inawezekana kwamba binadamu wa leo ameanza kuwa zuzu (zaidi?) pamoja na ukweli kwamba ana Google, Facebook, mtandao na makorokocho mengine ambayo anadhani kwamba yanamsaidia kuendesha maisha yake kwa urahisi zaidi?  Wanasayansi wametatanishwa na bado hawana jibu. 
        • Japo hawajasema utafiti huu umefanyika wapi, mimi nadhani umefanyika katika nchi za Kimagharibi. Kama hivi ndivyo, ningependa kuona kama ubongo wa Waafrika, hasa wale wanaoishi vijijini ambao kimsingi maisha yao hayajabadilika sana, umesinyaa ama la. Wewe una maoni gani? Binadamu!
          • Utafiti huu unapatikana hapa.

            Thursday, January 6, 2011

            TUHITIMISHE NINI KUTOKANA NA TASWIRA HIZI ZA MKE WA DR. SLAA?

            • Bila shaka picha hizi za anayesadikiwa kuwa mke au mchumba wa Dr. Slaa akibubujikwa na damu baada ya purukushani za maandamano ya Chadema jana kule Arusha zinasikitisha. Inasemekana kwamba kuna hata watu waliopoteza maisha. 
            *****************
            • Je, huu ni mwanzo mbaya kwa mwaka 2011?
            • Ni kielelezo na kiwakilishi cha mapambano na upepo "mkali" wa mabadiliko na mwamko unaovuma?
            • Ni matokeo ya uvunjaji wa sheria kwa walioamua kutumia ubabe, kuonyesha dharau na kuamua kufanya maandamano bila kibali?
            • Ni ubabe wa wamiliki mfumo na ujeuri wao wa kushindwa kusoma alama za nyakati, kutumia busara na kuwa na subira?
            • Nani alaumiwe na hata kuwajibishwa? Kwa nini tumefikia hatua hii na vipi huko tunakoenda?
            ***************** 
            • Nimesoma maoni mengi yaliyotolewa na wasomaji katika tovuti ya gazeti la Mwananchi na Michuzi na yanaonekana kulaumu pande zote kwa kukosa busara na uvumilivu. Kuna mengi ya kujifunza na natumaini kwamba pende zote mbili zitatumia busara ili purukushani kama hizi zisitokee tena. Mungu Ibariki Tanzania!

            Wednesday, January 5, 2011

            NENO LA LEO.....


            "Everything has been figured out except how to live"
            (Jean-Paul Sartre: 1905 - 1980)

            ***************

            Monday, January 3, 2011

            UCHAWI SASA NI KAZI HALALI NCHINI ROMANIA !!!

             Picha hii ni kutoka kwa wafalme wa udaku Bongo.
            *********

            Kuanzia juzi tarehe 1/1/2011, uchawi umetambuliwa rasmi kama kazi halali kule Romania na wachawi sasa wanatakiwa kulipa kodi kama wafanyakazi wengine. Kwa habari zaidi soma hapa. Kama nilivyowahi kugusia hapa, uchawi upo hata Ulaya na Marekani ingawa pengine ni kwa "rangi" tofauti na ile yetu ya kuua maalbino; na vikongwe kule kanda ya ziwa. Kwa habari zaidi kuhusu imani za uchawi Afrika, soma hapa na hapa.

            JIANDIKISHE HAPA

            Enter your email address:

            Delivered by FeedBurner

            BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO