NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, February 28, 2011

KABINTI KANGU KA MWISHO KAMEFIKISHA MIAKA MITATU

Kanaitwa Johari na ndiko kamalaika ka mwisho (gawalaga) katika familia yetu. 
Na sasa Mungu Amekajalia kufikisha miaka mitatu.
Tunakatakia kila la heri.
Hebu Mungu na Akajalie maisha marefu, yenye furaha, amani na ridhiko.

Keki ni lazima ziwe na Dora the Explorer!

Shamrashamra nyumbani na Chuck E. Cheese's

WAZIRI WA ELIMU AZUNGUMZIA SEKONDARI ZA KATA

Nimefurahi kusikia kwamba angalau kuna mikakati mizuri ya kuziimarisha shule za Sekondari za Kata. Fuatilia kauli za Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Dr. Kawambwa hapa chini.

**********


Dk Kawambwa akiri sekondari za kata kuchangia matokeo mabaya

Venance George, Morogoro

SERIKALI imekiri kuwa matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na upungufu unaozikabili sekondari za kata.

Akizungumza kwenye mahojiano na Mwananchi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alikiri matokeo hayo kutoifurahisha serikali.

Dk Kawambwa alisema kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na changanoto zilizoko sekondari za kata. Alisema sekondari za kata zilizoanza kujengwa mwaka 2006, zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo uhaba wa walimu, miundombinu, walimu, maabara na vifaa vingi vya utendaji kazi.

“Matokeo yake tunafika mahali wanafunzi wanamaliza kidato cha nne, kwa sababu ya upungufu mbalimbali ambao umejitokeza shule zetu hasa za kata ambazo ni idadi kubwa, tukapata matokeo ambayo sio mazuri, asilimia 49 ya vijana wamefeli kabisa,” alisema Dk Kawambwa.

Dk Kawambwa alisema kuwapo kwa upungufu wa walimu na vitendea kazi, matokeo yake ni kutopata matokeo mazuri kama ilivyojitokeza mwaka jana, serikali ilijikita zaidi ujenzi wa shule.

Alisema hatua ya kwanza ilikuwa kuhakikisha ujenzi wa shule hizo unakamilika, inayofuata ni kuimalisha madarasa ambayo yalikuwa hayajakamilika.

Waziri Kawambwa alisema programu ya serikali iliyoanza mwaka 2010 mpaka 2015, itahakikisha lengo linatimia la kuwa na vifaa, maabara, vitabu, maktaba na kuajiri walimu wa kutosha.

Alisema hivi sasa wanakabiliana kumaliza upungufu wa walimu 43,000 na kwamba, kupitia programu hiyo serikali imeanzisha kozi za ualimu vyuo vikuu, huku vingine vikibadilishwa kuwa vyuo vya ualimu.

Aliongeza kuwa kila mwaka vitakuwa vikizalisha wastani wa walimu 10,000 hadi 15,000, hivyo kuweza kumaliza tatizo la walimu ndani ya miaka mitano.

Kuhusu tatizo la vitabu vya shule, Dk Kawambwa alisema tayari serikali imesambaza vitabu 800,000, huku 2,250,000 vikitarajiwa kupokelewa na kusambazwa kwenye sekondari nchini.

Alisema serikali imekopa dola 1,050,000 za Marekani kutoka Benki ya Dunia (WB) kuboresha miundombinu ya elimu sekondari za kata na kuweka vitendea kazi.   

Chanzo: Mwananchi

Sunday, February 27, 2011

HATA KAMA MTU HUJUI KUSOMA HUWEZI KUSAINI MKATABA WA AINA HII !!!

Mikataba ya aina hii itatumaliza jamani.
Halafu tunashangaa eti ni kwa nini gharama za umeme 
zinapanda kila siku. Ni kwa nini lakini hatuwezi kuwa siriazi na raslimali zetu?


....WABUNGE WAPIGWA BUTWAA

...Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini waliotembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya TANESCO, wameshitushwa na gharama kubwa za uendeshaji wa mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi asilia Ubungo, Dar es Salaam.

Hatua hiyo inatokana na kuelezwa kuwa, wananunua gesi kwa kampuni ya Pan Afrika kwa fedha za kigeni, jambo ambalo limekuwa likiongeza gharama kwa watumiaji.

“Gesi inapatikana mkoani Lindi mnanunua kwa dola za Marekani, halafu mnauza umeme kwa shilingi, hamuoni mnawabebesha watumiaji mzigo usio na sababu,” aliuliza mmoja wa wajumbe hao, baada ya kupata maelezo kutoka kwa Meneja Mwandamizi wa Mitambo ya Gesi na Mafuta, Mhandisi Gregory Chegere.

Chegere alisema hayo ni masharti ya mkataba kati ya TANESCO na Pan Afrika, inayosafirisha gesi kutoka Kilwa hadi mtamboni hapo. Alisema mitambo hiyo inazalisha megawati 100, ambazo huingizwa kwenye gridi ya taifa kwa siku.

 
*********************
Kwingineko....

Mkuu wa Dowans kumbe yuko tayari kusamehe baadhi ya kale kadeni tunakodaiwa....

.....Al Adawi yuko tayari kusamehe fidia ya sh. bilioni 94 lakini kiasi cha dola za Marekani milioni 24 ni lazima kilipwe kwa kuwa ni deni halali.

“DOWANS ilizalisha umeme kwa kipindi cha miezi 10, watu wanaposema deni lote lisilipwe si sahihi. Hawajui fedha wanazolipa umeme zinakwenda wapi, tumezalisha tukawapatia umeme, wameuza lakini mpaka sasa hawajatulipa,” alisema.

Chanzo: UHURU

Saturday, February 26, 2011

Friday, February 25, 2011

MTAJI WA MASIKINI NI...........

Sikumbuki nilikoipata picha hii. 
Kama ni mali yako sema nikushukuru !

TAARIFA RASMI YA SERIKALI KUHUSU MABOMU YA GONGO LA MBOTO

Watu 24 wamethibitika kufa katika ajali ya milipuko ya mabomu iliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania kikosi cha 511, Gongo la Mboto Dar es Salaam tarehe 16/02/2011.

Taarifa ya Serikali imeeleza kwamba marehemu wote 24 walitambuliwa na Serikali kugharamia mazishi yao kama ilivyoahidi.  Baadhi ya marehemu walisafirishwa kwenda kuzikwa makwao katika Mikoa ya Kagera, Mara, Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Lindi, Mbeya, Mtwara na Dar es Salaam.

Hata hivyo maiti moja ya kichanga cha miezi minane mpaka sasa haijathibitika kuwa kifo chake kilitokana na milipuko ya mabomu, kutokana na taarifa zake za awali kutopatikana katika orodha ya majeruhi waliopokelewa katika dispensari ya Kitunda, Hospitali ya Amana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Taarifa ya awali kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospital ya Muhimbili ilimworodhesha Bwana Abdallah Magadi kuwa ni miongoni mwa marehemu wa milipuko hiyo, wakati yeyé ndiye aliyepeleka mwili wa marehemu Itato Madafu ambaye kifo chake kilitokana na ajali ya gari tarehe 29/1/2011 maeneo ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo.

Katika milipuko hiyo ya mabomu zaidi ya watu 512 walijeruhiwa, ambapo Hospitali ya Amana  iliwapokea majeruhi 256, Temeke 139, Muhimbili 87, na Zahanati ya Chanika 30.
Katika tukio hilo hadi sasa nyumba 75 zimethibitika kubomolewa, nyumba hizo zilikuwa na kaya 115 zenye watu 539.

Aidha, hadi taarifa hii inaandaliwa jumla ya watoto 140 hawajulikani mahali walipo na hivyo Serikali inatoa wito kwa wananchi pindi wawaonapo watoto ambao wanasadikiwa kupotea kufuatia tukio ya milipuko hiyo kutoa taarifa katika vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa na katika vyombo vya habari ili kurahisisha utambuzi wao.

Hadi hivi sasa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa fedha taslim shs. 500,000,000/= kwa ajili ya kulipia huduma za awali zikiwemo gharama za mazishi, rambirambi na kununua vyakula kwa ajili ya waathirika.  Pamoja na fedha hizo ofisi hiyo imetoa vifaa vifuatavyo mahema (101), magodoro (538), vyombo vya kupikia makasha (80), seti ya vifaa vya usafi wa mwili (100) Blanketi za wakubwa (400) na Blanketi za watoto (200).

Wakati huo huo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inayoratibu shughuli za maafa ya milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto imepokea misaada mbalimbali fedha na vifaa ikiwemo magodoro, blanketi, shuka, mito, vyandarua, nguo mchanganyiko sabuni, dawa mbalimbali, vyakula kwa ajili ya kuvigawa kwa waathirika.

Serikali kwa namna ya pekee inatoa shukrani za dhati kwa wale wote waliotoa misaada ya hali na mali kusaidia waathirika wa janga hili.

Aidha, Serikali inawahakikishia kuwa kazi ya ukusanyaji mabomu inaendelea na inawaomba wananchi kutoa taarifa pindi wayaonapo katika maeneo yao.

Imetolewa Na:
IDARA YA HABARI (MAELEZO)
24 Februari, 2011

Thursday, February 24, 2011

HIZI DATA ZA ELIMU ZINATISHA

...Wanafunzi 7 kati ya 10 wa darasa la tatu
hawawezi kusoma Kiswahili 

...8 kati ya 10 hawawezi hesabu za kuzidisha 

...9 hadi 10 hawawezi kusoma Kiingereza.

...Hata wanafunzi wengi wa darasa la 7, mambo ni yale yale.

Kama hivi ndivyo;

Hawa wa kidato cha nne tunategemea watafauluje?

Kwa habari kamili soma HAPA.

Wednesday, February 23, 2011

NINI KINAENDELEA HAPA ???

Anaonekana anafuatilia gazeti kwa makini sana...


Picha ni kutoka kwa SENGO

HEBU SIKILIZA MADUDU YA HUYU MWIZI UCHWARA

  • Ni hapa hapa jimboni Florida. Jina lake ni Kenneth Lucious White. Kaingia kwenye duka ili kuiba. Badala ya kumakinikia kilichompeleka humo, akawasha kompyuta, akaingia katika wavuti za ngono, akashusha suruali na kuanza "kujichakachua"
  • Inaonekana hata alikuwa hafuatilii kilichokuwa kinaendelea nje kwani polisi walifika na kumkamata "redi hendedi".
  • Matendo kama haya, japo ni ya kipuuzi, angalau yanatupa fununu muhimu kuhusu mnyama huyu machachari na tata ajabu aitwaye binadamu. Ati, hapa ustaarabu na u-Homo Sapiens wake viko wapi?
Kisa hiki kinapatikana HAPA.

Tuesday, February 22, 2011

"SIACHII MADARAKA WALA SIONDOKI, NITAKUFA KAMA SHAHIDI WA LIBYA, WAANDAMANAJI WANAWEWESEKA KUTOKANA NA KUTUMIA MADAWA YA KULEVYA..." - GADHAFI

  • Huku kiti cha madaraka alichokalia kikiwa kinawaka moto unaochochewa na maovu ya udikteta wa miaka zaidi ya 40 madarakani, Moammar Gadhafi ama ni mgonjwa au hajaelewa kinachoendelea. Katika hotuba yake ya kipayukaji iliyomalizika muda si mrefu uliopita ametoa matamko ya kushangaza - yakiwemo hayo juu. Huku akiwa mwenye hasira na akigonga meza kwa ngumi, amewaita waandamanaji kuwa ni "mbwa" na akawaonya kwamba wakae chonjo kwani bado hata hajatoa amri ya risasi ya moto hata moja kufyatuliwa; na akitoa amri hiyo basi Libya nzima itawaka moto. Ameendelea kusema kwamba yeye ni shujaa na kwamba ataipigania Libya mpaka tone lake la mwisho la damu!
  • Ametoa mwito kwa wanaomuunga mkono kujitoa mhanga kuanzia kesho na kujitosa mabarabarani ili kupambana na waandamanaji wanaoipinga serikali yake. Ili kujipambanua na wapinga serikali, inabidi wavae "bangili" za kijani katika mikono yao.
  • Amewauliza waandamanaji swali la Kitashtiti kwamba "nini kimewapata? Mbona tulikuwa tunaishi katika ustawi?" Kwa habari zaidi soma HAPA.
Sikiliza sehemu ya hotuba hiyo hapa chini

PROFESA MBELE KANIACHA HOI

  • Kama vile alivyoachwa hoi na mwanafunzi wake mwenye moyo wa shukrani, Profesa Mbele pia ameniacha hoi kwa wema, ukarimu na moyo wake wa kujali. Kama wiki mbili hivi zilizopita nilikuta bahasha kubwa ofisini. Muhuri wa posta ulionyesha kuwa ilikuwa imetoka Minnessota na mtumaji alikuwa ameingia gharama ya karibu dola nane kununulia stempu.
  • Nilipoifungua bahasha ile nilishangaa sana kukuta kwamba ilikuwa imetoka kwa Profesa Mbele na ndanimwe mlikuwa na nakala ya kile kitabu chake mashuhuri cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences -tena ikiwa imesainiwa kabisa! Kwa mwanataaluma makini na anayependa vitabu na kujiongezea maarifa kila kuchapo kama Profesa Mbele, hii ni zawadi ya muhimu sana!!!
    • Nimeamua kukisoma kitabu kwa uangalifu sana ili nigundue sababu inayokifanya kipendwe sana na watu wanaopenda kujifunza utangamano wa kitamaduni. Nikishafanya hivyo, nitaandika maoni mafupi hapa kukihusu.
    • Kwa moyo wangu wote, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Profesa Mbele kwa wema wake huu. Kwa hakika azima na shauku yake isiyoisha ya kutuhamasisha kusoma vitabu si bure. Kama vile ambavyo nimeshawahi kusema HAPA, mawazo na falsafa zake  kombozi siku moja zitawapambazukia waTanzania na mchango wake chanya usiotetereka katika ukombozi wa jamii yetu utajulikana na kuheshimiwa!
    Kitabu hiki mashuhuri kinapatikana mtandaoni HAPA.
    Kule Tanzania kinapatikana sehemu mbalimbali (bofya HAPA)

    Monday, February 21, 2011

    ZAWADI ZANGU ZA VALENTINE DAY !!!

    Zawadi hizi bora kabisa ni kutoka kwa mabinti 
    Minza (aka Zofa - darasa la kwanza) na Kija (darasa la 4). 
    Kwangu mimi, hakuna zawadi nzuri kushinda hizi !!!

    Saturday, February 19, 2011

    Friday, February 18, 2011

    WITO KWA WACHAGA: KISOMENI KITABU HIKI !!!

     Ganda la mbele
    • Baada ya kuona kuwa Wachaga wamebaki jina tu kwa wengi wao kutoifahamu lugha wala utamaduni wao, leo napenda kuwaletea habari nzuri juu ya kitabu kinachoelezea maisha na utamaduni wa Mchaga kwa undani. Kitabu hiki kiitwacho Maisha ya Mchagga Duniani na Ahera kimeandikwa (kwa Kiswahili) na Mangi Petro Itosi Marealle na kuchapishwa na Mkuki na Nyota Publishers 
    Ganda la nyuma
    • Nilikiona maktabani na mara moja nikakiazima na kuanza kukisoma (mimi ni Kyasaka niliyeoa binti wa Kichaga!). Ni kitabu kizuri ambacho kinaelezea mambo ya kina kuhusu maisha ya Mchaga tangu anapozaliwa mpaka anapofariki na baada ya hapo.
    Tabaruku


    Yaliyomo

    • Hata kuna sura nzima juu ya Uchawi na Jinsi ya Kuroga. Kutokana na kiwango chao cha elimu, sikujua kama Wachaga nao wanaamini sana katika mambo ya ushirikina mpaka nilipoisona sura hii. 
    • Ingependeza sana kama vitabu vingi vyenye kuelezea tamaduni mbalimbali za makabila yetu vingeandikwa kwani tutake tusitake lugha na tamaduni zetu nyingi zinaonekana kutishwa na wimbi la utandawazi na mabadiliko ya maisha ya kisasa.
    • Na kwa wavulana na wasichana wa Kichaga - na kama tabaruku ya kitabu hiki inavyosema - Mambo Makuu Zaidi Yanatarajiwa Kutoka Kwenu !!!
    Nyongeza Chekeshi
    • Mbali na "ukweli" kwamba mimi ni Kyasaka, jina langu pia huwa linawatatanisha Wachaga kwani katika Kichaga neno Matondo si neno zuri sana. Napenda tu kuwahakikishia kwamba mimi SIYO Itondo na binti yenu kabisa hajafanya makosa kuolewa na chasaka! Na kwa mnaotegemea kuoa mabinti wa Kichaga, hakikisheni mnasoma HAPA kwanza. 
    *******************
    Kuhusu Upatikanaji wa kitabu hiki kutoka Mkuki na Nyota Publishers

    Kitabu hiki kinapatikana kutoka Tanzania Publishing House Bookshop, Samora Avenue, Dar es salaam. Habari kuhusu kukinunua kutoka mtandaoni zitapatikana hivi karibuni !

    Thursday, February 17, 2011

    RAIS WA JAMHURI AZUNGUMZIA MIRIPUKO YA MABOMU GONGO LA MBOTO (VIDEO)



    Video kwa hisani ya Abdallah Mrisho wa Global Publishers.

    Kwa picha na habari kutoka vyanzo mbalimbali kuhusu tukio hili la kusikitisha tembelea HAPA HAPA, HAPA (kuna maoni 99 tayari) na HAPA. Hotuba kamili ya rais katika maandishi inapatikana HAPA.

    Kwa waathirika wote, poleni sana kwa msiba huu. Hebu Muumba na Akawatie nguvu katika saa yenu hii ya giza. 

    Mungu Ibariki Tanzania !!!

    Tuesday, February 15, 2011

    HUYU DAKTARI VIPI TENA ???

    Kama kawaida ni Said Michael

    WABUNGE WAZOA MILIONI 90 KILA MMOJA. NI ZA KUNUNULIA MAGARI !!!

    • Hivi mbunge ukimaliza muda wako, hilo shangingi lako unakwenda nalo au unalirudisha? Kwa wabunge waliorudi, mbona wasiendelee kutumia mashangingi yao ya zamani hasa ukizingatia kwamba Toyota Land Cruisers ni magari yanayodumu kwa muda mrefu sana? Mimi sizijui taratibu za hawa "waheshimiwa" na samahani kama haya ni maswali "ya kitoto" Inashangaza kidogo kuona kwamba kila tukibadilisha wabunge ni lazima tuingie hizi gharama za kununua mashangingi mapya.
    Hizi ni za 2009
     ************************

    Wabunge wazoa Sh. 90 Mil kila mmoja
    Tuesday, 15 February 2011 07:35 

    JUMLA ya Sh. 3.24 bilioni zimelipwa kwa wabunge ili kuwawezesha kununua magari binafsi kwa ajili ya shughuli za kibunge, imeelezwa.

    Kwa mujibu wa habari hizo kila mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amelipwa Sh. 90milioni  kwa ajili ya kujinunulia gari.

    Aidha, wabunge hao wapatao 360 wamekatiwa bima ya afya inayotarajiwa kuanza kutumika kabla ya mwezi Juni mwaka huu. Na wameomba kutibiwa hospitali za binafsi!

     Halafu Chadema nao wakaingia....

    "Ndugu zangu hali ni mbaya, siku moja tutafanya maandamano bungeni, sio kutoka nje ya ukumbi. Inashangaza, tumepewa Sh90 milioni za magari kwa wabunge wote, huku bungeni tunajadili bajaji kuwa 'ambulance' (gari ya kubebea wagonjwa),'" alisema mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.


    "..Wabunge tumeomba 'insurance' (Bima) kila mmoja amepewa na kabla ya Juni naamini zitaanza kutumika, tumeomba kutibiwa 'private hospital' (hospitali binafsi). Hii inaonyesha hospitali za serikali zilivyo mbaya na hao wenye uwezo wanazikimbia," alisema Lema.
     Isome habari kamili HAPA.

    Monday, February 14, 2011

    MBUNGE WANGU AJITAKASA KASHFA YA RADA

    • Atangaza kuwa yeye ni mwadilifu, mtu safi, hakutenda kosa lolote katika kashfa ya rada.
    • "Mimi ni muadilifu, nimefanya kazi katika awamu zote nne za uongozi wa nchi yetu. Hata nilipojiuzulu sikuwa na hofu wala mashaka ya kupoteza kazi, kwa kuwa nilijiamini kuwa sikutenda kosa lolote katika kashfa hiyo ya rada, na nilisema iko siku ukweli utajulikana"
    • "Uchunguzi umefanyika na sasa ukweli umejulikana. Wahenga wamenena 'kwenye ukweli uongo hujitenga'. SFO na TAKUKURU wamefanya uchunguzi wa kina na matokeo ya uchunguzi wa vyombo hivyo viwili yamedhihirisha kuwa mimi ni mtu safi," alisema Bw. Chenge.
    • Alimalizia kwa kusema kwamba ukweli umejulikana kuwa ununuzi wa rada ulifanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zote za serikali. 
    Kwa habari zaidi soma HAPA

      VALENTINE DAY: UKIMWI UPO TENA UNAPATIKANA KWA BEI POA TU...

      Kwa vile Valentine Day tumeivalia njuga hata kuwazidi Warumi wenyewe walioianzisha, basi Valentine ya mwaka huu na tukawe werevu na wenye kujihadhari na hili gonjwa hatari la UKIMWI. Ukweli ni kwamba gonjwa hili bado lipo, linaua na bado HALINA TIBA!!! Kwa hili tunaungana na Mama Regina Lowassa kusema kwamba Valentine Day isiwe ya anasa!
       


      ***Kwingineko***

      VALENTINE DAY, MASHINDANO YA UREMBO, NOECLEXIS NA DHANA YA UZURI.

      Angalizo: Hii ilitoka mwaka jana. Nimeongezea na kupunguza vitu vichache ili kuashiria mabadiliko ambayo yamekwishatokea tangu wakati huo. Maswali ya msingi, hata hivyo, bado ni yale yale. Tuwemo!
      ********************


      • Leo hii dunia inasherehekea sikukuu ya "kipagani" ya Valentine Day. Kwetu sisi Afrika nadhani siku hii bado ina ugeni fulani. Kwa mfano, wakati nikisoma pale mlimani miaka michache tu iliyopita,, sikumbuki kuona watu wakihangaika kusherehekea hii Valentine Day. Mambo yamebadilika kwa kasi mno na siku hii sasa ni muhimu kwa wapendanao kusherehekea kwa kwenda pwani, kwenye kumbi za starehe na kwingineko. Mwaka jana, kwa mfano, blogu kadhaa ziliwaonya na kuwakumbusha washerehekeaji wa sikukuu hii juu ya hatari ya kuambukizana gonjwa la UKIMWI. Hii imegeuka na kuwa siku ya kungonoka! (Tazama maoni ya wadau HAPA)
      • Siku hii ya wapendanao na mashindano ya urembo tunayoyashuhudia kila leo (vyote ni matokeo ya utandawazi) vimenikumbusha swali gumu ambalo limewasumbua wanafalsafa tangu enzi na enzi: Uzuri ni nini? Hili ni swali linalohusu kila kitu hapa duniani lakini leo nitatumia mifano ya washiriki wa mashindano ya urembo yaani mabinti.
      • Ni kweli kuna wazuri/warembo au pengine uzuri/urembo umo katika fikra za mtazamaji tu? Inakuwaje leo tunalazimishana kuwa na mrembo mmoja tu tena mwenye sifa zile zile za Kimagharibi- tineja, mkondefu, mrefu, mwenye miguu mchongoko na tumbo tambarare, mwenye madaha, nyanya msumari kifuani na ikiwezekana "aliyepigwa pasi"? Hebu chunguza picha hizi kwa makini halafu ufikiri tena dhana hii ya uzuri/urembo:
      (1) Tunalazimishana kuamini kwamba eti mrembo ni lazima awe hivi:

       
      (2) Huu ni uwongo kwa sababu katika jamii zingine za Kiafrika mrembo alitakiwa/anatakiwa awe hivi:



      (3) Na katika jamii zingine mrembo alitakiwa/anatakiwa apambike hivi:

      (4) Kwa wengine, mrembo ni lazima awe amenona kama hivi. Na kwa mwanamke wa Kiafrika, kunona hivi lilikuwa ni jambo jema!


      (5) Au awe na umbo namba 8 kama hili:


      (7) Wengine huwa hawajali umbo ali mradi kuwe na "kitu" wakipendacho!


      (8) NOECLEXIS - Waswahili walipatia waliposema kwamba "mwanamke tabia"! Msikilize Dudubaya hapa chini akitetea Noeclexis!



      (9) Swali: mbona tunalazimishana kwamba eti mrembo ni lazima awe hivi?


      • Na kama kila mtu ana dhana yake ya uzuri kama tulivyoona hapo juu, inawezekanaje tuwe na mzuri mmoja tu anayewakilisha dhana zote hizi? Ati, uzuri hasa ni nini? 
      • Kwangu mimi, mwanamke mzuri, mwandani mwema, rafiki wa kweli, shujaa wa moyo wangu, malkia wa dunia, Eva wangu na mshindi mwema ni HUYU (Tazama pia HAPA). Nina sababu nyingi; na nyingi hazihusishi umbile wala uzuri wa nje. Valentine njema wadau mnaposherehekea "uzuri" uliotamalaki katika kila kitu hapa duniani! Na vita vya UKIMWI ni lazima viendelee ati!

        JIANDIKISHE HAPA

        Enter your email address:

        Delivered by FeedBurner

        BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO