NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, March 30, 2011

WASUKUMA MPO? HAPA MNASEMAJE? MAKABILA MENGINE JE?

  • Ndiyo tu nimemaliza kukisoma kitabu hiki juu ya masimulizi ya Wasukuma. Kitabu kimeandikwa na John M. Masuha, kina kurasa 71 na kimechapishwa na East African Literature Bureau mwaka 1963.
Sura ya saba, ukurasa wa 40
  • Kwa vile hakuna jamii ambayo imesimama tisti, ni wazi kwamba mambo mengi yameshabadilika; na sina uhakika kuhusu uhusiano wa uchapakazi na ndoa miongoni mwa vijana wa kisasa. Ati, ni lazima kweli kijana wa Kitanzania wa kisasa awe mchapakazi ndiyo apate mwenzi kama ilivyokuwa kwa Wasukuma na makabila mengine?
Angalizo

Mimi ni mkereketwa wa mambo ya kitamaduni na nitakuwa nawaletea habari juu ya makabila na tamaduni zetu kila ninapozipata. Naamini kwamba hili ni jambo jema!

Tuesday, March 29, 2011

WAGONJWA WAJITOKEZA NA KUIFAGILIA DAWA YA BABU LOLIONDO - TAARIFA YA HABARI KUTOKA ITV


Taasisi nne za kitafiti pia zimesema kuwa dawa hiyo haina madhara. Utafiti kama dawa hiyo inaponya ama la bado unaendelea.


Ikithibitishwa kama kweli dawa hii inaponya basi itakuwa nafuu ya ajabu kwa watu wengi wanaohangaika na magonjwa mbalimbali. Tunaomba iwe hivyo !!!

MASULUHISHO YA KINGO WAKATI MWINGINE HUWA YANANISHANGAZA !!!

Monday, March 28, 2011

SERIKALI INAPOKIMBILIA LOLIONDO KUPATA KIKOMBE CHA BABU....

  • Ati, hii tabia ya "serikali" kukimbilia Loliondo "kutibiwa" inatoa taswira gani kwetu kama jamii? Na leo hii, baada ya kufanya utafiti wake, serikali imetoa tamko lake rasmi ikisema kwamba dawa hiyo haina madhara kwa binadamu; na kwamba inaendelea kuifanyia uchunguzi. Serikali pia itaboresha huduma kule Loliondo ili kupunguza vifo vya wagonjwa. Mungu Aendelee kuibariki nchi yetu!
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, akipata kikombe cha tiba ya babu, katika Kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro juzi. (Picha na Lilian Joel)

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa bunge ), William Lukuvi (wa pili kulia) na Rosemary Nyerere wakipata kikombe cha babu Loliondo. Picha kutoka kwa Mjengwa.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Teresya Huvisa akipata kikombe cha Babu Loliondo.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dk Yohana Balelel wakipata tiba ya mchungaji Ambilikile Mwasapile wa kijiji cha Samunge, Loliondo.


  Huyu bila shaka wamjua!

Hapa chini ni kikombe kipya cha Mama wa Tabora !

UTAFITI: UWEZEKANO WA KUPATA MSHTUKO WA MOYO HUONGEZEKA MARA TATU BAADA YA KUFANYA NGONO NA MARA TANO BAADA YA KUFANYA MAZOEZI MAKALI !!!

 Picha hii inapatikana HAPA
  • Sote tumeshasikia kuhusu wanamichezo walioanguka viwanjani na kukata roho. Pia tumeshasikia kuhusu watu waliofia kwenye majumba ya kulala wageni ambako walikuwa wamekwenda na wapenzi wao kujifurahisha. Vifo vya aina hii hutajwa sana katika vyombo vya habari na huonekana kwamba siyo vya kawaida.
  • Kwa mfano, mwaka jana nilipokuwa nyumbani, jamaa mmoja mashuhuri pale Bariadi kwa uuzaji wa bia za jumla jumla, na mwenye mke na watoto, alifia katika nyumba ya kulala wageni akiwa na mwanamke mwingine. Kifo hiki kilileta gumzo kubwa pale mjini na kama kawaida imani za kishirikina zilichukua nafasi kubwa huku wengine wakidai kwamba marehemu alikuwa amewekewa mtego. Wengine walidai kwamba pengine ni papara za kuzini ndizo zilikuwa zimemtoa roho. Tangu hapo mkamia maji hayanywi ati!
  • Wanasayansi sasa wanadai kwamba matukio kama haya, japo ni ya nadra sana, hayapaswi kutushangaza yanapotokea kwani wamegundua ushahidi kwamba uwezekano wa mtu kupata mshtuko wa moyo na kukata roho mara moja huongezeka mara tatu zaidi baada ya kufanya ngono na karibu mara tano baada ya kufanya mazoezi.
  • Watafiti hawa wanasisitiza kwamba japo hakuna haja ya kuogopa kufanya ngono au mazoezi, ni vizuri kuwa waangalifu na kuzingatia ushauri wa madaktari.
Habari zaidi kuhusu utafiti huu zinapatikana HAPA

Saturday, March 26, 2011

FIKRA YA IJUMAA: KWA NINI "UDAKU" UNAPENDWA SANA? TENA DUNIANI KOTE ???

  • Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko juu ya tabia ya Watanzania kutopenda kujisomea. Hata hao wachache wanaojisomea, inasemekana kwamba wengi wao huvutiwa zaidi na udaku na kukwepa magazeti na vitabu dhati pevu.
Picha ni kutoka Global Publishers .
  • Tabia hii ya kupenda udaku haipo kwetu pekee. Udaku unapendwa duniani kote! Hapa Marekani kwa mfano magazeti mengi makini (mf. Los Angeles Times, New York Times, Newsweek na Time) yamekumbwa na misukosuko ya kukosa wasomaji hadi kupelekea baadhi yake kupunguza wafanyakazi, kupunguza kurasa, kufungwa na mengineyo kuhamia mtandaoni.
    • Magazeti ya udaku (mf. US Weekely na The Globe) kwa upande mwingine yameendelea kufanya vizuri na hayajakumbwa na msukosuko wa aina yo yote; na yanazidi kujiimarisha. Swali ninalopenda kuuliza hapa ni kwamba kwa nini udaku unapendwa hivi - tena karibu duniani kote? Ati, kupenda udaku ni vibaya? Isome makala ya Padri Karugendo kuhusu suala hili HAPA

      Friday, March 25, 2011

      SERIKALI YAWAPIGA MARUFUKU WAGANGA WA KIENYEJI

      Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa bunge ), William Lukuvi (wa pili kulia) na Rosemary Nyerere wakipata kikombe cha babu Loliondo. Picha kutoka kwa Mjengwa.



      ********************
      Angalizo langu

      Ati, waganga wa kienyeji ni tatizo? Au tatizo ni jamii yenyewe na wale wanaoiongoza? Ni kweli kwamba kupiga marufuku waganga wa kienyeji (kujitangaza) ndiyo suluhisho? Serikali inajua ni kwa nini watu wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji; na kutafuta tiba zingine mbadala? Ni kwa nini imani za kishirikina zinazidi kujiimarisha katika jamii wakati huu ambapo dunia imepiga kasi kubwa ya kimaendeleo?  Waganga wote ni walaghai? Kutoa amri bila kuangalia hasa kiini cha tatizo lenyewe ni kupoteza muda tu.

      ***************************
      Serikali yawapiga marufuku waganga 
      (Alhamisi, 24/3/2011)
      Anthony Mayunga, Musoma

      WAGANGA wa tiba za jadi nchini ,wanatakiwa kuacha mara moja kudanganya watu kuwa wanatibu magonjwa kama kifua kikuu, kisukari na Ukimwi kwa kuwa sheria haziwataki kujitangazana badala yake wanapaswa kutangazwa na wanaopata tiba na kupona.

      Onyo hilo kali limekuja wakati maelefu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa wanaendelea kumiminika katika Kijiji cha Samunge kupata tiba kutoka kwa Mmchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile.

      Mchungaji huyo amekuwa akitibu  magonjwa sugu yakiwemo kifua kikuu, kisukari, Ukimwi, degedege na shinikizo la damu. Onyo dhidi ya waganga, lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Lucy Nkya, katika hotuba yake kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kifua kikuu Duniani yaliyofanyika  kitaifa mkoani Mara. Alisema kuenea ugonjwa wa kifua kikuu unaenea kwa kasi kwa sababu  wananchi wanakubali kudanganywa na waganga hao.

      “Nasema kuanzia sasa ni marufuku kwa waganga wa kienyeji, kuwadanganya wagonjwa kuwa wanatibu magonjwa kama hayo, maana mnadanganya watu na wanazidi kufa. Hatutaruhusu tena mchezo huo, narudia ni marufuku, tiba halisi inatolewa hospitalini si kwingineko," alisema Naibu Waziri.

      Alisema waganga wazuri hawajitangazi na kwamba wanaopaswa kujitangaza ni wafanyabiashara tu  ambao kazi yao kudanganya watu kwa kutumia matangazo mazuri mazuri.

      Hata hivyo Naibu Waziri huyo hakugusia tiba inayotolewa na Mchungaji Mwasapile, ambayo watu mbalimbali wakiwemo viongozi waandamizi wa serikali, wamewahi kuitumkia.

      Akizungumzia mikakati ya serikali kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu, alisema wizara imeanza kusambaza aina mpya ya darubini za kisasa za LED, zenye uwezo mkubwa zaidi wa  kugundua vimelea vya kifua kikuu katika makohozi.

      “Hadi kufikioa mwisho wa mwaka huu, asilimia 95 ya hospitali zote za wilaya, zitapata darubini hizi mpya na ifikapo mwishoni mwa 2012 hospitali zote zikiwemo za mashirika ya dini zitakuwa zimepata, vifaa vipya vya kuoteshea vimelea vya kifua kikuu,”alisema na kuongeza.

      Alisema  vifaa hivyo vitafungwa katika maabara za Hospitali za Muhimbili, Mbeya, Bugando na Kibong’oto.

      Alikiri kuwa wizara hiyo inakabiliwa na upungufu wa wataalam wakiwemo mafundi sanifu wa maabara na uelewa mdogo wa jamii  kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu. 

      Chanzo: Mwananchi

      HEBU SIKILIZA "MKASA" WA HUYU AJUZA WA MIAKA 92

      • Ni juzi tu hapa hapa Florida. Ajuza huyu pichani kwa jina Helen Staudinger (miaka 92) alikwenda kwa jirani yake mwanaume aitwaye Dwight Bettner (miaka 53). Jirani akamwomba mzee huyu aondoke. Ajuza wa watu akaomba apigwe angalau busu kwanza ndiyo aondoke. Dwight akakataa katakata.
      • Basi mwishowe Bi mkubwa akaondoka kwa shingo upande. Alipofika nyumbani akachukua bunduki yake na kuanza kuungurumisha risasi kibao kuelekea nyumba ya jirani yake aliyemnyima malavidavi. Bahati nzuri hakuna risasi zilizompata jirani yake Dwight. Polisi wakaitwa na ajuza wa watu akatupwa rumande. Masharti ya dhamana ni dola 15,000. Dwight anadai kwamba ajuza huyu ameonyesha kumzimia (kimapenzi) tangu ahamie hapo anapoishi karibu miezi sita hivi iliyopita, na hajui ni kwa nini.Tangu hapo mapenzi hayachagui rangi, umri, tabaka wala umbo ati!
      Mkasa huu unapatikana HAPA na HAPA.

      Wednesday, March 23, 2011

      UANASIASA NI KAZI NGUMU. KAMA UNABISHA TAZAMA HII PICHA KWA MAKINI

      • Mbunge wa Arusha Mjini Godbles Lema akihutubia wananchi mara baada ya kufungua tawi jipya la Chadema katika chuo kikuu ch Sebastiani Kolowa wilayani Lushoto jijini Tanga mwishoni mwa wiki iliyopita. Si wote wanaoweza kuwa wanasiasa; na nahisi kwamba mimi ni mmojawao!
      • Ukitaka kusoma zaidi kuhusu uanasiasa na changamoto zake, soma ingizo langu jingine fupi HAPA. Picha hii nimeipata HAPA.

      Tuesday, March 22, 2011

      NATUMAINI KWAMBA NDOA HII ILIDUMU (ANZIA 2:25)

      ETI, KUTUMIA LUGHA YENYE KUONYESHA USAWA WA KIJINSIA KATIKA BIBLIA (ZA KISASA) NI "KUCHAKACHUA" NENO LA MUNGU?

      Kwa tunaoamini kwamba Biblia ni neno la Mungu, ni sawa kweli kuibadilishabadilisha mara kwa mara ili lugha yake iendane na wakati uliopo na mazingira tuliyomo? 

      Swali hili limezuka baada ya wafasri wa toleo jipya la mwaka huu la Biblia inayopendwa sana ya New International Version Bible (NIV) kuamua kutumia lugha inayoakisi usawa wa kijinsia. Kwa mfano, badala ya kusema, "If anyone says, 'I love God,' yet hates his brother, he is a liar.", sasa Biblia hiyo inasomeka "If anyone says, "I love God,' yet hates his brother or sister, he is a liar."

      Kuna wanaodai kwamba Biblia ni neno la Mungu na kamwe haipaswi kuwa inabadilishwabadilishwa kila mara mikondo au matapo ya mawazo yanapobadilika  katika jamii kwani kwa kufanya hivyo itafikia mahali tutakuwa tunapotosha kabisa maana iliyokusudiwa. Wewe unasemaje kuhusu suala hili?

      Kwa habari zaidi kuhusu utata huu wa tafsiri bofya HAPA (Tazama maoni mengi yaliyotolewa hapo). Unaweza pia kusoma kitabu kinachochambua japo hili kwa kina HAPA (pdf - kurasa 357)

      Monday, March 21, 2011

      WAKE ZA WATU NI HATARI !!!

      Katuni zina uwezo wa kufundisha na kuzungumzia mambo muhimu kwa ufupi na kwa uwazi. Ni chombo muhimu cha uelimishaji. Ndiyo maana mimi nazipenda sana!
      *************
      Katuni ni kutoka  Mambo ya Uswazi

      Nadhani katuni hii ni kutoka Global Publishers.

      MTOTO WA TAJIRI NA MTOTO WA MASIKINI - NA DUNIA ZAO KINZANI (UCHESHI)


      Nikitafsiri naweza kuharibu. Naiacha kama ilivyo.

      A second grade tacher at a private school for rich kids was teaching her science class about magnets and how they pick up things like metals objects. After the lesson, she quizzed her class and asked:

      "My name starts with 'M' and I pick things up. What am I?"

      A boy in the front row raised his hand and said,
      "You'are my maid!"

      Ati, angekuwa mtoto wa masikini 
      hapa angetoa jibu gani?

      Sunday, March 20, 2011

      Friday, March 18, 2011

      JK: MAPROFESA WANANISIKITISHA

      Maprofesa mpo? Wito huu mzuri kutoka kwa J.K.

      JK: Maprofesa wananisikitisha

      Na Jane Mihanji

      RAIS Jakaya Kikwete amewataka maprofesa na wasomi nchini kutunga vitabu ili kukabiliana na tatizo la kushuka kiwango cha elimu, kunakochangiwa na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada.

      Amesema anasikitishwa na kitendo cha maprofesa na wasomi chini kulalamikia upungufu wa vitabu katika fani mbalimbali, huku wakikwepa kutoa mchango wa kutatua tatizo hilo.

      Rais Kikwete amewata kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha anafanya jitihada za kuboresha elimu ili kuwa na kizazi kilichowiva kitaaluma.

      Alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Taarifa ya wizara iliyosomwa na waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, ilieleza uhaba wa vitabu ni moja ya matatizo yanayokwamisha sekta ya elimu.

      Dk. Kawambwa alisema shule nyingi zinakabiliwa na upungufu wa vitabu na katika baadhi, wanafunzi hutumia vya tofauti, tatizo linaloweza kupatiwa ufumbuzi kwa wasomi kujikita katika uandishi wa vitabu.

      "Hili ni tatizo, wakati tunasoma Msoga kitabu cha Bulicheka, mwanafunzi aliyekuwa akisoma Lindi alikisoma, lakini siku hizi mambo yamebadilika," alisema rais Kikwete na kuiagiza wizara kutoa kipaumbele katika uchapishaji vitabu vya kiada na ziada.

      "Lazima tupange kila mwaka bajeti ya kuchapisha vitabu vya watoto wetu, hatuwezi kuacha waendelee kuchangia vitabu kwa kuwa hili ni la kwetu, na hatuwezi kusubiri wafadhili," alisema.

      Alionya fedha za vitabu, maabara na ujenzi wa nyumba za walimu zisipelekwe katika matumizi mengine.

      Kwa upande wake, Dk. Kawambwa alisema wizara inakabiliwa na upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari, hususan katika mikoa ya pembezoni.

      Alisema pia kuna tatizo la kiwango kidogo cha ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na ualimu, hususan masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza.

      Waziri Dk. Kawambwa alisema ufinyu wa bajeti katika utekelezaji programu za elimu  na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu pia ni tatizo kubwa.

      Akizungumzia kiwango cha ufaulu, rais Kikwete aliwataka walimu wanaotunga mitihani ya shule za msingi, sekondari na vyuo, kuacha kutunga migumu kupita kiasi, kwa kuwa yawezekana kuwa ndicho chanzo cha matatizo.

      "Changamoto ya ufaulu mdogo kama mnavyodai katika masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza pengine inatokana na ugumu wa mitihani... lakini msitunge rahisi sana," alisema na kuongeza ni lazima wahitimu wawe na viwango vinavyostahili.

      Chanzo: Uhuru

      FIKRA YA IJUMAA: HATA MAFISADI, WANAFIKI, WEZI, WASALITI, WALAMBA VIATU NA MABARADHULI BADO WANAWEZA KUSEMA UKWELI !!!

      Katuni ni kutoka kwa Nathan Mpangala

      "A statement cannot be shown to be false merely because the individual who makes it can be shown to be a person of defective character"

      (Kanuni mojawapo dhidi ya argumentum ad hominem)

      Thursday, March 17, 2011

      LOLIONDO, LOLIONDOO, LOLIONDOOO - MPAKA LINI ???

      • Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia amedai kwamba  serikali imefikia kikomo cha kufikiri kuhusu utatuzi wa matatizo ya wananchi hasa wakati huu ambapo juhudi zote zimeelekezwa Loliondo badala ya kumakinikia masuala ya msingi yanayoikabili jamii. Msikilize Mbatia hapa chini (video kwa hisani ya Mtaa kwa Mtaa Blog.)



       Kwingineko

      (1) Mke na mume wanapofumaniana kwa babu


      (2) Wenye pesa zao sasa wanatua kwa helikopta

      Picha inapatikana HAPA

      (3) Mzee wa Kiraracha akitoa ushuhuda

      • Inasemekana sasa watu kutoka mataifa ya nje mpaka Afrika Kusini wanakuja kwa babu (Bofya HAPA). Dawa hiyo pia inasemekana inasaidia kurudisha "netiweki" kwa wanaume. Wanasiasa nao eti wanajaribu kufaidika kisiasa na tiba hiyo. Mungu Ibariki Tanzania!

        HILI NALO NENO: POLISI WAZUIA MAANDAMANO YA KUMUUNGA MKONO JK !!!

         
        Maandamano yalilengwa kuunga mkono hotuba hii ya JK.


        Polisi wazuia maandamano ya kumuunga mkono JK

        Imeandikwa na Hellen Mlacky
        Tarehe: 16th March 2011

        POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesitisha maandamano ya Kamati ya Vijana ya Watanzania na Wapenda Amani (KVT) ya kuunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete baada ya taarifa za uchunguzi kuonesha yatasababisha uvunjifu wa amani.

        Badala yake, vijana hao wameruhusiwa kufanya mkutano wao wa hadhara leo kuanzia saa 9 alasiri katika viwanja vya Bakhresa ambako mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa TLP Taifa na Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema.

        Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Fulgence Ngonyani alisema, walipokea barua ya maombi ya maandamano hayo Machi 11 kutoka KVT na lengo lao ni kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete.

        Barua hiyo kwa mujibu wa Kamanda Ngonyani, ilieleza kwamba kaulimbiu ya maandamano hayo ni ‘Amani yetu bado tunaipenda’ na yalikuwa yaanze saa 4 asubuhi kutoka Mnazi Mmoja kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na barabara ya Morogoro mpaka Manzese ambako mkutano huo utafanyika.

        Kutokana na uchunguzi uliofanywa Jeshi hilo, imebainika kuwa maandamano hayo yana muitikio mkubwa wa watu hivyo yanaweza kusababisha msongamano mkubwa na kusababisha uvunjifu wa amani.

        “Baada ya Polisi kupata taarifa ya maandamano hayo, tulifanya tathmini na kuamua kusitisha maandamano haya ...yanaweza kusababisha msongamano ambao ungetokana na kufungwa kwa barabara kwa muda mrefu na kusababisha kero kwa watumiaji wengi wa barabara hiyo,” alisema.

        Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo kama ni ya kuwanyima vijana hao haki yao ya kimsingi ya kuandamana, Ngonyani alisema: “Uhuru wa Mtanzania usifikie mahali ukaingilia uhuru wa watu wengine na Polisi imeahidi kutoa ulinzi wa kutosha ili mkutano huo ufanyike kwa amani na utulivu.

        Katibu Mwenezi wa KVT, Omari Genzeli aliyekuwepo katika mkutano huo, alisema maandamano hayo yalilenga kuunga mkono hotuba ya Rais na kupinga kauli za uchochezi zinazotolewa na Chadema na kwamba kusitishwa kwake wameona ni sawa kwa sababu lengo lao ni kutafuta amani na si vurugu.

        Chanzo: Habari Leo

        Wednesday, March 16, 2011

        TATIZO LA WANAUME KUPIGWA NA WAKE ZAO LINAZIDI KUJIIMARISHA !!!

        Inaonekana hili tatizo la wanaume kupigwa katika ndoa zao ni kubwa. Nimeshangaa kusikia katika video hii kwamba nchini Kenya eti theluthi moja ya wanaume wanakung'utwa majumbani mwao. Pengine ndiyo maana wenzao wa Tanzania waliamua kuanzisha chama chao kabisa. Jamii, hata hivyo, imekazania tu kupigania haki za wanawake. Na wanaume hawa je?


        Tuesday, March 15, 2011

        BINADAMU !!! (DAKIKA 2:04)

        JAKAYA MRISHO KIKWETE: TUMAINI LILILOREJEA - NA PRINCE M. BAGENDA (PORIS PRESS AGENCY, 2006)


         Angalizo
        • Lengo langu la kukiweka kitabu hiki hapa siyo kuanzisha mashambulizi ya ki-Ad Hominem dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilipokiona maktabani nilivutiwa nacho na niliamua kukisoma mara moja. Prince Bagenda ninayemfahamu ni mchambuzi makini na mwandishi mahiri; na umakinifu na umahiri huu unaonekana bayana katika kitabu hiki hasa katika makala zake nyingi alizowahi kuandika katika gazeti la Rai (lile la zamani!) - makala ambazo zimerejelewa pia katika kitabu hiki. 
        • Ni wazi kwamba kitabu hiki kiliandikwa katika mazingira ya mhemko wa kisiasa na kinaweza kuonekana kama kitabu ambacho kinaegemea zaidi katika propaganda za kumpigia debe mgombea wa wakati ule. Pamoja na ukweli huu, Jakaya Mrisho Kikwete: Tumaini Lililorejea kinaonyesha harakati na mshikeshike uliokuwapo wakati wa uteuzi wa mgombea wa urais mwaka 1995; na baadaye 2005 kwa undani kama vile Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania cha Mwalimu Nyerere kilivyofanya - japo kwa mitazamo tofauti. 
        • Kitabu kinaonyesha sababu zilizomfanya Kikwete ateuliwe kugombea urais mwaka 2005 baada ya kupoteza nafasi hiyo mwaka 1995. Akiwa rais kijana kuliko wote, mchapakazi na mwenye nidhamu ya hali ya juu, uteuzi wake ulifumbata matumaini makubwa kwa Watanzania; na kauli-mbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya ilirindima sawasawa katika masikio ya Watanzania. Pengine hii ndiyo sababu iliyomfanya Bagenda akiite kitabu hiki Tumaini Lililorejea.
        • Sijui Prince Bagenda angetoa tathmini yake sasa baada ya Mh. Dr. Rais Kikwete kumaliza kipindi chake cha kwanza na kuanza cha pili angesema nini kuhusu tumaini hili (WanaChadema tayari wanamtafuta HAPA). Kwa ujumla hiki ni kitabu cha kihistoria kinachofaa kusomwa na watu wote wenye kufuatilia hekaheka za kisiasa nchini mwetu, mapito yetu; na safari yetu ya kujikomboa inavyosonga mbele pamoja na changamoto zake nyingi!
        (1) Shukrani
        • Kitabu kimefadhiliwa na Mh.Sabodo, kada wa CCM mkereketwa na mpigania demokrasia ambaye katika siku za karibuni ametoa mchango mkubwa wa kuimarisha upinzani nchini kwa kuwa mfadhili mkubwa wa chama cha Chadema. Mh. Sabodo anatoa ushauri mzuri kuhusu jinsi ya kutokomeza ufisadi, mfumo wa elimu na mengineyo.

        (2) Utangulizi


        (3) Sifa za JK


        (5) Sababu za kushindwa kwa upinzani


        Kitabu kina kurasa 289. 
        Sina uhakika kama bado kinapatikana katika maduka ya vitabu. Kama nilivyosema hapo juu, kitabu hiki kinafaa kusomwa, japo ni katika muktadha wa kihistoria zaidi. 

        Monday, March 14, 2011

        MGENI NJOO MWENYEJI APONE: TAARIFA YA HABARI NA STAR TV KUHUSU TIBA YA LOLIONDO


        Video kwa hisani ya Kennedy

        CCM YAMTABIRIA SLAA URAIS - BAADA YA MIAKA 50 !!!

        John Guninita - M'kiti wa CCM Dar


        *Yadai CHADEMA ilichangia mauaji Arusha
        Na Anneth Kagenda,Temeke

        CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, aendelee kufanya mazoezi ya kuingia Ikulu kwani huenda baada ya miaka 50 ijayo atanyakua nafasi hiyo. Pia kimeitaka Serikali kuacha kumtafuta mchawi katika tukio la mauaji lililotokana na maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Arusha na badala yake iwakamate viongozi wa juu wa chama hicho akidai kuwa wamekuwa wachochezi wakuu wa kuvuruga amani nchini.

        Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Temeke Mwembe Yanga wakati akijibu hoja mbalimbali zinazohusu chama hicho.

        Amesema Dk. Slaa aendelee kuhangaika kutafuta urais labda huenda ipo siku Mungu atamuona na kumbarikia urais.

        Amesema kama wao walijiona ni ‘ngangari’ kwanini hawakuingia kituoni kuchukua silaha na badala yake waliwashinikiza wananchi.

        “Naunga mkono kauli ya waziri Mizengo Pinda bungeni kwamba CHADEMA ndio waliosababisha vurugu na vifo vya watu na hii ni kutokana na kukosa hoja ya kuing'oa CCM madarakani na badala yake wanatangaza udini makanisani eti mchague Wakristo ndio wenye hoja za msingi,” amesema Gugunita.

        Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Ramadhan Madabida, amesema mfanyabiashara atakayepandisha bei ya sukari zaidi ya sh. 1,700 atanyang'anywa leseni yake ya biashara.

        CHANZO: Dar Leo

        Saturday, March 12, 2011

        KUISHI USWAHILINI KUNA RAHA ZAKE!!!!

        (1) Wapangaji wenzangu mko fuluu?

        • Ukizoea ya uswahilini kwenye uhuru, ya uzunguni kwenye mageti huyawezi; na ukizoea ya uzunguni kwenye mageti, ya uswahilini kwenye uhuru huyawezi. Uswahilini vs Uzunguni - dunia mbili kinzani: huku ni wasionacho na kule ni wenye kila kitu. Dunia ! 
        (2) Mithili ya helikopta ya Mbowe

        Friday, March 11, 2011

        KWA WOTE MLIOKO JAPAN NA HASA WATANZANIA WENZETU: POLENI SANA NA TUNAWAOMBEA !!!

        Ukurasa wa mbele wa Huffington Post leo
        • Poleni kwa kukumbwa na tetemeko hili kubwa pamoja na Sunami iliyofuatia. Mungu Awashike mkono na kuwatia nguvu. Tunaomba na kutumaini kwamba hakuna Mtanzania aliyepoteza/atakayepoteza maisha. Amina !!!

          FIKRA YA IJUMAA: PENYE NIA PANA NJIA (MAKALA YANGU YA KWANZA MAREKANI !!!)

          • Ilikuwa ndiyo tu nimefika kuanza shahada ya Uzamili (Isimu) katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA). Kutokana na misingi legelege niliyokuwa nayo katika uwanja wa isimu (japo kule nyumbani eti nilikuwa ndiyo kipanga!), masomo (hasa upande wa nadharia) yalikuwa magumu sana kiasi cha kukatisha tamaa kabisa (Watanzania wengi waliokuja kusoma shahada za juu moja kwa moja hapa Marekani nadhani wanalitambua hili!).
          • Japo nilikuwa nimeonywa kuhusu jambo hili, kamwe sikutegemea kwamba masomo yangenichachafya kiasi hiki na kuninyima hata muda wa kupumua. Na kama vile sikuwa na matatizo ya kutosha, nilikuwa pia sijui kutumia kompyuta. Kwa hivyo mazoezi yote ya darasani na makala ya muhula ilibidi yaandikwe kwa mkono!
          • Kama hii haitoshi, tofauti za kitamaduni pia zilikuwa zinanihangaisha. Kinyume na kule nyumbani ambako maprofesa wanaogopwa na kuonwa kama vile "miungu wadogo", hapa "wamiliki maarifa" hawa ni marafiki na mwanafunzi una uhuru wa kwenda kukaa nao wakati wo wote na kujadili masuala mbalimbali - ikiwemo alama yako ya mwisho wa muhula na hata masuala mengine ya maisha bila wasiwasi wo wote.
          • Pamoja na vipingamizi vyote hivi, kijana wa Kitanzania niligangamara na kupigana kiume mpaka mwisho. Haya ni makala yangu ya kwanza katika darasa la Fonolojia (tazama pia HAPA) wanafunzi wa shahada ya kwanza. Makala haya ya kitoto ni ya muhimu sana kwangu kwa sababu, mbali na sababu zinginezo, Profesa wa somo hili ni Mwanafonolojia anayeheshimika duniani kote na anajulikana pale idarani kwa "ukali" na uhitaji wake wa kazi zenye kiwango cha juu sana. Yeye huwa hapendi mzaha wala mchezo!
          • Nakumbuka aliponiita ofisini kwake na kuniambia kwamba alikuwa ameyapenda haya makala yangu ya kwanza. Alinihakikishia kwamba hakukuwa na sababu yo yote kwangu kuwa na wasiwasi kwani kulingana na maoni yake baada ya kuisoma makala yangu haya alikuwa amefikia hitimisho kwamba nilikuwa ninahitaji kozi nyingine moja tu ya shahada ya kwanza katika Fonolojia ili kuwa na misingi sahihi ya kufanya vyema sana katika masomo ya shahada zangu za juu.
          • Maisha ni mapambano na kabisa hakuna haja ya kukata tamaa. Na kweli baada ya miaka miwili nilipata shahada yangu ya uzamili; na baada ya miaka mitatu mingine nikaipata shahada ya Uzamifu (Ph.D).
          • Nakumbuka baada ya kutetea tasnifu yangu kwa mafanikio, profesa huyu alinishika mkono na kunikumbusha kuhusu karatasi yangu hii ya kwanza huku akiniambia kwa sauti ya msisitizo "Matondo, nilikwambia!" Aliendelea kuniambia kwamba utetezi wa tasnifu yangu ulikuwa umefanikiwa vizuri na uwasilishaji wa mada yangu ulikuwa umeandaliwa na kupangwa vyema kiasi kwamba hakuwa na maswali mengi. Kilichobakia ilikuwa ni kusherehekea. Na tangu siku hiyo nikaanza kuitwa Dr. Matondo !!! Ati, ningekatishwa tamaa na hekaheka za mwanzo ingekuwaje?
          • Tusikate tamaa na tukumbuke kwamba vitu vyema daima huwa havipatikani kwa urahisi wala kwa njia za mkato! Ukitaka kuyasoma makala haya au kuona alama ambayo nilipata bofya HAPA (pdf).
          Tuonane tena wakati mwingineo tukijaliwa!
          Tusikate tamaa !!!

          ***************************

          Thursday, March 10, 2011

          MWANAUME AUAWA KWA KUZUIA MVUA !!!

          • Kama jamii, bado tuna safari ndefu ya kwenda. Ni haki kweli katika karne hii na wakati huu bado tunauana kwa sababu ya kuzuia mvua? Imani hizi za kishirikina zinazozidi kujiimarisha zinatupeleka wapi lakini? Tatizo hasa ni nini? Ni umasikini? Ni ugumu wa maisha? Ni mfumo mbovu wa elimu? Ni nini? Tufanye nini?
          *************************
          Mwanamume auawa kwa kuzuia mvua 
          (Wednesday, 09 March 2011)

          Na Mwandishi Wetu, Dodoma

          EREST Khamis (45), mkazi wa Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kushiriki kumuua baba yake mzazi wakimtuhumu kuzuia mvua kunyesha mkoani humo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zellothe Stephen, amesema tukio hilo limetokea jana saa 2 usiku wilayani humo.

          Amesema mtuhumiwa huyo alimshambulia baba yake, Khamis Hussein (70), kwa kumpiga kwa madai kuwa ndiye aliyesababisha mvua isinyeshe katika mkoa huo.

          Ameongeza kuwa kulikuwa na taarifa za muda mrefu kuwa marehemu alikuwa akihusika katika uzuiaji wa mvua ambapo baadhi ya wanakijiji walimfuata mtoto wake huyo na kumuelezea kero hiyo.

          Kutokana na kitendo hicho, mtoto huyo aliamua kumpiga baba yake kwakuwa ndiye anayejua ukweli wa madai hayo na polisi watamfikisha mahakamani.

          Chanzo: Dar Leo 

          Mzunguko wa Maji - Kwa mtazamo wa "wanasayansi"

          JIANDIKISHE HAPA

          Enter your email address:

          Delivered by FeedBurner

          BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO