NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, April 27, 2011

Hatimaye Obama Awakata Ngebe Wanaodai Kwamba Hakuzaliwa Marekani

Picha hii ya kejeli iko HAPA
  • Hivi karibuni, Donald Trump, bilionea mhafidhina na mpenda majivuno amelifufua suala hili kwa nguvu zote wakati akijiandaa kupambana na Obama katika kinyang'anyiro cha urais mwaka kesho. Ngoja tuone kama cheti hiki kipya kitawanyamazisha hawa wahafidhina. Donald Trump mwenyewe tayari anajivuna kwamba juhudi zake ndizo zimemlazimisha Obama kutoa hiki cheti chake cha sasa. 
Nakala ya cheti kipya. 

Sunday, April 24, 2011

Friday, April 22, 2011

JELA MWEZI MMOJA KWA KUKOJOA OVYO !!!

  • Naona ile sheria ya usafi wa mazingira iliyopitishwa na serikali kimchezomchezo tu imeanza kuzingatiwa na mkazi mmoja wa Ubungo jijini Dar aitwaye Dismas Geogre (25) amehukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kujisaida haja ndogo katika eneo lililokatazwa kisheria. Japo tabia hii ya kukojoa hovyo hovyo inakera, mimi nadhani sheria hii peke yake haitaweza kutatua tabia hii kama kiini chake hasa hakitafahamika. 
  • Ati, ni kwa nini watu wanapenda kukojoa hovyo hovyo? Ni kwa sababu ni wachafu na hawajali? Ni matokeo ya mila na utamaduni wao? Au pengine ni kutokana na ukosefu wa vyoo vya umma vilivyo safi na tayari kwa matumizi? Vyoo vingi vya umma (hata vile vya kulipia) ni vichafu kupindukia, vinanuka sana na havina maji wala karatasi za kujisafishia. Kwa nini basi mtu asijibanze kando ya mti au uchochoroni akamaliza haja yake chapu chapu na kwenda zake? Si budi basi tatizo liangaliwe katika upana wake vinginevyo magereza yatafurika wafungwa wenye makosa ya kukojoa vichochoroni kama kweli serikali imedhamiria kuitekeleza sheria hii kwa hali na mali!
~~~~~~~~~~
Afungwa jela baada ya kukiri kukojoa ovyo

Imeandikwa na Oscar Job
Tarehe: 21 Aprili 2011 

MKAZI wa Ubungo, Dismas Geogre (25) amehukumiwa kifungo cha mwezi mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kujisaida haja ndogo katika eneo lililokatazwa kisheria.

Hukumu hiyo imetolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Sokoine Drive (Jiji), William Mutaki baada ya mshitakiwa huyo kukiri kutenda kosa hilo.

Awali Mwendesha Mashitaka, James Munga alidai kuwa Aprili 17 mwaka huu mshitakiwa alikutwa akikojoa katika eneo la Ubungo Kisiwani kinyume na sheria.

Kwa mujibu wa madai hayo, mshitakaiwa alikutwa na Ofisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Evarist Msigwa akikojoa katika eneo hilo ambalo si rasmi kwa shughuli hiyo na kukaidi agizo hilo lililotolewa na Manispaa hiyo.

Alisema, mshitakiawa huyo alifanya hivyo huku akitambua wazi kuwa kosa hilo ni kinyume na Sheria Ndogo ya Usafi wa Mazingira ya Manispaa ya Kinondoni iliyoanzishwa 2002.

Baada ya mshitakiwa kukiri kosa hilo, Mwendesha Mashitaka alimuomba Hakimu kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Kutokana na maombi hayo, Hakimu Mutaki alimuhukumu mshitakiwa huyo kulipa faini ya Sh. 50,000 au kwenda jela mwezi mmoja kutumikia kifungo na kutokana na mshitakiwa kukosa fedha hizo, alipelekwa jela kutumikia kifungo hicho.

Chanzo: Habari Leo.

Sunday, April 17, 2011

BAKITA LAWASHUKIA WABUNGE: NI KUHUSU KUCHANGANYA LUGHA BUNGENI

  • Huwa unajisikiaje unapomsikia mbunge wako akitoa hoja bungeni huku akichanganya Kiswahili na Kiingereza? Huwa unamwelewa? Kama huwa unamwelewa basi ni wazi kwamba unafahamu Kiingereza. Ingekuwaje kama ungekuwa hufahamu Kiingereza? Wabunge hawa wanapochanganya lugha namna hii, huwa wanafikiria kwamba kuna watu wanaowawakilisha ambao Kiingereza hawakifahamu (vizuri)? Kuna ulazima wowote kwa "waheshimiwa" hawa kuchanganya lugha namna hii? Wewe nawe huwa una tabia ya kuchanganya lugha katika mazungumzo yako? Kama jibu ni ndiyo, ni kwa nini huwa unafanya hivyo? 

****************
BAKITA lawashukia wabunge
(Alhamisi, 14/4/2011)

*Wadaiwa kuwaacha wananchi hewani
*Latamani kuwafunda
*Lugha yatajwa tatizo

Na Simon Nyalobi, Jijini

BARAZA la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) limewakumbusha wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutumia Kiswahili pekee badala ya kuchanganya na Kiingereza kwani linawafanya wananchi kutoelewa vizuri hoja zao.

Akizungumza juzi na Dar Leo Ofisini kwake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Bakita, Noel Karekezi, alisema wabunge wanatakiwa kulitambua hilo kila wanapochangia hoja zao ili waeleweke na wananchi.

“Malalamiko yetu tangu awali ni uchanganyaji wa Kiswahili na Kiingereza. Unakuta wanajisahau kuwa wanazungumza wenyewe kumbe wanasikilizwa na wananchi wengi,” alisema.

Amesema kuchanganya lugha hizo kunawafanya wananchi kushindwa kuelewa hoja wanazozitoa na hivyo kuwataka kujifunza kutumia Kiswahili wakati wakitoa hoja zao.

Amekiri suala la uchanganyaji wa lugha hizo ni la kitaifa kutokana na mazoea yaliyojengeka katika jamii.

“Wakati mwingine tatizo la kuchanganya lugha ni gumu kuliacha kwa sababu unakuta Kiswahili unatumia nyumbani na Kiingereza unatumia ofisini,” alisema.

Ameongeza kuwa BAKITA ina azma ya kuwapa semina wabunge hao, lakini kutokana ufinyu wa bajeti wameshindwa kutimiza azma yao lakini bado wataendelea kuwakumbusha juu ya matumizi ya Kiswahili.

Katika hatua nyingine, Kaimu Katibu Mtendaji huyo amesema wahisani wengi toka nje ya nchi wamekuwa wazito kukubali kufadhili uenezwaji wa lugha ya Kiswahili kwa kile alichodai kuwa wengi wanataka lugha na tamaduni zao ziendelezwe.

Chanzo: Dar Leo.
  • Ni kutokana na kikwazo hiki cha lugha kwamba serikali imeamru muswada tata wa katiba uandikwe katika Kiswahili kwanza ili uweze kusomwa na Watanzania walio wengi. Pengine huu ni ushahidi kwamba Kiingereza kimeshatushinda na inashangaza kidogo kuona kwamba hatufanyi lolote la maana katika kurekebisha sera yetu kengeufu ya lugha. Hata Profesa Mbele alishawahi kuombwa kuandika kwa Kiswahili kwa sababu Kiingereza hakieleweki!
  • Msikilize Anna Makinda hapa akitoa ufafanuzi kuhusu suala la lugha katika muswada wa sasa wa katiba. 

Wednesday, April 13, 2011

SALA YA KUOMBEA KUSHUKA KWA BEI YA MAFUTA HAPA MAREKANI !!!

Picha hii iko HAPA
  • Galoni moja sasa inakaribia kuwa dola 4. Hii ni bei kubwa mno kwa Wamarekani ambao, japo ndiyo watumiaji wakuu wa nishati hapa duniani, pia wamezoea kuipata nishati hiyo kwa bei rahisi. Naamini huko Uingereza na kwingineko (ambako mafuta yanauzwa kwa lita) pengine bei ni kubwa zaidi.  
  • Kama imani yaweza kuhamisha milima, bila shaka yaweza hata kushusha bei ya mafuta. Tazama HAPA kuhusu pasta mmoja kule Georgia ambaye ameamua kuendesha sala ili kuombea kushuka kwa bei ya mafuta.

      ETI, SASA HUYU NDEGE ATARUKA KWA KASI ZAIDI ???

      • Sote tumeona. Ndege mkongwe amejichojoa manyoya ya zamani na kujiotesha manyoya "mapya" yameremetayo japo kwa staili ya "kiurithirithi". Inavyoonekana ndege huyu mpya-mkongwe ameamua kweli kweli kujijengea mazingira mapya na ameanzisha "vita" kuhakikisha kwamba manyoya ya zamani yanabakia kuwa chojozi. Japo baadhi ya waangalizi wa ndege huyu wamefurahia kujichojoa kwake, swali linaloulizwa na mwanakatuni nambari wani wa Tanzania kwa sasa ni hili: Haya manyoya mapya kweli yatamwezesha huyu ndege mnono mpya-mkongwe kuruka kwa kasi zaidi? Tunamtakia urukaji wa kasi mpya mzuri !!! 
      • Wanachama wa CCM waliochaguliwa kuunda sekretarieti mpya  kutoka kushoto ni Mweka Hazina mpya wa CCM taifa Mwigulu Lameck Nchemba, Katibu Itikadi Mwenezi wa CCM taifa Nape Moses Mnauye, Katibu Organaizesheni NEC Bi Asha Abdullah Juma, Naibu Katibu mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai na January Makamba uhusiano Kimataifa. Picha hii na zingine kuhusu uchojoaji huu wa manyonya zinapatikana HAPA.

        Video kwa hisani ya Kennedy

        ~~~~~~~~~~~~~~~
        Nyongeza (16/4/2011)
         Picha kutoka kwa Mjengwa

        Sunday, April 10, 2011

        KUTIMULIWA KWA AKINA MAKAMBA NA WENZAKE: CCM IMEANZA KUJISAFISHA (AKA KUJIVUA MAGAMBA)!?!?

        • Na gamba mojawapo lililovuliwa ni la Mbunge wangu! Na kama alivyosema Mjengwa, ngoja tuone CCM itafanyaje na magamba haya yaliyovuliwa ambayo mimi napenda niyaite magamba sugu! Itayafukia, itayaacha yakitapakaa au itayachoma moto kabisa na kuyateketeza? Baada ya kusukwasukwa huku na huko katika uchaguzi uliopita, ni wazi kwamba CCM imeamka na naamini kwamba hatua hii ni mwanzo (mzuri) katika kujaribu kurudisha imani yake kwa wananchi kwani mwaka 2015 si mbali sana. Ikishupalia ufisadi inaweza kujiokoa! Ngoja tuone! Kwa habari zaidi soma HAPA na HAPA
        • Habari zaidi zinapatikana kutoka gazeti la Majira na Uhuru. Majigambo ya CHADEMA kuhusu suala hili yanapatikana HAPA.

        Friday, April 8, 2011

        BAJAJI YA ZIMA MOTO !!!

        Inaonekana bajaji zimegeuka kuwa mkombozi wetu. Tunazo za kubebea wagonjwa; na sasa zima moto.

        Waziri Mkuu Mizengo Pinda akikagua Bajaj ambayo imetengenezwa ili kumudu kazi ya kuzima moto hasa kwenye maeneo yenye barabara nyembamba katika maonesho yaliyoandaliwa na Kampuni ya Spray and Fumigation Services Limited, bungeni Dodoma Alhamisi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu). 

        Chanzo: Habari Leo (8/4/2011)

        FIKRA YA IJUMAA: ATI, ULIOWAACHA CHINI WANGALI BADO WANAKUONA???

        ...Au unasubiri mpaka siku utakayoporomoka (au siku watakayokuporomosha) ndipo muonane ? 
        ~~~~~~~~~~~~~~~
        Hebu tumpe nafasi Friedrich Nietzche (aka Mwanafalsafa Kichaa) atutafakarishe. Wikiendi Njema!

        Thursday, April 7, 2011

        NYUMBANI BARIADI KUNA NJAA MWAKA HUU !!!

        Mvua mwaka huu hazijanyesha kabisa Wilayani Bariadi; na kwa vile kilimo chetu bado ni cha kutegemea maji ya mvua, matokeo yake ndiyo haya: njaa! Hata hivyo wilaya hii ina bahati ya kuwa na wabunge machachari na wenye uwezo mkubwa wa kifedha na kiushawishi (Mzee wa Vijisenti na Bwana Mapesa). Natumaini kwamba wabunge hawa watashirikiana vyema na serikali pamoja na wananchi ili kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi wa Bariadi anayekufa kwa njaa. Naamini kuna maeneo mengine nchini ambayo yana tatizo hili lakini hatuyasikii kwa sababu kwa kawaida vyombo vyetu vya habari havina tabia ya kuripoti mambo ya vijijini (isipokuwa kama ni habari za kusisimua kama mauaji na ajali za kutisha). Kwa sasa hali ni mbaya zaidi kwani juhudi zote zimeelekezwa Loliondo. 
        *********************

        Wananchi Bariadi Walia Njaa

        Jumatatu, 04 Aprili 2011
        Zulfa Mfinanga,  Bariadi

        SERIKALI imeombwa kuwapelekea chakula wananchi wa Kata ya Kinangw’eli, Gilya na Mwaumatondo wilayani Bariadi mkoani Shinyanga ili kuwanusuru wananchi hao kupoteza maisha kwa kukosa chakula kutokana na mazao yao kukauka kwa  jua.

        Ombi hilo lilitolewa juzi kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hizo kwa nyakati tofauti kwa Mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga  ambaye yuko katika ziara ya wiki moja ya kutembelea kata za wilaya hiyo kujionea hali ya chakula sanjari na kukagua vocha za kilimo zilizotolewa na serikali kama zimewafikia walengwa.

        Kilio hicho cha wananchi kilifuatia siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuagiza kusambazwa kwa chakula cha msaada katika kukabiliana na tatizo la njaa maeneo mbalimbali hapa nchini.

        Baadhi ya wananchi hao, Paul Jilumbi na Pambalu Lufungulo wote wakazi wa Kijiji cha Kinang'weli, walisema kuwa ni vema serikali ikapeleka chakula cha msaada chenye bei nafuu ili wananchi wenye uwezo wanunuwe kabla hawajamaliza kuuza mifugo na akiba ya pesa walizoweka na hivyo chakula kuishia kwa baadhi ya watu wasio na uwezo kabisa.

        “Kilio chetu kikubwa wananchi wa kata hizi hatuna chakula, mazao yetu yamekauka na jua, tunaiomba msikie kilio chetu, tupatiwe mapema chakula cha msaada la sivyo njaa itatuua”, walisema.

        Naye mkuu wa wilaya hiyo, Baraka Konisaga alisema kuwa tayari tathimini imeshafanyika ili kujua hali halisi ya upungufu wa chakula katika wilaya hiyo na kupeleka takwimu hizo Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa kwa ajili ya kusaidia  maeneo yaliyokumbwa na njaa kali.

        Chanzo: Mwananchi

        Wednesday, April 6, 2011

        AKINA NGOSHA MPO? UGALI WA UHAKIKA HUOOO !!!

        IT IS OFFICIAL: TANZANIA NI NCHI YA "VIKOMBE". MMOJA AIBUKA IRINGA NA MWINGINE SUMBAWANGA !!!

        Kweli mpango mzima sasa ni kumfotokopi Ambilikile tu. 
        Hii ni katuni ya Mambo ya Uswazi.
        ~~~~~~~~~~~~~~~~~~
        Dkt Antony Mwandulami (58) mkazi wa kijiji cha Itunduma Wangama wilaya ya Njombe Mkoa wa Iringa, ameibuka na kuanza kutoa tiba kwa wagonjwa kwa mtindo wa babu wa Loliondo

        ******************
        • Ilianzia Samunge Loliondo. Baadaye Rombo, Mbeya (kule Mbarali pia kuna kingine), Bagamoyo, Tabora, Morogoro, Magu na sasa Iringa. Na kote huko kote kunafurika watu, na wengi wanadai kuponywa na kikombe. Na watoa dawa wote hawa wanadai kuwa wameoteshwa ama na Mungu au na ndugu zao ambao ni marehemu. Tuhitimishe nini kuhusu mkururo huu wa tiba hizi za miujiza (aka vikombe)? Ni Mungu Ameanua kuishushia neema Tanzania kwa kuiporomoshea waotaji wengi hivi kwa mpigo ama? 
        • Mjadala mkali kuhusu suala hili ulirindima kule kwa Mjengwa na kwingineko; na inavyoonekana Watanzania wamegawanyika kuhusu suala hili: (1) Wapo wanaoziona tiba hizi kama neema kwa Watanzania wengi ambao ni masikini na wameteseka kwa muda mrefu kutokana na huduma mbovu za kiafya kiasi kwamba wamekata tamaa. (2) Wapo wanaoona matukio haya kama dalili za mwisho wa dunia kama inavyorejelewa katika misahafu mbalimbali ya dini. (3) Wapo ambao hawajui kinachoendelea; na ambao wanasubiri uthibitisho wa kisayansi ili wajue kama kweli tiba hizi zinatibu ama la (bila kujali kwamba mambo ya kiimani kama haya wakati mwingine yanaweza kukinzana na sayansi!). (4) Wapo wanaoona jambo hili kuwa ni njama za wanasiasa ambao wanafurahia kuona kwamba mambo haya yanavutia sana vyombo vya habari kiasi kwamba mambo mengine ya muhimu hayapewi uzito wo wote. (5) Wengine wanaamini kwamba huu ni utapeli tu unaopoteza maisha ya watu bure!
          • Wakati huo huo kuna watu ambao wamekiri kabisa kuwa tiba hizi za kiimani zimewaponya magonjwa yao sugu. Wapo pia ambao wanadai tiba kama hizi hazikuwasaidia. Na kwa vile (eti) imani yako ndiyo inakuponya - ni vigumu kuweka tathmini ya kisayansi kuhusu madai haya na kufikia majumisho yenye kuelezeka. Imani!
          Kombora kwa Babu kutoka Global Publishers HAPA.
            • Ni nini hasa kinaendelea katika suala hili. Kwa nini Tanzania? Kwa nini wakati huu? Ni wazi kwamba maswali ni mengi kuliko majibu. Ngoja tuone hili sokomoko la vikombe litakakoishia. 
            Kwa picha na habari zaidi kuhusu kikombe cha Iringa bofya HAPA. Kikombe cha Sumbawanga bofya HAPA

              Tuesday, April 5, 2011

              LUGHA YA KUFUNDISHIA TANZANIA: TUTAENDELEA KUJICHANGANYA MPAKA LINI ???

              • Mimi nilikuwa nafikiri kwamba mapendekezo ya sera yetu mpya ya lugha iliyotolewa mwaka 1999 yalikuwa yanalenga katika kuanza kutumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia kuanzia shule za msingi; na kwamba maandalizi ya kiutekelezaji yalikuwa yakifanyika. Ina maana Kiswahili bado kinafikiriwa kuwa lugha ya kufundishia katika shule za sekondari na elimu ya juu japo ni mpaka kitakapokidhi haja? Kipi kinaendelea hapa? 
              • Yote kwa yote, nikiwa kama mkereketwa wa mambo ya lugha na utamaduni, kauli hii ya Mh. Dr. Nchimbi imenifurahisha. Kumbe mkabala wa Kiswahili si mbaya kama wakati ule wa Mh. Mungai.
               
              *****************

              Nchimbi: Kiswahili kutumika kufundishia kikikidhi haja

              NA HAMIS SHIMYE
              Monday, 04 April 2011

              SERIKALI imesema ipo tayari kuunga mkono jitihada za lugha ya Kiswahili kufundishiwa elimu ya juu, ikiwa utafiti na machapisho ya lugha hiyo yatakidhi haja. Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana, kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI). 

              Kilele kitakuwa Oktoba 26, mwaka huu. Dk. Nchimbi alisema dira ya TATAKI ni kuwa kitovu cha ufundishaji, utafiti, maendeleo, ubora na ubobezi katika lugha, fasihi na utamaduni wa Kiswahili.

              Chanzo: Uhuru

              Monday, April 4, 2011

              MAMA WEE: KATOTO KETU "KAKOROFI" KANACHARAZWA BAKORA HUKU KAKIWA MGONGONI MWETU !!!

              Hatujui malezi au katoto ketu "kakorofi" kanaonewa?

              Kama kawaida ni Said Michael.

              MWANABLOGU MWENZETU APONA UGONJWA WAKE SUGU BAADA YA KUNYWA KIKOMBE CHA BABU LOLIONDO !!!


              Ni Mwanamke wa shoka Florah Lauwo wa Florah Talent Promotion ya jijini Mwanza

              Bila woga wala aibu, ameeleza kwa undani jinsi safari yake ilivyokuwa, maajabu aliyoyaona kwa Babu Loliondo na mengineyo.

              Cha muhimu zaidi ni kwamba amekiri na kutoa ushuhuda kupona ugonjwa sugu wa pumu uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

              Ifuatilie safari yake ya kwenda Loliondo HAPA.

              ****Kwingineko*****

              (1) Pesa zilizopatikana Loliondo mpaka sasa ni milioni 50! 

              (2) Wagonjwa waliofariki Loliondo mpaka sasa ni 78!

              (3) Vigogo wa serikali wameanza tena kumiminika Loliondo. Safari hii ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira (aka Tyson) na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono. Pia usikose kuwatazama Orijino Komedi hapa chini wakilalamikia tabia ya Watanzania ya kuigaiga mambo  na kukosa ubunifu. 

                KIFO KINAWEZA KUBISHA HODI WAKATI WO WOTE: MHADHIRI UDSM AFARIKI AKIFUNDISHA.


                Pumzika salama Dr. Justine Katunzi!

                *******************

                Mhadhiri UDSM afa akifundisha

                NA MWANDISHI WETU

                MHADHIRI Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mbunge wa zamani wa Geita, Dk. Justine Katunzi, amefariki dunia, baada ya kuanguka akiwa anafundisha.

                Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, mhadhiri huyo alifariki dunia juzi, muda mfupi baada ya kuanguka akiwa darasani.

                Taarifa hiyo ilisema baada ya kuanguka alipelekwa katika zahanati ya chuo hicho, ambako alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa. Mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake Kimara Stop Over, Dar es Salaam.

                Dk. Katunzi alikuwa akifundisha katika Shule ya Biashara ya chuo hicho, na alijiunga na UDSM mwaka 1976 akiwa mkufunzi msaidizi na baadae mwaka 1978 alipandishwa cheo na kuwa mhadhiri msaidizi.

                Alipanda ngazi na mwaka 1980 alikuwa mhadhiri, na mwaka 1998 alipanda daraja kuwa mhadhiri mwandamizi hadi alipostaafu kwa mujibu wa sheria mwaka jana. Aliendelea na kazi kwa mkataba wa miaka miwili.

                Kitaaluma alikuwa amebobea katika fani ya menejimenti, akiwa mmoja wa waasisi wa Kitivo cha Biashara na Menejimenti (sasa Shule ya Biashara).

                Profesa Mukandala alisema katika kipindi chote cha utumishi wake ana mchango mkubwa katika uandishi wa majarida, utafiti na machapisho mbalimbali ya kitaaluma. Kati ya mwaka 1990 na 1995 alikuwa mbunge wa Geita.

                Chanzo: Uhuru

                JIANDIKISHE HAPA

                Enter your email address:

                Delivered by FeedBurner

                BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO