NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, May 17, 2011

Ati, Uraia wa Marekani wa Waziri Huyu Ndiyo Chanzo cha "Uvivu" Wake ???

  • Japo mimi si mwanasheria lakini pengine sitakosea nikisema kwamba Waziri huyu, kama kweli ana uraia wa Marekani atakuwa amevunja sheria kwani ninavyojua mimi Tanzania bado haijaruhusu uraia wa nchi mbili; na sina uhakika kama raia wa nchi nyingine anaweza kuwa waziri nchini Tanzania. Wanasheria mnajua.
  • Kilichonivutia katika habari hii ni lile dai kwamba waziri huyu anaonekana kuwa mvivu kutokana na ukweli kwamba eti anajali masuala ya Marekani zaidi kuliko ya Tanzania kutokana na ukweli kwamba yeye ni raia wa Marekani. 
  • Katika mijadala mingi kuhusu suala la uraia wa nchi mbili, hoja mojawapo ya msingi iliyotolewa na wale wanaopinga ni kuhusu wasiwasi wa kutokuwa na uzalendo kwa Watanzania watakaokuwa na uraia wa nchi mbili. Ni vigumu kuwatumikia mabwana wawili ati! 
  • Mimi nadhani "uvivu" wa mawaziri na watendaji wengine wakuu wa serikali ni tatizo la kimfumo zaidi kama bosi wao alivyowalalamikia kwa uchungu hivi karibuni HAPA na HAPA. Ni mawaziri wangapi ambao wanatazamwa vizuri na umma kuwa ni wachapa kazi, mawaziri ambao wanaweza kusimama na kusema kwamba wizara zao zimefanikiwa katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi? Wizara nyingi zinakumbwa na matatizo ya kiutendaji yakiwemo tuhuma za ufisadi. Hawa nao wana uraia wa nchi gani? Tunaweza kusema kwa uhakika kwamba "uvivu" wa Waziri huyu ni matokeo ya kuwa na uraia wa nchi mbili?
  • Unaweza kusoma mijadala mbalimbali kuhusu suala hili HAPAHAPA, HAPA na HAPA kuhusu suala hili.
**************

Pichani kushoto ni Waziri Cyril Chami na kulia ni 
Naibu wake Lazaro Nyalandu

Kufuatia sakata lililoibuliwa na gazeti la Dira ambalo liko mtaani leo lililoripoti kuwa kuna waziri mmoja kutoka wizara ya viwanda na biashara mwenye uraia wa Marekani, habari hiyo inaweka wazi kuwa waziri huyo amekuwa na tabia ya kipuuzi ya kumpeleka mkewe kujifungulia Marekani mara tu mkewe anapobakiza wiki mbili kabla ya kujifungua hali inayofanya watoto wake wawili kuwa na uraia wa taifa hilo tajiri zaidi duniani.

Waziri huyo kijana ana uraia wa Marekani hali inayodaiwa imeathiri uwajibikaji wake kwani amekuwa na uvivu wa kupindukia huku akili na moyo wake akielekeza Marekani. Blog yako hii ya kisiasa imefanya mahojiano na wasomi mbalimbali katika eneo la Mlimani la chuo kikuu cha Tanzania ambapo wasomi hao wamemtaka rais Jakaya Kikwete kumtimua kazi mara moja waziri huyo ambaye wamedai kuwa kwa tabia hiyo maana yake haipendi Tanzania, hana uzalendo, hafai kuwa kiongozi hivyo ang'olewe maramoja.

Chanzo: Nova Kambota

Monday, May 16, 2011

Shule ya Sekondari ya Buluba Mkoani Shinyanga Nayo Yapata Mtoa Kikombe !!!

  • Shule hii ya Buluba naifahamu vizuri kwani niliwahi kupangiwa kwenda kufanya mazoezi ya kufundisha hapo japo baadaye nilibadilisha na kwenda mgodini Mwadui kwenda kushangaa makaburu wanavyosomba almasi zetu huko na kuwaacha Wasukuma wakiwa hawana cho chote. 
  • Wapo vijana wengi wanaoacha masomo kwa sababu za kupita kama hizi halafu baadaye wanakuja kujuta. Mimi mwenyewe ni mfano mzuri kwani niliwahi kuacha shule kwa mwaka mmoja na nusu. Japo nilikuwa na sababu nzuri, mpaka leo hii huwa namshukuru kakangu mpendwa ambaye tu ndiyo alikuwa amerudi kutoka vitani Uganda kwa kunipiga mkwara mkali, mkwara ulionifanya nirudi shuleni japo kwa shingo upande. 
  • Japo nilikuwa sikusoma darasa la nne na nusu ya darasa la tano, ajabu ni kwamba niliporudi shuleni darasa la sita niliweza kuyamudu masomo bila matatizo sana na mtihani wa darasa la saba ulipofika nilifaulu. Na wakati ule hakukuwa na shule za kata! 
  • Sijui kama kuna ye yote anayehusika atakayesoma hapa lakini kijana huyu inabidi arudishwe shuleni kwa nguvu akamalizie masomo yake - atake asitake, akiwa na kikombe au bila kikombe !!! 
~~~~~~~~~~~~
Mwanafunzi aacha shule kutoa dozi ya ‘kikombe’

Imeandikwa na Marc Nkwame, Meatu; Tarehe: 14 Mei 2011

WIMBI la tiba ya kienyeji maarufu kama ‘Kikombe’ linaendelea kugubika nchi na safari hii mwanafunzi wa kidato cha tano wa sekondari ya Buluba, wilayani hapa, amelazimika kuacha shule na kujikita katika kutibu kwa ‘Kikombe.’ 


Akiwa na umri wa miaka 24, Sanagu Onesmo, ambaye ni miongoni mwa vijana wenye umri mdogo kati ya matabibu wa vikombe walioanza kuibuka Tanzania mwaka huu, anatoa huduma yake hiyo katika kijiji cha Mwambegwa kata ya Mwanuhuzi. 

Vijana wengine waliowahi kuibuka na vikombe ni pamoja na binti mwenye umri wa miaka 19 aliyekatisha masomo kidato cha tatu Singida na mwingine wa Mbeya. 

Onesmo ni mtoto wa Onesmo Mwigulu, Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Mwambegwa ambaye anadai kushangazwa na mwanawe kuanza kutoa dawa hiyo ya ‘miujiza’ kwani katika ukoo wao hakuna historia ya waganga wa kienyeji. 

“Onesmo alilazimika kuacha masomo akiwa kidato cha tano Buluba, baada ya walimu wake kugundua kuwa alikuwa akitumia muda mwingi darasani kulala, tena usingizi mzito,” alisema Mwigulu. 

“Ilibidi niache shule maana kila nilipokuwa darasani, nilijikuwa nimepitiwa na usingizi na ni katika hatua hiyo ndipo ghafla nilioteshwa dawa za mitishamba,” alisema Onesmo akiongeza kuwa katika ndoto hizo, aliletewa picha za miti na mimea ambayo hakuifahamu mara moja isipokuwa mmoja uliofanana na miti iliyokuwa katika eneo la nyumba ya marehemu babu yake. 

“Huu mti unaitwa ‘nditima’ kwa Kisukuma na ni kweli babu alikuwa ameipanda kwa wingi kwenye nyumba yetu ya zamani na nilishangaa, maana yeye hakuwahi hata siku moja kuitumia kwa dawa,” alisema Mwigulu. 

Hivi sasa Onesmo hupata wateja kati ya 100 na 200 kwa siku na anadai dawa yake, kama ile ya ‘Babu wa Loliondo’ –Ambilikile Mwasapile - pia inatibu Ukimwi na magonjwa mengine sugu, lakini kijana huyo ‘alitoa mpya’ alipodai kuwa tiba yake pia ina uwezo wa kurefusha maisha. 

Dawa hiyo mpya inatolewa kwa Sh 2,000 na mgonjwa ni lazima anywe vikombe viwili ikiwa ni kwa Sh 1000 kwa kikombe. 

Onesmo anasema kila kikombe kina dawa iliyotokana na miti tofauti. 

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Abihudi Saideya, alikiri kuwa uongozi wa wilaya umeshatoa kibali kwa Onesmo, aendelee kutoa tiba yake baada ya kuridhishwa kuwa mazingira ya eneo lake ni safi na dawa haina madhara ila kuhusu suala la uwezo wake wa kutibu, bado linafanyiwa kazi. 

“Nimemtuma Ofisa wa Afya wa Wilaya kuichunguza kwa makini dawa hiyo ya Meatu,” alisema Saideya. 

Tayari mwanamke (jina limehifadhiwa) ambaye ni mfanya biashara wa hapa, na anayedaiwa kuwa na Ukimwi, ametangaza kujisikia vizuri baada ya kupata ‘kikombe’ cha Onesmo. 

Wimbi la vikombe limeshika kasi karibu katika kila pembe ya nchini, tangu kuibuka kwa Mchungaji Mwasapila wa kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro ambaye pamoja na wengi kujitokeza `kuiiga’ tiba yake, bado umaarufu wake uko juu na ameendelea kupokea umati mkubwa wa wagonjwa, wakiwamo viongozi, watu mashuhuri wa kada za siasa na utumishi wa umma wa ndani na nje ya nchi.

Chanzo: Habari Leo

Tuesday, May 10, 2011

NAPE NNAUYE KUUANIKA UFISADI UNAOFANYWA NA DR. SLAA NDANI YA CHADEMA !!!

  • Baada ya kujivua magamba, inaonekana CCM wamezinduka na sasa wako tayari kujibu hoja na malumbano ya CHADEMA majukwaani badala ya kukaa na kulalamika kwamba wanazushiwa mambo na kuomba msaada wa vyombo vya dola. Hivi ndivyo demokrasia inavyoendeshwa na hili ni jambo jema. CCM kama chama kingine cho chote cha kisiasa inabidi nao wataabike kwa kwenda kwa wananchi na kuwaeleza mafanikio na changamoto zao. Vinginevyo wapinzani watawafanyia kazi hiyo. 
  • Nape amefikia hatua hii baada ya Dr. Slaa kudai kwamba ameunasa waraka wa siri wa CCM ambao unaeleza sababu za chama hicho kushuka umaarufu. Kwa habari zaidi kuhusu waraka huu wa siri wa Dr. Slaa soma HAPA. Tunaomba tu kwamba majibizano haya yasiwe ya ki-Ad Hominem
**************** 

Nape Nnauye  akihutubia mkutano wa hadhara viwanja 
vya Ushirika Ikungi nje ya mji wa Singida LEO


KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema leo atamwaga hadharani jinsi Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbrod Slaa anavyofanya ufisadi wa kutisha ndani ya chama hicho. Nape alisema ataeleza ufusadi huo, katika mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye Stendi Kuu ya Mabasi mjini Singida mjini, ukiwa ni mkutano wa pili, katika ziara ya viongozi wa Sektretarieti ya Halimashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM waliyoianza jana mkoani hapa.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya jengo la Ushirika Ikungi nje ya mji wa Singida, Nape alisema, anazo nyaraka zinazoonyesha Dk. Slaa na baadhi ya viongozi wa Chadema wanavyojinufaaisha na fedha za chama hicho huku wanachama wenyewe wakiendelea kumpigia makofi.


Katika ziara hiyo ya kujitambulisha msafara wa Sekretarieti hiyo ya CCM, unaoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Kapteni Mstaafu, John Chiligati Nape amefuatana pia na Katibu wa Uchumi na Fedha, Mchumi Mwigulu Nchemba na Katibu wa Oganaizesheni Asha Juma Abdallah.

Katika mikutano iliyofanyika jana, Ikungi na Ligwa, Nape alikanusha vikali kuwepo wa waraka wa siri wa Sekretarieti mpya ya  CCM ambao Dk. Slaa anadai kuwa nao. Amesema, kwa kujitapa kwenye majukwaa juzi mjini Sumbawanga, kwamba anazo nyaraka za siri za Sekretarieti hiyo, kwanza inadhimhirisha kwamba hajui nini maana ya siri  na dhahiri.Nape alisema, anachokiita Dk. Slaa kuwa siri ni udhanifu wa kupuuzwa kwa sababu yote yaliyoainishwa kwa ajili ya kutekelezwa na sekretarieti ya CCM baada ya kikao cha mjini Dodoma, hakuna hata moja ambalo ni siri hadi sasa.

Alisema, baada tu ya sekretarieti kukabidhiwa mikoba, imefanya mikutano ya hadhara zaidi ya kumi katika mikoa mbalimbali na kuelezwa kwa kinaga ubaga nini hasa kilichotokea Dodoma hadi kupatikana kwa sekretarieti mpya.Nape alisema, pamoja na mambo kadhaa wamekuwa wakieleza wazi kwamba kilichofanyika ni CCM kujifanyia tathmini kuona kama kweli hali ilimo sasa na inatosha kuipigisha hatua ya kuongoza sasa na baadaye.


Alisema, baada ya tathmini hiyo, kama chama komavu kiliyakubali mapungufu kiliyobaini na kuamua kwamba ili kuondokana na mapungufu yaliyobainika, lazima uongozi wa juu uliopo uwajibike, jambo ambalo hakuna chama kingine kinachoeweza kuthubu kikabaki salama."Jamani tilichofanya Dodoma ni kuwasha Mwenge kwa ajili ya kuongeza matumaini pale yalipoanza kufifia, kuongeza imani kwa chama pale ilipoanza kudorora, jambo ambalo kwa chama chenye umri mkubwa kama CCM lilikuwa la lazima", alisema Nape.


Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, Chiligati alisema, anachodai kuwa nacho Dk. Slaa na kukiona kuwa ni waraka wa siri, kama kweli anacho ni gamba ililotupa CCM ambalo linamyima usingizi.


Chiligati alisema, kwa kawaida kitu kinapokuwepo muda mrefu sana kisipojitazama upya kuendelea kuwepo kuwa kwa mashaka makubwa, na ndiyo maana CCM imeona umuhimu wa kujitathmini na kuamua bila kusita kujivua gamba.


Alifafanua kwamba, gamba ililojivua CCM si ngozi ila ni yale matendo maovu ambayo baadhi ya viongozi walianza kuyakumbatia kama ufisadi, na kutokifanya chama kuwa cha wanachama badala yake kuonekana cha wenye fedha. Chiligati alisema, kimsingi ufisadi na hali hiyo ya kutokifanya chama kuwa cha wanachama ndilo gamba lililovuliwa toka CCM amabalo sasa Dk. Slaa anataka kutamba nalo wakati CCM walishaachana nalo tangu mkutano ule mzito wa Dodoma.

Kwa upande wake, Nchemba alisema, kwa kujivua gamba sasa CCM ni mpya, wale waliokuwa wamekimbia kutokana na kero za baadhi ya viongozi, sasa warejee kwa sababu yale hayawezi kujirudia tena.

Alisema, sasa CCM itaendesha mambo yake kisasa na kisayansi zaidi kuliko ubabaishaji, ambapo mali na miradi ya chama popote ilipo haitaweza kutafunwa na mbadhirifu yeyote bali rasilimali hizo zitakuwa kwa manufaa ya wanachama wote.Miongoni mwa viongozi wa 

Sekretarieti hiyo mpya ambao hawapo kwenye ziara hiyo mkoani Singida ni Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama ambaye ana majukumu mengine.

Chanzo: H@ki Ngowi

Tujadili Viboko Mashuleni: Vifutwe au Visifutwe ???

Picha hii iko HAPA
  • Kama ulisomea Tanzania hasa katika shule za serikali bila shaka utakuwa bado unawakumbuka wale walimu waliokuwa wakisifika kwa kutembeza viboko. Ukichelewa shuleni, unaambulia viboko. Ukiwa hujafua nguo, kukata kucha, kuchana nywele, kusugua meno au kukoga unaambulia viboko. Ukizungumza darasani, viboko. Ukiulizwa swali na mwalimu halafu ukaboronga jibu ni viboko. Ukitoroka shuleni viboko tu. Viboko vilikuwa kila mahali na kama ulikuwa na siku yenye balaa basi mtu ungejikuta jioni inapoingia tayari unakuwa umeshaambulia viboko zaidi ya kumi. Na ukifika nyumbani napo unaweza pia ukaambulia viboko. Viboko !
  • Kwa sasa ukikaa na kufikiri vizuri, unaionaje adhabu ya viboko? Ilikusaidia kuwa na adabu njema, kuzingatia masomo na hatimaye kuwa mwanafunzi mzuri na mwanajamii mwenye manufaa; au adhabu hiyo ilikufanya uwe sugu na mtu asiyejali? Ni sawa kuwapiga watoto viboko? Unaunga harakati za kuifuta adhabu hii mashuleni?
  • Tafiti mbalimbali kutoka nchi za Kimagharibi zinaonyesha kwamba viboko na adhabu zingine zenye kuleta maumivu hazisaidii cho chote na zinaweza kuwafanya watoto kuwa na tabia mbaya na wasiojali. Ndiyo maana katika nchi nyingi za Kimagharibi, adhabu ya viboko imeshapigwa marufuku. Tafiti kama hizi ni kweli zinaakisi hali halisi katika mazingira yetu na malezi ya Kiafrika? Tufute viboko mashuleni?

*********

Adhabu ya viboko shuleni haijafutwa

Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga; 6 Mei 2011

ADHABU ya viboko kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini inayotolewa na walimu na kuibua malalamiko miongoni mwa wazazi na walezi, haijafutwa kisheria, imeelezwa. 

Hayo yamebainishwa na Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Rukwa, Albert Mloka kwenye mkutano wa wadau wa elimu uliondaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga uliofanyika katika Shule ya Sekondari ya Matai wilayani humo. 

Mloka alisema adhabu ya viboko shuleni imekuwa ikilaumiwa na wananchi wengi nchini kwa kuwa walimu katika kuadhibu, hawachapi viboko, bali wanapiga wanafunzi kwa mateke, viboko visivyo na idadi, ngumi na vichwa

“Kinachofanyika shuleni walimu wanakiuka taratibu na sheria zilizoainishwa na Serikali ambapo mbali ya kuwapiga viboko visivyo na idadi kwa wanafunzi wakosefu, lakini pia walimu wa kiume wanawapiga wanafunzi wa kike ambapo sheria haisemi hivyo,” alifafanua Ofisa Elimu wa Mkoa. 

Alisema mwanafunzi ataadhibiwa kuchapwa viboko pale itakapobainika kuwa kosa alilofanya ni ovu na adhabu yake ni viboko au kufukuzwa shule na si vinginevyo. 

Kuhusu viboko kwa wasichana, alisema wataadhibiwa kwa kuchapwa viboko na walimu wa kike pekee kama shule haina mwalimu wa kike, basi adhabu hiyo itatolewa na Mkuu wa Shule na Mwalimu Mkuu

Alisema ni viboko vinne tu vilivyoruhusiwa kisheria kwa wavulana kuchapwa kwenye makalio na wasichana mikononi na mwalimu akitoa adhabu hiyo, anaagizwa aandike kitabuni kuonesha tarehe na idadi ya viboko na aliyeadhibiwa lazima asaini kitabuni humo. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay aliwavunja mbavu wajumbe alipochangia  kwa kusema kuwa “mbona sisi (wanafunzi wa kiume) tunachapwa na walimu wa kike…this is not fair, mie ni Mmasai kule umasaini mtoto wa kiume kucharazwa viboko na mwalimu wa kike looh mwalimu huyo atapewa misukosuko kwa kweli atapata shida,” alisema. 

Wajumbe wengi wakichangia walidai kuwa walimu wanaotoa adhabu ya viboko visivyo na idadi shuleni hata kwa kosa la mwanafunzi kushindwa kujibu swali darasani, wengi wao hawana uwezo wa kutosha kufundisha au hawajiandai vizuri kufundisha. 

Si kweli shule zimeharibika, bali walimu baadhi yao wameharibika....viboko sio suluhisho la kumaliza utoro shuleni, walimu wanaotembea na fimbo mikononi kutwa nzima basi ujue wewe si mwalimu,” alisema mjumbe mmoja. 

Wajumbe hao pia walishauri kuwa adhabu hiyo ya viboko kwa wanafunzi kamwe isitolewe na mwalimu mwenye hasira kwani atapiga badala ya kuchapa. 

Baadhi ya wanafunzi ya Shule ya Sekondari ya Matai walioalikwa hapo, walikiri kuwa adhabu za viboko shuleni zimekithiri na ni mateso kwao. 

“Maisha ya shule yamekuwa ni mateso kwetu kwani adhabu za viboko zimezidi baadhi yetu wamekata tamaa ya kusoma na wanahudhuria shule kwa lazima na si kwa hiyari yao wenyewe” alisema mwanafunzi wa kidato cha nne, Paulo Maembe. 


Chanzo: Habari Leo.

  • Kwingineko, wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Rungwa katika Halmashauri ya Mji wa Mpanda wamegoma kuingia madarasani kwa muda usiojulikana wakipinga Mkuu wa Shule hiyo kuwacharaza viboko visivyo na idadi. Kwa habari kamili soma HAPA.

Sunday, May 8, 2011

KWA MAMA YANGU MPENDWA, MKE WANGU MWEMA NA AKINA MAMA WOTE DUNIANI: HONGERENI. LEO NI SIKU YENU. TUNAWAENZI !!!

Mamangu mpendwa nami mwaka jana nyumbani Bariadi. 
  • Kama nilivyokwisha kusema HAPA na HAPA kumhusu mamangu mpendwa, leo tena ni sikukuu ya Akina Mama hapa Marekani. Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza tena mamangu mzazi, mke wangu mpendwa pamoja na akina mama wote popote mlipo hapa duniani bila kuwasahau mashujaa wanablogu wenzetu kama mlivyorejelewa kiufundi sana na Mzee wa Changamoto  HAPA. Akina mama, ninyi ndiyo nguzo ya jamii na mchango wenu kamwe haupimiki wala kuelezeka. Tunawaenzi !!!
*******************
Kama picha hizi zinavyoonyesha, ni nani kama mama ???

imagebam.com imagebam.com imagebam.com imagebam.com imagebam.com imagebam.com

Wachaga Mpo? Hii Hapa CHAUKOLA: Chaga Univasiti Koleji Ofu Laifu !!!

Kibonzo kwa hisani ya Dennis wa gazeti la Msanii Afrika.

Saturday, May 7, 2011

Wataalamu: Kikombe cha 'Babu' ni Kinga Bomba


Japo mti huu wa Mugariga unaonekana kuwa na faida kibao za kiafya kama wataalamu hawa anavyothibitisha, muujiza bado ni ule ukweli kwamba kwa babu dozi ni kikombe kimoja tu, kwisha. Sijui kama kuna dawa nyingine ambapo mtu unakunywa mara moja tu halafu unapona magonjwa kibao namna hii. Miujiza!

**************

Wataalamu: Kikombe cha 'Babu' ni kinga bomba


Imeandikwa na Gloria Tesha; Tarehe: 6th Mei 2011

RIPOTI ya awali ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kuhusu tiba ya Mchungaji Ambilikile Mwaisapile, imeonesha tiba hiyo ina uwezo wa kukabiliana na magonjwa sugu ikiwemo Ukimwi, pumu, kisukari, saratani na shinikizo la damu.

Ripoti hiyo iliyolifikia gazeti hili, ambayo pia iliandaliwa na mtaalamu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), ni ile iliyotolewa serikalini baada ya wataalamu hao,

Dk.Hamis Malebo na Dk. Zakaria Mbwambo kufanya utafiti kuhusu usalama wa tiba hiyo maarufu kwa jina la Kikombe cha Babu. Baada ya Serikali kupata ripoti hiyo, ilitoa taarifa kuwa dawa hiyo ni salama, lakini ripoti hiyo imeonesha kuwa dawa hiyo ina mengi kuliko ilivyotangazwa na Serikali

Kuhusu Ukimwi, ripoti hiyo imeeleza kuwa utafiti wa mizizi na majani ya mti anaotumia Mchungaji Mwaisapile, kitaalamu mugariga, yana nguvu ya kupandisha kinga ya mwili.

Utafiti huo umenukuu utafiti uliofanywa Kenya na Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kenya (KEMRI) mwaka 2006, ulioonesha kuwa mizizi ya mti huo ina uwezo wa kukabiliana na virusi hivyo.

“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa mti una uwezo wa kupambana na moja ya virusi hatari vinavyoshambulia kinga ya mwili kwa mwanadamu, hivyo ni sahihi kwa Mchungaji Mwaisapile kudai kuwa tiba hiyo ya kijadi ina uwezo wa kupambana na HIV/AIDS,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Utafiti huo pia ulinukuu taarifa kadhaa za vitabu mbalimbali kikiwemo kitabu cha Activity of Liver, kilichoandikwa na Chatterjee na Roy mwaka 1965, kilichoonesha kuwa mti huo ni tiba kwa magonjwa sugu kama saratani na ini na una kinga kwa walemavu wa ngozi dhidi ya saratani ya ngozi. 

Kuhusu ugonjwa wa kisukari, wataalamu hao pia walinukuu utafiti uliofanywa mwaka 1996 kwa kumnywesha maji ya majani ya mti huo panya mwenye kisukari na matokeo kuonesha panya huyo akipunguza kiwango cha sukari katika damu yake katika saa tatu za mwanzo tangu anyweshwe. 

Katika utafiti huo wa 1996, panya asiyekuwa na kisukari alipopewa dawa hiyo, hakupata mabadiliko yoyote jambo linalodhaniwa kuwa dawa hiyo ina uwezo wa kutoa insulini kutoka katika kongosho ya mnyama wa kawaida. 

“Hivyo kuna usahihi kwa Mchungaji kueleza kuwa dawa anayoitoa ina uwezo wa kukabiliana  na kisukari,” ilieleza ripoti hiyo. Madaktari hao katika ripoti hiyo, wameonesha kuwa mti huo una uwezo wa kukabiliana na shinikizo la damu la kupanda kwa kuwa inashusha shinikizo na kufikia kiwango cha kawaida na hilo limedhihirishwa na utafiti wa kitabu cha Vohra na De cha mwaka 1963. 

NIMR imelithibitishia gazeti hili kuwa ripoti hiyo ni ya kweli, ndiyo iliyopelekwa serikalini kabla ya Babu kuruhusiwa kuendelea kutoa huduma yake, lakini ni taarifa ya awali, hawajaitoa rasmi. 

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela alilieleza gazeti hili jana kwamba katika  ripoti hiyo, vitu vingi vya kitaalamu vinakosekana na kuwashangaa watu walioitoa wakati haijakamilika, akiwalaumu kuwa wameitoa kwa makosa kwa kutafuta umaarufu. 

“Kuifahamu naifahamu, siwezi kusema ni ya kughushi ila ni ‘draft’ (rasimu) haijakamilika, nashangaa kuona mnayo, hii ni taarifa ya awali tu inayosaidia kutengeneza rasimu ya kufanyia kazi. 

“Kuna taarifa nyingine za kuambatanisha, haijakamilika kutolewa,” alisema Dk. Mwele alipoulizwa na mwandishi kuhusu ukweli wa ripoti hiyo. 

Hata hivyo, alipoulizwa lini utafiti kamili utakamilika, Mkurugenzi huyo alisita kutoa muda  kamili, lakini akasema itachukua muda mrefu. 

Hata hivyo, taarifa za kuaminika kutoka kwa wataalamu wa afya zilieleza kuwa uthibitisho wa kujua kama tiba fulani inatibu magonjwa, hukamilika baada ya utafiti wa miaka miwili. 

Katika utafiti wao, madaktari hao wamebaini kuwa kiwango cha dawa kinachopimwa na Mchungaji huyo kwenye kikombe cha ujazo wa mililita 200, kuchemshwa kwenye maji ya lita 60 yenye mizizi ya mti huo, ni salama kwa mtumiaji na hakuna sumu yoyote kwa kiwango hicho. 

Baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kwa nini taarifa ya jopo haielezi kiasi cha tiba ya kikombe kama kinafaa kwa tiba za magonjwa hayo sugu ama la, bila majibu, lakini ripoti hiyo imeonesha kuwa kiasi hicho ni tiba sahihi ingawa NIMR imesisitiza ni taarifa ya awali. 

Maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi wameendelea kumiminika kwa Babu kupata tiba hiyo inayomtaka mgonjwa asirudie kikombe. 

Mchungaji Mwaisapile anadai kuoteshwa na Mungu miaka zaidi ya 10 iliyopita kuhusu tiba hiyo ya miujiza. 

Mbali na Tanzania, mti huo anaotumiwa na Babu unapatikana pia Australia, Botswana, Cambodia, Cameroon, Eritrea, Ethiopia, Ghana, Guinea, Japan, Kenya, Myanmar, Namibia, Nigeria, Papua, Saudi Arabia, Senegal, Afrika Kusini, Sudan, Thailand, Uganda, Vietnam na Yemen. 

Katika kabila la Wamasai, mti huo unajulikana kama Engamryaki, Olmuriaki au Engamryaga. 

Pia umekuwa ukitumika kama chakula na makabila ya Wagogo, Wakurya na Wabarbaigi. 

Matunda ya mti huo yameelezwa katika ripoti hiyo kuwa ni matamu na nchini Ghana huongezwa kwenye chakula cha wagonjwa kuwaongezea hamu ya kula na Sudan na Kenya hutumika kutengenezea jemu. 

Pia mti huo umekuwa ukitumika kutibu maumivu ya kichwa, kifua, magonjwa ya ngono ya  kisonono na kaswende, gauti, homa kali, ugonjwa wa anemia selimundu (sickle cell anaemia ) na ngiri.


Chanzo: Habari Leo

Friday, May 6, 2011

Al-Qaeda Wakiri Osama Ameuawa. Watoa Mikwara Kibao Dhidi ya Marekani

  • Al-Qaeda hatimaye wamekiri kwamba kiongozi wao "mpendwa", Osama Bin Laden ameuawa. Al-Qaeda pia imechimba mkwara kwa kusema kwamba furaha ya Wamarekani itageuka na kuwa huzuni muda si mrefu ujao; na kwamba kifo cha Osama kichukuliwe kama kichochezi tu na kwamba Al-Qaeda kamwe haitakufa. Sijui kama taarifa hizi zitasaidia kuwanyamazisha wale wanaodai kwamba Osama hajauawa na kwamba hizi ni njama za Obama kujiongezea umaarufu kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Habari kamili kuhusu habari hii zinapatikana HAPA

Wanafunzi wadai Kiingereza kinawafelisha

  • Tafiti zimeshafanywa, makala mengi yameshaandikwa, vitabu vingi vimeshachapishwa na makongamano mengi yameshafanyika kuhusu matatizo ya sera yetu ya lugha mashuleni na utatuzi wake. Ajabu ni kwamba miaka nenda miaka rudi wahusika hawaonekani kulichukulia tatizo hili kwa uzito unaostahili na kulitafutia ufumbuzi. Tutatangatanga na sera hii kengeufu ya lugha mpaka lini? Kama elimu bora ndiyo mkakati mama katika  maendeleo na ukombozi wa jamii yo yote ile, tutawezaje kuendelea huku tukiwa na sera ya lugha ambayo kimsingi inawageuza vijana wetu kuwa kasuku wa kukariri mawazo na maarifa ambayo hawayaelewi kwa undani? Jambo hili linashangaza na hata kusikitisha sana !!! 
~~~~~~~~~~
Wanafunzi wadai Kiingereza kinawafelisha

Imeandikwa na Abby Nkungu, Singida

BAADHI ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chifu Senge, wamesema sababu kuu za wanafunzi wengi wa kidato cha nne kufeli Hisabati ni uelewa mdogo wa lugha ya Kiingereza inayotumika kufundishia mashuleni. 

Wakizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni kuhusu sababu za wanafunzi wengi wa sekondari kufeli hisabati, walisema msingi mbovu wa somo hilo katika shule za msingi umechangia.


Fadhila Solomon anayesoma kidato cha tatu mchepuo wa sayansi katika shule hiyo, alisema msingi hafifu wa lugha ya Kiingereza tangu shule ya msingi, umesababisha wanafunzi kushindwa kumudu somo la Hisabati. 

Mwanafunzi huyo alisema katika shule za msingi, lugha kuu inayotumika kwa karibu masomo yote ni Kiswahili lakini wanapoingia sekondari hukutana na Kiingereza kwa masomo yote na wakati mwingine walimu hawajali kuwa wanafunzi wanatoka shule zisizo na mchepuo wa Kiingereza. 

Maelezo hayo yaliungwa mkono na Asia Abdalla wa kidato cha pili na Regina Silas wa kidato cha tatu huku wakiwaomba walimu wachanganye lugha wakati wakifundisha ili wanafunzi wapate ujumbe kwa usahihi na ufasaha. 

"Kule tulikotoka ni Kiswahili tu kwa kila somo isipokuwa somo la Kiingereza...sasa hapa kila somo ni Kiingereza.... mwalimu anatema Kiingereza kitupu kuanzia mwanzo hadi mwisho, sisi tunatoka kapa...walimu wawe wanachanganya lugha ili tuwaelewe vizuri," alisema Asia. 

Regina alisema, lugha ya Kiingereza ni tatizo kubwa kwao na husababisha hata baadhi ya wanafunzi kumchukia mwalimu wa somo husika. 

Mwanafunzi Francis Sebastian na Makafoo Iddi walisema kuwa pamoja na sababu hiyo kuu, ukali wa baadhi ya waalimu, uchache wa vitabu na uhaba mkubwa wa walimu wa Hisabati ni sababu nyingine zinazochangia wanafunzi kufeli somo hilo. 

Sababu nyingine ni wanafunzi kutopenda somo la Hisabati na wengine kutojiamini; hasa wasichana. 

Mwalimu Benjamin Mayengela anayefundisha Hisabati katika shule hiyo, alisema kuwa wingi wa vipindi kwa mwalimu mmoja kutokana na uchache wa walimu, ukosefu wa vitabu na wanafunzi kutojituma ni sababu zinazochangia ufaulu duni wa Hisabati. 

Naye Ofisa Elimu wa Mkoa wa Singida, Yusufu Kipengere alisema ufaulu duni wa Hisabati unatokana na uhaba mkubwa wa walimu. 

"Kwa mfano mwaka huu, Mkoa ulipokea walimu 300 kati yao, walimu 15 tu ndio wa hisabati," alifafanua Kipengere. 

Shule ya Sekondari ya Chief Senge iliyopo mjini hapa ina kidato cha kwanza hadi cha nne na ina mikondo 16 lakini ina walimu wa hisabati wawili tu.

Chanzo: Habari Leo

Fikra ya Ijumaa: Hebu Tutafakari Haya Maswali Mawili Kuhusu Kifo.

Watu wakishangilia kuuawa kwa Osama Bin Laden Washington D.C

(1) Swali la Kwanza
  • Kuna mantiki au faida yo yote kweli kwa binadamu kushangilia kifo cha binadamu mwenzake (hata kama ni mbaya namna gani) wakati akijua kuwa naye anaweza kufa wakati wo wote ule? 
(2) Swali la Pili
  • Hivi kuna tofauti yo yote marehemu akizikwa na maelfu ya watu au akizikwa na mtu mmoja? Umati wa watu (au mtu mmoja) katika mazishi unamsaidiaje marehemu? Ati, mafarao wa Misri waliojijingea makaburi ya kifahari na kuzikwa na vito vingi vya thamani walikuwa na unafuu au tofauti yo yote na masikini waliozikwa katika makaburi ya kawaida yasiyo na mapambo wala ishara zo zote za utajiri? Kuna Matabaka hata baada ya kufa? Binadamu!
Picha ya Osama iliyochorwa mchangani na mchoraji wa India. 
Picha zote ni kutoka Reuters

Kwa maoni ya wanafalsafa mbalimbali kuhusu kifo bofya HAPA.

Thursday, May 5, 2011

Jamani Nimerudi - Tena Nimerudi na Misalaba

Baada ya kupotea kidogo kutokana na pilikapilika za kubeba maboksi, sasa nimerudi tena. Kuanzia sasa mambo yatakuwa sawia. Tuwemo !!!

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO