NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, August 31, 2011

TUMETHUBUTU, TUMEWEZA (KUJIVUA MAGAMBA) NA SASA TUNASONGA MBELE !!!

Hii kauli mbiu ya CCM kule Igunga kwa Rostam Aziz imenivutia. Ina maana ile operesheni ya kujivua magamba imeshakamilika? Kama jibu ni ndiyo basi hili ni jambo jema kwa WanaCCM na bila shaka uchaguzi wa Igunga utakuwa pimajoto mojawapo kuona jinsi operesheni hii ilivyopokelewa na wananchi. Tunaomba tu uchaguzi huu mdogo wa Igunga usikumbwe na kashfa zozote za uchakachuaji wa kura na badala yake uwe huru, wa haki na amani!

Friday, August 26, 2011

FIKRA YA IJUMAA: ETI WAJINGA NDIYO WANAJIAMINI !!!

  • Jamani, wenye maarifa na washika kurunzi wetu mashujaa mko wapi? Mbona mmejaa shaka? Ni nini kilichowafanya mpoteze kujiamini kwenu? Kwa nini mmewaachia wajinga waipalilie mimea japo mwajua wazi kwamba si wataalamu wa kilimo? Mnaridhia kweli ngalawa izame nanyi mpo mwakodoa macho tu? Kwa nini???
  • Bofya hapa kusoma wasifu wa Mwanafalsafa na Msomi Bertrand RussellWikiendi njema wadau!

Tuesday, August 23, 2011

ATI, MIHADHARA HII CHOCHEZI INA LENGO GANI HASA ???

Picha hii iko HAPA

Leo wakati natafuta nyimbo za Rose Muhando na Bahati Bukuku katika Youtube, nimekutana na mambo ya ajabu. Watu wameamua kuweka "mihadhara" yenye kutetea dini ya Kiislamu kwa kutumia majina ya waimbaji mashuhuri wa injili kama Rose Muhando, Bahati Bukuku na wengineo (mf. tazama HAPA).

Video ina jina la Rose Muhando lakini ukibofya unapelekwa kwenye video inayoonyesha mihadhara ya kitoto kati ya Uislamu na Ukristo - mihadhara ambayo lengo lake hasa mimi huwa silielewi japo kuna kipindi ilikuwa imejikita sana kule nyumbani.  Kwa kawaida katika mijadala hii Ukristo huwa unashambuliwa sana, Biblia hupotoshwa na kutafsriwa nje ya mandhari na muktadha wake; na Uislamu hushadidiwa kuwa ndiyo dini ya kweli na mwanzilishi wake kuwa ndiye hasa mtume wa mwisho aliyefunga kazi. Daima mwamba ngoma huvutia kwake ati!

Hata hivyo ukisikiliza na kufuatilia vizuri mijadala hii ni wazi kwamba hoja nyingi zinazotolewa zimeegemea katika mihemko, hazina nguvu, zimejaa jazba, hazina umakinifu na hazijachujwa vizuri. Unaweza hata kupata fununu kuhusu kiwango cha elimu-dunia cha watoa mihadhara hawa na wasikilizaji wao ambao wengi wao kazi yao kubwa ni kushangilia tu!

Sina ugomvi na Waislamu na mtume wao wala dini zingine na waanzilishi wao kwani naamini kwamba ni uhuru wa kila mtu kuamini dini yo yote anayotaka. Hata hivyo huwa nakerwa na watu wanaosimama kidete na kuanza kushambulia dini zingine hata ikibidi kwa kutumia matusi (ya kitashtiti) na udogoshaji. Historia inaonyesha kwamba mashambulizi ya aina hii mara nyingi yana madhara makubwa kijamii hasa upande mmoja unapokuwa hauna subira na uvumilivu. Ndiyo maana tukaonywa kwamba kama unaishi katika nyumba yenye vioo basi kamwe usishabikie mchezo wa kurusha mawe. Dini !!!

Ati,  Ukristo ndiyo dini ya kweli? Uislamu ndiyo dini ya kweli? Uhindu je? Dini zingine nazo? Vipi kuhusu dini zetu za Kiafrika tulizokuwa nazo kabla ya ujio wa Waarabu na Wazungu katika mwambao wa Afrika Mashariki? Kwa kuwa dini hizi tumezichanganya na dini tulizoletewa, je hizi nazo ni za kweli?

Ukiona jamii inaanza kubetuana kwa kutumia misingi ya udini, basi jua kwamba jamii hiyo inacheza na moto na inakoelekea si kwema! Na watu wanaoendekeza na kushabikia haya mambo ya udini (wakiwemo hawa watoa mihadhara uchwara) ni watu wa kuogopwa kama ukoma. Mwenye masikio na asikie !!!

Friday, August 19, 2011

FIKRA YA IJUMAA: HIVI LENGO HASA LA ELIMU TUNAYOIPATA VYUONI NI NINI ???

 
Nimejiuliza swali hili baada ya kuona orodha ya shahada 20 ambazo eti hazina faida hapa Marekani. Inawezekana kweli shahada ikawa haina faida kwa "msomi" aliyeipata? Tunaupimaje umuhimu wa elimu tunayoipata? Ni uwezo na uwezekano wake wa kutupatia ajira nzuri baada ya masomo au ni ule umuhimu wa elimu kama nyenzo kombozi inayomkaramsha aipataye na kumwondolea woga wa kupambana na mazingira yake? Ati, katika jamii yetu, elimu tunayowapatia vijana wetu ina lengo gani hasa?

MKANGANYIKO WA OPERESHENI YA KUJIVUA MAGAMBA

Bofya HAPA na HAPA ili kujikumbusha mambo ya msingi kuhusu operesheni hii ambayo mimi nadhani haijaeleweka vizuri. Katuni hii ni kutoka kwa Mwanaharakati Said Michael.

Sunday, August 14, 2011

UJUMBE WA LEO: WEWE NDIWE !!!

Kwa hili nakubaliana kabisa na Dr. Seuss. Kuishi kwa kujaribu kuwafurashisha watu wengine ni kazi bure. Mbali na ukweli kwamba jambo hili haliwezekani lakini pia mara nyingi watu hawa unaojaribu kuwafurahisha hata si watu wa muhimu kwako na kusema kweli hawajali. Ati, wawezaje kumfurahisha binadamu mwenzako ambaye mwenyewe hana furaha? 

Wewe ndiwe na hakuna mwingine kama wewe hapa duniani. Itupilie mbali hofu na kawe na furaha Jumapili hii njema.

BI ARUSI ANAPOSHIKWA NA UCHUNGU WA KUJIFUNGUA KANISANI, TENA KANISA LA KIKATOLIKI !!!

  • Wakatoliki ni wahafidhina (conservatives) katika mambo mengi hasa yanayohusu mapenzi, ndoa na uzazi. Bado hawajaruhusu waumini wao kutumia kondomu, wanapinga mambo ya kupanga uzazi na kabisa kabisa hawaruhusu ngono kabla ya ndoa. Ndiyo maana kasheshe hii ya Bi. Arusi kushikwa na uchungu wa kujifungua kanisani imenishangaza kidogo. Ina maana tumbo la ujauzito lilikuwa halionekani? Au pengine Wakatoliki siku hizi wamelegeza masharti ili kwenda na mabadiliko katika jamii ya sasa ambapo watu kuishi pamoja kabla ya ndoa ni jambo la kawaida? Nawaombea wanandoa hawa ndoa njema pamoja na kasheshe hii iliyowapata!
****************
Bibi harusi ashikwa uchungu, ajifungua kanisani Muheza 
Thursday, 11 August 2011 21:16
Mwandishi Wetu, Muheza

BIBI harusi aliyefahamika kwa jina la Mariam Shabani, ameshikwa na uchungu wa kujifungua kanisani wakati akifungishwa ndoa na mchumba wake, aliyefahamika kwa jina la Deo Massawe.Tukio hilo lilitokea juzi Kanisa Katoliki lililopo maeneo ya Majengo Shimoni, wilayani Muheza, huku umati wa watu ukiwa umejaa ndani ya kanisa hilo ukiisubiri kufungwa kwa ndoa hiyo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia tukio hilo ndani ya kanisa hilo, wakati Padri Martin Kihiyo, akiendelea na misa ya kufungisha ndoa hiyo, ghafla bibi harusi akiwa amevaa vazi rasmi la harusi, alianza kupiga kelele akidai anasikia uchungu wa kujifungua.

Hata hivyo, baada ya bibi harusi huyo kupiga kelele, Padri Kihiyo alisitisha misa hiyo  na Mariamu kuchukuliwa haraka na kuwekwa kwenye gari huku akiwa hajiwezi hadi Hospitali Teule Muheza.Pia, Mariamu anafahamika kwa jina la Sada Shabani, baada ya kufikishwa hospitali alipelekwa chumba cha kujifungulia huku akiwa na vazi lake la harusi.

Baada ya kuhudumiwa Mariamu, alijifungua mtoto wa kike na kulazwa wodi ya Azimio wanakolazwa wazazi.
Mmoja wa muuguzi hospitalini hapo aliyeomba asitajwe, alisema bibi harusi huyo alijifungua njiti akiwa na miezi saba.Kwa upande mwingine, kwenye ukumbi ambao ulikuwa umeandaliwa kwa sherehe ya  harusi hiyo, watu walikuwa wamekaa ndani wakisubiri maharusi bila kufahamu kilichokuwa kikiendelea.

Hata hivyo, kutokana na hali hiyo bwana harusi alilazimika kufunga ndoa na msichana mwingine wa pembeni kwa niaba ya bibi harusi, ili kuhalalisha sherehe hiyo huku bibi harusi mwenyewe akiwa hospitali analea.

Inasemekana Mariamu alianza kusikia uchungu akiwa saluni na aliwaeleza baadhi ya watu, lakini walimjibu kuwa huo ni woga wa harusi.Katika hatua nyingine, mbuzi wa ndafu aliyekuwa ameandaliwa alianguka chini kwenye mchanga.

Baadhi ya Wakristo walisikitishwa na tabia ya viongozi wa dini kuendelea kuwafungisha ndoa watu ambao wake zao wana mimba kwamba, ni aibu.

Chanzo: Mwananchi

Wednesday, August 10, 2011

UCHESHI: MWANAMKE ALIYEWASHINDA WENZIO, WEWE UTAMUWEZA ???

  • Wenyewe husema usivione vyaelea vimeundwa. Sisi tunapenda kubadilisha na kusema: Ukiona vyealea basi ujue vilishawashinda waundaji (na manahodha)! Kwa hekaheka wanazopambana nazo wanaume katika ndoa, soma HAPA

Tuesday, August 9, 2011

NENO LA LEO: NUKTA ZINAYOYOMA NA MUDA UNAKWENDA. UNAJUA KINACHOENDELEA ???


Ndiyo maana Heraclitus - mwanafalsafa wa kale wa Ugiriki aliwahi kusema kwamba "huwezi kuogelea mara mbili katika mto ule ule". Lakini pia tukumbuke kwamba kila kitu ni tofauti ingawa hakuna kilichobadilika. Tutafakari!

AFRIKA: BARA LENYE UTAJIRI USIO NA WENYEWE....

(1) Ni bara tajiri sana na lililonona kwa utajiri wa kila aina...


(2) Utajiri huo hata hivyo unafaidiwa na mabepari kutoka nje na mafisadi wachache wa ndani


(3) Mabepari wa nje wananenepeana na kuwaacha Waafrika wakiteseka na umasikini wa kutisha...


(4) Mama Afrika atateseka mpaka lini? Ni lini atajifungua watoto wenye uchungu na nia ya kweli ya kumkomboa? Ni lini utajiri wake utafaidiwa na watoto wote badala ya majibwa ya nje na mbweha wachache wa ndani?

Monday, August 8, 2011

HUYU MWANAMZIKI WA KIZAZI KIPYA KUTOKA UGANDA AMENISIKITISHA !!!

Mwana-Fleva Aziz Azion kutoka Uganda

Kwa nini alikubali kutoa hotuba katika lugha asiyoifahamu (vyema)? Kwa nini asitumie lugha yake ya mama au mkalimani kama kulikuwa na ulazima wa kufanya hivyo? Au  naye alitaka kuonekana "msomi" kwa kutema ung'eng'e hata kama umeparaganyika? 

Suala la lugha bado ni tete katika nchi nyingi za Kiafrika na mpaka tutakapoweka mikakati ya kiukombozi na yenye kumakinikia utamaduni wetu, wengi wetu tutaendelea kuadhirika kama huyu msanii mchovu. Ni lazima tujifunze hizi lugha za kigeni lakini tusifikie hali ya kujidhalilisha na kuzidharau lugha zetu za Kiafrika - lugha zilitotukuza na kutuonyesha ulimwengu. Ningefurahi sana kama angetema Kiganda na kuwaacha watu wasiokifahamu wameduwaa. Pengine nao ingewabidi waende wakajifunze Kiganda. Utumwa wa fikra huu sijui utatuisha lini sisi Waafrika. Soma kisa chake hapa chini.

************

Msanii Uganda...Hajui Kiingereza Kabisaaaaaa ...!


Msanii Aziz Azion toka Uganda,aliumbuka alipokua analazimisha kuongea ung'eng'e wakati hajui wakati anatoa speech pande za Serena Hotel kwenye uzinduzi wa Jarida la Black Flavour aka Black Flavour Magazine


Aziz Azion alialikwa kama guest performer na MC alipomuomba atoe speech kidogo kuhusiana na jarida hilo, alikamata mic na kuanza kujiuma uma kidogo apate ugonjwa wa moyo coz aliongea broken english kabla ya kuhamia kwenye lugha yake ya taifa ya Luganda. Artist huyo alifunguka longtime kitambo kuwa ameanza English Course ili ajifunze ung'eng'e....Coz aliripotiwa kuwa hawezi kabisa kuongea lugha hiyo....

Chanzo:  Chini ya Kapeti

*********************
Angalizo Zaidi


Hata hii lugha iliyotumiwa na huyu Chini ya Kapeti hapo juu nayo ni changamoto tupu....

Saturday, August 6, 2011

AISEE - UNA AKILI KAMA ULIZALIWA NA Ph.D !!!

  • Katuni hii ya Said Michael imenifanya nijiulize hili swali: Utendaji wa viongozi wetu wasomi wenye ma-Ph.D na maprofesa ukoje huko bungeni na serikalini hasa ukizingatia kwamba siku hizi kila Profesa na mwenye Ph.D anataka kuwa mbunge au waziri? Wanakwenda huko ili kutumia elimu yao ili kuiokoa jamii au wanafuata dili tu?
  • Wenyewe wanasema kwamba unaweza kutathmini uhai wa jamii na malengo ya mfumo wake wa elimu kwa kuangalia tabia na matendo ya wasomi wake. Ati, matendo ya wasomi wetu yanatuambia nini kuhusu mfumo wetu wa elimu - sisi tunaoishi katika nchi ya Ujamaa na Kujitegemea ambako binadamu wote ni sawa?

"SLIPINGI ALAWANSI" MJENGONI - HA HA HA !!!

 (1) Naibu Spika mwenyewe kautandika


(2) "Nambari wani eeh" naye kaucharaza


(3) Tyson anajitetea

(4) Mwananji wa Kiraracha naye hoi

(5) Tyson tena - kingunge wa kulala bungeni!

(6) Viti maalum hawa: Mmoja kautandika, mwingine anajinyonya kidole...

WIMBO MASHUHURI WA DINI KATIKA KISUKUMA - TULIBANG'WA YESU, TULIBANG'WANAMALIA, TULASHIKU NG'WIGULU !!!

-Sisi ni Watoto wa Yesu. Sisi ni Watoto wa (Bikra) Maria. Tutafika Mbinguni.....

Wimbo huu unapatikana katika ukurasa wa mwisho wa kitabu hiki. Sijui nitawezaje kuwasiliana na wenye hati miliki kwani kuna mambo mengi kuhusu imani na utamaduni wa Wasukuma ambayo ningependa kuyaweka hapa - ikiwemo ile hadithi mashuhuri ya Shing'weng'we na Masalakulangwa

Friday, August 5, 2011

FIKRA YA IJUMAA: ATI, KITU GANI NI CHA MUHIMU ZAIDI KWAKO HAPA DUNIANI ???

  • Ni kazi yako? Ni Nyumba yako nzuri? Ni Mkeo, mumeo au mpenzi wako? Ni ngono? Ni msosi? Ni ufisadi wako? Ni familia? Ni dini yako? Ni madaraka yako? Ni marafiki? Ni gari lako la bei mbaya? Ni elimu yako?, Ni kifo? Ni utajiri wako? Ni nini basi?
  • Fikiri vizuri halafu utoe jibu. Na pengine jibu lako litatoa fununu kuhusu lengo hasa la maisha na falsafa yako nzima kuhusu kuwako kwako katika sayari hii iitwayo Dunia. Binadamu !!!

MZAZI ANAPOMSHAWISHI MTOTO KUJIFELISHA MTIHANI ILI KUKWEPA GHARAMA ZA KUMLIPIA !!!


Nikiwa Kama Mzazi Habari Hii Imenisikitisha

Karibu wazazi wote tunawatakia watoto wetu maisha mema. Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana ili angalau safari yetu ikishakamilika hapa duniani basi tuwaachie angalau kitu kidogo kitakachowasaidia wakati sisi hatupo. 

Na katika urithi bora kabisa ambao tunaweza kuwaachia watoto wetu ni elimu bora. Wenye uwezo wanatumia maelfu ya dola kuwasomesha watoto wao nchi za nje. Wengine wanajibidisha kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi wakiamini kwamba huko watapata elimu bora. Wazazi leo wanakazana kuwapeleka watoto wao wanaoanza shule katika "akademi" zinazofundisha kwa kutumia lugha ya Kiingereza ili kuwapa misingi imara ya lugha hiyo watoto wao. 

Na sababu kubwa iliyotufanya wengi wetu tuliolowea huku ughaibuni na kubeba maboksi ni elimu bora kwa ajili ya watoto wetu. Elimu bora ndio urithi bora kabisa tunaoweza kuwaachia watoto wetu.

Nilipoisoma habari hii hapa chini kuhusu wazazi wanaowashawishi watoto wao kufeli ili kuepuka gharama za kuwasomesha niliwasikitikia wazazi hao pamoja na hawa watoto. Je, serikali inalijua tatizo hili? Kuna utaratibu wowote wa kuweza kuwasaidia watoto kama hawa ili nao wakaendelea kusoma? Kama upo, unafahamika kwa walengwa? Iweje tunapoteza mabilioni kutokana na ufisadi lakini hatuwezi kuwasaidia watoto wetu hawa kujipatia elimu? 
 ********
‘Wazazi wanawashawishi watoto wao kufeli’
Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga; Tarehe 7 Mei 2011

MATOKEO mabaya ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kila mwaka mkoani Rukwa yanasababishwa na baadhi wazazi na walezi ambao wamekuwa wakiwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani ya mwisho ili kukwepa wajibu wao wa kuwagharamia kielimu katika ngazi inayofuata.
 

Diwani wa Kata ya Milepa iliyopo wilayani Sumbawanga, Apolinary Macheta alisema hayo wakati akichangia mada kwenye mkutano wa Wadau wa Elimu wa Wilaya ya Sumbawanga uliofanyika juzi katika Kata ya Laela wilayani humo.

Alisema kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa na tabia kuwashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao ya kumaliza darasa la saba kwa lengo la kukwepa majukumu ya kuwalipia ada na michango mingine au wakati mwingine wakitaka kuwaoza watoto wao wa kike.
 
Diwani huyo aliongeza kuwa kwa upande wa watoto wao kiume, wazazi hao wamekuwa wakiwashawishi kufanya hivyo ili wajishughulishe na shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo ni kilimo, uvuvi na biashara kwa madai kuwa ndizo zenye tija kuliko kuendelea na elimu.

“Tatizo la kutofanya vizuri kwenye mtihani wa mwisho kwa watoto wengi wa vijijini ni wazazi wenyewe ….. hawataki waendelee na sekondari kwa hiyo wanawashawishi kufeli kwa lengo la kukwepa gharama ya kulipa ada na michango mingine, pia kutaka kuwaoza watoto wao wa kike sasa inapotokea mtoto mwenye uwezo mzuri darasani anafeli tufuatilie matokeo yake tangu awali yalikuwaje,” alisema Diwani Macheta.
 
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Christian Lazer alisema kuwa ni aibu wilaya hiyo kuendelea kuwa na watu wanaosoma kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) na kusema kuna kila sababu watendaji wa vijiji kuhamasisha wazazi na walezi kuwaandikisha watoto wenye umri wa kwenda shule kwa wakati.

Alisema kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuondokana na udhaifu huo wa uandikishaji uliopo hivi katika halmashauri hiyo wenye zaidi ya vituo vya 23 vya MEMKWA ambavyo vinawanufaisha watu wasiojua kusoma na kuandika.

Chanzo: Habari Leo

Thursday, August 4, 2011

DAWA YA BABU WA LOLIONDO: MARA INATIBU, MARA HAITIBU...


Dawa hiyo iliwahi kufagiliwa na wataalamu kwamba ni kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali. Serikali ikatoa tamko (japo kwa kuchelewa sana) kwamba dawa hiyo haifanyi kazi. Utafiti mpya wa Taasisi ya Synovate unasema dawa hiyo inaponyesha na kwamba asilimia 78 ya waliokunywa wamepona. Sasa yupi anasema ukweli?

Hili siyo jambo la mzaha kwa sababu linahusu maisha ya watu; na kule kwetu Unyantuzu wagonjwa wengi wa UKIMWI wameacha kutumia madawa ya kuongeza nguvu baada ya kunywa kikombe cha babu. Kuna ugumu gani kuwapima watu hawa kama wamepona UKIMWI au bado na hivyo kujua kwa uhakika kama dawa hii inaponyesha ama la? Japo kasi imepungua lakini vikombe vipya vingali vikiibuka. Je, vinatibu?

Hii pia inaonyesha kwa uwazi jinsi tunavyoendesha mambo yetu kimparaganyikoparaganyiko tu. Hakuna umakinifu hata kwa mambo ya muhimu kama haya. Halafu tunashangaa eti ni kwa nini mpaka leo bado hatuna umeme wa kuaminika!

UJUMBE WA LEO: NI NANI ALIKWAMBIA KWAMBA ATI HUWEZI ???

Katende !!!

Wednesday, August 3, 2011

MBUNGE WANGU KWELI NI NG'OMBE DUME MWENYE MAPEMBE ???


Maendeleo hafifu ya operesheni ya kihiari ya kujivua gamba inayoendelea ndani ya CCM inaendelea kuzusha mijadala na hata mikanganyiko. Baada ya "Mheshimiwa" Rostam Aziz kujivua gamba hivi karibuni, watu wamekuwa wakisubiri kuona matokeo zaidi ya operesheni hii. Jina la mbunge wangu limekuwa likitajwa sana kuwa ni gamba nambari wani ndani ya CCM na kama kweli chama hicho kimedhamiria kujisafisha ni lazima gamba hilo livuliwe. 

Katika makala zake za Neno la Leo, mwandishi na mchambuzi mahiri Maggid Mjengwa ameandika kuhusu ng'ombe dume wenye mapembe (ambao hujulikana kama kambako kule Usanguni) na ugumu wa kuwatoa zizini (Bofya HAPA). Katika makala yake fupi lakini yenye kufikirisha, Mjengwa anaashiria kwamba mbunge wangu Andrew Chenge a.k.a Mzee wa Vijisenti ni "kambako" ambaye amegoma kutoka zizini hata baada ya kuumwa mkia. Katika kuchangia maoni yangu huko nimesema yafuatayo kuhusu ng'ombe dume anayegoma kutoka zizini hata baada ya kumuuma mkia.


*********************
"Kule kwetu Usukumani kambako huitwa nzagamba au nziku; na wakati mwingine huwa tunawatumia katika kilimo. Nzagamba akizira; na ukamtandika viboko bila mafanikio, njia ya uhakika ni kuushika mkia wake na kuupinda - kama vile wataka kuuvunja. Hapo ni lazima atanyanyuka tu atake asitake.

Tahadhari hata hivyo ni kwamba akinyanyuka aweza kuwa na hasira kutokana na maumivu na inabidi uwe mwangalifu kwani aweza kukutwisha mapembe. Au anaweza kunyanyuka na bado akazira kuvishwa minyororo kwenda kulima. Hapa inabidi utafute wanaume hasa tena wenye uzoefu wanaoweza kumvisha minyororo na kumtoa zizini kwa nguvu atake asitake.

Swali pengine ni kwamba kama tukipinda mkia na nzagamba bado akaendelea kuzira, tunao wanaume wa shoka wa kuweza kumtoa zizini kwa nguvu?"

************* 
  • Pamoja na kwamba nimekuwa nikiandika hapa mara kwa mara kuhusu mbunge wangu huyu, pengine umefika wakati wa kujiuliza kama kweli ni gamba a.k.a kambako a.k.a nzagamba. Serikali na TAKURURU wameshamsafisha na yaliyobakia ni maneno tu ya hapa na pale. Kama kweli ni gamba mbona asijivue au kuvuliwa mara moja? Kama anayo kesi ya kujibu kuhusu mabilioni ya rada, mbona asipelekwe mahakamani? Tetesi, uvumi na udaku tu utatufikisha wapi kwa mtu aliyeliingizia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi?  Ndiyo maana nauliza: Tunao ushahidi wo wote kwamba mbunge wangu huyu ni "kambako?"

OOOPS! KUMBE ATC HAINA HATA NDEGE MOJA INAYOFANYA KAZI !!!

Ni Shirika letu la ndege la Taifa (ATC). Lilianzishwa mwaka 1973 likiwa na ndege 11. Kwa sasa hata hivyo hakuna hata ndege moja inayofanya kazi.

Tatizo hasa la Shirika hili ni nini? Kwa nini Precision ifanye vizuri hivi na shirika la taifa lishindwe?  Na bado serikali iko katika mchakato wa kulimwagia "vitendea kazi na mtaji" mpya. Shirika hili litaendelea kutafuna mabilioni ya walipa kodi mpaka lini? Kwa nini tunazidiwa hata na vinchi vidogo kama Burundi na Rwanda? Kwa habari zaidi soma HAPA

Tuesday, August 2, 2011

ATI, WENGINE HAWAKUSTAHILI KUNYANYULIWA MIKONO?


(2) Ati, bado kuna wengine ambao hawakustahili kunyanyuliwa mikono na bado "hawajaishusha"? Kama wapo, tuwafanyeje?

Ujumbe wangu (kwa njia ya picha) kwa wanyanyua na wanyanyuliwa mikono unapatikana HAPA. Mungu Ibariki Tanzania !!!

TUPO KATIKA MSIMU WA MASHINDANO YA UREMBO

Kuna misimu mingi. Kuna misimu ya mananasi, machungwa, mapera, maembe, kipindupindu n.k. Kwa sasa inavyoonekana tupo katikati ya msimu wa mashindano ya urembo ambayo yamejitandaza kila kona. Kuna Miss Vodacom Temeke, Ilala, Kinondoni….Kuna Miss Vodacom ngazi ya mikoa, kanda na hatimaye taifa. Kuna Miss Utalii katika ngazi mbalimbali. Kuna Miss Redds pia katika viwango mbalimbali. Kuna Miss Vyuo Vikuu. Kuna Miss Mlimani City Center. Kuna Miss Lake Zone. Kuna Miss...Hata huwezi kuelewa miss yupi ni yupi katika mtafaruku huu.

Japo mwanzoni niliyashambulia mashindano haya (Tazama pia HAPA), ukweli ni kwamba hayaepukiki hasa katika kipindi hiki cha utandawazi tulichomo. Maji tushayavulia nguo, ni lazima tuyakoge ati!

Kwa vile mashindano haya yanapendwa sana na yanatangazwa mno katika vyombo vya habari; ni wazi kwamba kupitia kwayo makampuni yanayoyafadhili yanapata muda mzuri wa kujitangaza kibiashara. Mteja ni lazima afikiwe kwa njia yo yote ati!

Jambo linalovutia na kutia moyo ni kwamba mengi ya makampuni haya pia yamejibidisha sana kushiriki katika miradi mbalimbali ya kijamii. Tumeshuhudia makampuni kama Vodacom yakinunua maelfu ya madawati na kujenga madarasa, nyumba na ofisi za walimu kwa ajili ya wanafunzi wetu wanaoendelea kusomea katika mazingira magumu. Hili ni jambo la kutia moyo na makampuni haya yanabidi kutiwa moyo ili yaendelee kumakinikia zaidi misaada hii ya kijamii kwani bila kuwa na uhusiano mzuri na jamii, kamwe hayawezi kufanya vizuri na kujijengea hadhi. Vita vya ukombozi wa kijamii si vya serikali peke yake. Ni vyetu sote yakiwemo makampuni haya!

"KICHENI PATI" INAPOSHINDWA KUZAA MATUNDA (UCHESHI)

(Sikumbuki nilikoipata katuni hii. Kama ni yako tuwasiliane!)

Nilishawahi kuuliza kuhusu maana hasa ya "kitchen party" na umuhimu wake kwa wanandoa HAPA. Mjadala unaweza kuendelea!

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO