NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Saturday, December 31, 2011

KATI YA HAWA KUNA RAIS WETU MWAKA 2015 !!!

...Wanasiasa vijana wanaotajwa ni pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye.


Katika kundi la umri wa kati wapo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye,  Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri Mkuu aliyejiuzulu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro.


Kundi hilo pia linawajumuisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Katika kundi la wenye umri zaidi ya miaka 60 wanaotajwa ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.....

Chanzo: Mwananchi

Friday, December 30, 2011

FIKRA YA IJUMAA: KARMA (TENDA WEMA NA USIENDE ZAKO ???)

Wakati mwingine umsaidiaye ndiye mwokozi wako, tena wa papo kwa papo. Hebu soma tukio hili fupi kwa makini kama una muda.
**************
  • Bwana Victor Giesbrecht (61) na mkewe Ann walikuwa safarini kutoka Winnipeg Canada kwenda katika jimbo la Indiana nchini Marekani. Walipokuwa wanapita katika jimbo la Wisconsin, waliona gari lililokuwa limepata pancha kando ya barabara. Wanawake wawili (Sara Berg na Lisa Meie) walikuwa nje ya gari lililokuwa limepata pancha huku wakiwa hawajui la kufanya. Bwana Victor ndiye alikuwa anaendesha; na kutokana na wema na ubinadamu wake aliamua kuacha safari na kwenda kuwasaidia wale wanawake kubadilisha tairi.
  • Baada ya kufanikiwa kubadilisha tairi, Bwana Victor na mkewe waliendelea na safari yao. Waliendesha kidogo tu na ghafla Bwana Victor alipatwa na mshtuko wa moyo na kupoteza fahamu. Mkewe alipatwa na kiwewe, na baada ya kupiga simu ya dharura (911) alibakia akihangaika tu akiwa hajui cha kufanya.
  • Kwa bahati nzuri wakati akihangaika, wanawake wawili walifika na mmoja alikuwa ni nesi na anayefahamu vyema kupambana na dharura za kiafya kama hii ya mshtuko wa moyo. Mara moja mwanamke yule alianza kumpa huduma ya kwanza Bwana Victor kwa kumpulizia pumzi kinywani na kuminya kifua chake ili kujaribu “kuufufua” moyo wake uliokuwa umezimika.
  • Aliendelea kufanya hivyo mpaka wataalamu wa mambo ya dharura walipofika. Bwana Victor alichukuliwa kwenda hospitalini ambako alikaa kwa wiki moja na baadaye kuruhusiwa kuondoka. Yule mwanamke aliyempa matibabu ya dharura katika zile dakika za mwanzo kabla ya wataalamu wenyewe kufika ndiye alikuwa ameokoa maisha ya Victor kwa kuzuia moyo wake “usife” kabisa.
  • Cha ajabu ni kwamba  mwanamke huyu shujaa mwokozi alikuwa ni  Sarah Berg - mwanamke yule yule ambaye dakika chache tu huko nyuma alikuwa amepata pancha na Victor akamsaidia kubadilisha tairi lake. Baada ya mambo kutulia na wahusika wote kutambua lililokuwa limetokea kila mmoja alimshukuru mwenzake kwa wema aliokuwa amemtendea.
Bwana Victor akiwa hospitalini
  • Tukio hili limeacha gumzo kubwa huku wengine wakisema ni muujiza na wengine wakisema ni kanuni ya Karma tu inafanya kazi: Kila tendo tulitendalo hapa duniani hutuathiri kwa namna moja ama nyingine – jema kwa wema, na baya kwa ubaya. Na wakati mwingine athari zenyewe zinaweza kuwa za papo kwa papo kama ilivyotokea kwa Victor.

  • Matendo kama haya ni ya kutia moyo sana na yanauonyesha ubinadamu wa binadamu kwa uangavu wa kutosha hata katika kipindi hiki ambapo binadamu analaumiwa kuwa ameupoteza ubinadamu wake na kutawaiwa na ubinafsi na uchoyo. Ndiyo maana hata mimi sijausahau wema niliofanyiwa na mzee mmoja mwenye kibaraghashia na kandambili za bluu miaka 18 iliyopita nilipokuwa nimelazwa katika hospitali ya Muhimbili.  
  • Kisa hiki chenye mafunzo tele kinapatikana HAPA. Unaweza kutazama video ya kisa hiki HAPA. Unaweza pia kusoma kipengele cha UBINADAMU katika blogu yangu HAPA.
****************
Wikiendi njema wadau.

Hebu basi kutenda wema na likawe
 azimio letu mojawapo katika 
mwaka mpya ujao (2012) !!!


****************

Thursday, December 29, 2011

HILI NALO NENO: ETI UFAULU WA KISWAHILI UMESHUKA ZAIDI UKILINGANISHWA NA ULE WA KIINGEREZA KWA WATAHINIWA WA DARASA LA SABA.

Ni wazi kwamba Kiingereaza kimeshatushinda, lakini je, hata Kiswahili nacho kinakaribia kutushinda? Lugha ya kufundishia ni nguzo muhimu katika mfumo wo wote ule wa elimu na kusema kweli bila kuwa na sera thabiti ya lugha ya kufundishia, elimu hugeuka na kuwa kama mchezo tu. Ni lini tutafanya marekebisho yanayotakiwa na kuhitajika sana katika sera yetu ya lugha ya kufundishia?
***********

Ni Aibu kwa Wanafunzi wa Tanzania Kufeli Kiswahili
(Ijumaa, 23/12/ 2011) 

HIVI karibuni tumesikia kuwa ufaulu katika somo la Kiswahili kwa matokeo ya darasa la saba mwaka huu, umeshuka ukilinganisha na  ufaulu wa somo  Kiingereza.

Hali hiyo inaweza kuwashangaza watu wengi waliopo nchini kwa wanafunzi kushindwa kumudu lugha yao ya taifa. 

Hasa kwakuwa  inafahamika wazi kuwa Kiswahili ndiyo lugha inayotumika kama  lugha ya mawasiliano kwa mwanafunzi  kwa ngazi ya shule ya msingi kwa kipindi chote cha  masomo kwa miaka saba, wakati Kiingereza kinafundishwa kama somo tu.

Kwa kiasi kikubwa, Watanzania wanaweza kuzungumza Kiswahili fasaha, lakini akiingia darasani kufanyia mtihani anaweza kufeli vibaya hata ukimshindanisha na mtu ambaye ni lugha yake ya tatu au ya kujifunza.

Waswahili husema “mdhaarau mwiba mguu huota tende,  hayo ndiyo tunayoyaona sasa katika kiwango cha ufaulu katika somo la Kiswahili. Lakini katika ngazi ya elimu ya msingi na shule za upili Kiswahili hutumika, ili kukidhi mahitaji ya mwanafunzi katika kumjenga ili kuwa na msingi mzuri katika kufahamu vyema lugha yake.

Tukiwa tunatafakari katika matokeo hayo, yapo mambo kadhaa yanayopaswa  kutazamwa na kuchukuliwa hatua ili kuepuka fedheha kwa wanafunzi kufeli somo hilo.

Hata hivyo kwa upande wa wanafunzi wa ngazi za juu ya elimu ya chuo kikuu na vyuo huwa, na rejesta zao mojawapo ni kukiona Kiswahili kuwa kigumu.

Hata hivyo usemi huo unaweza ukawa na athari chanya iwapo watu watachukua hatua kukabiliana na changamoto hiyo kwa  kubaini ugumu kwake uko wapi na kushirikiana na wenzake katika kupitia mada zinazomsumbua ama asizozielewa vyema kwa msaada zaidi, ikiwa ni pamoja na kupitia maandiko mbalimbali ya wataalamu wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.

Vilevile  wanafunzi wa shule za msingi wanapaswa kazingatia masomo na kwa kupunguza michezo na soga pamoja na mambo yasiyo na tija pamoja na kutafuta muda wa ziada kujisomea kwa bidii ili kuyatafutia ufumbuzi yale ambayo hayakueleweka vyema wakati wa vipindi vya darasani.

Upande wa walimu wanapaswa kuendelea kufundisha somo la Kiswahili kitaaluma zaidi kuliko kufundisha kwa mazoea na kurahisisha mbinu za kufundishia kwa wanafunzi hao.

Ushirikiano huo  wa walimu na wanafunzi ukiwa thabiti na kila mtu akatekeleza majukumu yake, hakuna sababu ya mwanafunzi kufeli  somo la Kiswahili katika  ngazi zote. 

Hii ni kutokana na mambo mengi yanayoelezwa katika lugha hiyo yanahusu mazingira yaliyo karibu na mwanafunzi. Hata hadithi zinazoelezewa  na watunzi wa vitabu ni kutoka mazingira hayo ambapo makabila ya Watanzania ni wazungumzaji wakubwa wa lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wa mwenendo wa kuendelea kushuka kwa ufaulu wa mwanafunzi nchini si jambo la kuachwa kwani hiyo inadhihirisha kwamba jamii ya Watanzania hawafahamu mambo mengi katika lugha yao licha ya kuzungumza kila wakati.

Kwa hali hiyo ningetegemea kuona somo la Kiswahili linakuwa la kwanza katika ufaulu wa masomo mengine licha ya kuwa masomo mengine  nayo yanafundishwa kwa lugha ya Kiswahili kwa ngazi zote kinakofundishwa.

Ipo haja ya kubaini chanzo cha wanafunzi hao kutofanya vyema katika somo hilo ikiwa ni njia ya kuelekea kupata ufumbuzi wa moja kwa moja. Lakini chanzo moja wapo ni    wanafunzi kutofahamu sarufi ya lugha yao ya  Kiswahili. Kwani  sarufi katika lugha yoyote ndiyo uti wa mgongo wa lugha hiyo.

Kuwa na walimu wenye uzalendo na waliopikwa katika kufundisha somo la  Kiswahili hilo, watumike ipasavyo katika maeneo yenye uhaba na si mwalimu yeyote anayezungumza lugha hiyo apewe nafasi ya kufundisha Kiswahili. Hilo linaweza kuwa na tija katika kuleta maendeleo ya kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Jambo lingine la kuzingatia ni kuimarisha kwa kiwango cha zana za kufundishia. Huku baadhi ya walimu wamekuwa hawazingatii hilo kwa wa kwa kuona kuwa ni kupoteza muda na gharama, wakati hata zipo njia mbalimbali za kuunda zana hizo bila gharama yeyote.

Aidha katika kukabiliana na changamoto hiyo ya kuendelea kushuka kwa kiwango cha Kiswahili, pia walimu wa Kiswahili kwa umoja wao wanapaswa kuliangalia katika umoja wao walimu wa Kiswahili kwa ngazi mbalimbali.

Tunapojiandaa kuingia mwaka mpya, natumaini wanafunzi wataendelea kujizatiti ili kuhakikisha kuwa wanafanya vyema katika mitihani yao ya Kiswahili kwa mwaka unaokuja.
Walimu ambao ndiyo walezi wakuu wa wanafunzi hao, nao wanapaswa kuangalia njia nzuri za kuondokana na aibu hii ya kila mwaka kuendelea  kushuka kwa ufaulu wa somo la Kiswahili.

Njia pekee ni kuwa na mipango endelevu inayoakisi maendeleo ya Kiswahili katika kukikuza na kukieneza.

Baraza la Kiswahili nchini kwa kushirikiana na taasisi za lugha ya Kiswahili nchini nalo linapaswa kutoa mchango wake kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla ili kukifikisha Kiswahili katika hadhi na kukitangaza nje ya Tanzania.

Mathalani, kuwapo na ushirikiano baina ya walimu wa Kiswahili na watendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa, kutaleta tija katika kusukuma gurudumu  la maendeleo nchini.

Chanzo: Mwananchi

VITUKO VYA WALIMWENGU: JAMAA APORA BENKI NA KURUDI BAA KUMALIZIA BIA ALIYOKUWA AMEIAGIZA

  • Huyu mwizi (kwa jina John Robin Whittle, 52) ametoa mpya. Alianza kwa kuingia kwenye baa na kuagiza bia. Baada ya kunywa kidogo alitoka na kwenda kupora benki iliyokuwa karibu. Baada ya kufanikisha uporaji wake, jamaa alirudi kwenye baa ile ile kumalizia bia yake. Wanywaji wenzake walishangaa baadaye walipoona polisi wanavamia baa hiyo na kumtia jamaa mbaroni.
  • Kisa hiki kimeleta gumzo kubwa kwa watu huku wengine wakidai kwamba mwizi huyu alijilengesha kwa polisi makusudi na kwamba alikuwa anataka kukamatwa. Wengine wanasema kwamba jamaa ni mwizi mzoefu na pengine alikuwa amejiamini kupita kiasi.
  • Miye huvutiwa na vituko vya aina hii kwa sababu kupitia kwayo tunaweza angalau kupata fununu kidogo kuhusu uasili na undani hasa wa huyu mnyama machachari ajiitaye “Homo Sapiens”

  • Kituko hiki kimetokea kule Tampa katika jimbo la Florida nchini Marekani. 

Wednesday, December 28, 2011

MAISHA YA KUMBUKONI - WAKUMBUKE WAZAZI (NA KILIMAMBOGO BROTHERS)

  • Nyakati zile kulikuwa na jamaa mmoja pale kijijini kwetu mwenye baisikeli iliyoandikwa "Kaminomino Mpenda Wasichana. Uliza Sababu Yake". Huyu jamaa alikuwa mashuhuri sana na ndiye pekee alikuwa na redio yenye uwezo wa kucheza kanda za kaseti. Ndipo nilipozisikia nyimbo hizi za Kakai Kilonzo na Kilimambogo Brothers kwa mara ya kwanza. 
  • Nashangaa kwamba hata baada ya miaka zaidi ya 20, ujumbe katika nyimbo hizi ungali hai mno. Ni kosa kubwa kukimbilia mijini au huku nje na kuwasahau wazazi waliotulea na kutusomesha hasa kwa sisi tuliotoka vijijini. Tuwakumbuke wazazi !!! 

MKATE WA USHOGA NDIO HUO UNAPAKWA "BLUE BAND." WAAFRIKA TUTAWEZA KUUEPUKA ?


Inaonekana mabwana wakubwa hawa hawajaridhika na utumwa wa kiuchumi, kifikra, kisaikolojia na kitamaduni waliouanzisha wakati wa biashara ya utumwa, kuupalilia wakati wa ukoloni na kuuendeleza kupitia ukoloni mamboleo hadi leo.

Hawajaridhika:
  • Pamoja na ukweli kwamba bado tunaendesha mifumo yetu ya elimu kwa kutumia lugha zao – lugha ambazo wala hatuzielewi vizuri; na hivyo kufanya elimu tuwapayo vijana wetu kuwa kichekesho.
  • Pamoja na ukweli kwamba tungali tunadhani kuwa kila kitu chao ni bora kuliko cha kwetu.
  • Pamoja na ukweli kwamba tungali tunaiga kila kitu wanachofanya: wakitembea uchi nasi tunaiga, wakilegeza suruali zao nasi tunalegeza, wakitoboa masikio na kusuka nyweli nasi tunafanya vivyo hivyo.
  • Pamoja na ukweli kwamba tumezungukwa na utandawazi wao kila kona.
Sasa wanatulazimisha kuhalalisha ushoga – jambo ambalo naamini katika makabila mengi ya Kiafrika (lilikuwa) linafanyika kwa siri ingawa sasa, kutokana na utandawazi tumeanza kuona “maanti” wakijitokeza waziwazi.

“Blue Band” hii inayopakwa kwenye huu mkate wa ushoga ni nini? Ni Donge nono la misaada ambalo, kama makinda ya ndege yasiyojiweza, tumezoea kumegewa pamoja na ukweli kwamba Mungu Ametujalia kila kitu; na sehemu kubwa ya donge hili huishia katika midomo mipana ya wachache.

Serikali ya Uingereza imeweka wazi kwamba haitatoa misaada yake kwa nchi ambazo hazikubaliani na ushoga. Serikali ya Marekani pia imetoa masharti kama hayo. 



Kutokana na mikwara hii, serikali ya Malawi ilibidi kulegeza kamba kuhusu msimamo wake kwa sababu asilimia kubwa ya bajeti yake inategemea misaada kutoka Uingereza na Marekani. Hata  Uganda  imeonyesha dalili za kutetereka katika msimamo wake kuhusu suala hili.

Ni nchi chache za Afrika zinazoweza kujiendesha bila “Blue Band” hii ya wakubwa na tusije kushangaa huko mbele tukisikia washika kurunzi wetu wameshatia sahihi mikataba ya kuukubali ushoga – hata kama majukwaani wanajipiga kifua na kulaani. Msimamo wa sasa wa Tanzania kuhusu suala hili ni wa kutia moyo sana. Natumaini kwamba hautabadilika; na hata ukibadilika basi usiwe ni kutokana na kulazimishwa na hawa wakubwa.



Bila kujali maoni na msimamo wangu kuhusu ushoga, kinachonikera mimi ni kulazimishwa kukubaliana na matakwa ya hawa wakubwa wetu. Utumwa haukutosha? Ukoloni haukutosha? Ukoloni mamboleo je? Pamoja na yote haya, mpaka tukubali ushoga kweli ndo tupate misaada? Ni lini tutaweza kusimama tisti na kuendesha mambo yetu bila kutegemea mikate hii iliyopakwa "Blue Band" yenye sumu ???

Friday, December 23, 2011

FIKRA YA IJUMAA: HIVI NI KWA NINI KILA KIONGOZI HUDHANI KUWA ANAPENDWA SANA NA WATU WAKE ?


"Wananipenda. Watakufa ili kunilinda. Watu wangu!"
Muammar Gaddafi (1942 - 2011)

Tumewaona. Wapo. Walikuwepo na Watakuwepo. Tena wamejaa tele katika jalala la Historia.

Hata muda wao wa kutawala ukiisha, utawaona wakihangaika kujaribu kubadili katiba za nchi zao ili waendelee kutawala. Utawasikia wakijigamba:

"Ninapendwa mno! Watu wangu bado wananihitaji. Siwezi kuiacha nchi yangu"

"Macho man" wa Urusi. Naye Anadai Anapendwa Sana!
  • Hata upepo wa mabadiliko unapoanza kuvuma, kama vile mazuzu, watawala hawa wapendwa waliojaa kiburi, dharau, ubilionea na ulevi wa madaraka hushindwa kujitafakari, kujisaili na kusoma alama za nyakati. Na matokeo yake daima huwa ni ya kusikitisha. Wengi wao huishia "kugadafishwa" na wengine hujikuta katika shimo la takataka la Historia kinyume na matarajio yao.
"Simba" wa Syria. Pia anadai anapendwa sana!
  • Kama kuna jambo ambalo hunifurahisha na kunifanya nijisikie vizuri na hata kunifanya nijimwambafai kama Mtanzania ni utaratibu wetu tuliojiwekea wa kubadilishana madaraka kwa njia za amani kila baada ya miaka 10 - tena bila kujali kama wanapendwa ama la. Natumaini kwamba tutauendeleza utaratibu huu. Mwalimu Nyerere alishatuonyesha njia. 
Mungu Ibariki Tanzania !!!  

Thursday, December 22, 2011

JAMANI EEH: HAYA MAGAMBA YENYE "SUPA GLUU" MWISHOWE YATAIDHOOFISHA AFYA YA NYOKA WETU.

  • Ni kweli amekosekana mkereketwa jasiri mshika korombo akayabobonyoa haya magamba sugu kwa nguvu? Kubembelezana mpaka lini wakati nyoka wetu anazidi kudhoofika? Kipi ni cha muhimu zaidi: magamba yaliyochoka na kumaliza muda wake au afya ya nyoka wetu? Aiiii !!!

Katuni hii ni kutoka kwa Said Michael.

Wednesday, December 21, 2011

WANAFUNZI HEBU SOMENI UTAFITI HUU: ETI KUTAFUNA BAZOKA DAKIKA TANO KABLA YA MTIHANI HUONGEZA KIWANGO CHA UFAULU.

  • Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba kutafuna bazoka (gamu/bigiji/chingamu/ubani wa kutafuna) kuna faida katika kuimarisha afya ya kinywa na hata jitihada za kupunguza uzito wa mwili na msongo wa mawazo. Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la kitaaluma la Appetite unaonyesha kwamba kutafuna bazoka dakika tano kabla ya mtihani kunawasaidia wanafunzi kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao kuliko wenzao ambao hawakufanya hivyo.
  • Utafiti huu unaonyesha kwamba kutafuna bazoka kunachangamsha na kusisimua ubongo na kufanya wanafunzi wakumbuke vitu vizuri na kwa urahisi; na hivyo kuweza kufanya vizuri katika mitihani yao.
  • Utafiti huu pia unaonyesha kwamba kutafuta bazoka wakati wa mtihani wenyewe kunaweza kuingiliana na shughuli za ubongo za kufikiri na kukumbuka mambo na hivyo kuwafanya wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao.
  • Wanasayansi hawa pia wanaonya kwamba wanafunzi wasitegemee kutafuna bazoka dakika tano kabla ya mitihani yao ili kufaulu. Wanabainisha wazi kwamba kutafuna bazoka kunasisimua tu kumbukumbu na mambo ambayo mwanafunzi tayari ameshajifunza, kujisomea na kuyahifadhi ubongoni mwake. Kama wanataka kufaulu mitihani yao, wanafunzi ni lazima wajisomee na kujiandaa vizuri kwa ajili ya mitihani yao.
  • Vidokezo vizuri kuhusu jinsi ya kujiandaa kufanya mitihani vinapatikana HAPA. Habari za utafiti huu zimedokezwa HAPA

Tuesday, December 20, 2011

HILI NALO NENO: ETI BABU WA LOLIONDO KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UTAPELI

  • Eti babu wa Loliondo anafunguliwa kesi za jinai na madai. Anafunguliwa kesi ya jinai kwa kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kwamba eti aliwahadaa watu kwamba dawa yake inatibu wakati hakuna mtumiaji aliyepona. 
  • Pia anafunguliwa kesi ya madai ili aweze kulipa fidia za watu waliopoteza maisha na wote waliosafiri kutoka sehemu mbalimbali huku wakitumia gharama kubwa ili kupata dawa isiyotibu.
Lakini je:
  • Vipi kuhusu mawaziri na vigogo wa serikali waliokuwa wakimiminika Loliondo huku wakiifagilia dawa hiyo kwamba ilikuwa imewasaidia na hivyo kuendelea kuchochea moto wa tiba hiyo?  Hawahusiki kwa namna yo yote na "utapeli" huu?
  • Maswali ya kujiuliza katika suala hili ni mengi na yote yanaonyesha jinsi tunavyoendesha mambo yetu kama jamii. Hatuko makini, hakuna uwajibikaji na mambo yetu mengi - hata yale ya muhimu kabisa - tunayafanya kimzahamzaha tu. Kama anavyosema mhusika mmoja katika vibonzo vya Pogo, adui wa maendeleo yetu si mwingine bali ni sisi wenyewe!
  • Jikumbushe habari mbalimbali kuhusu Babu wa Loliondo na "tiba" yake ya kimiujiza HAPA.

MANENO YA BUSARA KUTOKA KWA MWANDISHI MASHUHURI ERNEST HEMINGWAY


Haya ni maneno ya busara; na haijalishi kama Ernest Hemingway mwenyewe aliishia kujiua kwa kujipiga risasi. Maisha!

UTAFITI: MAPENZI YA KUTUMIA MIDOMO SASA CHANZO KIKUU CHA KANSA ZA KINYWA, KICHWA NA SHINGO.

Binadamu ni kiumbe wa ajabu sana; na ukichunguza vizuri matatizo yake mengi  ni ya kujiletea tu.  Hebu jaribu kufikiria: ni magonjwa mangapi ambayo anajisababishia mwenyewe? Tazama vita anavyopigana, tazama anavyoua wanyama wengine – na wakati mwingine ni kwa lengo la kujifurahisha tu! Tazama anavyoharibu mazingira. Tazama anavyoweza kuiba na kujilimbikizia mali na kuwaacha wenzake walio wengi wakiteseka. Akili, weledi, ulafi, uchoyo na uhasama vimemzidi. Tazama!

Akili na weledi huu wa binadamu umeingia hata katika tendo la kujamiiana, tendo ambalo kwa wanyama wengine limelengwa hasa katika kuhakikisha kuwa kizazi kipya kinazalishwa na maisha yanaendelea. Kwa binadamu, tendo hili limegeuka kuwa starehe naye anajaribu kila njia – potelea mbali hata kama ni kinyume na maumbile! Matokeo yake ni kujiletea matatizo.

Katika utafiti mpya, wanasayansi wanaonyesha kwamba mapenzi ya kulambana na kunyonyana sasa yanasababisha asilimia 64 ya kansa zote za kinywa, shingo na kichwa. Wanasayansi hawa wanaonyesha kwamba mtu ambaye amefanya mapenzi haya ya kulambana na kunyonyana na watu sita au zaidi katika maisha yake ana uwezekano wa kupata kansa za kinywa mara nane zaidi akilinganishwa na mtu ambaye hajawahi kufanya mapenzi ya aina hii.

Mbali na tumbaku, kansa nyingi za kinywa husababishwa na kirusi cha Genital humanpapillomavirus (HPV) ambacho huenezwa hasa kupitia mapenzi ya kulambana na kunyonyana.

Japo utafiti huu umefanyika nchini Marekani, mimi nadhani ni suala la muda tu kabla nasi hatujakumbwa na masaibu haya hasa kutokana na tabia yetu ya kuigaiga mambo kizembe na wakati mwingine hata kuwazidi hata hao tunaojaribu kuwaiga. Tuwe makini.

Kwa habari zaidi kuhusu kirusi cha HPV na jinsi ya kujikinga nacho soma HAPA. Habari kuhusu utafiti huu zinapatikana HAPA.

Monday, December 19, 2011

WANABLOGU WENZANGU NA WAPENZI WOTE WA KWELI WA BLOGU HII: SASA NIMERUDI RASMI !!!


Wapendwa wanablogu wenzangu na wapendwa wote wa blogu hii. 
  • Kwanza nianze kwa kuwaomba msamaha kwa kupotea bila kuaga. Wakati mwingine misukosuko ya maisha, kama vile dhoruba isiyo na soni wala utashi, hutuvamia na kututupa huku na huko mithili ya tiara iliyokatikiwa kamba au mtumbwi hafifu katikati ya dhoruba ya karne! Wasimamao tisti na kupigana kiume (kike?) hubakia na "viburi" vyao na tabasamu la ushindi baada ya dhoruba na misukosuko hii ya maisha. Nami nimepita dhorubani humo, nimeyaona niliyoyaona na kujifunza niliyojifunza, na kama vile chuma kilichopita tanuruni - kikafuliwa na kung'arishwa mithili ya kioo, nimetoka salama. Maisha ni lazima yaendelee ati - tena kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Maisha !!!

  • Na kwa tangazo hili napenda kuwaataarifu rasmi kwamba sasa nimerudi na kuanzia sasa mambo yatakuwa motomoto katika blogu hii. Na jicho na sikio langu sikivu sasa vitaonekana tena katika blogu zenu pendwa - kama kawaida vikiona na kudodosa yanayotokea huko. Tuko pamoja daima !!! 
  • Natumaini mambo yanaendelea vyema huko mliko. Hebu mwaka huu na ukaishe kwa amani na salama; na sote tukaweze kuuona mwaka mpya wa 2012 ingawa sina uhakika sana kama kuna faida yo yote ya kufanya hivyo. Maisha !!!

VITA VYA IRAQ VIMEMALIZIKA: WAMAREKANI WAMEPATA FAIDA GANI?

Batalioni ya mwisho ya jeshi la Marekani ikiingia nchini Kuwait
Jana Batalioni ya mwisho ya wanajeshi wa Marekani ilivuka mpaka na kuingia nchini Kuwait. Hii ilikuwa ni ishara ya mwisho kwamba vita vya Wamarekani nchini Iraq vilikuwa vimemalizika rasmi na rais Obama ametimiza mojawapo ya ahadi zake kuu alizozitoa wakati wa kampeni. 
Swali linaloulizwa na watu wengi ni hili: Wamarekani wamepata faida gani katika vita hivi vilivyodumu kwa takriban miaka tisa? Katika vita hivi:
  • Wamarekani hawakupokelewa kwa mbwembwe, nderemo na vifijo kama walivyodhani na matokeo yake wamepoteza wanajeshi 4,487 na majeruhi zaidi ya 30,000
  • Wairaq zaidi ya 100,000 wameuawa.
  • Wamarekani wametumia kiasi kikubwa cha pesa (pengine zaidi ya dola trilioni moja ukijumlisha na gharama za matibabu ya wanajeshi wanaorudi kutoka vitani). Pesa hizi ni za kukopa na zimechangia katika kuongeza na kukuza naksi ya bajeti na hivyo kusababisha uchumi wa Marekani kuyumba.
  • Wamarekani bado hawajaweza kuyapata mafuta ambayo watu wengi wanadhani kwamba ndilo lilikuwa hasa lengo la vita hivi.
  • Wamefanikiwa kumuua Saddam Hussein na watoto wake na hivyo wamefanikiwa “kuikomboa” Iraq kutoka mikononi mwa dikteta na kuifanya kuwa nchi ya kidemokrasia. Matumaini ya Rais Bush yalikuwa kwamba kuanguka kwa Saddam kungewasha moto wa mabadiliko katika nchi za Kiarabu. Hili halikutimia na kwa bahati nzuri moto wa mabadiliko ukawashwa na machinga wa Tunisia aliyeamua kujichoma moto baada ya kuchoshwa na unyanyasaji wa vyombo vya dola.

Ngoja tuone kama Wairaq wataweza kusimama kidete na kama hiyo demokrasia waliyopandikiziwa itadumu!

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

BLOGU ZA BURUDANI NA UREMBO