NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, January 30, 2012

ANA MIAKA 85. AMEBADILI KATIBA ILI AWEZE KUGOMBEA KIPINDI CHA TATU. SASA WATU WAKE WANAANDAMANA

  • Kwa upande mmoja kuna Mwalimu Nyerere na rafiki yake Madiba. Marafiki hawa daima watabakia kuwa nyota zinazong'ara barani Afrika. Pamoja na kuandika historia kwa kuwa mababa wa taifa, kuonyesha uadilifu wa kiwango cha juu wakati wakiwa madarakani na kuweka dira za kihistoria na kisiasa katika nchi zao, viongozi hawa waliamua kuachia madaraka pamoja na ukweli kwamba wangeweza kuendelea kubakia madarakani kama wangetaka. Ati, ni nani angeweza kumpinga Nyerere (na akafanikiwa) kama angeamua kubakia madarakani?
  • Kwa upande mwingine wapo akina Mubarak wa Misri na kundi lake - viongozi ambao hawakutaka na bado hawataki kuachia madaraka. Viongozi wa kundi hili, hata wazeeke vipi na fikra zao kuchakaa namna gani, bado watafanya kila wawezalo ikiwemo kubadilisha katiba na hata kuiba kura ili tu waweze kubakia madarakani. Ikibidi ni lazima wafie madarakani au wang'olewe kwa nguvu na hata kuuawa. Kuna msururu mrefu wa viongozi wa aina hii barani Afrika! 
  • Abdoulaye Wade - rais mkongwe (miaka 85) wa Senegal naye ameingia katika kundi hili. Yeye amebadilisha katiba ili aweze kugombea kipindi cha tatu. Pia amefanikiwa kumfanyia mizengwe mgombea wa upinzani, mwanamuziki mashuhuri Youssou N'Dour  ili asiruhusiwe kugombea. Jambo la kufurahisha ni kwamba umma wa Senegal umeonyesha kukerwa na jambo hili na tayari maandamano yanafanyika kujaribu kumpinga huyu babu kuendelea kubakia madarakani. Itafurahisha sana kama matakwa ya umma yatashinda kama ilivyokuwa kule Misri, Tunisia na Libya.
  • Pengine jambo la muhimu tunalopaswa kujiuliza hapa ni hili: Kwa nini viongozi wa Afrika wana uchu wa madaraka namna hii kiasi cha kupuuza matakwa ya watu wao na kufikia hata kubadilisha katiba za nchi zao ili tu waendelee kubakia madarakani? Utakuta kiongozi amekaa madarakani miaka nenda miaka rudi na hakuna la maana alilofanya mbali na ufisadi na kusikinisha watu wake lakini bado tu anataka aendelee kubakia madarakani. Kwa nini? Na umma wa Afrika, kama vile kondoo wapelekwao machinjioni, umeonyesha uvumilivu wa kupita kiasi kwa viongozi hawa wa milele. Ni mpaka hivi karibuni tu umeanza kuamka na kusema sasa yatosha. 
  • Tabia hii ya viongozi wapenda madaraka kung'ang'ania madarakani barani Afrika inabidi ikomeshwe; na natumaini kwamba umma wa Senegal utashinda
Mungu Ibariki Afrika !!! 

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU