NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, January 24, 2012

"MACHO YAKO MBONA HAYATULII MUME WANGU? WEWE LAZIMA UTAKUWA NA MWANAMKE WA NJE" !!!


Katika tamaduni nyingi za makabila ya Kitanzania, kukaziana macho wakati wa mazungumzo ni jambo geni. Mara nyingi watoto hawaruhusiwi kuwatazama watu wazima usoni wakati wa mazungumzo. Kufanya hivyo ni ukosefu wa adabu. Hali kadhalika katika makabila mengi wanawake pia hawakupaswa kuwaangalia wanaume usoni wakati wa mazungumzo. Kufanya hivyo ilikuwa dalili ya uchakaramu. 

Nakumbuka nilipofika hapa Marekani kuanza masomo swala hili lilinipa shida sana kwani nilikuwa siwezi kuongea na maprofesa, wanafunzi wenzangu na watu wengine huku nikiwa nimewakazia macho usoni. Nilizidi kuchanganyikiwa zaidi pale wasichana wa Kimarekani walipokuwa wakiongea nami huku wamenikazia macho usoni. 

"Wasichana gani hawa wasio na aibu?" Nilikuwa nikijiuliza mara kwa mara.


Sikujua kuwa hili lilikuwa ni tatizo mpaka siku moja mshauri wangu aliponiita ofisini kwake na kuniambia kwamba watu walikuwa wakilalamika kwamba nilikuwa siwaangalii machoni wakati wa mazungumzo. Aliniambia kwamba kwa Wamarekani kuongea na mtu bila kumwangalia usoni ni jambo baya sana. Linaonyesha kwamba pengine unachokisema si cha kweli na kwamba wewe siyo mtu wa kuaminika. 

Japo nilijibidisha sana kufanya mabadiliko na kuanza kuwakazia watu macho usoni wakati wa mazungumzo, ni lazima nikiri hapa kwamba hili halikuwa jambo rahisi. Na kusema kweli mpaka leo sijalizoea jambo hili na daima huwa sijisikii huru kufanya hivyo.

Ndiyo maana hii katuni kidogo imenishangaza. Pengine ni matokeo ya utandawazi na minyororo yake ya kitamaduni. Ni tangu lini mke na mume wa Kiswahili wakakaziana macho wakati wa mazungumzo? Pengine wanandoa wasomi wa mijini lakini siyo kule vijijini. Na simlaumu huyo baba kwenye katuni kwa kushindwa kwake kuhakikisha kwamba kunakuwa na "eye contact" kati yake na mkewe. Huu si utamaduni wetu na kwa sisi wazee hili ni jambo ambalo inabidi tujifunze kama kuna ulazima wa kufanya hivyo.

Kwa tofauti na mifano mbalimbali ya migongano ya kitamaduni kati ya Waafrika na Wazungu (hasa Wamarekani) jaribu sana kusoma kitabu mashuhuri cha Profesa Mbele kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

3 comments:

 1. Mwalimu Matondo, asante sana kwa katuni. Imenivutia sana. Nilpokuwa nasoma maelezo yako, kabla sijafika mwishoni, niliguswa, na mawazo yangu yakaenda moja kwa moja kwenye kitabu changu. Tena nilitaka niandike ujumbe na kuwajulisha wadau, kumbe wewe mwenyewe umefanya hivyo hapa mwishoni. Nashukuru.

  Jambo lisilopingika ni kuwa wa-Afrika waliomo humu Marekani wanataabika kutokana na hizi tofauti za tamaduni, lakini tatizo ni kuwa sio rahisi kuelewa kwa undani kinachotokea na kwa nini. Mtu anabaki na masuali, mshangao, msongo wa mawazo, na hasira. Nina hakika matatizo mengi ya kisaikolojia yanatokana na mambo hayo.

  Na kwa upande wa hao wa-Marekani ni hivyo hivyo. Akitoka hapa na kutua Bariadi bila kuelewa tofauti za tamaduni, naye anakumbana na yale yale yanayompata Msukuma hapa Marekani, ila tu inakuwa ni upande wa pili wa sarafu.

  Asante kwa kuibua mjadala huu muhimu.

  ReplyDelete
 2. Tamaduni:- Nilipata pia shida sana kuongea na kumtazama mtu mwanzoni kama alivyosema pro. hapo juu. Ahsante kwa kuliweka wazi hili natumaini wengi watasoma/wamesoma.

  ReplyDelete
 3. NDUGU YANGU ASANTE KWA KULETA HILI SWALA, MIMI BINAFSI SIWEZI KUONGEA NA MTU BILA KUMWANGALIA MTU USONI, SASA HUWA NAPATA TABU SANA NIKIJA TANZANIA KWASABABU WANAUME WANAKUWA NA FIKRA POTOFU NIKIWA NAWAANGALIA USONI, SASA MARA NYINGI MTU ANAKUFIKIRIA VIBAYA LKN NI KITU AMBACHO SIWEZI KUKICONTROL KWA KWELI.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU