NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, February 28, 2012

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM "WANASIKITISHA" !!!

Picha hii ya wasomi wa Mlimani inapatikana HAPA
 • Kabla hamjaanza kunirushia "mawe" inabidi nianze kwa kusema kwamba hii siyo kauli yangu. Ni kauli ya mwanafunzi wa Kimarekani aliyekuwa anafanya utafiti kwa ajili ya tasnifu yake ya uzamili kule Zanzibar na Dar es salaam. Mwanafunzi huyu pia alikuwa anahudhuria mihadhara michache ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
 • Alipotoa kauli hiyo hapo juu nilishtuka sana. Nilifikiria ni yale yale ya mababu zake waliokuja Afrika na kuanza kutuhukumu kwamba Waafrika tulikuwa na tamaduni za kipumbavu; na kwamba ustaarabu ulikuwa umetupiga chenga. Ilibidi nimsikilize kwa makini wakati alipojaribu kufafanua kauli yake hii. Kimsingi hoja yake ilikuwa imeegemezwa katika mambo yafuatayo:
(1) Lugha ya Kiingereza
 • Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam hawawezi kuendesha mazungumzo ya maana kuhusu jambo lolote katika lugha ya Kiingereza. Pamoja na shauku kubwa ya kutaka kumwonyesha wema na kumwingiza katika mazungumzo ya aina mbalimbali, Kiingereza cha wanafunzi wengi wa Mlimani kilikuwa kibaya kiasi kwamba wengi wao waliishia kumkodolea macho tu. Alisema kwamba alijisikia vibaya sana na alijaribu kutumia Kiswahili chake kibovu huku akichanganya na Kiingereza. Aliniomba nitoe maoni yangu kuhusu sababu zinazosababisha umuduji hafifu wa Kiingereza kwa wanafunzi wa chuo kikuu.
 • Baada ya kumpa maoni yangu ambayo yaliyojumuisha sera yetu tatanishi ya lugha ya kufundishia na changamoto zingine katika mfumo wetu wa elimu, nilijaribu kumchokoza kwa kumuuliza ni kwa nini alikuwa anategemea wanafunzi hawa kufahamu Kiingereza. Mbona yeye hakujiandaa vyema na kujifunza Kiswahili vizuri kabla hajaja kufanya utafiti wake? Aliniambia kwamba Kiswahili alichojifunza kilikuwa kinatosha kuuliza maswali yake hojaji (questionnaires) na kurekodi majibu aliyohitaji. Aliendelea kuniambia kwamba hakuendelea kujifunza Kiswahili zaidi baada ya kugundua kwamba Kiingereza kilikuwa ni lugha ya kufundishia na alitegemea kwamba wanafunzi hawa wangekuwa wanaifahamu vizuri lugha ya kufundishia.
(2) Maprofesa
 • Kimsingi alisema kwamba hakujifunza cho chote cha maana na anajihisi kama vile pesa za ada alizolipa zilikuwa zimeenda bure tu. Maprofesa ni haba sana na waliopo inaonekana wameelemewa na wingi wa wanafunzi. Kwa mfano, profesa wa darasa lake hakufika kwa karibu wiki zote nne za mwanzo wa muhula na hata alipofika alisema kwamba alikuwa amepangiwa kipindi kingine katika wakati ule ule aliopaswa kufundisha darasa la hawa Wazungu kutoka Marekani. Inaonekana Profesa alichagua kufundisha darasa la Watanzania kwani Mmarekani huyu alidai kwamba darasa lao halikukutana zaidi ya mara nne kwa muhula mzima.
 • Mara nyingine Profesa alipiga simu na kuwaambia wanafunzi waliokuwa wakimsubiri darasani kwamba alikuwa amekwama katika foleni ya magari, gari lake lilikuwa limeharibika na visingizio vingine. 
 • Tuliongea mengi kuhusu suala hili na nilijaribu kumwambia kwamba hali ya hewa ya kimasomo Mlimani inaweza kuonekana kuwa legevu hasa katika wiki mbili za mwanzo lakini ikija kuchangamka huko mbele ni moto mtindo mmoja. Alicheka tu na kusema kuwa si kweli. Yeye alikuwa haamini kama wanafunzi wale walikuwa wanasoma wanachopaswa kusoma; na alikuwa haamini kama kweli wanafunzi wetu wanaweza kupambana katika soko la ajira la Kimataifa!
(3) Matatizo ya Kimiundo mbinu 
 • Mfano udogo wa madarasa, wanafunzi wengi kupita kiasi, ukosefu wa maji na umeme mabwenini, ukosefu wa vitabu vya kisasa na matatizo mengine. Aliniambia kuwa matatizo haya ni "self explanatory" na alikuwa anayategemea ingawa katika baadhi ya mabweni hali ilikuwa mbaya sana.
 • Aliendelea kudai kwamba safari yake hii ya Tanzania ilikuwa imebadili kabisa mtazamo wake kuhusu mkakati mzima wa  maendeleo ya Afrika. Alisema kwamba kutokana na aliyoyaona ikiwemo tabia ya kutojali, uvivu na kutorekebisha hata mambo madogo madogo tu, anafikiri kwamba kipingamizi kikubwa cha maendeleo ya Afrika ni Waafrika wenyewe. Alisema kwamba safari yake hii imembadili mawazo kiasi kwamba ameamua kuitelekeza mada yake ya mwanzo na ameamua kuandika tasnifu ya Uzamili na Uzamivu juu ya mikakati ya maendeleo katika bara la Afrika huku akitumia Tanzania kama eneo rejea. Na kuanzia sasa atapinga sana mawazo yaliyotawala ya kujaribu kuiendeleza Afrika kwa kuipa misaada na mikopo ya kifedha. Tumepanga kukutana tena na kuzungumza juu ya changamoto za Kisiasa na kijamii alizoziona.
Swali

 • Ati, kuna ukweli wo wote katika hoja za mwanafunzi huyu mpekuzi? Ni kweli Waafrika tu wavivu na tusiojali; au watu wa nje hawatuelewi sisi na mfumo wetu wa maisha? 

4 comments:

 1. Kuna ukweli kiasi kwamba chanzo cha umaskini wa waafrika ni waafrika wenyewe,maana kama ni kutawaliwa kwa nguvu ilikuwa ni zamani leo tunajipeleka wenyewe.Suala la kutojali,ufisadi na kujuana bado vimetawala sana maofisini,kaka Matondo kwa hapa Tanzania huwezi kupandishwa cheo bila kujuana,rushwa,ngono,pombe n.k

  ReplyDelete
 2. ni ukweli mtupu hatujali,rushwa,wizi,uonevu,ulevi,uzembe,ubinafsi yote aliyoyasema ni sawa kabisa labda kidogo rais kagame ndio anaanza kuichangamusha rwanda

  ReplyDelete
 3. Hakuna lililo jipya kwa Mmarekani huyu kuhusu alichokisema. Labda jipya ni kule kutoukubali ukweli pindi unapowekwa wazi kama hivi. Mambo ni hovyo hovyo hata hayaandikiki.Namsifu kwa kuweza kuyaweka katika ufupisho wake. Tanzania/Afrika ni ya Watanzania/Waafrika. Kama imebomoka ama kujengeka mhusika namba moja ni Mtanzania/Mwafrika mwenyewe na si vinginevyo.
  Aksante

  ReplyDelete
 4. mzungu amekuwa direct mno, kiasi kwamba anawakasirisha wana ccm, wakuu na viongozi wa chuo, familia na ndugu za hawa viongozi wa chuo, lakini anawafurahisha wapinzani wa ccm husussan chadema, na mungu aliye mbinguni. nasema mungu kwasababu kwa imani yangu mungu ni mkweli na msema kweli ni mpenzi wa mungu. nachompinga mzungu ni swala la misaada, kwani nahisi amekurupuka hapo bila kui-study tanzania vizuri, binafsi mimi sio mvivu(mtanzania) kama angejua misaada ndio kila kitu kwa mlalahoi kwani hata rasilimali tulizonazo zina wanufaisha wazungu waarabu na tabaka laviongozi wachache na familia zao, hii ni kujumuisha ardi, madini , wanyama, n.k sasa kama nchi ikakosa msaada kabisa si tutakufa kabisa.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU