NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, March 9, 2012

FIKRA YA IJUMAA: MADARAKA NA UWAJIBIKAJI - KWA NINI NI VIGUMU SANA KWA VIONGOZI WETU KUJIUZULU ???

Picha hii iko HAPA
  • Ulaya na Marekani uwajibikaji ni jambo la kawaida na linalotegemewa. Kosa au kashfa kidogo tu (hata kama inahusu mambo binafsi) inatosha kumfanya waziri, mbunge, mwakilishi au mshika madaraka ye yote kujiuzulu. Halafu kuna Afrika. Huku kwetu madaraka yanahodhiwa; na ukishayapata basi ni mali yako ya kudumu. Hata uboronge na kufanya madudu namna gani, umo tu. Hata watu walalamike namna gani, umo tu unadunda.
  • Kama dai mojawapo la wagomaji hawa ni kukutaka wewe ujiuzulu, na bila kujali kama una makosa ama la, huwezi kweli kuweka mbele maslahi na maisha ya wagonjwa masikini wasio na kitu na kuwajibika?  Ni nini kinachokufanya ufikiri kwamba wewe kubakia madarakani kama Waziri au Katibu Mkuu wa wizara ni muhimu kuliko maisha ya hawa wagonjwa masikini wasio na uwezo wa kwenda kwenye mahospitali ya binafsi au nchi za nje?
  • Na baada ya kasheshe yote hii, ni kweli bado utasimama mbele ya umma na kujipiga kifua kwamba ungali kiongozi halali na anayejali maisha ya watu unaowaongoza? Una sifa na maarifa gani ya kipekee kiasi kwamba serikali inasimama kidete na kukukingia kifua huku watu wako wakipoteza maisha?
  • Ni lini viongozi wa Afrika watajifunza kuwajibika na kuanza kuwajali watu wao hasa wale wa tabaka la chini ambao wanawaona kuwa ni wajinga tu na wasio na thamani?
  • Naamini kwamba siku moja masikini wa Afrika wataamka na kukataa kutendewa kama wanyama. Naamini pia kwamba siku moja Historia itawasamehe viongozi wetu waliowahi kuwajibika na kuachia madaraka kama akina Rostam Aziz, Edward Lowassa na wengineo.  Na hawa viongozi vichwamaji wasiowajali watu wao siku moja watajikuta katika shimo la takataka la Historia.
  • Kwa maoni mbalimbali ya wadau kuhusu mgogoro huu wa serikali na madaktari bofya HAPA. Taarifa ya habari kuhusu suala hili inapatikana hapa chini.

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU