NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Friday, April 6, 2012

MAKUNDI RUKSA CCM - MUKAMA

Wapo wanaoamini kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinapita katika dhoruba na misukosuko. Kwamba eti makundi  na magamba yanakiandama na kutishia uhai wake. Katibu wake mkuu hata hivyo amewahakikishia wakereketwa wa chama hicho kikongwe na chenye hadhi ya pekee hapa nchini kuwa makundi ni kitu chema na pengine cha lazima na kwamba afya ya chama hicho ni nzuri. Tathmini hii ni sahihi? Jibu sahihi tutalipata mwaka 2015.

************
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, amesema makundi katika chama ni jambo la kawaida na ni afya kwa chama na hayana uhusiano na kushindwa kwa mgombea wake katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki. 

Mukama aliyasema hayo jana wakati akitoa ufafanuzi wa kukanusha taarifa zilizochapishwa hivi karibuni na gazeti moja akihusishwa na ubadhirifu katika mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa Dar es Salaam. 

Miongoni mwa maswali kutoka kwa waandishi yalikuwa ni kutaka maoni yake juu ya kile kinachodaiwa kuwa miongoni mwa sababu za kushindwa kwa mgombea wa CCM, Sioi Sumari, ni makundi ndani ya chama hicho. 

“Msimamo wa chama ulishatolewa. Kauli ya Nape (Nnauye-Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itifaki na Uenezi) ndio msimamo rasmi. Ukiniuliza mimi binafsi kama Katibu Mkuu juu ya makundi, huu ni uelewa mdogo…makundi ni afya na ni kitu cha kawaida,” alisema Mukama. 

Alisema katika mfumo wa jumuiya yoyote kama kilivyo chama hicho kikubwa nchini chenye wanachama wapatao milioni 5.8, ni vigumu kukosa makundi. Alisema ni lazima iwepo misimamo ya makundi yasiyo rasmi ambayo ni afya kwa chama. 

Alitoa mfano kwamba kupitia makundi yasiyo rasmi, ndipo inajitokeza misimamo kama vile ya kutaka urais kwa kuzingatia kanda . 

"Kuna makundi yenye misingi ya kikanda. Watu wengine wanaweza kusema sasa hivi ni zamu ya Kanda ya Kusini, wengine wakasema Kanda ya Mashariki ilishatoa Rais, Nyerere alikuwa wa Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu nao wakadai Rais…hii ni afya kwa chama,” alisema. 

Hata hivyo, alisema CCM ni chama kikubwa kuliko hayo makundi ambayo alisema yanakuzwa na vyombo vya habari. 

Alisema hajaona vikundi vyenye malengo binafsi isipokuwa ni kwa ajili ya chama. Katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki, Nassari aliyekuwa mgombea wa Chadema, aliibuka mshindi kwa kura 32,972, na kumshinda Sioi aliyepata 26,757. 

Baada ya matokeo hayo, CCM kupitia kwa Nape ilitangaza kuyakubali na kusema inajipanga kufanya tathmini. 

Katika hatua nyingine, Mukama amezishutumu baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge kwa alichosema zimekuwa zikitoa taarifa kwenye vyombo vya habari juu ya mahojiano zinazofanya na watendaji na kutoa kauli za kuwahukumu, badala ya kusubiri kuwasilisha taarifa husika bungeni. 

Aliishutumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa, inayoongozwa na Augustino Mrema na ya Hesabu za Mashirika ya Umma inayoongozwa na Zitto Kabwe, akisema sababu ya wabunge hao kuendesha mahojiano hadharani kwa vyombo vya habari, ni kutafuta umaarufu. 

“Kamati inatakiwa iendeshe kazi zake kwa faragha, ikimaliza inawasilisha kwa Spika kabla ya kupelekwa bungeni…mnafikiri katika chama hiki kila mtu ni Richmond, mimi ni msafi,” alisema Mukama wakati akikanusha na kushutumu taarifa zilizoandikwa na gazeti moja akihusishwa na machinjio zilizoinukuu Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa .

Chanzo: Habari Leo
Katuni zote ni kutoka kwa Said Michael.

2 comments:

  1. Mkuu tumekupata...! TUPO PAMOJA

    ReplyDelete
  2. Siwapendi com.hawaleti.maendleo.vijijini.wsmekazana u.kujipendela.wao na familiar.zao.wananchi.hufa.njaa.ccm.sitaki.kuona.washamba.hawajali.wananchi.wao.kama.mataifa.yahoo nje

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU