NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, May 23, 2012

ATC NA UNUNUZI WA NDEGE "OBSOLETE" ILIYOANGUKA KULE KIGOMA: KAMA SIYO UUAJI NI NINI?

  • Picha hii inaonyesha ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) - shirika ambalo pengine ndilo linashikilia rekodi ya kufa na kufufuka mara kwa mara  duniani. Ndege hii aina ya  Dash 8-300  ilianguka kule Kigoma tarehe 8/4/2012 wakati ikijaribu kuruka kuelekea Dar-es-salaam. Kwa bahati nzuri, abiria wote 35 waliokuwemo katika ndege hii walisalimika. 
  • Sasa imethibitika kwamba ndege hii ilinunuliwa kimiujizaujiza kutoka kampuni moja ya China na kwamba ilikuwa ni "obsolete". Hata napata shida kidogo kupata neno sahihi kabisa la Kiswahili kueleza dhana hii ya kuwa obsolete. Kwa kifupi tu ni kwamba ndege hii ilikuwa ni mbovu na haikupaswa kuruka, achilia mbali kubeba abiria. Ni ndege iliyokuwa imepitwa na wakati wake. Ilipaswa kuwa "kaburini"
  • Lakini vigogo wetu wa ATC wakaenda huko Uchina, wakapewa kitu chao kidogo na kulibeba jeneza hili kulileta Tanzania huku wakijua kabisa kuwa Watanzania wenzao ambao ndiyo walipa kodi na hivyo wanunuzi wa ndege hii "obsolete" wangepanda ndege hii na kupoteza maisha. Ni miujiza tu ya Mungu ndiyo ilisaidia siku ile Watanzania wale 35 wasipoteze maisha kule Kigoma. 
  • Vigogo hawa wa ATC walionunua na kutuletea hili jeneza si wauaji hawa? Ni tamaa gani hii inayovuka ubinadamu wetu na kutufanya tuwe tayari kuhatarisha maisha ya Watanzania wenzetu ili mradi tu tupate mamilioni ya kujengea majumba ya kifahari na kujinunulia magari ya bei mbaya? Ubinadamu na undugu wetu kama Watanzania, undugu ambao Mwl. Nyerere aliupigania kwa nguvu zote uko wapi? 
  • Na cha kushangaza zaidi ni kwamba, vigogo hawa hawatafanywa cho chote. Na walipa kodi watatozwa tena mabilioni ya shilingi ili kulifufua shirika hili lililojaa mauzauza ya kufa na kufufuka. Na vigogo wale wale mafisadi watakwenda tena na kununua/kukodi ndege ambazo ni obsolete na kutuletea tena. Na mzunguko ule ule utaendelea tena na tena. Mpaka lini? Ni lini tutakuwa wakali na kuwaadhibu mafisadi na watu wanaofuja mali zetu kama hawa wauaji wa ATC? Sisi kwa sisi tukilana, safari ni lazima iendelee?
  • Kwa habari zaidi kuhusu sakata la unununi wa ndege hii kaburi soma HAPA

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU