NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, May 8, 2012

BADALA YA KUJIUZULU ETI WANAKIMBILIA KWA WAGANGA WA KIENYEJI !!!
Kule majuu kwa "watawala" wetu (Ulaya na Marekani)
  • Kakosa kadogo tu - hata tuhuma ambazo hazijathibitishwa zinatosha kumfanya mtu ajiuzulu ili kupisha uchunguzi. Ikibainika kuwa hana kosa jina lake linakuwa limesafishika na anakuwa amekwepa kuburuzwa katika shimo la takataka la Historia. Akibainika kuwa ana makosa, sheria inafuata mkondo wake. Wenzetu hawa huwa hawaangalii makunyanzi. Hata uwe rais au waziri mkuu, wembe ni ule ule. Kawaulize akina Ehud Olmert na Jacques Chirac  watakwambia. 
Huku kwetu
  • Imedhihirika wazi kuwa wewe ni fisadi, mzembe, mbadhirifu; na kwamba uzembe na ufisadi wako vimelisababishia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi. Badala ya kuwajibika na kujiuzuru ili kukwepa aibu eti unakimbilia kwa mganga wa kienyeji ili kusafisha nyota yako. Na unaamini kuwa nguvu za kishirikina zitamfanya bosi wako azisahau tuhuma zinazokuandama. Wakati huo huo wewe ni kiongozi wa serikali ambayo inaamini kuwa hakuna ushirikina !!! Kweli katika karne hii inayoshuhudia maendeleo makubwa ya kisayansi na kiteknolojia sisi bado ni jamii ambayo bado inategemea nguvu za kishirikina ili kutatua matatizo yake ! 
  • Mwanzoni nilifikiri kwamba, kwa vile viongozi wengi kule kwa "watawala" wetu ni matajiri tayari, kwao kujiuzulu siyo jambo gumu kwani hawategemei madaraka yao katika kuendesha maisha yao. Fikra hii siyo sahihi kwa sababu hata viongozi wetu wanaokumbwa na kashfa hizi za ufisadi na utendaji mbovu tayari ni mabilionea wenye uwezo wa kununua (tena kwa pesa taslimu) mahekalu yenye thamani ya dola za Kimarekani 700,000 (laki saba!). Ni wazi kuwa hata viongozi wetu hawa si masikini na wanaweza kujiuzulu na kuendelea kutanua bila wasiwasi wo wote hasa ukizingatia kwamba hawawezi kufikishwa katika vyombo vya kisheria. 
  • Swali ambalo napenda kuuliza hapa ni hili: Hivi ni kwa nini ni vigumu sana kwa viongozi wetu kuwajibika na kujiuzulu hata pale ambapo umma unalalamika na tuhuma zao ziko wazi? Ni dharau ya kujua kuwa hawatafanywa cho chote. Ni kuamini kuwa nguvu za kishirikina wanazoziamini zitawasaidia? Ni nini?

2 comments:

  1. Hulka haibanduki, hata usome vipi,...nafikiri wangelishukuru kuwa wameondolewa mzigo wasioweza kuubeba....

    ReplyDelete
  2. ya lazima wakadhibiti lakini ndohivyo wamechelewa

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU