NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Thursday, May 24, 2012

EZEKIEL MAIGE ALIONEWA? NI KWELI TUMEPOTEZA MPIGANAJI? SOMA UJUMBE WAKE WENYE KUGUSA MOYO KUTOKA FACEBOOK.

 • Ndiyo nimemaliza kuusoma ujumbe huu wa kihubiri wa ndugu yangu Ezekiel Maige. Katika ujumbe huu anajitetea sana huku akipamba utetezi wake na neno la Mungu. Ni utetezi mzuri unaogusa moyo.
 • Katika utetezi huu hata hivyo hakuna mahali popote ambapo Ndg. Maige anajivisha jukumu lolote kuhusiana na yaliyotokea. Yeye ameonewa tu na wabaya wake wa kisiasa na yote yaliyosemwa juu yake ikiwemo ile nyumba yake mashuhuri ni uzushi mtupu. Kwa vile hakuna aliye malaika miongoni mwetu, binafsi huwa nina wasiwasi na watu ambao huwa hawapendi kujitwisha lawama japo kidogo na kukiri makosa waliyofanya. Na hili ndilo jambo kubwa linalokosekana katika utetezi huu mzuri.
 • Ati, tunajifunza nini kutokana na mkasa huu? Siasa ni mchezo mchafu tena wa hatari na uzushi usipozimwa mapema basi huweza kuenea kwa kasi mithili ya moto wa nyika na kugeuka kuwa ukweli mara moja. Kama tuhuma zote alizokuwa akirundikiwa ni uzushi, alikuwa wapi kuzikana mara moja kabla hazijageuka na kuwa ukweli? 
 • Inabidi pia tujenge tabia ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi tuhuma kama hizi zinapozuka. Kujiuzulu ni jambo jema na historia ina upendeleo sana kwa watu waliokubali kujiuzulu bila kujali kama walikuwa na makosa ama la. Rais Mwinyi ni mfano mzuri. Naamini pia kuwa pengine ndiyo sababu inayowafanya watu wamwangalie Lowassa kwa jicho jingine na hata kuendelea kumtajataja katika kinyang'anyiro cha urais mwaka 2015. Ndiyo maana nilisitikitika iliporipotiwa kuwa badala ya kujiuzulu, Maige alikuwa ameonekana kwa mganga wa kienyeji wakati sakata hili likiendelea. 
 • Haya yameshapita bila shaka na historia ipo na imeona. Kama kweli Ndg. Maige ameonewa historia itathibitisha huko mbele ya safari lakini sote tuna jambo la kujifunza kutokana na kisa hiki. 
 • Bwana Maige, kama ulivyomwita Mungu wako katika ujumbe wako huu chini, bila shaka Mungu Hatakuacha. Hata kama Akikuacha, si umetajirika bwana? Maisha ni lazima yaendelee ati !!!
*Ujumbe wa Maige Kutoka Facebook *


Ndugu zangu na rafiki zangu. Kwanza niwape pole kwa mshituko mlioupata kwa haya yaliyojitokeza. Naomba msisikitike sana. Kila jambo alilopanga Mola hutokea kadiri ya mapenzi yake. Route ya maisha ya mwanadamu hupangwa na Mola mara tu anapompulizia pumzi ya uhai. Hili lilipangwa hata kabla sijatokea duniani miaka 42 iliyopita! 


Mungu hakushindwa kumwokoa mwanawe Yesu asisulubiwe, tena kwa kuonewa! Hasha, tungeupataje ukombozi bila hilo kutokea? Wakati mwingine Mungu hutoa nafasi kwa mambomagumu kuwafika waja wake, si kwamba hawapendi,bali ili unabii utimie. Ilifika wakati hata Yesu akaona kama Mungu kamuacha! Hasa sisi kwa hili tunaweza kudhani Mungu katuacha! Hasha, ni njia ya kuufikia ukombozi wa kweli. 


Pili, kwa kifupi sana, niwafahamishe kuwa, yaliyotokea ni ushahidi kwamba maliasili ni ngumu. Kukabiliala na wabaya ni kazi ngumu. Wapo waliojipanga ukiwavamia ovyoovyo unaondoka wewe. Ndivyo ilivyotokea. Niwahakikishie, wazalendo wamepoteza mpambanaji. Nimepambana na wahalifu angani, majini, porini, mijini na vijijini ndani na nje ya nchi. Nilitumia kila aina ya uwezo wangu kulizawadia taifa langu utumishi uliotukuka. Sikubakisha chembe ya energy. 


Waziri gani aliyesimamia sheria na kuwapa vitalu watanzania maskini wenye sifa na kuwaacha wazungu kama sheria ilivyoelekeza? Waziri gani aliyewafikisha mahakamni watorosha twiga akina Kamrani na wenzake? Watu wametumia records za matukio ya 2009/10 kuficha matendo na maamuzi ya kishujaa ya Maige ya 2011. Yawezekana hawakutaka nipate sifa, lakini ipo siku nitaipata. Tena si siku nyingi. Niliwaomba wenzangu wamwogope Mungu. Bado nasisisitza hivyo, si Mungu wangu kama ilivyodhaniwa, bali Mungu wetu wa haki. Waziri gani aliyefunga biashara ya wanyamahai? Waziri gani aliyeonyesha mfano wa kuchukua hatua kwa watumishi pale alipoona hawatendi sawa? Maige hakusita kuchukua hatua. 


Maamuzi haya ni magumu na yamegusa watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa. Nilitegemea vita hii, na ninaamini tutashinda. Nilisema Bungeni, watanzania wapenda haki wanisikilize kwa makini. Muda haukuruhusu, ila nitarudi Bungeni na nitasema. 


Imesemwa issue ya nyumba. Nimefafanua na kutoa vielelezo. Kila mbunge aliyetaka amekopeshwa shs 290m, wengine wameanzisha biashara na wengine wamenununua magari na wengine majumba. Wapo walioficha, na tupo tuliojiweka wazi! Mkopo wangu huo umekuwa my contribution na balance kulipwa na benki na nyumba kuimortgage. Nimetoa nyaraka zote kwa wanahabari na vyombo vyote husika. Nimesema mwenye mashaka aende kwa Msajili wa hati wizara ya ardhi, au kwa kamishna wa maadili, au CRDB Azikiwe na Dodoma nilikokopa au amtafute muuzaji. Kote huko utapata rekodi ya bei na mode of payment. Wapo wahuni, kwa maslahi ya kisiasa na chuki binafsi wametangaza bei tofauti na niliyonunulia. Mwanasheria wangu anashughulikia hilo. 


Niwahakikishie, vita nimepigana, imani na dhamana nimeilinda, muda wa kutuzwa na mwenye kumbukumbu sahihi, Mungu utafika. Naamini nimejiwekea akiba isyooza Mbiguni. 


Yapo mengi yasiyo sahihi yaliyosemwa. Nitakuwa nafafanua kila nipatapo fursa na muda utazidi kutufunua. Kwa kifupi, kwa suala la vitalu, hakuna kampuni hata moja iliyopewa kitalu cha uwindaji bila kuomba, kukaguliwa na kamati ya ushauri na hatimaye kupewa alama. Kampuni zisizokuwa na sifa ni zile zilizopata chini ya alama 50. Na kwa kampuni zilizokuwa kwenye biashara, passmark ni alama 40 kwa mujibu wa kanuni ya 16(5) ya kanuni za uwindaji wa kitalii za mwaka 2010. Hakuna kampuni iliyopata chini ya alama 50 iliyopata kitalu. Hakuna kampuni ya kizalendo iliyopendekezwa na kamati ya ushauri ambayo haikupewa kitalu. 


Kwa upande wa report ya CAG, haikunigusa binafsi kwani ilikuwa inaishia juni 2010 wakati mimi ilishika dhamana Novemba 2010. 


Kwa upande wa biashara ya wanyama hai, hakuna wanyama waliosafirishwa kinyume cha sheria wakati wangu (2011), na matukio ya utoroshaji tulipoyabaini, tulifungua mashitaka kwa watuhumiwa nakufnug biashara hiyo. 


Naanza kazi ya kuwawakilisha wananchi wa Msalala. Nitawawakilisha kwa mujibu wa katiba na ahadi zangu kwao hadi 2015 watakapopata fursa ya kuamua vinginevyo. 
Mara nyingi watenda mema hufanyiwa hiyana. Kwa wakristo, naomba msome Mwanzo 4:1-15. 


Wasalaam.

2 comments:

 1. Ndugu yangu Matondo, kwanza nakushukuru kwa kunikaribisha tena kwenye janvi lako hili Lililojaa mambo mazuri yenye hekima na weledi pamoja na kwamba huwa ni kawaida yangu kuchungulia mara kwa mara, vile vile  nawe ninakuasa usiwe kama 'kaka kuona' ambaye unatokea tu hapa janvini kama kuna jambo au mambo makuu ya kusema au kuihabarisha Jamii, si hata yale  madogo madogo pia ni muhimu kuyaleta janvini!.

  Kwanza sina budi kutoa masikitiko yangu kidogo kwa ndugu yangu Ezekiel Maige  kwa tafrani ilitompata kisiasa kama binadamu lakini masikitiko yangu makubwa nayaelekeza kwa jamii yangu ya ukanda ninaotoka(Wasukuma) hasa sisi vijana. Kwa majumuisho yangu, Ezekiel Maige ametuangusha na kwa kufanya hivyo amezidi kushindilia zaidi ile imani na tetesi (myth) zilizojengeka kuwa Wasukuma tuna tatizo la 'kimaadili' hasa pale linapokuja swala la uongozi.

  Nisingependa kumuhukumu ndugu yangu Ezekiel Maige  lakini dalili zinaonyesha  kuwa wizara aliyokuwa amekabidhiwa kuiongoza ilikuwa na matatizo makubwa ambayo kwa binadamu mwenye hekima na busara angejiuzuru badala ya kusubili kusukumwa pembeni.

  Matondo nakumbuka Sunday, April 3, 2011 ulileta hapa janvini mada isemayo
  SI WOTE WANAOKWENDA LOLIONDO NI WAGONJWA. WENGINE WANAKWENDA HUKO "OUT OF CURIOSITY" NA KUONA JINSI HIYO DAWA INAVYO"TASTE" ikiwa na video ya mheshimiwa aliposhitukizwa swali na waandishi wa habari lakini katika majibu yake ukimwangalia ilionyesha kama anaudanganya umma, baada ya kueleza wasiwasi wangu, ulionekana kumtetea na kusema tumpatie muda lakini nilisema 'siku njema huonekana asubuhi'

  Hakuna ubishi na hii inaeleweka kuwa wanasiasa wengi ni waongo kisiasa lakini vilevile mwanasiasa makini na mweledi kisiasa ni yule anajua ni namna gani na mahali papi pa kutembeza uongo. Ndugu yangu Ezekiel Maige kuanza kulalamika na kutumia vifungu kwenye biblia hakutaondoa wingu baya la kisiasa alilogubikwa  kwa sasa.

  Maelezo haya alipaswa kuyatoa mapema na kwa kutokufanya hivi, inaonyesha ni jinsi gani yeye na timu yake ya kisiasa hawakuwa  mweledi kisiasa, na hapa ndipo tatizo linajitokeza la Wasukuma wengi kuonekana  kama hatuna 'maadili' ya uongozi.

  Nafikili tatizo letu Wasukuma ni wepesi mno wa kuwaamini watu na hii ni kutokana na mila na desturi zetu ambazo mgeni, jirani na ndugu wote ni sawa na siyo jambo la ajabu kwa Msukuma kumpa jirani masikini sehemu ya mifugo yake bila maandishi kisheria ili imsaidie  bila hata ya kufikili, je, itakuwaje kama akiiuza?.  Na ndivyo hivyo kazini, kwa lugha ya mbali tunakuwa viongozi (leissez faire or rein style) na matokeo yake ni msururu wa viongozi Wasukuma ambao wamebolonga majukumu waliyopewa  wakati huo huo jamii yao inawalaumu kama hawakuisaidia (favouritism) , na hii yote ni kwa sababu ya  desturi zetu za usawa kwa kila mtu(jirani, mgeni na ndugu).

  Mpaka hapo tutakapoweza kuachana na mila na desturi hizi ambazo zinapingana na mazingira ya sasa ambayo yamejaa jamii isiyo adilifu, tutaendelea kuanguka katika majukumu ya kijamii huku tukichochea 'myth' ya kuwa Uadilifu unatushinda.......

  Haya ni mawazo yangu na mchango wa mawazo yako yenye hekima ndiyo nguvu ya kukutana janvini 'gashikome'

  ReplyDelete
 2. Ng'wanaMwamapalala - Nitarudi baadaye kutoa maoni yangu. Nikiandika kwa kuparaza saa hizi pengine sitayatendea haki maoni yako haya mazuri...

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU