NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, May 22, 2012

KWA HILI WAZUNGU NAWAFAGILIA

 • Kutokana na tofauti za kitamaduni, kuna mambo mengi ya kizungu ambayo sikubaliani nayo. Kwa upande mwingine, kuna mambo mengi mema ya kizungu ambayo huwa yananivutia na hata kunifurahisha. Mojawapo ni hili la kutojivuna, kutojiona na kujigamba. Nitafafanua kidogo.
 • Si jambo la ajabu kumwona mzungu tajiri akienda kazini kwa baisikeli au gari lake kuukuu. Yeye hahitaji gari la bei mbaya ili kujionyesha; na si ajabu siku moja ukisikia kuwa jirani yako uliyemfahamu vizuri sana kama mtu wa kawaida tu, kumbe ni milionea. Hili ni jambo la kawaida kwao.
 • Kwetu sisi mara nyingi sivyo mambo yalivyo. Ukiwa na pesa inabidi ujionyeshe. Inabidi ununue shangingi la kutambia mitaani. Inabidi ujenge hekalu la kutisha. Inabidi ujionyeshe katika jamii ili ikutambue. Na ukiwa na madaraka, jamii inakutegemea uendeshe gari la aina fulani, uishi katika nyumba ya kiwango fulani na uendeshe maisha ya kiwango cha juu. 
 • Mimi naamini kuwa mtazamo huu ndiyo unachochea ufisadi. Mtu ukibahatika kuukwaa uwaziri au cheo kingine kikubwa - hata kama ni kwa muda mfupi tu - jamii inakutegemea utajirike. Ukizubaa na ukaja kutoswa ukiwa huna kitu jamii inakucheka. Matokeo yake, watu wanashindana kuiba ili wasije wakachekwa huko mbele ya safari. Ati, mambo yangekuwaje kama jamii ingekuwa kali na wababe hawa wanaoingia madarakani wakiwa hawana kitu na baada ya miaka michache tu wanakuwa wameshajitajirisha kiasi cha kununua mahekalu kwa pesa taslimu dola 700,000? 
 • Nimelikumbuka hili baada ya harusi ya Mark Zuckerberg - yule kijana mdogo aliyeanzisha Facebook. Japo ni mmojawapo wa watu matajiri kabisa duniani, harusi yake juzi ilikuwa ni ya kushtukiza na ilifanyika nyuma ya nyumba yake. Wageni walioalikwa walifikiri kwamba wameenda kusherehekea kumaliza shule kwa mchumba wake. Kumbe ilikuwa ni sherehe ya arusi. Kwa wenzetu hawa, kufanya sherehe kubwa na kuumiza watu vichwa kwa michango si jambo la muhimu sana. Si lazima kujionyesha na kutamba.
 • Na kwetu je? Hata ambao hawana uwezo eti nao wanashindana kufanya harusi za kifahari zenye kugharimu mamilioni ya shilingi. Imefikia hatua sasa michango ya harusi ni mojawapo ya sehemu ya bajeti kwa watu wengi na ni jambo la kuumiza kichwa kweli kweli. Mtu anakuomba mchango wa milioni moja kwa ajili ya harusi yake ya kifahari; na usipoutoa basi urafiki unavurugika nawe unaonekana kuwa mchoyo. Kweli? Mimi nahusikaje na harusi yako ya kifahari? 
 • Sina ugomvi na watu wenye pesa zao kufanya haya maharusi ya kifahari. Lakini kama wewe huna uwezo, ni haki kweli uwabane watu wakuchangie mamilioni ili tu nawe uweze kufanyia harusi yako katika ukumbi wenye hadhi ya kimataifa huku ukiwa na msururu wa magari ya kifahari na zawadi za bei mbaya? Ukifanyia harusi yako katika ukumbi wa kawaida au katika ua wa nyumba yako kama Mark Zuckeberg alivyofanya kuna ubaya gani? 
 • Siipendi kabisa tabia hii na KAMWE usije kuniomba milioni moja ili kuchangia harusi yako ya kifahari. Sihusiki na SI LAZIMA. Halafu tukisema tuchangishane hayo mamilioni ili tukanunue madawati au kuchimba visima vya maji huko vijijini tunakotoka, hakuna mtu wa kujitolea. Kwa nini harusi ni muhimu zaidi kuliko madawati au visima vya maji?

9 comments:

 1. Matondo umenikumbusha harusi yangu. Pamoja na kuwa mfanyabiashara mwenye nazo wakati ule, wakwe zangu walinishangaa nilipowaambia kuwa sina pesa ya kutumia kwenye sherehe. Ilikuwaje? Niliwaambia wakwe zangu wafanye sherehe zao ima kwa kunikaribisha au watakavyo na wakimaliza wanipe mali zangu. Mwanzoni walidhani nilikuwa natania. Kwa ufupi tulikubaliana na mke wangu kufanya sherehe ndogo. Ilipoisha hatukuwa na hata msindikizaji. Tulichukua zawadi zetu na kuweka kwenye gari na kwenda kuzipakuwa wenyewe nyumbani na ukawa mwisho wa sherehe. Kimsingi waswahili ni watu wa ajabu wanaotengeneza umaskini kutokana na kutojiamini. Utawaona kwa mfano mtu akiwa anasomea PhD atatangaza utadhani anafanya kitu cha ajabu wakati ni kitu cha kawaida. Waone wanavyoshindana kuitana madaktari na maprofesa hata kwa shahada za kughushi. Ni aibu. Imefikia mahali hata rais anaonea ujiko kutumia shahada za heshima bila kujua kuwa watu kama Mwl Nyerere walikuwa nazo kwa makumi na hawakuwahi kuruhusu waramba viatu wawaite daktari.

  ReplyDelete
 2. Matondo umenigusa! Uliyosema ni sahihi kabisa na mdau hapo juu yupo sahihi kabisa. Imefikia wakati tuachane na mambo yasiyo na tija katika maendeleo yetu1

  ReplyDelete
 3. Ni ngumu sana kuwabadilisha watu kwani imani waliyonayo kufanya harusi bila kuchangishana ni jambo lisilowezekana, hasa kwa upande wetu sisi wanawake, hatupendi kuolewa kimyakimya labda kama ni nyumba ndogo inafunga ndoa tena kwa area commissioner vinginevyo shamra shamra ndo order of the day.
  Baada ya fungate walio wengi ni kuexperience kipindi cha ukata mkali kwani resources zote zilitumika kwenye harusi.
  Lakini tunaweza kubadilika ikiwa tunataka, badala ya kukaa mavikao ya harusi/send off/kitchen part mavikao hayo yangegeuzwa kama ma-fund raising kwa issues mbalimbali za shule ama hata mambo ya afya ni aibu. Na jamaa wakikuchangia wanategemea kuja kula na kunywa basi.
  Mengine ni reception umefanyia wapi hayo ndo mashindano ya mjini.
  Tena ni lazima kila mwezi uwe na budget ya kuchangia harusi/send off au kitchen part sijui kama tutafika.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Hujambo ndugu. Mimi naitwa Gikuri niko Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. Nafanya utafiti juu ya uendeshaji wa sherehe za harusi kutumia mfumo wa uchangishaji. Ningependa kutumia haya maneno yako katika utafiti wangu. Unaniruhusu? Ningejua jina ningefurahi pia. Asante na samahani kama nitakuwa nimekuwa nimekwaza.

   Delete
  2. Mimi ninaitwa Anthony Gikuri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. Ninafanya utafiti juu ya MTAZAMO WA WATU JUU YA ATHARI ZA KIJAMII NA KIUCHUMI ZINAZOTOKANA NA UENDESHAJI WA SHEREHE ZA HARUSI KWA KUTEGEMEA MFUMO WA UCHANGISHAJI. TAKWIMU HIZI ZITATUMIKA KWA MINAJIRI YA KITAALUMA TU. NATANGULIZA SHUKRANI
   I've invited you to fill out the form FINANCING WEDDING CEREMONIES IN TANZANIA. To fill it out, visit:
   https://docs.google.com/forms/d/11OygsXrLv7Vf17KLFjv4luXQzzfadh13pI6MH1fnUos/viewform?c=0&w=1&usp=mail_form_link

   Delete
 4. Pamoja na kwamba ninapita tu, siyo vibaya na mimi angalau nikaacha neno kwa vile mada inachombeza.

  Matondo, hapo umenena, Kwanza kabisa, U-maana wa harusi haupo tena, unakuta watu wamejuana kwa muda mrefu na wanagawiana ''tunda la mti wa katikati'' kila wanapohitaji lakini eti wanapoamua kujiharalisha kwenye jamii(harusi),wanaanza kupatwa na kiwewe cha kuwa na harusi itakayoacha gumzo katika jamii wakati ndoa yao waliifanya muda mrefu na wanaendelea kuifanya kila wanapojisikia kufanya hivyo. Kwangu nafikili huu ni ulimbukeni wa hali ya juu na ulimbukeni huu ndiyo unaotutafuna kimaisha.

  Kwa sasa hata kwenye misiba napo kumeanzishwa michango si kwa ajiri ya huduma ya marehemu(usafiri, sanda, jeneza) bali kwa vile watu inabidi wale na kunywa sana, hata bendi zinakodiswa kenda kutumbuiza ili mazishi yaache gumzo kwenye jamii.

  Sherehe tu kwa kila jambo wakati hata uwezo hatuna. na kama ulivyodokeza, tukiangalia picha kwa ukubwa, hiki ni chanzo cha wizi, rushwa na ufisadi.

  Hata hivyo, pamoja na kwamba jamii yetu ingali bado kama 'dodoki' ninatumaini tutafika...

  ReplyDelete
 5. Mwalimu Mhango - hata mimi harusi yangu ilikuwa kama yako. Ilikuwa ni mimi na binti wa watu na mashahidi kwisha. Halafu jioni chakula cha kawaida tu na marafiki wa karibu basi. Hata ukifanya harusi ya kusimuliwa mpaka vizazi vijavyo - then what? Kama una uwezo fanya lakini usisumbue watu wakuchangie mamilioni kama huna uwezo...

  Anony. wa tatu - niliona mdau mmoja akilalamika kule kwa Michuzi kwamba maisha yamekuwa magumu sana. Na katika bajeti aliyoiweka ili kuunga mkono hoja yake, michango ya harusi na kitchen party ilikuwa juu kabisa kuliko hata mambo mengine ya msingi. Hili lilinishangaza sana.

  Hata wanawake wanaweza kufanya harusi ndogo na yenye kushirikisha marafiki zetu wa karibu tu na familia. Mbona mke wangu aliweza, tena ni yeye aliyetaka sana tufanye hivyo?

  Kama nilivyosema hapo juu, ukiwa na uwezo fanya harusi kuubwa kama za mafarao wa Misri lakini siyo vizuri kufikia hatua ya kukosana na watu eti kwa vile hawajachangia harusi yako. Siyo lazima; na ni fikra hizi hizi zinazochochea ufisadi.

  Ng'wanaMwamapalala - Karibu tena kwani ulikuwa umepotea sana. Asante kwa maoni yako ya kina. Pengine tafsiri ya ndoa imeshabadilika ili kuendana na usasa na utandawazi; na yale mambo ya zamani eti mpaka siku ya harusi ndiyo mnaonjana yameshakuwa nadra. Ni vurugu tupu !!!

  Fikra hii ya kushindana katika kila kitu hata katika mambo yasiyo na umuhimu sana ndiyo mojawapo ya nguzo za ufisadi. Ndiyo maana mimi naamini kwamba ufisadi hautakaa uishe bila jamii kwanza kubadilisha fikra zake na kuelekeza nguvu na juhudi zake katika mambo ya msingi. Safari bado ni ndefu !!!

  ReplyDelete
 6. Nini tofauti ya tajiri na maskini?Tofauti ya msomi na mwenye elimu ndogo?duniani kuna tofauti nyingi sana Makabila,Elimu,Mali,Tabia. Nahii ndiyo utamu wa maisha.Katika kamusi utaona yupo Bahili au Karimu. Swali langu ni kwa nini hamuipi haki majina kama cheo cha elimu au akiwa bahili,wewe unamuona ni mtunzaji wa mali,na elimu kama hajaitangaza inafaida gani kusoma?

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ni kweli kabisa msemayo sote twaweza kubadilika wanawake kwa wanaume. Je kaka Matondo kama harusi yako ungalifanyia Tanzania ambako wanakufahamu watu wengi usukumani na mkeo uchagani mngefunga ndoa ya kimyakimya au mazingira yaliwabana? Najakuliona hili kwa jicho la tatu.

   Japokuwa hata na mimi maharusi ya kifahari sifagilii, yangu ilikuwa ya kawaida tu, ila pia baada ya harusi niliona maisha magumu kwani resources zote zilitumika huko.

   Michango ni mingi mno na ipo katika budgets zetu. TWAWEZA TUBADILIKE

   Delete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU