NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, June 12, 2012

HONGERA BIA YA SERENGETI KUFADHILI MASHINDANO YA NGOMA ZA KISUKUMA

Kundi la ngoma la Makilikili kutoka Shinyanga.
  • Kwa muda sasa nimekuwa nikiyashutumu makampuni mbalimbali hapa nchini kwa kuwa maajenti wa utandawazi. Kwa mfano nimekuwa nikijiuliza: ni kwa nini makampuni haya yamejikita zaidi katika kudhamini mashindano ya urembo ambayo yamezagaa kila kona ya nchi badala ya kujikita katika mambo yenye tija zaidi kwa jamii kama ujenzi wa madarasa, ununuzi wa madawati, uchimbaji wa visima vya maji huko vijijini na miradi mingine ya kimaendeleo?
  • Inabidi niseme hapa kwamba sasa hali imebadilika na makampuni mengi, japo bado yamemakinikia shughuli za burudani ili kujitangaza zaidi, yamejibidisha sana kudhamini shughuli za kimaendeleo pia. 
  • Makampuni kama Vodacom na mengineyo yamekuwa yakijenga madarasa na ofisi za walimu, kununua madawati, kuchimba visima, kusaidia vituo vya kulelea watoto yatima na miradi mingineyo. Hili ni jambo jema kwani kama tukishupalia tu mashindano ya urembo na burudani basi ni wazi kuwa hatutafika popote. 
  • Ni katika mtazamo huu, nimefurahishwa sana na taarifa kuwa kampuni ya Bia ya Serengeti  imetoa milioni 12 ili kudhamini mashindano ya ngoma za Kisukuma kule Mwanza. Hili ni jambo la muhimu, si kwa sababu mimi ni Msukuma, bali kutokana na ukweli kwamba wengi wetu sasa tumefunikwa na kunguku la utandawazi na usasa kiasi kwamba hatujali tenda utamaduni na lugha zetu za mama zilizotulea na kutukuza. Hali ni mbaya zaidi kwa vijana wetu ambao hawajui wala kujali kuhusu tamaduni zao na lugha zao za kikabila. Tumekuwa watu tusiojifahamu, watu tusio na utamaduni wetu wenyewe. 
  • Shughuli hizi za kitamaduni zikiendelea kuimarishwa na kudhaminiwa na makampuni binafsi kama tunavyoshuhudia katika mashindano ya urembo, zitasaidia japo kutukumbusha kuwa sisi ni watu wenye utamaduni wetu wenyewe na kwamba kabla ya ujio wa watawala wetu kutoka huko walikotoka tulikuwa watu huru kifikra, kisaikolojia na kitamaduni. Hongereni Serengeti Brewerlies na Mkurugenzi wenu wa Masoko Bwn. Balozi Mafuru kwa hatua yenu hii ya kimapinduzi kufadhili shughuli hizi za kitamaduni. Bila shaka makampuni mengine yataiga mfano wenu. 
Hata Mh. Dr. J.K. Alishaonja utamu wa ngoma zetu !

No comments:

Post a Comment

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU