NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Monday, July 16, 2012

BLOGU ZIMETUFANYA TUWE KAMA NDUGU: ASANTE DADA SUBI KWA WEMA WAKO !!!

 • Kwa wanablog ambao tulianza kublog tu "kikomandoo" bila kujua cho chote kuhusu mambo ya kompyuta na mitandao, Dada Subi wa wavuti.com ni mkombozi na mlezi wetu. Kila mara tunapokwama au tunapokuwa na swali kuhusu blogu zetu hizi zisizo na wafadhili basi tunakimbilia kwake. Naye bila choyo amekuwa akitusaidia bure na bila kusita. Hata swali liwe gumu namna gani; au linalohitaji jibu la kitaalamu zaidi, yeye yuko tayari kuacha kazi zake na kusaka jibu rahisi na linaloeleweka kwa kila mtu. Na mara nyingi hubandika misaada hii kwa wanablogu katika tovuti yake pendwa ya wavuti. Ni wazi kuwa siku historia ya tovuti na blogu nchini Tanzania itakapokuja kuandikwa, jina la Dada Subi litatajwa kama mmojawapo wa watu waliosaidia sana katika kuimarisha, kutoa mwongozo na kuwasaidia wanablogu wachanga. Dada Subi, usikate tamaa wala kuchoka. Historia inakuona na siku moja itakuzawadia !!!
 • Wema wa Da Subi hata hivyo hauishii katika maswala ya mitandaoni tu. Juzi juzi hapa nilipata kifurushi katika sanduku langu la posta. Nilipokifungua nilikutana na viboksi vya dawa ya Hedex - dawa pekee ambayo huninyamazishia maumivu ya kichwa kwa kasi. Kulikuwa pia na kipande cha karatasi kilichokuwa na maneno mawili tu - Dada Subi. Ndipo nikakumbuka: Akiwa kama mtaalamu wa mambo ya tiba, niliwahi kumtajia kuhusu udhaifu wa dawa nyingi za Kimarekani katika kupunguza maumivu na hasa maumivu ya kichwa. Ndipo nilimtajia kuwa dawa kiboko ya kichwa ni Hedex pekee. Kumbe angali anakumbuka. 
 • Japo viboksi hivi vya tembe za Hedex vyaweza kuonekana kuwa si lolote si cho chote lakini kwa hapa Marekani si jambo la kawaida mtu kukukumbuka, kuacha shughuli zake, kwenda posta na kupiga foleni ndefu na ya pole pole na kutoa pesa zake kulipia gharama za kukutumia kifurushi. Na huyu ni mtu ambaye wala hamjaonana na kufahamiana isipokuwa tu katika blogu. 
 • Nimeguswa sana na wema huu wa Dada Subi na kama nilivyowahi kusema HAPA, matendo ya wema kama haya, hata yakiwa ni madogo namna gani ndiyo hasa yanaonyesha ubinadamu  na uhalisi wetu. Asante sana Dada Subi !!!
 • Na hapa napenda kurudia tena maneno ya Mwanablogu mashuhuri Yasinta (aka Kapulya) kuwa wanablogu sisi ni ndugu. Hebu na tuendelee kusaidiana, kuelimishana, kupendana; na kuitetea, kuielimisha na kuionyesha njia jamii yetu. Tuko pamoja na Mungu Aendelee kutubariki!!!

10 comments:

 1. Kaka yangu, Prof. Matondo, mimi nimefurahi kwa wewe umepata ulichokihitaji na umefurahi.

  Nimefanya lile linalowezekana. Namshukuru Maggie niliyemwomba azinunue na akafanya hivyo na kuwezesha hizi kukufikia.

  Pole sana kwa masumbufu ya kichwa, naijua adha yake, si kwa kuugua bali kwa uzoefu wa kazi yangu kila leo. Pole sana. Tuendelee kuwasiliana kwa lolote. Linalowezekana tutasaidiana tu, ndiyo thawabu ya ubinadamu, kinyume cha hapo, haina maana.

  Asante kwa kushukuru.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Amani iwe nanyi..mimi pia ni mwana-blogu na ningependa tushirikiane..

   Lakini nashawishika kujua baadhi ya mambo tunayoweza kusaidiana kama wana blogu.

   Asante(ni);
   Abdallah Toyo
   www.toyojr.blogspot.com

   Delete
 2. Hata mimi niliwahi kumuuliza swali la blog nikitumia jina jingine. Nilishangaa sana kwani alinijibu hapo hapo mara moja na jibu lake lilikuwa correct 100%.

  Even though she is a famous blogger, yeye hana nyodo kama hao mablogger wanaojifanya kuwa wamefika na hawana msaada wo wote kwa young bloggers. In my opinion, Subi katoa contribution ya maana in blogging than Issa Michuzi na wenzake.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Asante dada Nancy kwa ku-share nasi msaada ulioupata kutoka kwa Dada Subi.

   Naamini hii ndiyo mara yako ya kwanza kupita hapa kibarazani kwangu. Profile yako iko private lakini haina neno. Tuko pamoja !!!

   Delete
 3. Kuna tofauti kubwa sana ya bloggers wa zama zile na hawa wa zama hizi. Wengi wa walioanza enzi zile, walikuwa na malengo ambayo yalikuwa ni pamoja na kuwa karibu na wengine wenye kupendelea mambo ya kimtandao, kuelimisha nk. Hawa wa sasa wengi wamekaa kibiashara zaidi. Enzi zile kulikuwa na watu wanafanya maboresho ya blogs za wengine bure kabisa, siku hizi matangazo ya unataka kuboreshewa blog yako piga simu namba..... kwa gharama ya tzs kadhaa hivi. Lakini hatuwezi kumlaumu yeyote yule. Kizazi cha zamani kilikuwa cha kiujamaa zaidi, hiki cha sasa ni cha kibepari zaidi.

  Prof & Dada Subi, mie siku zote huwa nawaambia watu kuwa fedha si lolote> Huwa natolea mfano wa tajiri mwenye fedha zake magunia kadhaa lakini akaishiwa maji jangwani. Endapo akitokea mtu akakubali kushare naye glasi ya maji alonayo, je, anaweza kupima value ya hayo maji in terms oc cash?

  Msisimko wa zawadi huwa hautokani na aina ya zawadi, aloituma au thamani yake, bali ule ukweli kuwainarepresent upendo alio nao huyo aliyeitoa kwako wewe.

  Niliwahi kupokea zawadi ya kadi ya mwaka mpya toka kwa dada yetu mtaalamu wa mapishi, Miriam. Aisee, siku ile ilikuwa kama nimepokea kipande cha dhahabu kwakweli. Nilikuwa na furaha ambayo siwezi ielezea. Na leo hii ninaposoma kuhusu Subi, hakina nasisimka kuwa kumbe bado watu wa kizazi cha ujamaa bado tupo.

  Nancy, uko ok ndugu yangu?

  ReplyDelete
  Replies
  1. Rama;

   Umesema kweli. Siku hizi kila kitu ni biashara. Hata mamanju wa Kisukuma kule nyumbani siku hizi bila laki tano hawaimbi. Mambo yamebadilika sana.

   Kuhusu hili suala la zawadi pia nakubaliana nawe. Kama wanavyosema wenyewe "what matters is the idea" na wala siyo thamani ya zawadi.

   Watu wenye mioyo kama akina Subi wapo ili kutukumbusha kuwa Ubinadamu ungalipo !!!

   Delete
 4. Mimi nimefurahi kwa jinsi ulivyotoa shukrani zako na nimependa mno. Kwasababu nawe umekuwa si mchoyo umetushirikisha na ndivyo inavyotakiwa kama ndugu na pale inapowezekana basi tushirikishana.
  Subi kwa kweli anastahili hizo shukrani zote ni mdada ambaye si mchoyo kwa kweli. Pamoja daima.

  ReplyDelete
 5. Kuhusu Da Subi mie sina maneno mengi ya kumwelezea. Nakumbuka kipindi fulani mwaka juzi niliandika hadi utenzi kumshukuru na kumpongeza namna alivyo mtu wa watu. Tazama hapa http://fadhilimshairi.blogspot.com/2010/05/subi-nukta.html

  Niungane na kaka Rama Msangi kusema kuwa wanablog wa zamani ni tofauti kabisa na wanablog wa sasa. Tazama jinsi blogs zinavyoibuka mithili ya uyoga. Tazama kilichomo ndani ya blogs hizo. Pengine hilo si hoja.

  Wanablog tumekuwa tukiishi kama ndugu (old bloggers)

  Nina mengi ya kuzungumza kuhusiana na wanablog. Labda tu kuonesha jinsi wanablog tulivyo kitu kimoja ngoja niwakumbushe shairi hili hapa http://fadhilimshairi.blogspot.com/2009/07/salamu-wanablog-i.html

  Nisiharibu mchuzi. Niungane na wengine wote katika kumpongeza dada yetu Subi kwa kazi yake iliyotukuka, kwa moyo wake wa ihsani, kwa hulka yake ya kutojikweza wala kujipiga kifua mbele kuwa yeye ni yeye. Ni dada yetu mnyenyekevu ambaye kila uchao anatufanya tujivunie kufahamiana naye.

  Ninamwombea baraka tele katika maisha yake.

  Pia ninawaombea kheri wanablog wenzangu wote.

  Alamsiki.

  ReplyDelete
 6. Nahisi nikisema zaidi ya ambayo nimeshasema kuhusu NINYI wapendwa wangu, NTAONEKANA MUONGO.
  Lakini niwaeleze kuwa NAWAOMBEA NA NAWAPENDA MNO.
  Najifunza na najivunia hilo mno.
  Nawaheshimu na nawathamini sana.

  Ninyi ni ndugu zaidi ya ndugu kwa kuwa undugu wenu wa hiari unazidi udugu.

  Mu wema. Na wema uwaandame katika mema na usambae kwa wale wote wenye mema kwenu

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU