NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Tuesday, July 17, 2012

HILI NALO NENO: WABUNGE WANAOSINZIA WACHAPWE VIBOKO !!!


‘Wabunge wanaosinzia wachapwe viboko’

Sunday, 15 July 2012 10:04

Burhani Yakub, Muheza.


WAKAZI wa Kata ya Misalai Tarafa ya Amani Wilayani hapa, wamependekeza kuwepo kwa kipengele cha adhabu ya kumwagiwa maji ya baridi na kisha kuchapwa viboko kwa mbunge atakayesinzia akiwa kwenye kikao bungeni.


Wamependekeza pia kwamba adhabu hiyo iambatane na kutoruhusiwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo pamoja na kuzuiwa kugombea tena kipindi kingine mara muda wake utakapomalizika.

Walitoa mapendekezo hayo kwa wajumbe wa Tume ya maoni ya marekebisho ya Katiba ilipofika Kijiji cha Misalai kukusanya maoni ya wananchi wa Tarafa ya Amani Wilayani Muheza.

Shukrani Said (23) ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Ziarai Kata ya Misarai wilayani hapa alisema kutokana na baadhi ya wabunge kuonekana mara kwa mara kupitia runinga inayoonyesha vikao vya Bunge kuonekana wakiwa wamesinzia kuna kila haja ya Katiba mpya kuwekwa vifungu vitakavyowabana wasilale bungeni.

“Wabunge hatukuwatuma waende wakalale, matokeo yake zinapitishwa sheria zinazotubana, tuliwachagua waende wakatuwakilishe, kwa hiyo kuwe na kipengele cha adahabu ya viboko,” alisema Shukrani na kusisitiza kuwa adhabu hiyo inavyofanyika ionyeshwe kwenye runinga.

Richard Lutangilo wa Kijiji cha Bulwa Wilayani hapa alisema pamoja na adhabu ya viboko, Katiba iongeze kipengele cha kumwagiwa maji kila mbunge atakayesinzia na kama haitoshi asipewe ruhusa ya kuhudhuria vikao vitatu mfululizo na pia asiruhusiwe kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo mara kipindi chake cha miaka mitano kinapomalizika.

“Hili la viboko likiwekwa kwenye Katiba litaleta umakini wa wabunge wetu kwani tunawaona inatuhuzunisha sana sisi wapiga kura tunapowaona wakiwa wamelala fofofo bungeni wakati vikao vikiendelea,” alisema Jackob Zephania.

Hadi Mlowe (50) mkazi wa Kijiji cha Mgambo Wilayani hapa alipendekeza umri wa wagombea wa nafasi ya ubunge uanzie miaka 45 kwa kuwa amebaini wabunge vijana ndiyo chanzo cha kukosekana kwa nidhamu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Napendekeza katiba mpya iweke ukomo wa umri wa kuanzia kwa nafasi ya ubunge ili kuondokana na chombo hiki muhimu kukosekana kwa nidhamu tunasikia jinsi wabunge vijana wanavyoropoka linaonekana kama ni Bunge la kihuni,” alisema Mlowe.

Cleopas Mutabuzi (50) mkulima wa Kijiji cha Misalai alipendekeza madaraka ya Rais yapunguzwe hasa katika kuteua mawaziri, ambapo alitaka waajiriwe na Tume ya Utumishi kwa kufuata taaluma zao na siyo kuchaguliwa kisiasa.

Kadhalika nafasi ya Spika, naibu Spika na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipendekeza zisitokane na wabunge bali waajiriwe kupitia Tume ya Utumishi na baadaye majina yao yapitishwe bungeni kwa ajili ya kupewa baraka na wabunge.

Kamati hiyo ya kupokea maoni ya marekebisho ya Katiba  ilikuwa wilayani hapa kwa muda wa siku tatu ambapo iliendesha mikutano Majengo, Kwafungo, Mkuzi, Misozwe, Amani na Misalai.

Chanzo: Mwananchi

6 comments:

 1. Viboko vinavyofaa kutumika kuwachapa hawa vilaza na vilala si vingine bali kuwanyima kura ili wakae majumbani mwao walale vizuri kuliko kwenda kuwaaibisha na kuwachuuza wapiga kura wao. Mbunge anapolala bungeni maana yake ni kwamba jimbo lake nalo linalala kihuduma. Tunao wabunge wengi ambao hawajawahi kuuliza swali wala kutoa wazo lolote. Wao wanawahi kwenye daftari la mahudhurio ili kuzoa posho ya makalio. Hii ndiyo siri ya kudhoofu kwa hali yetu kiuchumi, kisiasa hata kijamii. Huwezi kuwa na wabunge kama huyo hapo anayesifika kwa kupayuka ukaendelea. Tafakarini na chukueni hatua haraka wapiga kura.

  ReplyDelete
 2. Hili swala linatakiwa liangaliwe kwa upana zaidi.

  Kitu tunachojifunza hapa ni jinsi gani binadamu (a.k.a) Homo Sapiens anapofikia kufanya maamuzi fulani (kudhalilisha, kujeruhi au kuua) bila kujali kama yana athali zingine baada ya kuwa na ghafiliko kubwa. Maoni haya yanatupa ujumbe na fundisho kuwa wananchi wamechoka na siasa za bora liende na wanasiasa wa kauli za ndiyo, ndiyo, ndiyo bungeni wakati hata hawajui wanachokikubali kutokana na kutokuwa makini.

  Kuna kisa kimoja ambacho Matondo alikielezea hapa na kilimshangaza sana ambapo Mzee mmoja alikuwa anaomba dola mbili tu ili aweze kununua maji ya machungwa akiwa mgonjwa lakini hakuna mtu aliyempatia na wengine walikuwa hata hawamsikilizi kabisa huku wakiendelea kupata "kifungua kinywa". Kisa hiki nitakifananisha na wanasiasa wetu ambao kwa uroho wa madaraka(ubinafsi) ambayo ni mlango wa kujinufaisha kimaslahi hawataki kuyaacha hata kama wamechoka kimawazo na kifikra kutokana na uzee.

  Uroho wa madaraka unawafanya pia washindwe kuwa na mpangilio wa kazi ambapo kila swala wanataka walifanye wao wenyewe kwa vile linafanyika kwa usiri wenye harufu ya rushwa ndani ya kundi furani tu na matokeo yake ni mrundikano wa shughuli zinazosababisha uchovu wa akili na mwili.

  Tatizo jingine ni wanasiasa wetu kufanya siasa kama ni ajira wakati siasa ni kipaji cha kuwatumikia wananchi. Matokeo yake tunajikuta tunakuwa na wanasiasa wanaoendeleza ajira zao kwa kuingia tena serikalini kupitia mlango wa pili (ubunge) baada ya kulazimishwa kustaafu na sheria ya nchi. Kibaya zaidi, bunge linakuwa limejaa wazee waliochoka kifikra na kimwili kwa uzee wakati ndiyo wanatakiwa wawe shupavu (active) katika kuisimamia serikali. Kwa mtaji huu, ndiyo maana tunakumbana nchini na mikataba ya kuchekesha kama siyo ya kuhuzunisha kama ile ya Tanesco.

  Lakini, kwa kuangalia kwa jicho moja, mbona naona wabunge wengi wanaosinzia ni kama vile wanene tu (obese). labda bunge linatakiwa liwe na siku maalum ya lazima katika wiki kwa wabunge wote kuwa na session kwenye gym ili kujifua. Hahahah

  ReplyDelete
 3. Wananchi wawe makini kuwaangalia wawakilishi wao katika bunge ili wabaini kuwa wanawakilishwa au wanaibiwa haki yao. Hii itasaidia sana katika uchaguzi ujao na hatimae kuwa na ufanisi na maamuzi sahihi.

  ReplyDelete
 4. Swali kubwa la kujiuliza ni kwanini mpaka wakafikia hapo,...kulala. Je ni kuwa wengine wanaongea wao wamelala...? Tusije tukahukumu bila ya kuwa na ushahidi halisi.

  Kwanini, hilo halina maana, lakini je hawo waliosinzia hko majimoni kwao kukoje, maana pia kuna kuongea nakutenda, wapo wanaoongea sana. lakini ikija kwenye kutenda ni zero!

  Jamboo jingine ni mbinu za kisiasa, maana hadi mtu akaja kuwapiga picha, hawa watu alikuwa na lengo, maalumu, huenda ni jema, kwa nia ya kuwafichua hawa walalaji bungeni, lakini, pia inaweza ikawa njia ya kuwavunja hawa jamaa nguvu, yote yamo.

  LAKINI vyovyote iwavyo, sisi kama wabunge, wawakilishi wa wanachi tukumbe dhima, tukumbuke dahamana tuliyokabidhiwa na wananchi, hilo ni deni, ujue umekula nguvu zao, posho na msahara unaopata ni nguvu yao, ipo siku utaulizwa!

  ReplyDelete
 5. Wameshazeka.mda.wao.umeisha.lakiniwanziba.nafasi.Zach vijana.wschspwe.

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU