NG'WANAKANUNDO - MANJU MASHUHURI WA KISUKUMA KUTOKA MWANZA

Wednesday, November 21, 2012

KWA WOTE MLIOSOMA SHULE YA SEKONDARI KAHORORO ENZI ZILE. MWALIMU WETU MPENDWA MR. CHRISTIAN AGRICOLA AMEFARIKI DUNIA !!!


Picha kwa hisani ya Wahakaroro Group (FB)

Kwa mliosoma Shule ya Sekondari ya Kahororo mjini Bukoba bila shaka mtakuwa mnamkumbuka mwalimu wa Fizikia Mr. Agricola. Pengine mtakuwa mnakumbuka ule mwandiko wake maridadi ubaoni. Au lile tabasamu pana usoni mwake. Au wema wake na kutopenda kuchapa wanafunzi hovyo hovyo hata enzi zile ambapo fimbo zilikuwa ndo mfalme mashuleni. Vipi kuhusu umaridadi na uhodari wake wa kufundisha Fizikia - somo gumu, lisilo na bashasha na lisilopendwa na wanafunzi wengi? Mnakumbuka alipoanguka na baisikeli katika kona za milima ya Rugambwa akaja kutupa mchapo kuhusu madhara na athari za centrifugal force? Mnakumbuka msisitizo wake kuhusu nidhamu, maadili na kuwa watu wema maishani?

Basi Mwalimu Agricola alifariki tarehe 7 Novemba 2012 jijini Dar es salaam kwa kansa ya koo. Watu waliopata bahati ya kuongea naye siku za mwisho mwisho kabisa wakati madaktari wakiwa wameshakata tamaa walisema kuwa walishangazwa na utulivu wake na imani kuu aliyokuwa nayo. Japo alikuwa katika maumivu makali, alikuwa akitabasamu na kuwaambia kuwa wasiwe na wasiwasi kwani alikuwa na imani kubwa kwamba atapona.

Binafsi namkumbuka sana Mwalimu Agricola kwani alikuwa anapenda sana mwandiko wangu. Wakati ule tukiwa kidato cha nne na akina Matungwa Lwamwasha, Samsoni Nkaitwabo, Ngulingwa Balele, Medadi Kalemani, Juma Ndekwa, Mihayo Msikela, Edwin Kalisa, Kulwa Kindija, Tindyebwa Nkunuzi, Marko Nyanda, Bundi Sida, Shega Nkingwa, Stanslaus Ephraimu .....aliwahi kunipa madaftari yenye kurasa nyingi kutokana na kuvutiwa na mwandiko wangu.  

Pumzika salama mwalimu wetu mpendwa. Wanafunzi wako uliowajali na kuwapenda ndani na nje ya darasa lako la Fizikia wapo kila mahali. Na kupitia kwao, utaendelea kuishi !!!

6 comments:

 1. Pumzika mahali pema peponi mwalimu Galileo. Agricola alisifika kwa usemi kuwa Galileo alikuwa ni mshenzi mshenzi sana akimaanisha gwiji.

  ReplyDelete
 2. Pumzika kwa amani mwalimu ..naamini umefanya kazi nzuri maana matunda twayaona.

  ReplyDelete
 3. Twamuombea mwalimu huyo makazi mema peponi

  ReplyDelete
 4. Mwalimu Matondo kulikoni mbona ugani kwako kumejaa vumbi na nyasi... Mzima huko? Kila nikitembelea ugani mwako nakuta kitu kile kile... tanzia. Hebu tafadhali tujuze kilichokupata hadi ukakimbia uga wako.

  ReplyDelete
 5. Nilipata habari hizi hivi majuzi Novemba 2013 kutoka kwa injinia Kalumna aliyenitangulia Kahororo mwaka 1993. Mwalimu alikuwa ni mahiri na hakuweza kuacha kazi kipindi wafanyakazi walipokuwa wanakwenda kufanya biashara au UN. Eng. Geofrey Kato Kahororian 93-96

  ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

VITAMBULISHO VYETU