Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kisukuma
  
Audio ya Sinema ya Yesu Katika Kiswahili

Monday, June 11, 2012

PATA NENO LA KUTIA MOYO HAPA KILA ASUBUHI - KIPENGELE KIPYA


Kwa muda sasa nimekuwa nikisoma kazi mbalimbali za Dr. Wayne Dyer. Katika kazi zake nyingi, mwalimu huyu mashuhuri anasisitiza kuhusu umuhimu wa kuanza kila siku yako ukiwa katika utangamano na usawazisho wa fikra na roho. Na njia mojawapo ya kufikia utangamano huu ni kukwepa habari (zenye nguvu) hasi.

Kwa bahati mbaya, habari hizi hasi ndizo zimetawala vyombo vya habari - vifo, vita, mauaji, magonjwa, umasikini n.k. Habari hizi zikiendelea kufyonzwa kila siku basi pole pole zinaanza kujenga mtazamo hasi wa ulimwengu na mwishowe hufanya mtazamo wetu wa kijumla kuhusu ulimwengu na maisha kuwa wa hasi. Habari hizi hazifai kuwa ndizo kifungua kinywa cha ubongo wetu kila siku!

Badala ya kufyonza habari hizi za kusikitisha kila asubuhi, Dr. Dyer anafundisha kuziepuka. Badala ya kuzifyonza taarifa hizi kupitia runinga na magazeti, pengine ni bora kuianza siku yako kwa mambo rahisi rahisi tu kama:

(1) Kwenda nje na kuvuta hewa baridi yenye kusisimua hisia. 
(2) Kutazama uzuri na maajabu ya maumbile - mf. maua mazuri yalivyochanua asubuhi ile, vipepeo walivyopambika na wanavyoruka kwa furaha, sikiliza sauti nzuri za ndege wakifurahia uhai wao......

(3) Kumshukuru Mungu (au cho chote unachokiamini) kwa maajabu ya uhai na ukweli kwamba uko hai na salama. Baada ya kugundua kuwa u hai na kwamba u sehemu ya furaha ya siku hiyo, basi jiaminishe kuwa siku hiyo itakuwa njema na yenye furaha; na kwamba hukuzaliwa kwa bahati mbaya bali u kiungo muhimu katika mnyororo mrefu na changamano wa msimbo wa maumbile (ecological system). Kwa hakika u sehemu ya uumbaji na nguvu za Muumba wako zimo ndani mwako. 

(4) Kama huyo Aliyekuumba (Mungu) ndiye Aliyekupa uzima na afya, basi hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi. Jiaminishe kuwa uko salama na kwamba siku hiyo itakuwa njema, iliyojaa matumaini, afya njema na uzima wa kweli. 

Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa, watu wanaoutazama ulimwengu kwa jicho chanya ndiyo huishi maisha marefu na ndiyo wanaongoza kwa kupona hata wanapopambana na magonjwa hatari angamizi kama saratani na mengineyo. Kumbe nguvu ya uponyaji imo ndani mwetu na kamwe hatupaswi kuishi kwa wasiwasi kama ambavyo vyombo vya habari vinajaribu sana kutuaminisha kila siku. 

Ni katika mtazamo huu kwamba kuanzia leo, nitakuwa nikiweka ujumbe wa kutia moyo hapa kila asubuhi. Pita hapa ukiweza, jifunze (nifundishe) na iache nuru njema yenye matumaini ikaipambe siku yako. Mungu Atubariki sote na nakutakia siku njema !!!

**** Hebu na Tuanze Sasa ****


Neno la Kutia Moyo Asubuhi ya Leo (11/6/12)

=> Unakijua kikupacho furaha ya kweli hapa duniani?<=

- Kakitende hicho
- Kawe kitu hicho 
- Kawashirikishe na wengine
- Kadumu nacho
- Kafurahi zaidi tena na tena !!!

=> Angalizo Muhimu <=

Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba, watu wengi hupata furaha ya kweli wanapowasaidia watu wengine wenye uhitaji wa kweli. Tendo moja tu lenye kuonyesha upendo na ubinadamu wetu linayo nguvu ya kugeuza kabisa maisha na mtazamo wa mtu hapa duniani. Soma HAPA kuona jinsi tendo moja tu jema nililoshuhudia pale Muhimbili mwaka 1993 lilivyoweza kubadili kabisa mtazamo wangu kuhusu binadamu na ubinadamu wake. Japo najua kuwa binadamu ni mnyama na anaweza kufanya matendo mengi ya kinyama kama vyombo vya habari vinavyohubiri kila siku, najua pia kuwa binadamu huyu huyu pia bado ni binadamu na anaweza kutenda matendo mengi ya kibinadamu. Hebu na ukawe na siku njema !!!

1 comment:

  1. VIPI HII YS KUTUTIA MOYO KILA ASUBUHI BADO UNAENDELEA KUTOA?

    ReplyDelete

JIANDIKISHE HAPA

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

ASANTE KWA MAONI YAKO

Widget by ReviewOfWeb